2021
Miujiza Midogo Midogo Iliyojengeka Juu ya Ndoto Zilizokufa
Juni 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Miujiza Midogo Midogo Iliyojengeka Juu ya Ndoto Zilizokufa

Ninapohesabu baraka zangu, nimegundua kwamba Bwana yupo kwenye udhibiti wa vipengele vingi vya maisha yangu. Yeye ananifahamu mimi kibinafsi na nina thamani Kwake.

Miaka mitano iliyopita, niliingia kwenye safari ya kuelekea kufanikisha masomo yangu ya shahada ya pili katika Kilimo, nikijikita katika uzalishaji wa mimea. Nilipewa msaada wa masomo kutoka kwenye Taasisi maarufu ya Utafiti ya Afrika Kusini. Licha ya changamoto ya kuitunza familia, nilikumbatia ndoto hii yenye uwezekano mwingi. Tangu nikiwa na umri mdogo nimekuwa daima nikivutiwa na shughuli za nje ambazo zinahusu kugusa udongo na kupanda mimea ya kijani. Nikiwa nimekulia Msumbiji, nilipenda kumsindikiza bibi yangu kufanya kazi kwenye eneo dogo nje ya mji wa Beira ambapo alipanda kati ya vitu vingine, viazi vitamu na mpunga. Ninathamini kumbukumbu hizo na kuziweka karibu sana na moyo wangu.

Nilipoingia kwenye safari ya kuwa mzalishaji mimea, nilikuwa na uhakika wa kumaliza masomo yangu na kuhitimu kipindi cha majira ya baridi ya mwaka 2020. Nilikuwa na ndoto zisizo na mwisho za jinsi maisha yatakavyokuwa makamilifu. Nikitazama hitaji la ujuzi huo nadra sana katika ajira kwa miaka iliyopita, nilivutiwa sana kwa uwezekano mpya ambao ulikuwa ukijifunua mbele yangu. Nilikuwa mshauri wa kujitegemea wa lugha na vyombo vya habari kwa sehemu kubwa ya maisha yangu ya kazi. Nilikuwa nikitazamia hatimaye kuweza kufanya kazi katika utafiti na kutumia ujuzi ambao nimekuwa nikiupata kwa miaka mingi ya kujifunza.

Kwa kuenea kwa kasi kwa janga la ulimwengu la COVID-19 Afrika Kusini, ilikuwa wazi kwamba japokuwa nilikuwa nimewasilisha tasnifu yangu mwishoni mwa mwaka 2019, nisingeweza kufikia mahafali ya majira ya baridi, kama nilivyokuwa nimetumainia. Jambo muhimu sana kwangu halikuwa sherehe ya mahafali, bali kuweza kumaliza shahada na kupata kazi nzuri. Nilifahamu kwamba ingechukua muda kupata aina ya kazi niliyokuwa nikiitafuta—nilituma barua moja ya maombi ya kazi, kisha ya pili—na hatimaye kulikuwa na nyingi zilizotumwa kiasi kwamba sikuweza kuzihesabu.

Uzoefu huu ulinifunza masomo yenye thamani: baadhi ya mipango yetu katika maisha haijifunui sawasawa na jinsi tunavyotamani ifanyike. Hapa, mwaka mmoja baadaye, bado naendelea kutafuta kazi hiyo ya ndoto yangu. Hii si kwangu pekee, bali kwa familia yangu na jamii kwa ujumla pia wana matarajio makubwa kwa mtu mwenye mafanikio kielimu kama haya.

Nilikutana na rafiki, aliuliza jinsi mambo yalivyokuwa yakienda katika maisha yangu na ikiwa niliweza kupata kazi. Ambapo kwa urahisi sana nilijibu kwamba sikuwa nimefanikiwa katika kupata kazi. Tulizungumza kuhusu mambo kadha wa kadha. Nilipokuwa nikiendesha gari kwenda nyumbani, nilikuwa nikitafakari juu ya mtindo wangu wa maisha na hali yangu ya akili kipindi cha janga la ulimwengu. Kisha nilitambua jinsi mikono ya Bwana ilivyokuwa imebariki maisha yangu. Wakati nikikumbukia niliweza kutambua baadhi ya ujuzi mwingi niliokuwa nimeupata na kiasi cha muda wa thamani nilioweza kuutumia pamoja na familia yangu. Kulikuwa na miujiza midogo midogo mingi sana ya kuhesabu. Nilikuwa nimeweza kukidhi mahitaji yangu ya msingi. Nilichukua bajeti yangu kabla ya COVID-19 na kuipanga upya. Nikiwa na muda mwingi mikononi mwangu, nilivutwa kwenye kipenda roho changu cha kufanya kazi ardhini. Nilipanda bustani ya mboga, mimi na watoto tulijifunza jinsi ya kufyeka nyasi na kupogoa miti—orodha haina mwisho. Leo bustani yetu ya mboga inatupatia mazao mengi ya mboga za kijani, kama vile mchicha, letusi na roketi. Tulipata muda wenye maana wa kucheza na kufanya kazi kama familia. Tulijenga utamaduni wa kwenda kwenye matembezi mafupi ya usiku katika ujirani wetu.

Ninapotafakari juu ya uzoefu wangu katika miezi tisa iliyopita—licha ya kutokuwa na vitu ambavyo vilikuwa ndoto yangu—kwa ujumla nimeridhika. Ninaona mazuri mengi kunizunguka kuliko mabaya. Nimepata uelewa wa kina wa kutumaini katika wakati wa Bwana. Yeye anajua kile kilicho bora na ana mipango mizuri zaidi kwa ajili yangu na familia yangu. Ninapohesabu baraka zangu, nimegundua kwamba Bwana yupo kwenye udhibiti wa vipengele vingi vya maisha yangu. Yeye ananifahamu mimi kibinafsi na nina thamani Kwake. Yeye anajali matamanio yetu ya haki. Anatutaka tumtumaini Yeye na tuwe na furaha. Nimekuja kulijua hilo kwa moyo wangu wote.

Sonia Naidoo ni muumini wa Kata ya Centurion 1st katika kigingi cha Centurion Afrika Kusini, ambapo anahudumu kama mshauri katika Urais wa Msingi.