2021
Kujifunza Historia ya Kanisa Kunaimarishaje Imani Yangu
Januari 2021


Je, Kujifunza Historia ya Kanisa Kunaimarishaje Imani Yangu?

Picha
illustration of African woman with basket on head

Picha kutoka Getty Images

Kama mwanafunzi wa shule ya upili katika Afrika ya Kusini, nilifurahia kujifunza historia. Nilipokwenda chuo kikuu, nilipokea digrii yangu katika historia. Kama mwanafunzi wa seminari na kisha kama mwanafunzi wa dini ngazi ya chuo, nilifurahia kozi zangu zote, lakini hasa nilifurahia Mafundisho na Maagano kwa sababu ilinitambulisha historia ya Kanisa. Miaka inavyopita, nimekuwa nikifurahia kusoma vitabu vya historia ya Kanisa—hata zile ambazo zinaongelea mada ngumu katika historia yetu. Ninapoendelea kujifunza historia ya Kanisa kutoka vyanzo mbali mbali, imani yangu mwenyewe inaimarishwa. Hapa kuna njia tatu ambavyo inatokea.

Historia ya Kanisa inatoa uhusiano kwangu mimi, hasa wakati inapokuja kwenye desturi za kale, ikijumuisha vizuizi vya ukuhani na baraka za hekaluni. Nilipojifunza kwa mara ya kwanza kwamba kulikuwa na wakati ambapo wanaume weusi walizuiliwa kuwa na ukuhani, imani yangu ilitikisika. Je, iliwezekanaje kwa Kanisa nililolipenda kuzuia ukuhani kwa watu weusi. Baadhi ya watu walijaribu kunionyesha mimi maelezo wakidai ilikuwa ni maelezo ya kimafundisho au kimaandiko. Haya yalikuwa yananichanganya na kunitatiza sana.

Kadiri muda ulivyopita, ilikuwa ni maelezo ya kihistoria ambayo yalileta maana na kutoa faraja. Utangulizi wa kihistoria kwa Tamko Rasmi 2, kwa mfano, unaelezea kwamba Joseph Smith aliwatawaza wanaume wachache weusi lakini viongozi wa Kanisa walisimamisha kuwatunukia ukuhani kwa watu weusi mapema katika historia ya Kanisa. Kisha inafanya maelezo haya muhimu: “Kumbukumbu za Kanisa hazitoi utambuzi wa wazi wa asili ya desturi hii.”1 Insha za Mada za Injili2 na vitabu vingine vya kiada vya Kanisa vinatoa maelezo ya kina zaidi na maudhui ya nyongeza ya kihistoria.3 Ufafanuzi huu wa kihistoria ulileta maana kwangu na kuimarisha imani yangu.

Historia ya Kanisa inanisaidia kuwa na shukrani kwa wale ambao wametangulia mbele. Hii hususani ni kweli wakati mtu anapofikiria michango ambayo inaonekana waumini wa “kawaida” wamefanya. Kwa mfano, majengo ya kanisa yaliyojengwa kuzunguka kote Afrika ya Kusini, Zimbabwe, na Zambia katika miaka ya 1950 na 1960 yalifanywa yawezekane kwa michango ya waumini. Kupokea baraka za hekaluni kulihitaji dhabihu kubwa zaidi. Wakijua ingechukua miongo kadhaa kabla wao kuweza kuwa na mahekalu katika Afrika waumini wengi waliuza mali zao, ikijumuisha majumba yao, ili kupata fedha za kusafiri kwenda hekaluni na kushiriki katika ibada hizo takatifu. Kanisa katika bara la Afrika limejengwa juu ya imani ya waumini hawa wa mwanzo ambao walikuwa na kidogo lakini walitoa dhabihu kubwa. Ninaposoma kumbukumbu zao, imani yangu inaimarika na utayari wangu wa kutoa dhabihu unaongezeka.

Picha
illustration of African continent

Historia ya Kanisa inanitia moyo wa kuwa mtunzaji bora wa KUMBUKUMBU. Viongozi wa Kanisa wametuhimiza kutunza shajara. Kwa nini? Kwa sababu historia ya Kanisa ni kumbukumbu ya “namna ya maisha, … imani, na matendo” ya waumini wake (ona Mafundisho na Maagano 85:2). Wakati wowote ninaposoma historia ya Kanisa, kama vile historia mpya, Watakatifu, inavutia kwamba juzuu hizi zimewezekana tu kwa sababu ya shajara, barua, na kumbukumbu nyingine za waumini wa kawaida wa Kanisa. Historia ya wazi kabisa ya mtu wa kwanza inanitia moyo wa kuwa mtunzaji bora wa shajara, kwa njia hiyo niwasaidie wanahistoria wa baadae kuandika historia ya kweli ya Kanisa katika Afrika.

Pia kuna baraka ya kibinafsi kutokana na kusoma historia ya Kanisa na kujitahidi kutunza kumbukumbu zangu mwenyewe. Kama Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, ambavyo amefundisha, nimebarikiwa kuona na kuukumbuka mkono wa Bwana katika maisha yangu na maisha ya washiriki wa familia yangu.4 Ukumbusho huu unaimarisha ushuhuda wangu na kuongeza uwezo wangu wa kukabili changamoto katika maisha yangu. Ninapotunza kumbukumbu zangu mwenyewe na kufikiria kuhusu waumini wengine nao kwa uangalifu wakiandika, ninaanza kuona mpangilio mkuu wa Bwana akiwa analirejesha Kanisa Lake na ufalme katika siku za mwisho.

Masomo haya na mengine mengi niliyojifunza kutokana na kujifunza historia ya Kanisa yamechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yangu mwenyewe ya kiroho. Masomo haya yamenipa ujasiri wa kuitetea imani yangu kwa sababu ninaelewa kwa nini tunafanya kile tunachofanya. Kuwa mwenye kufahamu muktadha wa kihistoria wa desturi na imani nyingi kumenifanya niwe mwalimu mahiri na mfuasi mahiri.

Muhtasari

  1. Ona utangulizi wa Tamko Rasmi.

  2. Ona “Jamii na Ukuhani,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org.

  3. Ona, kwa mfano, Foundations of the Restoration (Kitabu cha kiada cha Church Educational System), 2016, mlango wa 26.

  4. Ona Henry B. Eyring, “Ee Kumbuka, Kumbuka,” Liahona, Nov. 2007, 66-69.

Picha kutoka Getty Images