2019
Tuliongozwa kwa Monica
Oktoba 2019


Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Tuliongozwa kwa Monica

Rosana Soares

Utah, USA

Picha
woman standing on balcony watching other woman at window

Kielelezo na Stan Fellows

Wakati nikiishi São Paulo, Brazil, nilipata kumfahamu mwanamke wa kipekee aliyeitwa Graça. Alikuwa mwanamke wa kupendeza na mkarimu na rafiki wa wote.

Graça alikuwa mwenza wangu katika mafundisho ya kutembeleana. Alikuwa mama wa watoto watatu, alifanya kazi ya muda, na hakuwa na gari wala simu, lakini haya hayakumzuia kutumikia.

Kutoka kwenye ubaraza wangu wa ghorofani ningeweza kuona dirisha moja la nyumba yake. Alipokuwa nyumbani, Graça angeweka kipande cha nguo nyekundu kwenye dirisha lile kuashiria kuwa alikuwa tayari kwenda kutembelea. Hakuwahi kupata sababu ya kutohudumia. Mara nyingi nimefikiria kuhusu ishara ya Graça na mfano wake wa kupendeza wa huduma ya uaminifu na rahisi.

Uzoefu mmoja unajitokeza katika akili yangu. Tulijiandaa na kuomba kabla ya kwenda kumtembelea mmoja wa dada zetu. Tulipoikaribia nyumba, tuligundua tulikuwa tumeenda kwenye nyumba ya dada tofauti! Tulikuwa tumepangiwa kumtembelea dada huyu, mama wa watoto watatu asiyeshiriki kikamilifu, lakini hatukuwa tumepanga kumtembelea siku hiyo. Kwa sababu tulikuwa pale, tuligonga, lakini hakuna aliyejibu.

Tuliamua kuwa wavumilivu na kusubiri. Dada yule, Monica, hatimaye alikuja na kutuambia kwamba alikuwa na shughuli nyingi. Tuligundua alikuwa amechoka na machozi yalimlengalenga. Tuliposema tulikuwa pale kusaidia, alituruhusu kuingia. Mtoto wake alikuwa akilia, hivyo tulimwambia amshughulikie mtoto na sisi tungesubiri. Wakati Monica alipopanda ngazi kwenda juu pamoja na mtoto, tulianza kazi, tukisafisha vyumba kadhaa na kukunja nguo zote ambazo tungeweza kuziona.

Wakati Monica alipoona jinsi nyumba yake ilivyopendeza, alianza kulia, akafungua moyo wake kwetu, na kushiriki baadhi ya changamoto zake. Tuliahidi kumsaidia, na tulizungumza na rais Muungano wa Usaidizi wa Akina mama kuhusu changamoto zake. Jumapili iliyofuata, Monica alikuwa kanisani.

Monica alikuwa dada aliyeshiriki kikamilifu na mwenye furaha, na tuliendelea kumhudumia kwa upendo na kujali. Bado ana changamoto zilezile, lakini aliweza kukabiliana nazo kwa imani zaidi na ujasiri kwa sababu ya kushiriki kwake kikamilifu Kanisani.

Nina shukrani kwa mfano wa Graça wakati tulipotumikia pamoja. Tuliomba kwa ajili ya mwongozo, na Mungu alituongoza kwa Monica.