2019
Kumtumikia Bwana kwa Kihispania
Oktoba 2019


Mifano ya Ujasiri

Kumtumikia Bwana kwa Kihispania

Mwandishi anaishi Utah, Marekani.

Picha
Serving the Lord in Spanish

Fikiria kwamba rafiki yako amekupa kitabu kizuri kuliko vyote ambacho amewahi kusoma. Unafunua jalada … na unagundua huwezi kusoma kitabu. Kimeandikwa kwa lugha tofauti! Ungefanya nini?

Katika miaka ya mwanzo ya Kanisa, Kitabu cha Mormoni kilikuwa kimechapishwa kwa Kiingereza tu. Rais Brigham Young aliwaita wamisionari wawili kuhubiri injili Mexico na kutafsiri Kitabu cha Mormoni kwa Kihispania. Lakini walihitaji msaada zaidi kufanya hilo. Walijua kidogo tu kwamba ng’ambo ya bahari, Mungu alikuwa amemuandaa mtu ambaye angewapa msaada hasa waliouhitaji.

Meliton Gonzalez Trejo alitoka kwenye familia ya kitajiri huko Hispania. Alisoma kwa bidii shuleni na kuwa afisa katika jeshi la Hispania. Daima alivutiwa na dini, lakini hakuna alichopata kilihisi kuwa sahihi. Siku moja alisikia afisa mwingine akizungumza kuhusu kundi la watu waliojiita “Watakatifu.” Walikuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na nabii wa Mungu alikuwa amewaongoza hadi Rocky Mountains Marekani. Meliton alihisi hamu kubwa ya kukutana nao. Alijiunga na kikosi cha jeshi kilichopelekwa Ufilipino, akitumaini hii ingesaidia kumfikisha Marekani baadaye. Lakini Meliton alijikuta akiwa na shughuli nyingi kwamba kuwatembelea Watakatifu kulianza kuonekana si muhimu sana.

Kisha Meliton akawa mgonjwa sana. Alikumbuka sababu ya kwa nini alikuwa amekuja Ufilipino na alimwomba Mungu kuhusu kile alichopaswa kufanya. Usiku ule, Meliton alipata ndoto maalumu. Alijua alipaswa kwenda kwenye Rocky Mountains.

Pale Meliton alipopona ugonjwa wake, aliendelea na safari yake kuelekea Marekani. Aliwasili California mnamo Julai 4, 1874, na kuelekea Jiji la Salt Lake.

Wakati Meliton alipofika Salt Lake, alipata tatizo: angeweza kusoma Kiingereza lakini hakuwa amewahi kukizungumza. Asingeweza kuzungumza na yeyote! Lakini aliamua kwamba ikiwa asingeweza kuzungumza na watu, angepata umakini wao kwa njia nyingine. Meliton alivaa sare yake ya jeshi la Hispania na kutembea kote katika mitaa ya jiji. Kama alivyotumaini, watu wengi walimtambua! Hatimaye alionekana na muumini wa Kanisa aliyeitwa Kaka Blanchard, profesa wa chuo kikuu ambaye alizungumza Kihispania. Kaka Blanchard alimsaidia Meliton kupata makazi Salt Lake na kumfundisha injili. Punde Meliton alibatizwa.

Kaka Blanchard pia alimtambulisha Meliton kwa Rais Brigham Young. Meliton alimwambia Rais Brigham Young kwamba zaidi ya kitu chochote, alitaka kutafsiri Kitabu cha Mormoni kwa Kihispania.

Rais Young alimuomba Meliton kuwasaida wamisionari ambao walikuwa wanakwenda Mexico kutafsiri sehemu za Kitabu cha Mormoni kwa Kihispania. Meliton alitumia wiki nyingi kutafsiri maneno ya Kiingereza kwa Kihispania. Kila usiku alirejea tafsiri yake pamoja na wamisionari. Walizungumza Kihispania kidogo lakini walihisi tafsiri hii muhimu ilihitaji mzungumzaji mzawa wa Kihispania. Walijua Meliton alikuwa jibu la sala zao. Mnamo 1875 tafsiri ilichapishwa. Ilikuwa ikiitwa Trozos Selectos del Libro de Mormon (Vifungu Vilivyochaguliwa kutoka Kitabu cha Mormoni).

Wamisionari sasa walikuwa tayari kwenda Mexico. Walipakia nakala 1,500 za maandiko yaliyotafsiriwa juu ya farasi na kuanza safari yao. Kwa mara ya kwanza, wazungumzaji wa Kihispania waliweza kusoma Kitabu cha Mormoni kwa lugha yao wenyewe! Japokuwa Meliton alikuwa ameishi maelfu ya maili mbali na Hispania, Baba wa Mbinguni alimuongoza mahali ambapo alihitaji kuwa hasa. Kwa sababu ya ujasiri na imani ya Meliton, alisaidia kuleta neno la Mungu kwa watu wasio na idadi.