2021
Kuwa Mwenye Kujitegemea ili Kumtumikia Bwana Vyema Zaidi
Juni 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA UKUHANI WA ENEO

Kuwa Mwenye Kujitegemea ili Kumtumikia Bwana Vyema Zaidi

Tunayo fursa ya kutatua matatizo yetu wenyewe na kujitahidi kuwa wenye kujitegemea, kutokana na kwamba kujitegemea ni kanuni ya wokovu.

Nilikua na umri wa miaka kumi na sita wakati baba yangu alipotualika mimi na kaka yangu mdogo kufanya kazi pamoja naye katika shamba lake. Kwetu sisi, lengo kuu lilikuwa kutunza fedha za kutosha kwenda kusoma katika jiji la mbali. Mimi na kaka yangu hatukujua lolote kuhusu kazi ya shamba na tulipaswa kujifunza kila kitu. Mwanzoni, ilikuwa ngumu na yenye changamoto kwa vijana wadogo kama sisi ambao hatukuwahi kufanya kazi ya nguvu kama hiyo. Hatua kwa hatua, baba yetu alitufunza jinsi ya kuifanya.

Hapa ni moja ya masomo mengi aliyotufunza: “Ni kazi pekee ndiyo humfanya mtu kujitegemea na inawaadilisha. Wakati mtu anapokuwa amejitosheleza, wanakuwa wenye staha, wanapata heshima na wanaweza kukamilisha mambo mengi kwa ajili yao na wengine.”

Baba yetu wa Mbinguni Yeye mwenyewe alifanya kazi na uumbaji wa Mbingu na dunia ni matokeo ya kazi Yake.

Wakati Adamu alipopata hatia ya kuvunja sheria katika Bustani ya Edeni, ardhi ililaaniwa, na Mungu alimwamuru tangu hapo na kuendelea kufanya kazi ili kuweza kukidhi maisha. Alimwambia: “Kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako . . .

“Kwa jasho la uso wako utakula chakula” (Mwanzo 3:17, 19).

Katika ufunuo wa siku za leo, Joseph Smith amefundisha katika M&M 42:42: “Usiwe mvivu; kwani yule aliye mvivu hatakula mkate wala kuvaa mavazi ya mfanya kazi.”

Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amefundisha:

“Kwa kazi tunahimili na kustawisha maisha. . . . Kazi hujenga na kurekebisha tabia, hutengeneza uzuri na ni chombo cha huduma yetu kwa kila mmoja wetu na kwa Mungu. Maisha yaliyowekwa wakfu yamejazwa kwa kazi, wakati mwingine ya kujirudia, wakati mwingine kazi ya uboi, wakati mwingine isiyopewa shukrani lakini daima kazi inayoboresha, inayoleta nidhamu, inayoendeleza, inayoinua, inayohudumu, inayovutia, inayoleta hamasa.”1

Kwa kipato ambacho tulipata, mimi na kaka yangu tuliweza kununua chakula, vifaa na nguo za shule na kufokasi kwenye masomo yetu bila wasiwasi mkubwa. Kwa kuwa wenye kujitegemea, tulianza kukua.

Mafundisho niliyopokea kutoka kwa baba yangu yalibaki yametia nanga ndani yangu kote katika masomo yangu. Sikuchukulia juu juu masomo yangu kwa sababu nilijua dhabihu na kazi ngumu iliyohitajika ili kufika pale. Ninaendelea kuepuka uvivu na kufanya kazi kwa bidii ili kuitunza familia yangu.

Ninapata pia fursa, si tu kufundisha kanuni hii kwa watoto wangu, lakini pia kufanya kazi pamoja nao ili wajifunze thamani ya kazi na kujitosheleza.

Miezi kadhaa iliyopita binti yetu, ambaye anajiandaa kuhudumu misheni, alihudhuria madarasa ya kutengeneza vitobosha. Sasa anauza keki, donati na biskuti ili kupata akiba ya pesa kwa ajili ya misheni yake. Kazi na masomo ya kujitegemea tuliyomfunza vimempa hamasa.

Kuna methali ya Kifaransa inayosema “kila biashara ina thamani yake.” Haijalishi ikiwa mtu anafanya kazi kwenye kampuni, shambani au anafanya useremala, uokaji, ulinzi, uchomeleaji au usafirishaji wa bidhaa. Kitu muhimu ni kufanya jambo lililo aminifu.

Tunaelewa kwamba kazi ni kanuni takatifu ambayo huinua na kuongoza kwenye kujitegemea.

Handbook 2: Administering the Church kinatuambia kwamba “kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu mwenyewe na familia.”2

Tunahitaji kuwa wenye bidii na kutumia uwezo wetu wote na nguvu zetu zote ili kujifanya sisi wenyewe kuweza kutumika.

Jukumu hili la kujikimu mwenyewe haliwezi kuwa juu ya kichwa cha mtu mwingine. Kila mtu anawajibika kwa ajili ya ustawi wao wenyewe wa kimwili na kiroho. Tukiwa tumebarikiwa zawadi ya haki ya kujiamulia, tuna fursa ya kutatua matatizo yetu wenyewe na kujitahidi kuwa wenye kujitegemea, kutokana na kwamba kujitegemea ni kanuni ya wokovu.

Handbook 2 inaendelea kusomeka kwamba “pale waumini wanapokuwa wenye kujitegemea, wanaweza kuwatumikia vyema na kuwajali wengine.”3

Kupitia kujitegemea, tunakuza nidhamu binafsi inayohitajika kutii amri za Mungu. Tunakuwa na nguvu ya kumtumikia Bwana katika kufanikisha kile Yeye anachotarajia kwetu. Tutaweza kutembea, kuzungumza na kufundisha mafundisho ya Kristo, kushuhudia juu ya Mungu na Mwana Wake, kuhudumu, kutimiza majukumu yanayohusiana na wito wetu wa Kanisa. Tutakuwa na muda kwa ajili ya kazi ya Bwana.

Tunaweza kufanikisha kuhudumu misheni. Tutafundisha mafundisho ya Kristo kwa uwazi chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Tutawatumikia wengine kwa kutoa matoleo ya mfungo kwa ukarimu ili kwamba maskini na wenye uhitaji waweze kusaidiwa katika njia ya Bwana. Tutalipa zaka zetu kamili na za uaminifu ili kusaidia ufalme. Tutaweza kujifunza maandiko na kuzijua vyema kanuni za injili.

Ninashuhudia kwamba kazi inaongoza kwenye kujitegemea ambako kunatengeneza hali zinazofaa kwa ajili ya kuwatumikia vyema Baba yetu wa Mbinguni na majirani zetu.

Alfred Kyungu aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Oktoba 2019. Amemuoa Lucie Kabulo; wao ni wazazi wa watoto watatu. Mzee na Dada Kyungu wanaishi Kinshasa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Muhtasari

  1. D. Todd Christofferson, “Reflections on a Consecrated Life,” Liahona, Nov. 2010, 17.

  2. General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 22.0, ChurchofJesusChrist.org

  3. General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, “Providing for Temporal Needs and Building Self-Reliance,” 166.