2021
Baraka za Kugundua, Kukusanya, na Kuunganisha Familia
Juni 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Baraka za Kugundua, Kukusanya, na Kuunganisha Familia

Kuanza shughuli ya historia ya familia halikuwa jambo rahisi kwa familia ya Shamola, lakini wameona milango ikifunguka na baraka nyingi kufunuliwa kadiri walivyoendelea kuifanya.

Kama waongofu wengi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Frederick na Irene Shamola wanajua changamoto za kuwa watu wa kwanza katika familia yao kufanya historia ya familia.

Frederick alijiunga na Kanisa akiwa na umri wa miaka 19 baada ya kutambulishwa na wanafamilia kwenye injili ya urejesho. Irene pia aliongoka akiwa kijana baada ya wamisionari kugonga mlango wa familia yao. Miongo ikasonga kwa haraka, na Frederick na Irene wana ndoa yenye furaha na wanaishi Nairobi, Kenya pamoja na watoto wao watano.

Wakati Kaka na Dada Shamola walipojiunga na Kanisa, walikuwa hawajafanya utafiti wowote wa historia ya familia hapo kabla, na awali walijua tu taarifa za vizazi vichache vya familia zao.

Wamekumbana na vikwazo vingi walipokuwa wakiwatafuta mababu zao kwa ajili ya ibada za hekaluni. Hakukuwa na kumbukumbu iliyoandikwa ya historia ya familia iliyopatikana, hivyo ilibidi wategemee kumbukumbu za ndugu walio hai.

Kuwasiliana na ndugu hao imekuwa vigumu: wanakaa kilometa nyingi kutoka wanapoishi, na watu wachache kwenye vijiji vya mbali vya familia zao ndio wenye simu za mkononi.

Bila kujali changamoto hizi, Bwana ameibariki familia ya Shamola kwenye juhudi zao za kuwatambua mambabu zao.

Hivi karibuni, Kaka Shamola alifurahishwa kwa kupokea taarifa za ziada kuhusu mababu zake kutoka kwenye mahojiano ya mdomo yaliyofanywa katika kijiji cha bibi yake huko Homa Bay, pwani ya magharibi ya Kenya.

Mahojiano yalifanywa kwa mdomo na mwanafamilia na kurekodiwa kwa ajili ya marejeleo kwa wengine siku za baadae. Mahojiano yalimpa taarifa kuhusu vizazi saba vya familia yake, na aliweza kuwatambua mababu wengi ambao hapo awali hakuwajua. Amekwisha wasilisha baadhi ya majina hayo hekaluni na anapanga kuwasilisha mengine mengi baadae.

Dada Shamola pia amekuwa akiwasilisha majina ya wanafamilia kwa ajili ya kazi ya hekalu. Maelfu ya familia zingine wataweza kutambua mababu zao wengi na kuwafanyia kazi ya hekaluni kwa ajili yao kadiri mahojiano ya mdomo ya vizazi yatakavyoendelea kupatikana kwenye FamilySearch.org.

Historia ya familia imewasaidia akina Shamola kuwa wamoja.

Wakifanya kazi kwa pamoja, Kaka na Dada Shamola wamewasaidia watoto wao kutengeneza akaunti za FamilySearch kama sehemu ya shughuli ya Jioni ya Familia Nyumbani. Wanapofanya kazi ya historia ya familia kwa pamoja, familia ya Shamola inasema wanahisi ukaribu kama familia. Watoto wanatazamia kushiriki.

“Ni muhimu sana kujifunza kuhusu historia ya familia kwa sababu itawasaidia watoto wetu na vizazi vingine kutambua wametoka wapi,” Dada Shamola anasema.

Mnamo 2012 familia ya Shamola ilisafiri takribani kilometa 3,000 kwenda Hekalu la Johannesburg Afrika Kusini ili kupokea baraka kuu ya kuunganishwa pamoja kama familia. Hata hivyo, kwa kukosa hekalu katika nchi yao ya asili kumefanya iwe vigumu kwao kurejea hekaluni ili kufanya ibada kwa ajili ya mababu zao. Walizidiwa kwa shangwe wakati Rais Thomas S. Monson (1927–2018) alipotangaza ujenzi wa Hekalu la Nairobi Kenya kwenye Mkutano Mkuu wa Aprili 2017. Kwa shangwe wanatazamia kuwa na hekalu karibu na nyumbani kwao ili waweze kufanya ibada kwa ajili ya mababu zao kwa urahisi. Wana hamu ya kufanya kazi hii kwa ajili ya wale waliowazaa.

“Tumebarikiwa kuwa hai wakati huu na kuijua injili,” Kaka Shamola anasema. “Kuna watu walipenda hilo litokee, lakini hawakuwa na fursa. Tunaweza kuwabariki kwa uzoefu huo na fursa hiyo. Tunaweza kwenda hekaluni na kuwasaidia mababu hao kupokea baraka hizo.

“Tunahisi hisia ya amani tunapowafikiria wao na kuwasilisha majina yao na kufanya kazi kwa ajili yao. Baba wa Mbinguni anakusanya Israeli, na anatumia hekalu na kazi ya historia ya familia kukamilisha kazi Yake. Ni . . . heshima kwangu kuwa chombo kwenye mikono ya Baba wa Mbinguni cha kuweza kufanya hivyo na kushiriki katika wakati huu muafaka. Nina shukrani kwa kuwa muumini wa Kanisa, na ninataka watoto wangu waweze kushiriki hilo kadiri wanavyokua.”

Shadrack Barasa ni muumini wa Tawi la Misikhu, Wilaya ya Kitale Kenya, Kenya. Tyler Mills ni muumini wa kata ya Meadowpark ya Vijana Wadogo Waseja iliyopo eneo la Syracuse, Utah, Marekani.