2010–2019
Kupata Shangwe katika Kushiriki Injili
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Kupata Shangwe katika Kushiriki Injili

Tunaye Baba mwenye upendo Mbinguni, ambaye anasubiri sisi tumgeukie Yeye ili abariki maisha yetu na maisha ya wale wanaotuzunguka.

Mojawapo ya nyimbo zangu ninazozipenda za msingi unaanza na maneno haya:

Mimi ni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Ninajua mimi ni nani.

Ninajua Mpango wa Mungu.

Nitamfuata kwa imani.

Ninaamini katika Mwokozi, Yesu Kristo.1

Ni maelezo rahisi na ya kupendeza yaliyoje juu ya kweli tunazoamini!

Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunajua sisi ni akina nani. Tunajua kwamba “Mungu ni Baba wa roho zetu. Sisi ni … watoto Wake, na Yeye anatupenda. Tuliishi [pamoja Naye mbinguni] kabla [hatujaja] duniani.”

Tunajua Mpango wa Mungu. Tulikuwepo pamoja Naye wakati alipouwasilisha. Lengo “kamili la Baba yetu wa Mbinguni—kazi yake na utukufu Wake—ni kutuwezesha kila mmoja wetu kufurahia baraka zake zote. Yeye … ametoa mpango mkamilifu kwa ajili ya kukamilisha lengo Lake. Tulielewa na kukubali mpango huu … wa furaha, … ukombozi, na … wokovu” kabla ya kuja duniani.

“Yesu Kristo ni kitovu cha mpango wa Mungu. Kupitia Upatanisho Wake, Yesu Kristo alitimiza lengo la Baba Yake na kufanya iwezekane kwa kila mmoja wetu kufurahia maisha ya kutokufa na kuinuliwa. Shetani, au ibilisi, ni adui wa mpango wa Mungu” na amekuwa tangu mwanzo.

“Haki ya kujiamulia, au uwezo wa kuchagua, ni mojawapo ya karama kuu za Mungu kwa watoto Wake. … Lazima tuchague ikiwa tutamfuata Yesu Kristo au tutamfuata Shetani.”2

Hizi ni kweli rahisi ambazo tunaweza kushiriki na wengine.

Acha niwasimulie wakati mama yangu aliposhiriki kweli rahisi kama hizo kwa kukubali tu kuwa na mazungumzo na kutambua fursa.

Miaka mingi iliyopita, mama yangu alikuwa akirejea Ajentina kuzuru pamoja na kaka yangu. Mama yangu hakupenda ndege, hivyo alimuomba mmoja wa wanangu kumpa baraka ya faraja na ulinzi. Alihisi ushawishi kumbariki pia bibi yake kwa ulinzi maalumu na mwongozo kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kuimarisha na kugusa mioyo ya wengi ambao walikuwa na hamu ya kujifunza injili.

Picha
Familia ya Pol

Katika uwanja wa ndege wa Salt Lake, mama na kaka yangu walikutana na msichana wa miaka 7 aliyekuwa akirejea nyumbani kutoka safari ya kuteleza kwenye theluji pamoja na familia yake. Wazazi wake waligundua ni kwa muda mrefu alikuwa akizungumza na mama na kaka yangu na waliamua kuungana nao. Walijitambulisha wao na binti yao kama Eduardo, Maria Susana, na Giada Pol. Kulikuwa na muunganiko asilia na wa kipekee kwa familia hii nzuri.

Familia zote zilifurahia kusafiri pamoja katika ndege moja kwenda Buenos Aires, Ajentina. Mazungumzo yao yalipoendelea, mama yangu aligundua kwamba mpaka wakati ule, walikuwa hawajawahi kusikia kuhusu Kanisa la Urejesho la Yesu Kristo.

Mojawa ya maswali la kwanza Susana alilouliza lilikuwa, “Je, ungeweza kuniambia kuhusu makumbusho yale yenye sanamu ya dhahabu juu yake?”

Mama yangu alielezea kwamba jengo zuri halikuwa makumbusho bali hekalu la Bwana ambapo tunafanya maagano na Mungu ili tuweze kurudi kuishi pamoja Naye siku moja. Susana alikiri kwa mama yangu kwamba kabla ya safari yao ya Salt Lake, alikuwa ameomba kwa ajili ya jambo la kuimarisha roho yake.

Wakati wa safari, mama yangu alitoa ushuhuda wake rahisi lakini imara wa injili na kumualika Susana kuwatafuta wamisionari kwenye mji wake. Susana alimuuliza mama yangu, “Nitawezaje kuwapata?”

Mama yangu alijibu, “Huwezi kuwakosa; huwa wanakuwa wavulana wawili waliovalia shati nyeupe na tai au wasichana wawili waliovalia vizuri, na mara zote wanavalia beji inayoonesha majina yao na pia ‘Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.’”

Familia zilibadilishana namba za simu na kuagana katika uwanja wa ndege wa Buenos Aires. Susana, ambaye tangu hapo amekuwa rafiki yangu kipenzi, amenisimulia mara nyingi kwamba alihisi huzuni kumwacha mama yangu uwanja wa ndege. Alisema, “Mama yako aling’ara. Siwezi kulielezea, lakini alikuwa na mng’aro kumzunguka ambao sikutaka kuuacha nyuma.”

Punde tu baada ya Susana kufika katika mji wake, yeye na binti yake, Giada, walikwenda kushiriki uzoefu huu pamoja na mama wa Susana, aliyeishi nyumba kadhaa kutoka nyumbani kwao. Walipokuwa wakiendesha gari, Susana alitokea kuwaona wavulana wawili wakitembea mtaani wakiwa wamevalia jinsi mama yangu alivyoelezea. Alisimamisha gari yake katikati ya mtaa, akatoka nje, na kuwauliza wavulana hawa, “Je, ninyi mnaweza kuwa mmetoka Kanisa la Yesu Kristo?”

Walisema, “Ndiyo.”

“Wamisionari?” aliuliza.

Kwa pamoja walijibu, “Ndiyo ni sisi!”

Kisha alisema, “Ingieni kwenye gari yangu; mnaenda nyumbani kunifundisha.”

Picha
Familia ya Pol

Miezi miwili baadaye, Maria Susana alibatizwa. Binti yake, Giada, pia alibatizwa alipotimiza miaka tisa. Bado tunafanya kazi na Eduardo, ambaye tunampenda bila kujali chochote.

Tangu hapo, Susana amekuwa mmoja wa wamisionari mashujaa niliowahi kukutana nao. Yeye ni kama wana wa Mosia, akileta nafsi nyingi kwa Kristo.

Katika mojawapo ya mazungumzo yetu, nilimuuliza, “Ni nini siri yako? Ni kwa jinsi gani unashiriki injili pamoja na wengine?”

Alinijibu, “Ni rahisi sana. Kila siku kabla sijaondoka nyumbani, ninasali, nikimuomba Baba wa Mbinguni aniongoze kwa mtu anayehitaji injili katika maisha yao. Wakati mwingine ninabeba Kitabu cha Mormoni ili kushiriki nao au kadi ndogondogo kutoka kwa wamisionari—na ninapoanza kuzungumza na mtu, ninawauliza ikiwa wamewahi kusikia kuhusu Kanisa.”

Susana pia alisema, “Nyakati zingine ninatabasamu tu wakati nikingojea gari moshi. Siku moja mtu aliniangalia na kusema, ‘Nini kinakufanya utabasamu?’ Alikuwa kama vile amenishtukiza.

“Nilijibu, ‘ninatabasamu kwa sababu nina furaha!’

“Kisha akasema, ‘Nini kinakufanya uwe na furaha?’

“Nilijibu ‘mimi ni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na hilo linanipa furaha. Je, umewahi kulisikia?’”

Wakati aliposema hapana, alimpa kadi ndogo na kumwalika kuhudhuria ibada za Jumapili iliyofuata. Jumapili iliyofuata, alimpokea mlangoni.

Rais DallinH. Oaks alifundisha:

“Kuna vitu vitatu kila muumini anaweza kufanya ili kusaidia kushiriki injili. …

Kwanza, wote tunaweza kuomba ili kuwa na hamu ya kusaidia katika sehemu hii muhimu ya kazi ya wokovu. …

Pili, tunaweza kutii amri. … Waumini waaminifu daima watakuwa na Roho ya Mwokozi … pamoja nao ili kuwaongoza pale wanapotafuta kushiriki katika kazi kuu ya kushiriki injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Tatu, tunaweza kuomba kwa ajili ya msukumo juu ya kile sisi tunachoweza kufanya … ili kushiriki injili pamoja na wengine. … [na] kusali kwa kujitolea kutenda juu ya msukumo ambao [sisi] tunaupokea.”3

Akina kaka, akina dada, watoto, na vijana, je, tunaweza kuwa kama rafiki yangu Susana na kushiriki injili na wengine? Je, tunaweza kumwalika rafiki ambaye si wa imani yetu kuja kanisani pamoja nasi Jumapili? Au pengine je, tunaweza kushiriki nakala ya Kitabu cha Mormoni na ndugu au rafiki? Je, tunaweza kuwasaidia wengine kupata mababu zao kwenye FamilySearch au kushiriki na wengine kile tulichojifunza katikati ya wiki wakati tulipokuwa tukijifunza Njoo, Unifuate? Je, tunaweza kuwa zaidi kama Mwokozi wetu, Yesu Kristo, na kushiriki na wengine kile kinachotuletea shangwe kwenye maisha yetu? Jibu lamaswali haya yote ni ndiyo! Tunaweza kufanya hivyo!

Katika maandiko tunasoma kwamba “waumini wa Kanisa la Yesu Kristo wanatumwa ‘kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu kwa ajili ya wokovu wa nafsi za watu’ (Mafundisho na Maagano 138:56). Kazi hii ya wokovu hujumuisha kazi ya umisionari wa waumini, kuwabakiza waongofu, kuwaimarisha waumini wasioshiriki kikamilifu, kazi ya hekalu na historia ya familia, na kufundisha injili.’”4

Rafiki zangu wapendwa, Bwana anatutaka tuikusanye Israeli. Katika Mafundisho na Maagano, Yeye amesema, “Wala msiwaze kabla nini cha kusema; bali yahifadhini katika akili zenu daima maneno ya uzima, nanyi mtapewa saa ile ile mtakayosema sehemu ile ambayo itakayokusudiwa kwa kila mtu.”5

Kwa kuongezea, Ametuahidi:

“Na kama itakuwa kwamba utafanya kazi siku zako zote katika kutangaza toba kwa watu hawa, na kuleta, japo iwe nafsi moja kwangu, shangwe yako itakuwa kubwa jinsi gani pamoja naye katika ufalme wa Baba yangu!

“Na sasa, kama shangwe yako itakuwa kubwa kwa hiyo nafsi moja ambayo umeileta kwangu katika ufalme wa Baba yangu, itakuwa shangwe kubwa namna gani kwako kama utazileta nafsi nyingi kwangu!”6

Wimbo wa Msingi nilioanza nao unahitimisha kwa maelezo haya ya kupendeza:

Ninaamini katika Mwokozi, Yesu Kristo.

Nitaliheshimu jina Lake.

Nitafanya kilicho chema;

Nitafuata nuru yake.

Ukweli Wake nitatangaza.7

Ninatoa ushahidi kwamba maneno haya ni ya kweli na kwamba tunaye Baba mwenye upendo Mbinguni, ambaye anasubiri tumgeukie ili Abariki maisha yetu na maisha ya wale wanaotuzunguka. Na tuwe na hamu ya kuwaleta kaka na dada zetu kwa Kristo ndilo ombi langu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “The Church of Jesus Christ,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,77.

  2. Hubiri Injili Yangu: Mwongozo kwa Huduma ya Umisionari, toleo jipya (2018), 48.

  3. DallinH. Oaks, “Kushiriki Injili ya Urejesho,” Liahona, Nov. 2016, 58.

  4. Handbook 2: Administering the Church, 5.0, ChurchofJesusChrist.org; ona pia L. Whitney Clayton, “The Work of Salvation: Then and Now,” Liahona, Sept. 2014, 23.

  5. Mafundisho na Maagano 84:85.

  6. Mafundisho na Maagano 18:15–16.

  7. “Kanisa la Yesu Kristo,” 77.