Maandiko Matakatifu
Joseph Smith—Historia ya 1


Joseph Smith—Historia ya

Dondoo kutoka Historia ya Joseph Smith, Nabii

Mlango wa 1

Joseph Smith aelezea historia ya ukoo wake, watu wa familia yake, na sehemu walizoishi mwanzoni—Msisimko usio wa kawaida juu ya dini waenea magharibi mwa New York—Anaazimia kuomba hekima kama alivyoelekezwa na Yakobo—Baba na Mwana wamtokea, na Joseph aitwa kwenye huduma yake ya unabii. (Mstari ya 1–20.)

1 Kutokana na taarifa nyingi ambazo zimesambazwa na watenda maovu na watu wenye hila, juu ya akuzaliwa na kukua kwa bKanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ambazo zote zimebuniwa na watunzi wa taarifa hizo ili kupigana dhidi ya sifa zake kama Kanisa na kukua kwake ulimwenguni—Nimeshawishiwa na taarifa hizo kuandika historia hii, ili kuyasahihisha mawazo ya umma, na kuweka watafutao ukweli wote waupate ukweli, kama ulivyotokea, juu yangu mimi mwenyewe na Kanisa, kwa kadiri nilivyo nazo kweli hizo katika miliki yangu.

2 Katika historia hii nitaelezea matukio mbali mbali yahusianayo na Kanisa hili, katika ukweli na haki, kama yalivyotokea, au kama yalivyo sasa, ikiwa sasa [1838] mwaka wa nane tangu akuanzishwa kwa Kanisa linalosemwa.

3 aNilizaliwa katika mwaka wa Bwana wetu wa elfu moja mia nane na tano, siku ya ishirini na tatu ya Desemba, katika mji wa Sharon, wilaya ya Windsor, Jimbo la Vermont, … Baba yangu, bJoseph Smith, Mkubwa, aliondoka katika Jimbo la Vermont, alihamia Palmyra, wilaya ya Ontario (sasa Wayne), katika Jimbo la New York, nilipokuwa katika mwaka wangu wa kumi, au karibu na umri huo. Karibu miaka minne baada ya baba yangu kuwasili katika Palmyra, yeye pamoja na familia yake walihamia Manchester katika wilaya hiyo hiyo ya Ontario—

4 Familia yake ilikuwa ya watu kumi na mmoja, ambao ni baba yangu, aJoseph Smith; bmama yangu, Lucy Smith (ambaye jina lake kabla ya kuolewa lilikuwa Mack, binti wa Solomon Mack); kaka zangu, cAlvin (ambaye alifariki 19 Novemba 1823, katika mwaka wa 26 wa umri wake), dHyrum, mimi mwenyewe, eSamuel Harrison, William, Don Carlos; na dada zangu, Sophronia, Catherine, na Lucy.

5 Wakati fulani katika mwaka wa pili baada ya kuhamia kwetu Manchester, katika sehemu tuliyokuwa tukiishi palitokea msisimko usio wa kawaida juu ya suala la dini. Lilianza na Wamethodisti, lakini mara likawa jambo la kawaida miongoni mwa madhehebu mengine katika eneo lile la nchi. Hata, wilaya yote ya nchi ile ilionekana kuathiriwa na jambo hilo, na umati mkubwa ulijiunga kwenye dini hizi tofauti, ambazo zilileta vurugu ambayo si ndogo na mgawanyiko miongoni mwa watu, wengine wakilia, a“Tazama huku!” na wengine “Tazama kule!” Wengine walikuwa wakishindania imani ya Kimethodisti, wengine Kipresbiteri, na wengine Kibaptisti.

6 Kwani, licha ya upendo mkubwa ambao waongofu hawa wa imani mbali mbali walikuwa wakiuelezea wakati wa uongofu wao, na ari kubwa iliyoonyeshwa na wachungaji husika, ambao walikuwa wakijihusisha katika kuanzisha na kuikuza hali hii ya hisia ya kidini isiyo ya kawaida, ili kumfanya kila mtu aongolewe, kama wao walivyoona vyema kuiita, acha wajiunge na dhehebu lolote watakalochagua; lakini wakati waongofu hao walipoanza kuhama, wengine wakienda dhehebu jingine na wengine kwingine, ilionekana kwamba hisia zile njema zilizoonekana kwa wote wachungaji na waongofu zilikuwa za kujisingizia zaidi kuliko ukweli; kwa kuwa hali ya mchafuko mkubwa wa hisia mbaya ilijitokeza—kuhani akibishana na kuhani, na mwongofu dhidi ya mwongofu; hivyo ile hali yao yote ya hisia njema iliyokuwepo miongoni mwao, kama ilikuwepo, ilikuwa imepotea kabisa katika augomvi wa maneno na ushindani juu ya maoni yao.

7 Ilikuwa wakati huu katika mwaka wangu wa kumi na nne. Familia ya baba yangu ilikuwa ikishawishika kubadili dini katika imani ya Kipresbiteri, na wanne kati yao walijiunga na kanisa hilo, nao ni mama yangu Lucy; kaka zangu Hyrum na Samuel Harrison; na dada yangu Sophronia.

8 Wakati huu wa msisimko mkubwa akili yangu ilizinduliwa na tafakuri nzito na yenye mashaka makubwa; lakini ingawa hisia zangu zilikuwa nzito na daima kali, hata hivyo nilijiweka mbali na dini hizi, ingawa nilikuwa nimehudhuria mikutano yao kadha wa kadha kadiri nafasi ilivyoniruhusu. Baada ya muda akili yangu ikawa kwa kiasi fulani ikipendelea madhehebu ya Kimethodisti, nami nilijisikia hamu ya kutaka kujiunga nao; lakini mchafuko mkubwa na mzozo ulikuwepo miongoni mwa madhehebu mbali mbali, ilikuwa vigumu kwa mtu kijana mdogo kama mimi nilivyokuwa, na kwa jinsi nisivyowafahamu watu na mambo yao, kuweza kufikia uamuzi wa nani ni sahihi na nani si sahihi.

9 Akili yangu wakati mwingine ilisisimka sana, kwani kilio na mayowe yalikuwa makuu na yasiyokwisha. Wapresbiteri walikuwa wameamua kuwa dhidi ya Wabaptisti na Wamethodisti, na walitumia uwezo wao wote wa hoja na ujanja ili kuwaonyesha makosa yao, au, angalau, kuwafanya watu wafikiri kwamba wao walikuwa katika makosa. Kwa upande mwingine, Wabaptisti na Wamethodisti walikuwa wamejidhatiti kujaribu kuyaeneza mafundisho yao wenyewe na kuwakanusha wengine wote.

10 Katikati ya vita hivi vya maneno na makelele ya maoni, daima nilijisemea mimi mwenyewe: Ni nini cha kufanya? Nani kati yao hawa wote aliye asahihi; au, je, wote si sahihi? Kama yeyote kati yao yu sahihi, ni yupi, na nitajuaje?

11 Wakati nikiwa nateseka kwa matatizo makali yaliyo sababishwa na makundi haya ya wanadini, siku moja nilikuwa nikisoma Waraka wa Yakobo, mlango wa kwanza, na mstari wa tano, ambao unasomeka: Kama mtu yeyote kati yenu akipungukiwa na hekima, na aombe kwa Mungu, awapaye watu wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.

12 Kamwe kifungu chochote cha maandiko hakijawahi kumwingia mtu moyoni kwa nguvu nyingi kuliko hiki kilivyofanya kwangu wakati huu. Kilionekana kuniingia kwa nguvu nyingi katika kila hisia za moyo wangu. Nilikitafakari tena na tena, nikijua kwamba kama mtu yeyote alihitaji hekima kutoka kwa Mungu, nami nilihitaji. Ni kwa jinsi gani nifanye hilo, sikujua, na kama nisingeweza kupata hekima zaidi kuliko nilizokuwa nazo, nisingeliweza kujua jinsi ya kufanya; kwa kuwa walimu wa dini wa madhehebu haya tofauti awalikielewa kifungu hicho hicho cha maandiko kwa kutofautiana kiasi cha kuharibu kujiamini kote katika kutatua swali hilo kwa kutafuta jibu kutoka katika bBiblia.

13 Hatimaye nilifikia uamuzi kwamba ama nibaki katika giza na mchafuko, au vinginevyo lazima nifanye kama Yakobo anavyoelekeza, ambako ni, kuomba kwa Mungu. Hatimaye nilifika kwenye azimio la a“kuomba kwa Mungu,” nikihitimisha kwamba kama yeye alitoa hekima kwa wao waliopungukiwa na hekima, na angelitoa kwa ukarimu, na wala hakemei, nami nitajaribu.

14 Hivyo, kufuatana na dhamira yangu ya kuomba dua kwa Mungu, nilienda msituni kufanya jaribio. Ilikuwa asubuhi nzuri, ya siku angavu, mapema katika majira ya kuchipua ya mwaka elfu moja mia nane na ishirini. Ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yangu kufanya jaribio la jinsi hii, kwani licha ya wasi wasi wangu wote kamwe sikuwahi kufanya jaribio la akuomba kwa sauti.

15 Baada ya kufika mahali ambapo awali nilichagua kwenda, baada ya kuangalia kila upande, na kujikuta niko peke yangu, nilipiga magoti na kuanza kutoa matakwa ya moyo wangu kwa Mungu. Nikiwa ninaanza tu kufanya hivyo, mara nikashikwa na nguvu fulani ambazo zilinishinda nguvu kabisa, na ambazo zilikuwa na uwezo wa ajabu juu yangu kiasi cha kufunga ulimi wangu kiasi cha kushindwa kusema chochote. Giza nene lilijikusanya kunizunguka, na ilionekana kwangu kwa muda kama kwamba nilikuwa niangamizwe kwa angamizo la ghafla.

16 Lakini, nilitumia nguvu zangu zote akumlingana Mungu ili anikomboe na nguvu za adui huyu ambaye alikuwa amenishikilia, na muda huo huo ambao nilikuwa tayari kuzama katika kukata tamaa na kujiachilia ili niangamizwe—siyo kwa maangamizo ya kufikirika, bali kwa nguvu halisi za kiumbe kutoka ulimwengu usioonekana, ambaye alikuwa na nguvu hizi za kushangaza ambazo kamwe sijapata kuzisikia kabla katika kiumbe chochote—katika wakati huu wa hofu kubwa, niliona nguzo ya bmwanga juu ya kichwa changu, ambao ulikuwa ni mngʼaro uliozidi mwangaza wa cjua, ambao ulishuka taratibu hadi ukashuka juu yangu.

17 Mara ulipoonekana nilijiona kuwa nimekombolewa kutokana na adui huyu aliyenifunga. Mwanga ulipotua juu yangu anikawaona Viumbe bwawili, ambao mngʼaro na cutukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni dMwanangu eMpendwa. Msikilize Yeye!

18 Kusudi langu la kwenda akumwomba Bwana lilikuwa ni kutaka kujua ni lipi kati ya madhehebu yale yote lilikuwa sahihi, ili nipate kujua lipi nijiunge nalo. Mara niliporejewa na fahamu zangu, niliwauliza Viumbe wale waliosimama juu yangu katika mwanga, ni lipi kati ya madhehebu yale lililo sahihi (kwani kwa wakati huu kamwe ilikuwa haijaingia moyoni mwangu kwamba yote yalikuwa si sahihi)—na ni lipi nijiunge nalo.

19 Nilijibiwa kwamba nisijiunge na lolote kati yao, kwani yote yalikuwa asi sahihi; na Mtu aliyenieleza alisema kwamba kanuni za imani zao zote zilikuwa ni machukizo mbele zake; kwamba wale watangaza imani wote walikuwa wameharibika; kwamba: “Wao bhusogea karibu nami kwa midomo yao, ila cmioyo yao iko mbali nami, wao hufundisha mafundisho yaliyo dmaagizo ya wanadamu, yenye eaina ya uchamungu ndani yake, lakini wakikana nguvu zake.”

20 Tena akanikataza nisijiunge na lolote kati yao; na mambo mengine mengi akaniambia, ambayo siwezi kuyaandika kwa wakati huu. Niliporejea katika fahamu zangu tena, nikajikuta nimelala chali, nikiangalia juu mbinguni. Mwanga ule ulipokuwa umeondoka, nilikuwa sina nguvu; lakini mara nilipojisikia nafuu kwa kiwango fulani; nikaenda nyumbani. Na nilipokuwa nimeegama kwenye sehemu ya kuotea moto, mama aliniuliza kama nilikuwa na tatizo gani. Nilimjibu, “Usijali, sina tatizo lolote—mimi sijambo.” Halafu nikamwambia mama yangu, “Nimejua mimi mwenyewe kwamba dini ya Presbiteri siyo ya kweli.” Ilionekana kana kwamba aadui alilijua hilo, katika kipindi cha awali kabisa cha maisha yangu, nilikusudiwa kuthibitisha kwamba nilikuwa mchafuzi na msumbufu wa ufalme wake; kama sivyo, basi kwa nini nguvu za giza ziungane dhidi yangu? Kwa nini bupinzani na mateso yainuke dhidi yangu, takribani katika uchanga wangu?

Baadhi ya wahubiri na watangaza imani za dini wanakataa taarifa za Ono la Kwanza—Mateso yanaludikwa juu ya Joseph Smith—Yeye anashuhudia juu ya ukweli wa ono hilo. (Mstari ya 21–26.)

21 Siku chache baada ya kupata aono hili, nilitokea kuwa pamoja na mmoja wa wahubiri wa Kimethodisti, ambaye alikuwa akijishughulisha sana katika msisimko huo wa dini uliotajwa hapo awali; na, katika kuongea naye juu ya jambo la dini, nilichukua nafasi hiyo kumsimulia historia ya ono hilo nililokuwa nalo. Nilishangazwa sana na tabia yake; siyo tu hakuipa uzito taarifa yangu, bali kwa dharau kubwa, alisema hii yote ilikuwa ni ibilisi, kwamba hakuna kitu cha jinsi hiyo kama bmaono au cmafunuo katika siku hizi; kwamba mambo ya jinsi hiyo yamekoma pamoja na mitume, na kwamba kamwe hayatakuwepo tena.

22 Mara niligundua, hata hivyo, kwamba kuzungumza kwangu juu ya hadithi hii kumeamsha mateso makubwa dhidi yangu kutoka kwa miongoni mwa watangaza imani za dini, na ilikuwa chanzo cha amateso makubwa, ambayo yaliendelea kuongezeka; na ingawa nilikuwa mvulana bnisiyefahamika, nikiwa na umri kati ya miaka kumi na minne na kumi na mitano tu, na ingawa hali yangu ya maisha ilikuwa ya kunifanya kuwa mvulana asiye na umuhimu katika ulimwengu, lakini watu wenye nafasi za juu wangelitaka taarifa ya kutosha ili kuchochea mawazo ya jamii dhidi yangu, na kutengeneza mateso makali; na hii ilikuwa jambo la kawaida miongoni mwa madhehebu yote—yote yaliungana ili kunitesa mimi.

23 Ilinisababishia tafakuri nzito hatimaye, na baada ya hapo mara kwa mara iliniletea shutuma hizo, ni ya kushangaza jinsi gani mvulana asiyefahamika, na wa umri unaozidi kidogo tu miaka kumi na minne, na pia ni mtu ambaye alilazimika kupata mahitaji yake madogo ya kujikimu kwa kazi za mikono yake kila siku, afikiriwe na madhehebu makubwa na maarufu kuwa mtu aliye maarufu vya kutosha kuwavutia wakubwa wa madhehebu maarufu ya siku hizo, na kwa kiasi cha kujenga ndani yao mateso na shutuma kali. Lakini kama ilikuwa ya ajabu au hapana, hivyo ndivyo ilivyokuwa, nayo daima ilikuwa ndicho chanzo cha huzuni kubwa kwangu.

24 Kwa hali yoyote ile, ilikuwa hata hivyo ni kwa sababu ya kwamba niliona ono. Nilijiona tangu hapo, kwamba nilijisikia kama aPaulo, alipokuwa bakijitetea mbele ya Mfalme Agripa, na akaelezea historia ya ono alilolipata alipoona mwanga, na kusikia sauti; lakini bado palikuwepo na wachache tu waliomwamini; wengine walisema yeye ni mdanganyifu, wengine wakasema alikuwa mwendawazimu; naye akabezwa na kutukanwa. Lakini hii yote haikuharibu ukweli wa ono lake. Aliliona ono, alijua kuwa aliona, na mateso yote yaliyoko chini ya mbingu hayakuweza kufanya vinginevyo; na ingawa wao wangemtesa hadi kifo, lakini yeye alijua, na angejua hadi mwisho wa mauti yake, kwamba ameona mwanga na kusikia sauti ikimwambia yeye, na ulimwengu wote haungeweza kumfanya yeye afikiri au aamini vinginevyo.

25 Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Hakika nilikuwa nimeuona mwanga, na katikati ya mwangaza huo niliwaona aWatu wawili, nao kwa hakika waliongea nami; na ingawa nilichukiwa na kuteswa kwa kusema kwamba nimeona ono, lakini ilikuwa ni kweli; na wakati wakiwa wananitesa, kunitukana, na kuninenea aina zote za uovu dhidi yangu kwa ajili ya kusema hivyo, niliongozwa kusema moyoni mwangu: Kwa nini wanitese kwa ajili ya kusema ukweli? Hakika nimeona ono; na je, mimi ni nani hata niweze kupingana na Mungu, au kwa nini ulimwengu wafikiria kunifanya mimi nikane kile ambacho hakika nimekiona? Kwani nimeona ono; nami najua hivyo, nami nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza bkukataa, wala kuthubutu kufanya hivyo; angalau nilijua kwamba kwa kufanya hivyo ningelimkosea Mungu, na kuwa chini ya hukumu.

26 Sasa nilikuwa nimeridhika akilini mwangu juu ya ulimwengu wa madhehebu—kwamba halikuwa jukumu langu kujiunga na lolote kati yao, bali kubaki kama nilivyokuwa hadi nitakapoelekezwa zaidi. Nimejua aushuhuda wa Yakobo kuwa ni wa kweli—kwamba mtu akipungukiwa hekima aweze kuomba kwa Mungu, naye atapata, na wala hakemei.

Moroni anamtokea Joseph Smith—Jina la Joseph litajulikana kwa mema na maovu miongoni mwa mataifa yote—Moroni anamweleza juu ya Kitabu cha Mormoni na juu ya kuja kwa hukumu za Bwana na ananukuu mistari ya maandiko mengi—Mahali yalipofichwa mabamba ya dhahabu panafunuliwa—Moroni anaendelea kumwelekeza Nabii. (Mstari ya 27–54.)

27 Niliendelea kufanya kazi zangu za kawaida katika maisha hadi tarehe ishirini na moja ya Septemba, elfu moja mia nane na ishirini na tatu, wakati wote huu nikiteseka kwa mateso makali katika mikono ya makundi yote ya watu, wanadini na wasio wanadini, kwa sababu niliendelea kusisitiza kuwa nilikuwa nimeona ono.

28 Katika kipindi cha kati ya wakati nilipoona ono na mwaka wa elfu moja mia nane na ishirini na tatu—nikiwa nimekatazwa kujiunga na dhehebu lolote la dini la wakati huo, na nikiwa bado katika umri mdogo, na nikiwa nimeteswa na wale waliopaswa kuwa marafiki zangu na ambao wangepaswa kunitendea wema, na ambao kama wao walidhania kuwa nimedanganywa ili wajaribu katika namna sahihi na ya upendo ili kunirudisha—niliachwa katika aina zote za amajaribu; na, kuchanganyika na aina zote za jamii, mara kwa mara niliangukia katika makosa mengi ya kipumbavu, na kuonyesha udhaifu wa ujana, na kasoro za kiasili za mwanadamu; ambazo, nasikitika kusema, ziliniongoza katika majaribu mbalimbali, yaliyokuwa na hatia machoni pa Mungu. Katika kukiri haya, mtu yeyote asidhanie ya kuwa nilikuwa na hatia yoyote kubwa. Tabia ya kufanya dhambi za jinsi hiyo kamwe haikuwa kawaida yangu. Lakini nilikuwa na hatia ya utovu wa staha, na wakati mwingine nilijishirikisha na makundi, yasiyopendeza tabia ambayo haikukubaliana na tabia ambayo inapaswa kufanywa na mtu ambaye bameitwa na Mungu kama mimi nilivyokuwa. Lakini hii haitaonekana kuwa ngeni sana kwa mtu yeyote ambaye ana kumbukumbu ya ujana wangu, na mwenye kuifahamu vyema tabia yangu ya furaha ya asili.

29 Kama matokeo ya mambo haya, daima nilijisikia kuwa mwenye hatia kutokana na udhaifu na kutokuwa kwangu mkamilifu; na kisha, jioni ya siku iliyotajwa hapo juu yaani tarehe ishirini na moja ya Septemba, baada ya kupanda kitandani usiku huo, nilifanya asala na maombi kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya msamaha wa dhambi na upuuzi wangu wote, na pia kwa ajili ya kupata mafunuo, ili nipate kujua juu ya hali na msimamo wangu mbele zake; kwa kuwa nilikuwa nikiamini kabisa katika kupata mafunuo matakatifu, kama nilivyopata hapo awali.

30 Wakati nikiwa katika kumlingana Mungu, niligundua mwangaza ukitokeza chumbani mwangu, mwangaza ambao uliendelea kuongezeka hadi chumba chote kikawa na mwanga mkali zaidi kuliko jua la saa sita mchana, na hatimaye mara amtu alionekana kuwa amesimama kando ya kitanda changu, amesimama hewani, kwani miguu yake haikugusa sakafu.

31 Alikuwa amevaa joho kubwa ajeupe zuri sana. Weupe wake ulikuwa weupe upitao kitu chochote cha kidunia nilichopata kukiona; wala siamini kwamba kitu chochote cha kidunia chaweza kufanywa kionekane cheupe na kiangavu kama hilo. Viganja vyake vilikuwa wazi, na mikono yake pia, juu kidogo ya kifundo; hivyo, pia, nyayo zake zilikuwa wazi, kama ilivyokuwa miguu yake, hadi juu kidogo ya vifundo. Kichwa chake na shingo pia vilikuwa wazi. Niliweza kugundua kuwa hakuwa na nguo nyingine aliyoivaa ila joho hili, kwa sababu lilikuwa wazi, kwani niliweza kuyaona maungo yake.

32 Siyo tu joho lake lilikuwa jeupe zaidi, lakini hata kiwiliwili chake kilikuwa na autukufu usioelezeka, na uso wake hakika ulingʼara kama bradi. Chumba kikajawa na mwangaza, lakini siyo sana kama ilivyokuwa kuzunguka pale alipokuwa yeye. Mara ya kwanza nilipomwangalia, cniliogopa; lakini mara woga ukanitoka.

33 Aliniita kwa ajina, na kuniambia kwamba alikuwa mjumbe aliyetumwa kwangu kutoka uwepo wa Mungu, na kwamba jina lake lilikuwa Moroni; kwamba Mungu alikuwa na kazi ambayo mimi ningefanya; na kwamba jina langu litafikiriwa kwa mema na maovu miongoni mwa mataifa yote, makabila, na lugha, au lingetajwa kwa wema na kwa uovu miongoni mwa watu wote.

34 Alisema kulikuwepo na akitabu kilichohifadhiwa, kilichoandikwa kwenye bmabamba ya dhahabu, chenye kutoa historia ya wakazi wa zamani wa bara hili, na asili yao walikotokea. Yeye pia alisema kwamba cutimilifu wa Injili isiyo na mwisho ulikuwepo ndani yake, kama ilivyoletwa na Mwokozi kwa wakazi hao wa kale;

35 Pia, kwamba yalikuwepo mawe mawili katika pinde za fedha—na mawe haya, yalifungwa kwenye adera ya kifua, yalifanya kitu kinachoitwa bUrimu na Thumimu—yamehifadhiwa pamoja na mabamba; na umiliki na utumiaji wa mawe haya ndiyo yalifanya watu waitwe c“waonaji” katika nyakati za kale au zilizopita; na kwamba Mungu alikuwa ameyatengeneza kwa ajili ya madhumuni ya kutafsiri kitabu.

36 Baada ya kuniambia mambo haya, alianza kunukuu unabii wa aAgano la Kale. Kwanza alinukuu sehemu ya bmlango wa tatu wa Malaki; na pia alinukuu wa nne au mlango wa mwisho ya unabii huo huo, ingawa kwa kutofautiana kidogo na jinsi isomekavyo katika Biblia zetu. Badala ya kunukuu mstari wa kwanza kama unavyosomeka katika vitabu vyetu, alinukuu hivi:

37 Kwa maana tazama, asiku ile inakuja ambayo bitawaka kama tanuru, na wote wenye kiburi, ndiyo, na wote watendao uovu wataungua kama cmakapi; kwani wao wanaokuja watawaunguza, asema Bwana wa Majeshi, kwamba haitawaachia mzizi wala tawi.

38 Na tena, alinukuu mstari wa tano hivi: Tazama, nitakufunulieni aUkuhani, kwa mkono wa bEliya nabii, kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya kuogofya ya Bwana.

39 Na pia alinukuu mstari unaofuata tofauti: Naye atapanda katika mioyo ya watoto aahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto bitawageukia baba zao. Kama haingekuwa hivyo, dunia yote ingeliharibiwa kabisa wakati wa kuja kwake.

40 Kwa nyongeza ya haya, alinukuu mlango wa kumi na moja wa Isaya, akisema kwamba ilikuwa inakaribia kutimia. Alinukuu pia mlango wa tatu wa Matendo, mistari ya ishirini na mbili na ishirini na tatu, sawa sawa kama ilivyo katika Agano Jipya letu. Alisema kwamba yule anabii alikuwa Kristo; bali ile siku bado haijafika wakati “wao ambao hawangeisikia sauti yake bwatatengwa mbali na watu,” lakini karibu itakuja.

41 Naye pia alinukuu amlango wa pili wa Yoeli, kutoka mstari wa ishirini na nane hadi wa mwisho. Pia akasema kwamba hili bado halijatimia, lakini karibu litatimia. Na zaidi akaelezea kwamba utimilifu wa bWayunani ulikuwa karibu kuingia. Alinukuu vipengele vingine vingi vya maandiko, na kutoa maelezo mengi ambayo hayawezi kutajwa hapa.

42 Tena, akanieleza, kwamba nitakapoyapata mabamba hayo ambayo ameyasema—kwa maana wakati ambao yanapaswa kupatikana ulikuwa bado haujatimia—nisiyaonyeshe kwa mtu yeyote; wala dera ya kifua pamoja na Urimu na Thumimu; isipokuwa kwa wale tu ambao nitaamriwa niwaonyeshe; kama nitayaonyesha nitaangamizwa. Wakati alipokuwa akizungumza nami juu ya mabamba, ono lilifunguliwa aakilini mwangu kwamba nikaweza kuona mahali ambapo mabamba yale yalihifadhiwa, na kwamba kila kitu nilikiona vizuri na kwa uwazi zaidi kiasi kwamba nilipajua mahali pale tena wakati nilipopatembelea.

43 Baada ya mazungumzo haya, nikaona mwanga katika chumba ukianza mara moja kumzingira mtu ambaye alikuwa akizungumza nami, na ukaendelea kufanya hivyo, hadi chumba kikawa tena na giza, isipokuwa tu mahali alipokuwa amesimama, mara, nikaona, ni kama njia imefunguka hadi mbinguni, na yeye akapanda nayo hadi akatoweka kabisa, na chumba kikaachwa kama vile kilivyokuwa kabla ya mwanga huu wa mbinguni haujatokea.

44 Nililala huku nikiwaza juu ya upekee wa hilo jambo, na nikishangazwa sana na yale niliyokuwa nimeambiwa na huyu mjumbe asiye wa kawaida; na halafu, katikati ya atafakuri yangu, nikagundua kwa ghafla kwamba chumba changu kilianza tena kuangazwa, na ikawa kwamba mara moja, kama ilivyokuwa, mjumbe yule yule wa mbinguni alikuwa tena kando ya kitanda changu.

45 Akaanza, kuniambia tena vitu vile vile kama alivyofanya hapo awali, bila tofauti yoyote; baada ya kufanya hivyo, akanijulisha kuhusu hukumu kali ambazo zilikuwa zinakuja ulimwenguni, pamoja na ukiwa mkubwa utakaoletwa na njaa, upanga, na tauni; na kwamba hizi hukumu kali zitakuja ulimwenguni katika kizazi hiki. Baada ya kusimulia vitu hivi, akapanda juu tena kama alivyokuwa amefanya hapo awali.

46 Kwa wakati huu, mawazo mazito yalikuwa yamejengwa akilini mwangu, kiasi kwamba usingizi ulitoroka machoni mwangu, nami nililala nikiwa nimezidiwa na mshangao kwa yale niliyokwisha kuyaona na kusikia. Lakini mshangao wangu ulikuwa ni wakati nilipomwona tena mjumbe yule yule kando ya kitanda changu, na nikamsikia akirejea au kurudia tena kwangu mambo yale yale kama hapo awali; na kuongeza tahadhari kwangu, akinieleza kwamba aShetani angejaribu bkunishawishi (kutokana na hali ya ufukara wa familia ya baba yangu), ili kupata mabamba haya kwa madhumuni ya kupata utajiri. Hili alinikataza, akisema kwamba ni lazima nisiwe na lengo jingine lolote katika nia ya kupata mabamba haya isipokuwa kwa ajili ya kumtukuza Mungu, na nisichochewe na cnia nyingine yoyote zaidi ya ile ya kuujenga ufalme wake; vinginevyo nisingeliweza kuyapata.

47 Baada ya kuja mara hii ya tatu, akapaa tena mbinguni kama hapo mwanzo, na mimi tena nikaachwa nikitafakari juu ya ugeni wa yale ambayo nilikuwa nimeyashuhudia; ambapo punde tu baada ya mjumbe yule wa mbinguni kupaa mara ya tatu, jogoo akawika, na nikafahamu kwamba siku mpya ilikuwa inapambazuka, hivyo basi mahojiano yetu lazima yalikuwa yamechukua huo usiku wote.

48 Muda mfupi baadaye niliamka kutoka kitandani pangu, na, kama kawaida, nilienda kufanya kazi muhimu za siku hiyo; lakini, katika kujaribu kufanya kazi kama nyakati zingine, nilijiona kuwa nguvu zangu zimeniishia hata kunifanya nisijiweze kabisa. Baba yangu, ambaye alikuwa akifanya kazi pamoja nami, aligundua kwamba nilikuwa na matatizo, na akaniambia niende nyumbani. Nilianza kwa dhamira ya kwenda nyumbani; lakini, katika kujaribu kuvuka ukingo wa shamba ambamo tulikuwepo, nguvu zangu ziliniishia kabisa, nami nilianguka chini kabisa, na kwa muda nilikuwa sijiwezi kabisa kwa chochote.

49 Kitu cha kwanza ambacho ninaweza kukikumbuka kilikuwa ni sauti ikinisemesha, ikiniita kwa jina. Niliangalia juu, na nikamwona mjumbe yule yule akiwa amesimama juu ya kichwa changu, akiwa amezungukwa na mwanga kama vile awali. Kisha akayarudia tena yale yote aliyonieleza usiku uliopita, na akaniamuru niende kwa ababa yangu na kumwambia juu ya lile ono na amri nilizozipokea.

50 Nilitii; nikarudi kwa baba yangu shambani, na kumweleza jambo lile lote. Yeye alinijibu kwamba lilikuwa la Mungu, na akaniambia niende na kufanya kama nilivyoamriwa na yule mjumbe. Niliondoka shambani, na kwenda mahali ambapo yule mjumbe alinieleza kwamba mabamba yamehifadhiwa; na kwa sababu ya uwazi wa lile ono ambalo nililipata juu yake, nilipajua mahali pale mara baada ya kufika hapo.

51 Karibu na kijiji cha Manchester, wilaya ya Ontario, New York, kimesimama akilima cha ukubwa wa wastani, na ndicho kilima kirefu kuliko chochote katika maeneo ya jirani. Upande wa magharibi ya kilima hiki, siyo mbali kutoka kileleni, chini ya jiwe la ukubwa wa wastani, yalilala mabamba, yakiwa yamehifadhiwa ndani ya kisanduku cha jiwe. Jiwe hili lilikuwa nene na la mviringo katikati juu ya upande wa juu, na jembamba zaidi kuelekea kwenye kingo, hivyo sehemu yake ya katikati ilikuwa ikionekana juu ya udongo, lakini kingo zake zote kuzunguka zilifunikwa kwa udongo.

52 Baada ya kuondoa udongo, nilipata wenzo, ambayo niliitia chini ya kingo za lile jiwe, na kwa kutumia nguvu kidogo nililiinua. Niliangalia ndani, na humo hakika niliona amabamba hayo, bUrimu na Thumimu, na cdera ya kifuani, kama ilivyoelezwa na yule mjumbe. Lile sanduku ambalo ndani yake yaliwekwa lilitengenezwa kwa kuyapanga mawe pamoja kwa aina fulani ya saruji. Ndani, chini ya sanduku yaliwekwa mawe mawili yakikingama na sanduku, na juu ya mawe haya yaliwekwa mabamba hayo na vitu vingine pamoja nayo.

53 Nilifanya jaribio la kuvitoa nje, lakini nilikatazwa na yule mjumbe, na tena niliarifiwa kuwa wakati wa kuvichukua ulikuwa bado haujafika, wala haungefika, hadi miaka minne kutoka wakati huo; lakini alinieleza kwamba yanipasa kuja mahali pale baada ya mwaka mmoja barabara kutoka wakati ule, na kwamba atakutana nami pale, na kwamba itanipasa kuendelea kufanya hivyo hadi wakati utakapofika wa kuyapata mabamba yale.

54 Hivyo, kulingana na nilivyokuwa nimeamriwa, nilikwenda kila ilipofika mwisho wa mwaka, na kila wakati nilimkuta mjumbe yule pale, na nikapokea maelekezo na maarifa kutoka kwake katika kila mahojiano yetu, juu ya yale Bwana atakayoyafanya, na namna gani na kwa jinsi gani aufalme wake utaendeshwa katika siku za mwisho.

Joseph Smith amwoa Emma Hale—Anapokea mabamba ya dhahabu kutoka kwa Moroni na anatafsiri baadhi ya maandishi—Martin Harris anayaonyesha maandishi na tafsiri kwa Profesa Anthon, ambaye anasema, “Siwezi kusoma kitabu kilichofungwa.” (Mstari ya 55–65.)

55 Kwa kuwa hali ya kiuchumi ya baba yangu ilikuwa duni sana, tulilazimika kufanya kazi kwa mikono yetu, tukikodiwa na watu wengine kwa kibarua cha siku moja moja, kulingana na kazi kadiri itakavyopatikana. Wakati mwingine tulikuwepo nyumbani, na wakati mwingine nje ya nyumbani, na kwa kuendelea kufanya kazi mara kwa mara kulituwezesha kupata mahitaji ya kutosha.

56 Katika mwaka wa 1823 familia ya baba yangu ilipatwa na huzuni kubwa kwa kifo cha kaka yangu mkubwa, aAlvin. Katika mwezi wa Oktoba, 1825, niliajiriwa na mzee mmoja muungwana kwa jina la Josiah Stoal, ambaye alikuwa akiishi wilaya ya Chenango, Jimbo la New York. Yeye alikuwa amesikia juu ya kufunguliwa kwa machimbo ya fedha na Wahispania huko Harmony, wilaya ya Susquehanna, Jimbo la Pennsylvania; na alikuwa, kabla ya kuajiriwa kwangu, akichimba, ili, kama ikiwezekana, kuyagundua madini hayo. Baada ya kwenda kuishi naye, alinichukua mimi, pamoja na wafanyakazi wake waliobakia, kwenda kuchimba madini hayo ya fedha, ambapo niliendelea kufanya kazi kwa karibu mwezi mzima, pasipo mafanikio ya kazi yetu, na hatimaye nilifanikiwa kumshawishi mzee yule kuacha kuchimba kutafuta madini hayo. Kuanzia hapo ndipo chimbuko la hadithi ya mimi kuwa mchimba fedha.

57 Katika wakati huo nilipokuwa nimeajiriwa kwa kazi hiyo, nilikuwa nimewekwa kuishi pamoja na Bwana Isaac Hale, mwenyeji wa mahali pale; ilikuwa hapo ndipo nilipomwona mke wangu (binti yake) kwa mara ya kwanza, aEmma Hale. Mnamo tarehe 18 ya Januari, 1827, tulioana, wakati nikiwa bado nimeajiriwa katika utumishi wa Bwana Stoal.

58 Kwa sababu ya kuendelea kwangu kudai kuwa nimeona ono, amateso yaliendelea kunifuata, na familia ya baba wa mke wangu walikuwa wamepinga sana sisi kuoana. Kwa sababu hiyo, nilikuwa ninalazimika kumchukua na kwenda naye sehemu nyingine yoyote; hivyo tulienda na huko tukaozwa katika nyumba ya Squire Tarbill, huko South Bainbridge, wilaya ya Chenango, New York. Mara baada ya ndoa yangu, niliacha ajira ya Bwana Stoal, na kwenda nyumbani kwa baba yangu kulima pamoja naye msimu ule.

59 Hatimaye wakati ulifika wa kuyachukua mabamba, Urimu na Thumimu, na dera ya kifuani. Tarehe ishirini na mbili ya Septemba, elfu moja mia nane na ishirini na saba, ikiwa nimeenda kama kawaida mwishoni mwa mwaka mwingine mahali vilipokuwa vimehifadhiwa, mjumbe yule yule wa mbinguni alinipa pamoja na amri hii: kwamba nitawajibika juu yake; kwamba kama nitayaacha yaende kwa akukosa uangalifu, au kwa uzembe wangu, nitakatiliwa mbali; lakini kama nitatumia uwezo wangu wote bkuyalinda, hadi yeye, yule mjumbe, atakapoyataka, yatalindwa.

60 Muda si mrefu nilitambua sababu ya mimi kupokea amri ile kali ya kuyatunza kwa usalama, na kwa nini ilikuwa mjumbe aseme hivyo kwamba nitakapokuwa nimefanya yale yaliyotakiwa kutoka kwangu, atayataka. Kwani haikuwa muda mrefu ilijulikana kwamba nilikuwa nayo, juhudi ya nguvu nyingi zaidi ilitumika ili kuyapata kutoka kwangu mimi. Kila hila ambayo iliweza kubuniwa ilitumiwa kwa dhumuni hili. Mateso yakawa machungu zaidi na makali kuliko mwanzoni, na umati ulikuwa uko tayari daima kuyachukua kutoka kwangu kama ikiwezekana. Lakini kwa hekima ya Mungu, yalibaki salama mikononi mwangu, hadi nilipoyamalizia kazi ile iliyotakiwa kutoka kwangu. Hatimaye, kulingana na mipangilio, mjumbe yule akayataka, nikampa; naye anayo katika himaya zake hadi siku hii, ikiwa siku ya pili ya Mei, elfu moja mia nane na thelathini na nane.

61 Msisimko, hata hivyo, bado uliendelea, na minongʼono pamoja na ndimi zake elfu wakati wote ilikuwa ikitumiwa katika kueneza uongo juu ya familia ya baba yangu, na juu yangu mimi mwenyewe. Kama ningetaka kuzihadithia sehemu moja ya elfu yake, ingelijaza vitabu vingi. Mateso, hata hivyo, yakawa hayavumiliki hata nikalazimika kuhama Manchester, na kwenda na mke wangu katika wilaya ya Susquehanna, katika Jimbo la Pennsylvania. Wakati nikiwa najitayarisha kwanza—nikiwa fukara sana, na mateso ni mazito sana juu yetu kiasi kwamba hapakuwa na uwezekano kwamba tungeliweza kuondoka lakini—katikati ya mateso yetu tulimpata rafiki muungwana kwa jina la aMartin Harris, aliyekuja kwetu na kunipa dola hamsini ili kutusaidia sisi katika safari yetu. Bwana Harris alikuwa ni mkazi wa mji wa Palmyra, wilaya ya Wayne, katika Jimbo la New York, na mkulima mwenye kuheshimika.

62 Kwa msaada huu uliokuja wakati uliohitajika uliniwezesha kufika mahali nilikokusudia kufika katika Pennsylvania; na mara baada ya kuwasili huko nilianza kunakili maandishi yale kutoka katika yale mabamba. Nilinakili kiasi cha kutosha, na kwa njia ya aUrimu na Thumimu nilitafsiri baadhi yake, kitu ambacho nilikifanya kati ya kipindi nilichofika nyumbani kwa baba wa mke wangu, katika mwezi wa Desemba, na Februari iliyofuata.

63 Wakati fulani katika mwezi huu wa Februari, Bwana Martin Harris ambaye nimemtaja hapo mwanzoni alikuja kwetu, akapata michoro ambayo nimeichora kutoka kwenye mabamba yale, na kwenda nayo mjini New York. Kwa vile lililotokea juu yake na michoro ile, nitayanukuu katika historia ya matukio yake, kama alivyonieleza baada ya kurudi kwake, ambayo yalikuwa kama ifuatavyo:

64 “Nilikwenda mjini New York, na nikaipeleka michoro ile iliyokwisha tafsiriwa, pamoja na tafsiri yake, kwa Profesa Charles Anthon, mtu maarufu kwa kiwango chake cha elimu. Profesa Anthon alieleza kwamba tafsiri ilikuwa sahihi, zaidi kuliko yoyote aliyopata kuiona iliyotafsiriwa kutoka lugha ya Kimisri. Kisha nikamwonyesha yale ambayo yalikuwa bado hayaja tafsiriwa, naye akasema kwamba yalikuwa katika lugha ya Kimisri, Kikaldayo, Kisiria, na Kiarabu; na akasema ile ilikuwa ni michoro ya kweli. Alinipa hati, akiwahakikishia watu wa Palmyra kuwa ilikuwa michoro ya kweli, na kwamba tafsiri yake kama ilivyotafsiriwa pia ilikuwa sahihi. Nilichukua ile hati ya uthibitisho na kuiweka mfukoni, na kuanza kuondoka, Bwana Anthon akanirudisha, na akaniuliza ni namna gani huyo kijana alijua kwamba palikuwa na mabamba hayo ya dhahabu mahali hapo alipoyakuta. Nilimjibu kwamba malaika wa Mungu alimfunulia.

65 “Kisha yeye akaniambia, ‘Acha nione hiyo hati.’ Hivyo nikaitoa mfukoni mwangu na kumpa, aliichukua na kuichana katika vipande, akisema kwamba hakuna kitu kama hicho siku hizi kama kuhudumiwa na amalaika, na kwamba kama nitamletea mabamba hayo angeliweza kuyatafsiri. Nikamwarifu kwamba sehemu ya mabamba hayo yalikuwa byamefungwa, na kwamba nilikatazwa kuyaleta. Yeye alijibu, ‘Siwezi kusoma kitabu kilichofungwa.’ Nilimwacha na kwenda kwa Dk. Mitchell, ambaye aliunga mkono yaliyosemwa na Profesa Anthon kuhusu michoro na tafsiri.”

· · · · · · ·

Oliver Cowdery anatumika kama mwandishi katika kutafsiri Kitabu cha Mormoni—Joseph na Oliver wanapokea Ukuhani wa Haruni kutoka kwa Yohana Mbatizaji—Wanabatizwa, kutawazwa, na kupokea roho ya unabii. (Mstari ya 66–75.)

66 Katika siku ya 5 ya mwezi Aprili mwaka wa 1829, aOliver Cowdery alikuja nyumbani kwangu, kabla ya wakati huu nilikuwa sijapata kumuona. Aliniambia kwamba alikuwa akifundisha shule ya jirani na mahali baba yangu alipokuwa akiishi, na baba yangu alikuwa mmoja wa wale wenye kuwapeleka watoto wao shuleni hapo, alikwenda kuishi nyumbani kwake kwa muda fulani, na akiwa hapo familia ilimweleza juu ya mimi kupokea mabamba, na hivyo yeye amekuja kuniulizia.

67 Siku mbili baada ya kuwasili kwa Bwana Cowdery (ikiwa ni tarehe 7 ya mwezi wa Aprili) nilianza kutafsiri Kitabu cha Mormoni, naye akaanza kuwa mwandishi wangu.

· · · · · · ·

68 Bado tuliendelea na kazi ya tafsiri, na halafu, katika mwezi uliofuata (Mei, 1829), siku fulani sisi tulienda msituni kusali na kumwomba Bwana juu ya aubatizo kwa ajili ya bondoleo la dhambi, tuliloliona limetajwa juu ya mabamba hayo. Wakati tukiwa hivyo, tukifanya maombi na kumlingana Bwana juu ya jambo hilo, cmjumbe kutoka mbinguni alishuka katika dwingu la mwanga, na akiwa ameweka emikono yake juu yetu, fakatutawaza, akisema:

69 Juu yenu ninyi watumishi wenzangu, katika jina la Masiya, ninawatunukia aUkuhani wa Haruni, ambao hushikilia funguo za huduma ya malaika, na za injili ya toba, na za ubatizo kwa uzamisho kwa ajili ya ondoleo la dhambi; na hizi kamwe hazitaondolewa kutoka duniani mpaka wana wa bLawi watakapotoa tena matoleo kwa Bwana katika haki.

70 Yeye alisema Ukuhani huu wa Haruni hauna uwezo wa kumwekea mtu mikono kwa ajili ya akipawa cha Roho Mtakatifu, lakini kwamba alisema utatunukiwa juu yetu hapo baadaye; na akatuamuru kwenda kubatizana, na akatupa maelekezo kwamba nimbatize Oliver Cowdery, na kwamba baadaye naye anibatize mimi.

71 Hivyo tukaenda na tukabatizana. Mimi nilimbatiza yeye kwanza, na baadaye yeye akanibatiza mimi—baada ya hapo nilimwekea mikono yangu juu ya kichwa chake na kumtawaza kwenye Ukuhani wa Haruni, na baadaye yeye akaniwekea mikono yake juu yangu na kunitawaza mimi kwenye Ukuhani huo huo—kwani hivyo ndivyo tulivyoamriwa.*

72 Mjumbe yule aliye tutembelea sisi katika tukio hili na kuweka Ukuhani huu juu yetu, alisema kwamba jina lake lilikuwa Yohana, yule yule aitwaye aYohana Mbatizaji katika Agano Jipya, na kwamba yeye alitenda hayo chini ya maelekezo ya bPetro, cYakobo na dYohana, ambao walishikilia efunguo za Ukuhani wa fMelkizedeki, Ukuhani ambao, yeye alisema, ungelitunukiwa juu yetu wakati ukifika, na kwamba mimi nitaitwa gMzee wa Kwanza wa Kanisa, na yeye (Oliver Cowdery) wa pili. Ilikuwa katika siku ya kumi na tano ya Mei, 1829, ambayo tulitawazwa chini ya mkono wa mjumbe huyu, na kubatizwa.

73 Mara katika kuinuka kutoka majini baada ya kubatizwa, tulihisi baraka kubwa na tukufu kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni. Muda mfupi baada ya kumbatiza Oliver Cowdery, aRoho Mtakatifu alishuka juu yake, naye akasimama na bkutoa unabii juu ya mambo mengi yatakayokuja kutokea baada ya muda mfupi. Na tena, mara mimi baada ya kuwa nimebatizwa naye, pia nilipata roho wa kutoa unabii, mara, nilisimama, nikatoa unabii juu ya kuinuka kwa Kanisa hili, na mambo mengine mengi yanayohusiana na Kanisa, na kizazi hiki cha wanadamu. Tulijawa na Roho Mtakatifu, na kufurahia katika Mungu wa wokovu wetu.

74 Akili yetu sasa ikiwa imeangazwa, tulianza kuona maandiko yamewekwa wazi katika afahamu zetu, na bmaana na dhamira ya kweli ya vipengele vigumu ilifunuliwa kwetu katika jinsi ambayo kamwe hatukuweza kuipata hapo awali, wala hapo awali hatukuifikiria. Kwa wakati huu tulilazimika kutunza siri ya tukio hili la kuwa tumepokea Ukuhani na kubatizwa kwetu, kwa sababu ya kuogopa roho wa mateso ambaye tayari alijionyesha mwenyewe katika maeneo ya jirani.

75 Tulikuwa tumetishiwa kuvamiwa na wahuni, mara kwa mara, na mara hii, pia, na watangaza imani za dini. Na dhamira zao za kutuvamia sisi ilizuiliwa tu na uwezo wa familia ya baba wa mke wangu (kwa majaliwa ya Mungu), ambao walikuja kuwa marafiki zangu sana, na ambao walipinga uhuni, na walikuwa radhi kwamba niruhusiwe kuendelea na kazi ya tafsiri bila kuingiliwa, na kwa hiyo wao walitupa ulinzi kutokana na matendo yasiyo ya kisheria, kwa kadiri walivyokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

  • Oliver Cowdery aelezea matukio haya kama ifuatavyo: “Hizi zilikuwa siku ambazo kamwe hazitasahaulika—kukaa chini ya sauti iliyotoa imla kwa mwongozo wa kutoka mbinguni, iliamsha hisia za shukrani ya juu kabisa ya moyo huu! Siku hadi siku niliendelea, bila kubughudhiwa, kuandika kutoka kinywani mwake, kama alivyokuwa akitafsiri kwa Urimu na Thumimu, au, kama Wanefi ambavyo wangelisema, ‘Vikalimani,’ historia au kumbukumbu iliyoitwa ‘Kitabu cha Mormoni.’

    “Kwa kutaja, katika hata maneno machache, historia ya kupendeza iliyotolewa na Mormoni na mwanawe mwaminifu, Moroni, ya watu ambao wakati fulani walipendwa na kupendelewa na mbingu, ingepita historia yangu ninayoitoa sasa; kwa hiyo nitaahirisha hilo hadi kipindi kijacho, na, kama nilivyosema katika utangulizi, nitapita moja kwa moja kwenye mambo machache ambayo yanahusiana kwa karibu sana na kuibuka kwa Kanisa hili, ambayo yatawafurahisha baadhi ya maelfu ambao wamejitokeza mbele, katikati ya nyuso zilizo kunjamana za watu wanaongʼangʼania mawazo au imani yao kupita kiasi na uzushi wa wanafiki, na wakaikumbatia Injili ya Kristo.

    “Hakuna watu, katika utimamu wa akili zao, ambao wangeliweza kutafsiri na kuandika maelekezo yaliyotolewa kwa Wanefi kutoka kinywa cha Mwokozi, juu ya jinsi sahihi ambayo kwayo watu watalijenga Kanisa Lake, na hususani wakati uharibifu umeenea au mashaka juu ya aina zote na mifumo itumikayo miongoni mwa watu, bila kutaka nafasi ya kuonyesha uradhi wa moyo kwa kuzikwa katika kaburi la maji, ili kujibu ‘dhamira safi ya ufufuko wa Yesu Kristo.’

    “Baada ya kuandika historia iliyotolewa juu ya huduma ya Mwokozi kwa baki la uzao wa Yakobo, juu ya bara hili, ilikuwa rahisi kuonekana, kama nabii alivyosema ingekuwa, kwamba giza litaifunika dunia na giza nene litazifunika akili za watu. Kwa kutazama kwa undani ilikuwa rahisi kuonekana kwamba katikati ya ugomvi na kelele juu ya dini, hakuna hata moja iliyekuwa na mamlaka kutoka kwa Mungu ya kuhudumu ibada za Injili. Kwani swali laweza kuulizwa, je, watu wanayo mamlaka ya kuhudumu katika jina la Kristo, watu wenye kukana mafunuo, wakati ushuhuda Wake ni zaidi ya roho wa unabii, na dini Yake inategemea, inajengwa, na kuendelezwa kwa mafunuo ya moja kwa moja, katika miaka yote ya ulimwengu wakati Yeye alipokuwa na watu duniani? Kama kweli hizi zilizikwa, na kwa uangalifu mkubwa zikafichwa na watu ambao ujanja wao ungelikuwa katika hatari ya kufichuliwa kama ungeliruhusiwa kuangaza usoni pa watu, kwetu haukuwa umezikwa; na sisi tulisubiri tu amri itolewe ‘Simama na ukabatizwe.’

    “Hii siyo tu tuliitamani kabla ya kupata. Bwana, aliye tajiri wa rehema, na daima aliye tayari kujibu sala thabiti ya wanyenyekevu, baada ya kumlingana Yeye kwa njia ya ari, mbali na makao ya watu, yeye alijishusha ili kutuonyesha sisi mapenzi Yake. Mara, kama vile kutoka katikati ya milele, sauti ya Mkombozi ikasema amani kwetu sisi, wakati pazia lilipofunguliwa na malaika wa Mungu akashuka chini amevikwa utukufu, na kutuletea ujumbe uliokuwa ukitazamiwa kwa shauku, na funguo za Injili ya toba. Ni shangwe gani! ni mshangao gani! ni mastaajabu gani! Wakati ulimwengu ukiwa unateswa na kuvurugwa—wakati mamilioni wakipapasa kama kipofu apapasavyo kwa ajili ya ukuta, na wakati watu wote walipokuwa wakitegemea utovu wa uhakika, kwa idadi kubwa ya watu, macho yetu yalitazama, masikio yetu yalisikia, kama katika ‘wakati wa jua kali’; ndiyo, zaidi—kupita kimulimuli cha mwali wa jua la kiangazi, ambalo halafu likamwaga uangavu wake juu ya uso wa asili. Kisha sauti yake, ingawa laini, ilipenya hadi katikati, na maneno yake, ‘Mimi ni mtumishi mwenzenu,’ yaliifukuza kila hofu. Tukasikiliza, tukaangaza, tukastaajabia! Ilikuwa sauti ya malaika kutoka kwenye utukufu, ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Aliye Juu Sana! Na tulivyosikia tulifurahia, wakati upendo Wake ukiwaka juu ya roho zetu, nasi tukafunikwa katika ono la Mwenyezi! Je, wapi palikuwa na nafasi ya shaka? Hakuna; mashaka yalitoweka, mashaka yalizama yasiibuke tena, wakati habari za kubuni na udanganyifu zimetoweka milele!

    “Lakini, ndugu yangu, fikiri, fikiri zaidi kwa muda, ni shangwe gani iliijaza mioyo yetu, na kwa mshangao gani tulipiga magoti, (kwani nani asingelipiga magoti kwa baraka ya jinsi hii?) tulipopokea chini ya mkono wake Ukuhani Mtakatifu kama alivyosema, ‘Juu yenu ninyi watumishi wenzangu, katika jina la Masiya, ninawatunukia Ukuhani huu na mamlaka hii, ambayo itabakia duniani, ili Wana wa Lawi wapate kutoa sadaka kwa Bwana katika haki!’

    “Sitajaribu kuwapaka ninyi hisia za moyo huu, wala kuwapaka uzuri wa ufahari na utukufu ambao ulituzunguka sisi katika tukio hili; lakini mtaniamini nitakaposema, kwamba dunia, wala watu, pamoja na ushawishi unaotokana na uzoefu wa muda mrefu, hauwezi kuanza kuvisha nguo lugha katika jinsi ya kupendeza na ya hali juu kama mtu huyu mtakatifu. Hapana; wala dunia hii haina uwezo wa kutoa shangwe, kuzawadia amani, au kutambua hekima ambayo ilikuwemo katika kila sentensi kama zilivyokuwa zikitolewa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu! Mwanadamu kumdanganya mwanadamu mwenzake, udanganyifu waweza kufuata udanganyifu, na watoto wa mwovu wanaweza kupata uwezo wa kumshawishi mpumbavu na asiyefundishwa, hadi akawa kazi bure lakini hadithi ya hubuni kuwalisha wengi, na matunda ya uongo humbeba katika mawimbi yake mtu asiye na msimamo hadi kaburini; lakini guso moja la kidole cha upendo wake, ndiyo, mwali mmoja wa utukufu kutoka ulimwengu wa juu, au neno moja kutoka kinywa cha Mwokozi, kutoka kifua cha milele, huyapiga yote na kuwa katika kutokuwa na maana, na kuyafuta milele akilini. Uhakikisho kwamba tulikuwa katika uwepo wa malaika, uhakika kwamba tuliisikia sauti ya Yesu, na ukweli usiopakwa matope kama ulivyotiririka kutoka kwa mtu msafi, uliosemwa kwa imla kwa mapenzi ya Mungu, kwangu mimi unanishinda kuelezea, na daima nitayatazamia maelezo haya ya wema wa Mwokozi kwa mshangao na shukrani wakati ninaporuhusiwa kuishi; na katika makao yale ambayo ukamilifu hukaa na dhambi kamwe haifiki, natumaini kumwabudu katika siku ile ambayo kamwe haitakoma.”—Messenger and Advocate, kitabu cha. 1 (Oktoba 1834) uk. 14–16.