Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 88


Sehemu ya 88

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii huko Kirtland, Ohio, 27 na 28 Desemba 1832 na 3 Januari 1833. Nabii aliupa jina na akauita kama “‘jani la mzeituni’ … lililochumwa kutoka katika Mti wa Peponi, ujumbe wa Bwana wa amani kwetu sisi.” Ufunuo ulitolewa baada ya makuhani wakuu kwenye mkutano kuomba “mmoja mmoja na kwa sauti kwa Bwana ili afunue mapenzi yake kwao kuhusiana na ujenzi wa Sayuni.”

1–5, Watakatifu waaminifu humpokea yule Mfariji, ambaye ni ahadi ya uzima wa milele; 6–13, Vitu vyote vinaongozwa na kutawaliwa kwa Nuru ya Kristo; 14–16, Ufufuko huja kupitia Ukombozi; 17–31, Utii kwa sheria za selestia, terestria au telestia huwatayarisha wanadamu kwa falme na fahari husika; 32–35, Wale wanaotaka kukaa katika dhambi hubakia wachafu; 36–41, Falme zote zinatawaliwa kwa sheria; 42–45, Mungu ametoa sheria kwa vitu vyote; 46–50, Mwanadamu atamjua hata Mungu; 51–61, Ule mfano wa mtu kuwatuma watumishi wake shambani na kuongea nao mmoja mmoja; 62–73, Mkaribieni Bwana, na mtauona uso Wake; 74–80, Jitakaseni wenyewe na kufundishana mafundisho ya ufalme; 81–85, Kila mwanadamu aliyeonywa anapaswa kumwonya jirani yake; 86–94, Ishara, mvurugiko wa vitu vya asili, na malaika wanaitengeneza njia kwa ajili ya kuja kwa Bwana; 95–102, Parapanda ya malaika kuwaita wafu katika utaratibu wao; 103–116, Parapanda ya malaika yatangaza urejesho wa injili, anguko la Babilonia, na pambano la Mungu mkuu; 117–126, Tafuteni kujifunza, jengeni nyumba ya Mungu (hekalu), na jivikeni ninyi wenyewe kwa kifungo cha hisani; 127–141, Utaratibu wa Shule ya Manabii unawekwa, ikiwa ni pamoja na ibada ya kutawadha miguu.

1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu mliokusanyika wenyewe pamoja ili kupokea mapenzi yake juu yenu:

2 Tazama, hii inampendeza Bwana wenu, na malaika wanafurahi juu yenu; sadaka za sala zenu zimefika juu katika masikio ya Bwana wa Sabato, na kuandikwa katika kitabu cha majina ya waliotakaswa, hata wale wa ulimwengu wa selestia.

3 Kwa hiyo, sasa ninampeleka kwenu Mfariji mwingine, hata juu yenu ninyi marafiki zangu, ili aweze kukaa katika mioyo yenu, hata Roho Mtakatifu wa ahadi; Mfariji mwingine ambaye ni yule yule niliyewaahidi wanafunzi wangu, kama ilivyoandikwa katika ushuhuda wa Yohana.

4 Mfariji huyu ni ahadi ambayo ninawapa ninyi ya uzima wa milele, hata utukufu wa ufalme wa selestia;

5 Utukufu ambao ni wa kanisa la Mzaliwa wa Kwanza, hata wa Mungu, mtakatifu kupita wote, kupitia Yesu Kristo Mwana wake—

6 Yeye yule aliyepaa juu, vile vile pia alishuka chini ya vitu vyote, kiasi kwamba alielewa vitu vyote, ili aweze kuwa katika vyote na ndani ya vitu vyote, nuru ya ukweli;

7 Ukweli ambao hungʼara. Hii ndiyo nuru ya Kristo. Kama vile pia yu katika jua, na ni nuru ya jua na nguvu yake ambayo kwayo liliumbwa.

8 Kama vile pia yu katika mwezi, na ni nuru ya mwezi, na nguvu yake ambayo kwayo uliumbwa;

9 Kama vile pia ni nuru ya nyota, na nguvu yake ambayo kwayo ziliumbwa;

10 Na dunia pia, na ni nguvu yake, hata dunia hii ambayo juu yake mmesimama.

11 Na nuru ingʼarayo, ambayo hukupa mwanga, hutoka kwake yeye ayaangazaye macho yako, ambayo ndiyo nuru hiyo hiyo ambayo huhuisha ufahamu wako;

12 Nuru itokayo kutoka katika uwepo wa Mungu ili kuijaza sehemu kubwa—

13 Nuru iliyo ndani ya vitu vyote, ambayo hutoa uhai kwa vitu vyote, ambayo ndiyo sheria ambayo kwayo vitu vyote hutawaliwa, hata uwezo wa Mungu aketiye juu ya kiti chake cha enzi, yeye aliye kifuani pa milele, yeye aliye katikati ya vitu vyote.

14 Sasa, amini ninawaambia, kuwa kwa njia ya ukombozi ambao umefanyika kwa ajili yenu huleta kukamilika kwa ufufuko wa wafu.

15 Na roho na mwili ndiyo nafsi ya mwanadamu.

16 Na ufufuko wa wafu ni ukombozi wa nafsi.

17 Na ukombozi wa nafsi ni kupitia kwake yeye ambaye anavihifadhi hai vitu vyote, ambaye kifuani mwake aliadhimia kuwa maskini na wapole wa dunia watairithi nchi.

18 Kwa hiyo, haina budi kusafishwa udhalimu wote, ili iweze kuandaliwa kwa ajili ya utukufu wa selestia;

19 Kwani baada ya kuwa imetimiza kipimo cha uumbaji wake, itavikwa taji la utukufu, hata na uwepo wa Mungu Baba;

20 Kwamba miili ile iliyo ya ufalme wa selestia itaimiliki milele na milele; kwani, kwa kusudi hili, ilitengenezwa na kuumbwa, na kwa kusudi hili wametakaswa.

21 Na wale ambao hawakutakaswa kwa sheria ambayo nimeitoa kwenu, hata sheria ya Kristo, lazima warithi ufalme mwingine, hata ule ufalme wa terestria, au ule ufalme wa telestia.

22 Kwani yule ambaye hawezi kuishi kwa sheria ya ufalme wa selestia hawezi kustahimili katika utukufu wa selestia.

23 Na yule asiyeweza kuishi kwa sheria ya ufalme wa terestria hawezi kustahimili utukufu wa terestria.

24 Na yule asiyeweza kuishi kwa sheria ya ufalme wa telestia hawezi kustahimili utukufu wa telestia; kwa hiyo hafai kwa ufalme wa utukufu. Kwa hiyo yeye lazima aishi katika ufalme usio na utukufu.

25 Na tena, amini ninawaambia, dunia huishi sheria ya ufalme wa selestia, kwa kuwa inatimiza kipimo cha uumbaji wake, na wala haivunji sheria—

26 Kwa hiyo, itatakaswa; ndiyo, ijapokuwa itakufa, itahuishwa tena, na itastahimili nguvu ambayo kwayo ilihuishwa, na wenye haki watairithi.

27 Kwani ijapokuwa wanakufa, pia wataamka tena, na mwili wa kiroho.

28 Wale walio wa roho za selestia watapokea mwili huo huo ambao ulikuwa mwili wa asili; hata ninyi mtapata miili yenu, na utukufu ule ambao kwa huo miili yenu ilihuishwa.

29 Ninyi ambao mnahuishwa kwa sehemu ya utukufu wa selestia halafu ndipo mtapokea huo huo, hata utimilifu.

30 Na wale ambao huhuishwa kwa sehemu ya utukufu wa terestria watapokea huo huo, hata utimilifu wake.

31 Na pia wale ambao huhuishwa kwa sehemu ya utukufu wa telestia watapokea huo huo, hata utimilifu wake.

32 Na wale waliosalia nao pia watahuishwa; hata hivyo, watarejeshwa tena mahali pao, ili kufurahia kile ambacho wako tayari kukipokea, kwa sababu hawakuwa tayari kufurahia kile ambacho wangelikipokea.

33 Kwani itamfaidia mtu nini kama zawadi imewekwa juu yake, na hapati zawadi hiyo? Tazama, hafurahii katika kile ambacho kimetolewa kwake, wala hamfurahii yeye aliyetoa zawadi.

34 Na tena, amini ninawaambia, kile kitawaliwacho kwa sheria pia hulindwa kwa sheria na kukamilishwa na kutakaswa kwa sheria hiyo hiyo.

35 Kile kivunjacho sheria, na hakiishi kwa sheria, lakini chatafuta chenyewe kuwa sheria, na kiko tayari kuishi katika dhambi, na moja kwa moja kinaishi katika dhambi, hakiwezi kutakaswa kwa sheria, si kwa rehema, haki, wala hukumu. Kwa hiyo, lazima wazidi kuwa wachafu.

36 Falme zote zinayo sheria zilizotolewa;

37 Na ziko falme nyingi; kwani hakuna nafasi ambamo ndani yake hakuna ufalme; na hakuna ufalme ambamo ndani yake hakuna nafasi, iwe falme kubwa au ndogo.

38 Na kwa kila ufalme sheria imetolewa; na kwa kila sheria kuna mipaka maalumu pia na taratibu zake.

39 Viumbe wote wasioishi katika taratibu hizo hawahesabiwi haki.

40 Kilicho akili huambatana na akili; hekima hupokea hekima; kweli huikumbatia kweli; wema hupenda wema; nuru huambatana na nuru; rehema huonyesha huruma juu ya rehema na hudai chake; haki huchukua mkondo wake na kudai chake; hukumu huenda mbele ya uso wa yule ambaye huketi juu ya kiti cha enzi na atawalaye na kuviongoza vitu vyote.

41 Ajuaye vitu vyote, na vitu vyote viko mbele yake, na vitu vyote humzunguka yeye; na yeye yu juu ya vitu vyote, na ndani ya vitu vyote, na apita vitu vyote, na amevizunguka vitu vyote; na vitu vyote viko kwake, na ni vyake yeye, hata Mungu, milele na milele.

42 Na tena, amini ninawaambia, yeye ametoa sheria kwa vitu vyote, ambazo kwa hizo vinakwenda katika nyakati zake na majira yake;

43 Na njia zao zimewekwa, hata njia za mbinguni na duniani, ambazo huielewa dunia na sayari zote.

44 Nazo hupeana nuru katika nyakati zao na majira yao, katika dakika zao, katika masaa yao, katika siku zao, katika wiki zao, katika miezi yao, katika miaka yao—hivi vyote ni mwaka mmoja kwa Mungu, lakini siyo kwa mwanadamu.

45 Dunia hubiringika kwa mabawa yake, nalo jua hutoa mwanga wake mchana, nao mwezi hutoa mwangaza wake usiku, nazo nyota pia hutoa mwanga wake, wakiwa wanabingirika juu ya mbawa zao katika utukufu wao, katikati ya uwezo wa Mungu.

46 Nitazilinganisha na nini falme hizi, ili muweze kuelewa?

47 Tazama, hizi zote ni falme, na mtu yeyote aliyoiona yoyote au ndogo ya hizi amemwona Mungu akitembea katika ukuu na uwezo wake.

48 Ninawaambia, huyo amemwona; hata hivyo, yule ambaye alikuja kwa walio wake hakutambuliwa.

49 Nuru yangʼara gizani, na giza haiitambui; hata hivyo, siku itakuja mtakayomjua Mungu, mkiwa mmehuishwa ndani yake na yeye mwenyewe.

50 Ndipo mtajua ya kuwa mmeniona Mimi, kwamba Mimi ndiye, na kwamba Mimi ni nuru ya kweli niko ndani yenu, na ninyi mu ndani yangu; vinginevyo msingelifanikiwa.

51 Tazama, nitazilinganisha falme hizi na mtu mwenye shamba, na aliwapeleka watumishi wake katika shamba ili kulima.

52 Na akamwambia wa kwanza: Nenda ukafanye kazi shambani, na saa moja nitakuja kwako, nawe utaiona shangwe usoni mwangu.

53 Na akamwambia wa pili: Nenda pia shambani, na mnamo saa mbili nami nitakutembelea nikiwa na shangwe usoni mwangu.

54 Na pia kwa yule wa tatu, akisema: Nitakutembelea;

55 Na kwa wanne, na kuendelea hadi wa kumi na wawili.

56 Na Bwana wa shamba akaenda kwa wa kwanza katika saa ya kwanza, na akakaa naye saa hiyo yote, naye alifanywa mwenye furaha kwa nuru ya uso wa Bwana wake.

57 Na halafu akajitoa kwa yule wa kwanza ili aweze kumtembelea wa pili pia, na wa tatu, na wa nne, na kuendelea hadi wa kumi na wawili.

58 Na hivyo wote walipata nuru ya uso wa bwana wao, kila mtu katika saa yake, na katika wakati wake, na katika majira yake—

59 Akianzia yule wa kwanza, na kuendelea hadi wa mwisho, na kutoka wa mwisho hadi wa kwanza, na kutoka wa kwanza hadi wa mwisho;

60 Kila mtu katika mpangilio wake, hadi saa yake ilipokwisha, hata kulingana na bwana alivyomwamuru, ili bwana wake apate kutukuzwa ndani yake, na yeye ndani ya bwana wake, ili wote waweze kutukuzwa.

61 Kwa hiyo, kwa mfano huu ninazifananisha falme hizi zote, na wakazi wake—kila ufalme katika saa yake, na wakati wake, na katika majira yake, hata kulingana na kiwango ambacho Mungu amekiweka.

62 Na tena, amini ninawaambia, marafiki zangu, ninayaacha maneno haya kwenu ili muyatafakari katika mioyo yenu, pamoja na amri hii ambayo ninaitoa kwenu, kwamba mtanilingana maadamu Mimi nipo karibu—

63 Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na ninyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

64 Na lolote muombalo kwa Baba katika jina langu mtapewa, lile lililo muhimu kwenu;

65 Na ikiwa mtaomba kitu chochote ambacho siyo muhimu kwenu, kitageuka kuwa hukumu kwenu.

66 Tazama, kile mkisikiacho ni kama sauti ya mtu aliaye nyikani—nyikani, kwa sababu hamwezi kumwona—sauti yangu, kwa sababu sauti yangu ni Roho, Roho yangu ndiyo kweli; kweli hudumu na wala haina mwisho; na kama ikiwa ndani yenu mtafanikiwa.

67 Na kama macho yenu yatakuwa katika utukufu wangu pekee, miili yenu yote itajazwa na nuru, na hakutakuwa na giza ndani yenu; na mwili ule uliojazwa na nuru hufahamu mambo yote.

68 Kwa hiyo, jitakaseni, ili mawazo yenu yawe juu ya Mungu, na siku zitakuja ambazo mtamwona yeye; kwani ataufichua uso wake kwenu, nayo itakuwa katika wakati wake mwenyewe, na katika njia yake mwenyewe, na kulingana na mapenzi yake mwenyewe.

69 Ikumbukeni ahadi ile iliyo kuu na ya mwisho niliyoifanya kwenu; yaondoeni mbali mawazo yenu potovu na vicheko vyenu vilivyokithiri.

70 Kaeni, kaeni mahali hapa, na itisheni kusanyiko la kiroho, la wale wote walio wafanyakazi wa kwanza katika ufalme huu wa mwisho.

71 Na wale ambao wameonywa katika safari zao na wamlingane Bwana, na kutafakari onyo hilo walilolipokea mioyoni mwao, kwa kipindi kifupi.

72 Tazama na lo, nitalichunga kundi lenu, na kuwainua wazee na kuwatuma kwao.

73 Tazama, nitaiharakisha kazi yangu katika wakati wake.

74 Na ninatoa kwenu, ninyi mlio wafanyakazi wa kwanza katika ufalme huu wa mwisho, amri kuwa jikusanyeni pamoja, na jipangeni, na jiandaeni, na jitakaseni; ndiyo, itakaseni mioyo yenu, na iosheni mikono na miguu yenu mbele zangu, ili niweze kuwafanya kuwa safi;

75 Ili niweze kushuhudia kwa Baba yenu, na Mungu wenu, na Mungu wangu, kwamba ninyi ni wasafi kutokana na damu ya kizazi hiki kiovu; ili niweze kutimiza ahadi hii, ahadi iliyo kuu na ya mwisho, niliyofanya kwenu, wakati nitakapotaka.

76 Pia, ninatoa amri kwenu ya kuwa endeleeni katika sala na kufunga tangu sasa na kuendelea.

77 Na ninatoa kwenu amri ya kuwa mfundishane mafundisho ya ufalme.

78 Fundishaneni kwa bidii na neema yangu itakuwa pamoja nanyi, ili mpate kuelekezwa kiukamilifu zaidi katika nadharia, katika kanuni, katika mafundisho, katika sheria za injili, katika mambo yale yote yahusuyo ufalme wa Mungu, yale yaliyo muhimu kwenu kuyafahamu;

79 Juu ya mambo kote mbinguni na duniani, na chini ya dunia; mambo yaliyokuwepo, mambo yaliyopo, mambo ambayo hayana budi kutokea upesi; mambo yaliyoko nyumbani, mambo yaliyoko ngʼambo; vita na mifadhaiko ya mataifa, na hukumu zilizoko juu ya nchi; na maarifa pia juu ya nchi na falme—

80 Ili mpate kuandaliwa katika mambo yote wakati nitakapowatuma tena kutukuza wito ambao nimewaitia, na huduma ambayo kwayo nimewapa mamlaka.

81 Tazama, nimewatuma ninyi kwenda kushuhudia na kuwaonya watu, na ni wajibu wa kila mtu ambaye ameonywa amwonye jirani yake.

82 Kwa hiyo, wameachwa pasipo udhuru, na dhambi zao ziko juu ya vichwa vyao wenyewe.

83 Yule anitafutaye mapema ataniona, na wala hatasahaulika.

84 Kwa hiyo, kaeni, na fanyeni kazi kwa bidii, ili mpate kukamilishwa katika huduma yenu ya kwenda miongoni mwa Wayunani kwa mara ya mwisho, wengi kadiri kinywa cha Bwana kitakavyo wataja, ili kuifunga sheria na kutia muhuri ushuhuda, na kuwaandaa watakatifu kwa ajili ya saa ya hukumu ambayo itakuja;

85 Kwamba roho zao ziweze kuepuka ghadhabu ya Mungu, chukizo la uharibifu ambalo linawangoja waovu, kote katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Amini, ninawaambia, acha wale wazee ambao sio wa kwanza waendelee katika shamba la mizabibu hadi kinywa cha Bwana kitakapowaita, kwani wakati wao bado haujafika; mavazi yao bado hayajawa safi kutokana na damu ya kizazi hiki.

86 Kaeni katika uhuru ambamo humo mmefanywa kuwa huru; wala msinaswe dhambini, bali mikono yenu na iwe safi, hadi Bwana ajapo.

87 Kwani baada ya siku hizi chache na dunia itatetemeka na kulewa lewa kama mlevi; nalo jua litauficha uso wake, na litakataa kutoa mwangaza; nao mwezi utaogeshwa katika damu; nazo nyota zitashikwa na hasira, na kujiangusha chini kama mti wa mtini upukutishavyo mapooza yake.

88 Na baada ya ushuhuda wenu yaja ghadhabu na uchungu kwa watu.

89 Kwani baada ya ushuhuda wenu waja ushuhuda wa matetemeko ya ardhi, ambayo yatasababisha sauti za kuelemewa katikati yake, na watu wataanguka juu ya ardhi na wala hawataweza kusimama.

90 Na pia waja ushuhuda wa sauti ya ngurumo za radi, na sauti za radi, na sauti za tufani, na sauti za mawimbi ya bahari yakipanda na kushuka yenyewe hata nje ya mipaka yake.

91 Na vitu vyote vitakuwa katika vurugu; na hakika, watu watavunjika mioyo; kwa kuwa hofu itakuja juu ya watu wote.

92 Na malaika wataruka katikati ya mbingu, wakilia kwa sauti kuu, wakipiga parapanda ya Mungu, wakisema: Jitayarisheni, jitayarisheni, Enyi wakazi wa dunia; kwani hukumu ya Mungu wetu imefika. Tazama, na lo, Bwana harusi anakuja; nendeni nje kumlaki.

93 Na mara patatokea ishara kuu mbinguni, na watu wote wataiona kwa pamoja.

94 Na malaika mwingine atapiga parapanda yake, akisema: Lile kanisa kuu, mama wa machukizo, aliyeyafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake, ambaye huwatesa watakatifu wa Mungu, ambaye humwaga damu zao—yeye aketiye juu ya maji mengi, na juu ya visiwa vya bahari—tazama, yeye ndiye magugu ya dunia; amefungwa katika mafungu; kamba zake zimefanywa imara, hakuna mtu awezaye kuzifungua; kwa hiyo, yuko tayari kuchomwa. Naye atapiga parapanda yake nayo itazidi kulia sana, na mataifa yote yataisikia.

95 Na patakuwa na ukimya mbinguni kwa kipindi cha nusu saa; na mara baada ya hapo mapazia ya mbinguni yatafunguliwa, kama ukurasa uliokunjuliwa baada ya kukunjwa, na uso wa Bwana utafunuliwa;

96 Na watakatifu waliopo juu ya dunia, walio hai, watahuishwa na kunyakuliwa mawinguni kwenda kumlaki yeye.

97 Na wale waliolala makaburini mwao wataamka, kwani makaburi yao yatafunuliwa; nao pia watanyakuliwa kwenda kumlaki yeye katikati ya nguzo ya mbinguni—

98 Hawa ndiyo walio wa Kristo, malimbuko ya kwanza, hawa ndiyo watakaoshuka pamoja naye kwanza, na wale walioko juu ya dunia na katika makaburi yao, ambao watanyakuliwa kwenda kumlaki yeye; na hii yote ni kwa sauti ya kupigwa parapanda ya malaika wa Mungu.

99 Na baada ya hii malaika mwingine atapiga, ambayo ni parapanda ya pili; na halafu utakuja ukombozi wa wale walio wa Kristo katika ujio wake; wale ambao wamepata sehemu yao katika kile kifungo kilichotayarishwa kwa ajili yao, ili wapate kuipokea injili, na kuhukumiwa kulingana na wanadamu katika mwili.

100 Na tena, parapanda nyingine italia, ambayo ni parapanda ya tatu; na halafu zitakuja roho za watu ambao wanatakiwa kuhukumiwa, nao wanapatikana na hatia;

101 Na hawa ndiyo masalia ya wafu; nao hawakuwa hai tena hadi itimie ile miaka elfu, wala hawataishi tena, hadi mwisho wa dunia.

102 Na parapanda nyingine italia, ambayo ni parapanda ya nne, ikisema: Wamepatikana miongoni mwa wale ambao watasalia hadi siku ile kuu na ya mwisho, hata mwisho, wenye uchafu ambao watazidi kuwa wachafu.

103 Na parapanda nyingine italia, ambayo ni parapanda ya tano, ambayo ni ya malaika wa tano ambaye ataleta injili isiyo na mwisho—akiruka katikati ya mbingu, kwa mataifa yote, makabila, lugha, na watu;

104 Na hii itakuwa sauti ya parapanda yake, ikisema kwa watu wote, kote mbinguni na duniani, na wale walioko chini ya dunia—kwani kila sikio litasikia, na kila goti litapigwa, na kila ulimi utakiri, wakati wasikiapo sauti ya parapanda, ikisema: Mcheni Mungu na kumtukuza yeye aketiye juu ya kiti chake cha enzi, milele na milele; kwani saa ya hukumu yake imefika.

105 Na tena, malaika mwingine atapiga parapanda yake, ambaye ni malaika wa sita, akisema: Ameanguka yule aliyefanya mataifa yote kunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake; ameanguka, ameanguka!

106 Na tena, malaika mwingine atapiga parapanda yake, ambaye ni malaika wa saba, akisema: Imekwisha; imekwisha! Mwanakondoo wa Mungu ameshinda na amelikanyaga shinikizo pekee yake, hata shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mwenyezi Mungu.

107 Na halafu malaika hawa watavikwa mataji ya utukufu wa uwezo wake, nao watakatifu watajawa na utukufu wake, na kupokea urithi wao na watafanywa kuwa sawa naye.

108 Na halafu malaika wa kwanza atapiga parapanda yake tena katika masikio ya wote walio hai, na kufunua matendo ya siri ya wanadamu, na matendo makuu ya Mungu katika miaka elfu moja ya kwanza.

109 Na halafu malaika wa pili atapiga parapanda yake, na kufichua matendo ya siri ya wanadamu, na mawazo na dhamira za mioyo yao, na matendo makuu ya Mungu katika miaka elfu moja ya pili—

110 Na kuendelea, hadi malaika wa saba atakapopiga parapanda yake; naye atasimama juu ya nchi na juu ya bahari, na kuapa katika jina lake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; na Shetani atafungwa, yule nyoka wa zamani, anayeitwa ibilisi, na hataachiliwa kwa kipindi cha miaka elfu.

111 Na halafu ataachiliwa kwa kipindi kifupi, ili apate kuyakusanya pamoja majeshi yake.

112 Na Mikaeli, yule malaika wa saba, hata malaika mkuu, atayakusanya pamoja majeshi yake, hata majeshi ya mbinguni.

113 Naye ibilisi atayakusanya pamoja majeshi yake; hata majeshi ya jehanamu, na atakuja kupambana dhidi ya Mikaeli na majeshi yake.

114 Na halafu linakuja pambano la Mungu mkuu; na ibilisi na majeshi yake watatupwa mahali pao wenyewe, kiasi kwamba wasipate kabisa uwezo tena juu ya watakatifu.

115 Kwani Mikaeli atapigana mapambano yao, na atamshinda yule atafutaye kiti cha enzi cha yule aketiye juu ya kiti cha enzi, hata Mwanakondoo.

116 Huu ndiyo utukufu wa Mungu, na walio takaswa; nao kamwe hawataona mauti tena.

117 Kwa hiyo, amini ninawaambia, marafiki zangu, itisheni kusanyiko lenu la kiroho, kama nilivyowaamuru.

118 Na kwa vile wote hamna imani, tafuteni kwa bidii na kufundishana maneno ya hekima; ndiyo, tafuteni kutoka kwenye vitabu vizuri maneno ya hekima; tafuteni maarifa, hata kwa kujifunza na pia kwa imani.

119 Jiandaeni wenyewe; tayarisheni kila kitu kinachohitajika; na ijengeni nyumba, hata nyumba ya sala, nyumba ya kufunga, nyumba ya imani, nyumba ya kujifunza, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu;

120 Ili kuingia kwenu kuweze kuwa katika jina la Bwana; na kutoka kwenu kuweze kuwa katika jina la Bwana; kwamba salamu zenu zote zipate kuwa katika jina la Bwana, na kuinua mikono kwa Aliye Juu Sana.

121 Kwa hiyo, acheni mazungumzo yenu yasiyo na maana, vicheko na tamaa zenu zote zilizo mbaya, na majivuno na upuuzi wenu wote, na matendo yenu yote yaliyo maovu.

122 Chagueni mwalimu miongoni mwenu, na wote wasiwe wazungumzaji kwa wakati mmoja; bali azungumze mmoja na wengine wote wasikilize maneno yake, ili wote watakapokuwa wamezungumza wote wapate kujengana, na kwamba kila mmoja apate kuwa na nafasi sawa.

123 Jitahidini kupendana; acheni kutamani; jifunzeni kupeana kama injili inavyotaka.

124 Acheni kuwa wavivu; acheni kuwa wachafu; acheni kutafutana makosa; acheni kulala kupita inavyotakiwa; laleni vitandani mwenu mapema, ili msichoke; amkeni mapema, ili miili yenu na akili zenu zipate kutiwa nguvu.

125 Na zaidi ya yote, jivikeni wenyewe kwa kifungo cha hisani, kama vile joho, lililo kifungo cha ukamilifu na amani.

126 Ombeni daima, wala msikate tamaa, hadi nitakapokuja. Tazama, na lo, naja haraka, niwakaribishe kwangu. Amina.

127 Na tena, utaratibu wa nyumba uliotayarishwa kwa ajili ya urais wa shule ya manabii, iliyoanzishwa kwa ajili ya mafundisho yao katika mambo yote yaliyo muhimu kwao, hata kwa maofisa wote wa kanisa, au katika maneno mengine, wale walioitwa kwenye huduma katika kanisa, kuanzia makuhani wakuu, hata chini kwa mashemasi—

128 Na huu ndiyo utakuwa utaratibu wa nyumba ya urais wa shule: Yule aliyeteuliwa kuwa rais, au mwalimu, atasimama katika mahali pake, katika nyumba ambayo itaandaliwa kwa ajili yake.

129 Kwa hiyo, atakuwa mtu wa kwanza katika nyumba ya Mungu, katika mahala ambapo mkutano uliomo ndani ya nyumba utaweza kusikia maneno yake kwa usahihi na ufasaha, pasipo sauti kubwa.

130 Na wakati ajapo ndani ya nyumba ya Mungu, kwa kuwa yampasa kwanza kuwa katika nyumba—tazama, hii ni vizuri ili apate kuwa mfano—

131 Na ajitoe yeye mwenyewe katika sala kwa kupiga magoti mbele za Mungu, katika ishara na kumbukumbu ya agano lisilo na mwisho.

132 Na wakati mtu yeyote atakapoingia baada yake, mwalimu na asimame, na, akiinua mikono mbinguni, ndiyo, hata wima, amsalimu kaka yake au ndugu yake kwa maneno haya:

133 Wewe ni kaka au ndugu? Ninakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo, katika ishara au kumbukumbu ya agano lisilo na mwisho, agano ambalo kwalo ninakupokea wewe kuwa mshiriki mwenzangu, katika dhamira ambayo ni imara, isiyoondosheka, na isiyobadilika, kuwa rafiki yako na kaka yako kwa neema ya Mungu katika kifungo cha upendo, kutembea katika amri zote za Mungu pasipo doa, na kwa shukrani, milele na milele. Amina.

134 Na yule ambaye atapatikana hastahili salamu hii hatakuwa na nafasi miongoni mwenu; kwani ninyi hamtaruhusu nyumba yangu ichafuliwe na mtu huyo.

135 Na yule aingiaye na kuwa mwaminifu mbele zangu, na ni ndugu, au kama wao wakiwa ndugu zake, watamsalimu rais au mwalimu wakiwa wamenyanyua mikono mbinguni, kwa sala hiyo hiyo moja na agano hilo, au kwa kusema Amina, katika ishara hiyo hiyo.

136 Tazama, amini ninawaambia, huu ndiyo utaratibu kwenu kwa kusalimiana katika nyumba ya Mungu, katika shule ya manabii.

137 Nanyi mmeitwa kufanya hivi kwa sala na kwa shukrani, kama Roho atakavyonena katika shughuli zenu zote katika nyumba ya Bwana, katika shule ya manabii, ili ipate kuwa mahali patakatifu, na hema takatifu ya Roho Mtakatifu kwa kuwajenga ninyi.

138 Na hamtampokea yeyote miongoni mwenu katika shule hii isipokuwa amekuwa safi kutokana na damu ya kizazi hiki;

139 Na atapokelewa kwa ibada ya kutawadha miguu, kwani ni kwa madhumuni haya ibada hii ya kutawadha miguu ilianzishwa.

140 Na tena, ibada ya kutawadha miguu itahudumiwa na rais, au mzee kiongozi wa kanisa.

141 Itaanza kwa sala; na baada ya kupokea mkate na divai, atajifunga yeye mwenyewe kulingana na utaratibu uliotolewa katika mlango wa kumi na tatu ya ushuhuda wa Yohana juu yangu mimi. Amina.