Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 18


Sehemu ya 18

Ufunuo kwa Joseph Smith, Nabii, Oliver Cowdery, na David Whitmer, uliotolewa huko Fayette, New York, Juni 1829. Kulingana na Nabii, ufunuo huu uliojulikana kama “kuitwa kwa mitume kumi na wawili katika siku hizi za mwisho, na pia maelekezo yahusuyo kuanzishwa kwa Kanisa.”

1–5, Maandiko yanaonyesha namna ya kulijenga Kanisa; 6–8, Ulimwengu unakomaa katika dhambi; 9–16, Thamani ya nafsi ni kuu; 17–25, Ili kupata wokovu, wanadamu yawalazimu kujichukulia juu yao wenyewe jina la Kristo; 26–36, Wito na huduma ya Kumi na Wawili yafunuliwa; 37–39, Oliver Cowdery na David Whitmer wawatafute Kumi na Wawili; 40–47, Ili kupata wokovu, mwanadamu inamlazimu kutubu, kubatizwa na kushika amri.

1 Sasa, tazama, kwa sababu ya jambo ambalo wewe, mtumishi wangu Oliver Cowdery, umetaka kulijua kwangu, ninakupa maneno haya:

2 Tazama, nimekwisha jidhihirisha kwako, kwa Roho yangu mara nyingi, kwamba mambo ambayo umeyaandika ni ya kweli; kwa hiyo unajua ni ya kweli.

3 Na kama wewe unajua kwamba ni ya kweli, tazama, ninakupa wewe amri, kwamba utegemee mambo ambayo yameandikwa;

4 Kwani katika hayo mambo yote yameandikwa kuhusu msingi wa kanisa langu, injili yangu, na mwamba wangu.

5 Kwa hiyo, kama utalijenga kanisa langu, juu ya msingi wa injili yangu na mwamba wangu, milango ya jehanamu haitakushinda.

6 Tazama, ulimwengu unaiva katika dhambi; na ni lazima inahitajika kuwa wanadamu wachochewe katika toba, wote Wayunani na pia wa nyumba ya Israeli.

7 Kwa hiyo, kama ulivyobatizwa kwa mikono ya mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, kulingana na vile nilivyomwamuru, ametimiza jambo ambalo nilimwamuru.

8 Na sasa, usishangae kwamba nimemwita yeye kwa madhumuni yangu, madhumuni ambayo yanajulikana kwangu; kwa hiyo, kama atafanya bidii katika kushika amri zangu atabarikiwa kwa uzima wa milele; na jina lake ni Joseph.

9 Na sasa, Oliver Cowdery, ninasema na wewe, na pia na David Whitmer, kwa njia ya amri; kwani, tazama, ninawaamuru watu wote kila mahali kutubu, na ninasema nanyi, hata kama vile kwa Paulo mtume wangu, kwani mmeitwa kwa wito ule ule ambao yeye aliitwa.

10 Kumbuka thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu;

11 Kwani, tazama, Bwana Mkombozi wako aliteseka hadi kifo katika mwili; kwa hiyo aliteseka maumivu ya watu wote, ili kwamba watu wote waweze kutubu na kuja kwake.

12 Na yeye amefufuka tena kutoka kwa wafu, ili kwamba aweze kuwaleta watu wote kwake, kwa masharti ya toba.

13 Na ni shangwe kubwa kiasi gani kwake katika nafsi ambayo hutubu!

14 Kwa hiyo, wewe umeitwa kutangaza toba kwa watu hawa.

15 Na kama itakuwa kwamba utafanya kazi siku zako zote katika kutangaza toba kwa watu hawa, na kuleta, japo iwe nafsi moja kwangu, shangwe yako itakuwa kubwa jinsi gani pamoja naye katika ufalme wa Baba yangu!

16 Na sasa, kama shangwe yako itakuwa kubwa kwa hiyo nafsi moja ambayo umeileta kwangu katika ufalme wa Baba yangu, itakuwa shangwe kubwa namna gani kwako kama utazileta nafsi nyingi kwangu!

17 Tazama, unayo injili yangu mbele yako, na mwamba wangu, na wokovu wangu.

18 Mwombe Baba katika jina langu kwa imani, ukiamini kwamba utapokea, nawe utapata Roho Mtakatifu, ambaye hudhihirisha mambo yote yaliyo muhimu kwa wanadamu.

19 Na kama wewe hauna imani, matumaini, na hisani, huwezi kufanya lolote.

20 Usishindane na kanisa lolote, isipokuwa kanisa la ibilisi.

21 Ujichukulie juu yako jina la Kristo, na sema ukweli katika utulivu.

22 Na kadiri wengi wanavyotubu na kubatizwa katika jina langu, ambalo ni Yesu Kristo, na kuvumilia hadi mwisho, hao ndiyo wataokolewa.

23 Tazama, Yesu Kristo ndilo jina ambalo limetolewa na Baba, na hakuna jina lingine lililotolewa ambalo kwa hilo mwanadamu aweza kuokolewa;

24 Kwa hiyo, wanadamu wote yawalazimu kujichukulia juu yao jina ambalo limetolewa na Baba, kwani katika jina hilo wataitwa katika siku ya mwisho;

25 Kwa hiyo, kama wao hawajui jina ambalo wanaitwa, hawawezi kupata nafasi katika ufalme wa Baba yangu.

26 Na sasa, tazama, wapo wengine ambao wameitwa kuihubiri injili yangu, kote kwa Myunani na kwa Myahudi;

27 Ndiyo, hata kumi na wawili; na hao Kumi na Wawili watakuwa wanafunzi wangu, na wao watajichukulia juu yao jina langu; na hao Kumi na Wawili ni wale ambao hutamani kujichukulia juu yao jina langu kwa dhamira ya moyo wao wote.

28 Na kama wao hutamani kujichukulia juu yao jina langu kwa dhamira ya moyo wao wote, hao wameitwa kwenda ulimwenguni kote kuhubiri injili yangu kwa kila kiumbe.

29 Na hao ndiyo wale ambao wametawazwa na Mimi kubatiza katika jina langu, kulingana na yale yaliyoandikwa;

30 Na wewe unayo yale ambayo yameandikwa mbele yako; kwa hiyo basi, ni lazima ufanye kulingana na maneno ambayo yameandikwa.

31 Na sasa ninasema na ninyi, Kumi na Wawili—Tazama, neema yangu inatosha kwenu; lazima mtembee wima mbele zangu na msitende dhambi.

32 Na, tazama, ninyi ndiyo wale ambao wametawazwa na mimi ili kuwatawaza makuhani na walimu; kuitangaza injili yangu, kulingana na uwezo wa Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, na kulingana na miito na vipawa vya Mungu kwa wanadamu;

33 Na mimi, Yesu Kristo, Bwana wenu na Mungu wenu, nimeyasema haya.

34 Maneno haya si ya wanadamu wala mwanadamu, bali ni yangu; kwa sababu hiyo, mtayashuhudia hayo kuwa ni yangu na siyo ya mwanandamu;

35 Kwani ni sauti yangu ambayo huyasema kwenu; kwani yanatolewa kwa Roho yangu kwenu, na kwa uwezo wangu ninyi mnaweza kusomeana; na isingekuwa kwa uwezo wangu msingeweza kuyapata hayo;

36 Kwa hiyo basi, ninyi mnaweza kushuhudia kwamba mmesikia sauti yangu, na mnayajua maneno yangu.

37 Na sasa, tazama, ninatoa kwako wewe, Oliver Cowdery, na pia kwako David Whitmer, kwamba mtawatafuta Kumi na Wawili, ambao watakuwa na matamanio haya ambayo nimeyataja;

38 Na kwa matamanio yao na matendo yao mtawajua.

39 Na mkiisha wapata mtaonyesha mambo haya kwao.

40 Na ninyi mtaanguka chini na kumwabudu Baba katika jina langu.

41 Na ninyi lazima mhubiri kwa ulimwengu, mkisema: Lazima mtubu na mbatizwe, katika jina la Yesu Kristo;

42 Kwani, watu wote lazima watubu na wabatizwe, sio tu wanaume, bali hata wanawake, na watoto ambao wamefikia umri wa wajibikaji.

43 Na sasa, baada ya kuwa ninyi mmepokea haya, ni lazima mzishike amri zangu katika mambo yote;

44 Na kwa mikono yenu nitafanya kazi ya kushangaza miongoni mwa wanadamu, kwa kuwashawishi wengi juu ya dhambi zao, ili waweze kuja kwenye toba, na ili waweze kuja kwenye ufalme wa Baba yangu.

45 Kwa hiyo basi, baraka ambazo ninazitoa kwenu ni juu ya mambo yote.

46 Na baada ya kupokea hii, kama hamtashika amri zangu hamtaweza kuokolewa katika ufalme wa Baba yangu.

47 Tazama, Mimi, Yesu Kristo, Bwana wenu na Mungu wenu, na Mkombozi wenu, kwa uwezo wa Roho yangu nimeyasema haya. Amina.