2021
Upendo wa Kiungu
Januari 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Upendo wa Kiungu

“Tunayo fursa ya kupata uzoefu wa maisha ya duniani kwa sababu tuliidhinisha Mpango Wake. Kwa nini? Kwa sababu hata hapo awali, tulikuwa tayari tu mashahidi wa upendo Wake kwetu na matamanio yake ya kuinuliwa kwetu.”

Yeyote anayechukua muda kutafakari kwa kina kuhusu uhalisia wa uwepo wetu hapa duniani hufikia hitimisho kwamba maisha kama tunavyoyajua ni fumbo kubwa la zama zote. Fikiria kuhusu dunia inayoonekana yenye akili inayozunguka mchana na kisha usiku, na inayofanya kuwepo kwa misimu kadiri inavyozunguka anga wakati ikilalia upande mmoja na kisha mwingine bila kupinduka, kufunua kiasi kikubwa cha uso wake kadiri inavyoweza kwa ajili ya jua. Au vitu mbalimbali vya kustaajabisha vyenye aina ya kipekee ya maisha na watu wa kipekee wa kila aina ya maisha kwenye uso wa dunia ndani na juu ya aina kadhaa za udongo na kati ya miamba iliyosimama, na kuyumba kusikopungua kwa bahari zake kuu na maziwa yake. Zaidi, wakati mtu anapogeuza jicho lake kuelekea anga angavu la giza, ataona mandhari ya kushangaza ya nukta za mwanga zinazotangaza mabilioni ya mabilioni ya nyota zilizoficha dunia zisizoonekana. Ilifaa vyema kwa nabii Mtunga Zaburi kushangaa:

“Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! . . .

“Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;

“Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie?

“Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima.

“Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (Zaburi 8:1, 3–6).

Kipimo halisi cha upendo wa mzazi kwa mtoto ni maandalizi na fursa ambayo mzazi anaandaa kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Tangazo la Mungu Baba: “Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (ona Musa 1:39) ni dhahiri kwa wote wanaotafuta ushahidi. Kazi ya na utukufu wa Baba vinadhihirika kwanza kupitia uzoefu wetu hapa duniani wa uhalisia wa ukuu wa ulimwengu Aliouandaa kwa ajili ya uwepo wetu hapa duniani. Pili, vinadhihirika kupitia imani katika ahadi ya uzima wa milele kupitia zawadi ya Upatanisho wa Mwana Wake wa Pekee, na amani na shangwe kuu kwa wale wote wanaokumbatia tumaini hili. Katika hili ni ushuhuda wa upendo endelevu wa Baba kwa ajili yetu sisi kama watoto Wake.

Kabla ya msingi wa dunia hii, Yeye—kupitia Mwana Wake wa Pekee—aliwasilisha kwa watoto wake wote, mpango ambao uhalisia wetu wa sasa utautegemea, na kupitia huo maisha yetu yajayo yatajengwa:

“Sisi tutakwenda chini, kwani kuna nafasi huko, nasi tutachukua vifaa hivi, nasi tutaifanya dunia mahali ambapo hawa watapata kukaa;

“Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru;

“Na wao ambao watatunza hali yao ya kwanza wataongezewa; na wao ambao hawatatunza hali yao ya kwanza hawatapata utukufu katika ufalme ule ule pamoja na wale walioitunza hali yao ya kwanza; nao wale watakaoitunza hali yao ya pili watapata kuongezewa utukufu juu ya vichwa vyao kwa milele na milele” (ona Ibrahimu 3:24-26).

Tunayo fursa ya kupata uzoefu wa maisha ya duniani kwa sababu tuliidhinisha Mpango Wake. Kwa nini? Kwa sababu hata hapo awali, tulikuwa tayari tu mashahidi wa upendo Wake kwetu na matamanio yake ya kuinuliwa kwetu.

Katika vipindi vyote vya injili ya Mwanaye, Baba wa Mbinguni ametuonyesha kupitia mfano wa watumishi Wake wapakwa mafuta jinsi ya kumpenda Yeye kama vile Yeye anavyotupenda sisi. Mwaliko wake kwetu wa kumpenda Yeye ni ule ule katika vipindi vyote vya maongozi ya Mungu:

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako” (ona Luka 10:27).

Kwa kuuangalia, mwaliko huu unaonekana kuwapa mzigo waalikwa. Hata hivyo, kinyume chake ni kwamba wale wote watakaoitikia katika njia ambazo ni chanya hupokea baraka kuu za mbinguni juu yao. Kumpenda Mungu Baba hakika ndiyo njia iliyo nzuri zaidi kwa yeyote yule kujipenda mwenyewe.

Tunaliona hili katika hali ya upana katika maisha ya Yesu Kristo, ambaye kuhusu Yeye Nabii Abinadi alitangaza kwamba Alimpenda sana Baba kiasi kwamba nia Yake “ikamezwa na nia ya Baba” (ona Mosia 15:7).

Wakati wa kuweka msingi wa dunia, Alichagua kuweka mapenzi ya Baba mbele ya mapenzi yake:

“Baba, mapenzi yako na yatimizwe, na utukufu uwe wako milele na milele” (ona Musa 4:2).

Katika maisha Yake hapa duniani, Alishuhudia na kuishi kulingana na kanuni ya unyenyekevu mkamilifu kwa mapenzi ya Baba:

“Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka” (ona Yohana 6:38).

Na tunayo kwenye kumbukumbu kwamba mwishoni mwa huduma Yake duniani, baada ya kuonyesha upendo Wake usioshindwa kwa Baba katika mafundisho Yake na kupitia mateso Yake yote, Yesu aliwafunulia wanafunzi Wake:

“Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (ona Mathayo 28:18).

Kamwe hakutafuta kujiinua Mwenyewe mbele ya Baba wala kujiinua Mwenyewe juu ya wanadamu wenzake katika kipindi chote cha maisha Yake hapa duniani, Alipokea utimilifu wa karama ya upendo wa kiungu, na Baba akamuinua. Kwa hiyo, katika kumshuhudia Yeye kwa ulimwengu, Baba alitangaza:

“Tazama Mwana wangu Mpendwa ninayependezwa na yeye, ambaye ndani yake nimetukuza jina langu—” (ona 3 Nefi 11:7).

Sisi tumekuwa mashahidi wa upendo wa kiungu wa Baba tangu misingi ya uwepo wetu hata kwenye uhalisia wa hali yetu ya sasa ya maisha ya duniani. Basi kila mmoja wetu na atafute kwa bidii kuitikia mwaliko wa kumpenda Yeye kwa moyo wetu wote, uwezo, akili na nguvu kwa kumpenda Baba yetu wa Mbinguni kwa upendo mkamilifu Aliotuonyesha kupitia Mwana Wake wa Pekee—na kwa kuwapenda kaka na dada zetu kama tunavyojipenda sisi—kwamba tulitukuze jina la Baba, kwamba Afurahishwe nasi, na kwamba Atujaze nguvu zake.

Joseph W. Sitati aliidhinishwa kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini mnamo Aprili 2009. Amemuoa Gladys Nangoni; wao ni wazazi wa watoto watano.