Liahona
Kusoma Polepole: Kumwona Mwokozi katika Maandiko
Januari 2024


“Kusoma Polepole: Kumwona Mwokozi katika Maandiko,” Liahona, Jan. 2024.

Kusoma Polepole: Kumwona Mwokozi katika Maandiko

Kuazima mtazamo huu kutoka katika sanaa kunatusaidia kumwona Yesu Kristo katika Kitabu cha Mormoni.

Picha
sanamu ya Maria akiwa ameshikilia mwili wa Yesu baada ya Kusulubiwa.

La Pietà, na Michelangelo

Ilimchukua Michelangelo zaidi ya mwaka mmoja kutengeneza La Pietà, sanamu ya kuvutia ya Maria akiwa ameshikilia mwili wa Yesu baada ya Kusulubiwa. Leonardo da Vinci alitumia muda mrefu zaidi, karibia miaka mitatu, kuchora kwa kupaka rangi picha maarufu ya Karamu ya Mwisho.

Kama ungetakiwa kukisia, ni muda mrefu kiasi gani ungesema kwamba mgeni katika makumbusho ya sanaa anapaswa kutumia—kwa wastani—ili kuangalia kila kazi ya sanaa?

Jibu ni sekunde 17, kulingana na utafiti mmoja.1

Fikiria: sekunde 17 kuangalia kazi moja ya sanaa ambayo msanii yawezekana ametumia miaka kadhaa kuitengeneza.

Inaweza kueleweka. Kuna mamia ya picha za rangi na sanamu katika makumbusho, na sisi ni watu wenye shughuli nyingi. Hivyo tunapitia kwa haraka haraka na kutazama vingi kadiri tuwezavyo. Kiuhalisia, tukiendeshwa na hofu yetu ya kukosa kitu fulani, tunaishia kukosa dhumuni hasa la sanaa ile—hisia na mawazo ya msanii aliyotaka sisi tuyapate. Tunapitisha macho yetu juu ya kila kipande katika makumbusho, lakini hakika hatuoni chochote kati ya hivyo. Basi tunaondoka kwenye jumba lile la makumbusho tukiwa tumechoka na hatujavutiwa. Yawezekana hata tukajiuliza ni kitu gani watu wanakiona katika sanaa hata hivyo—ukiwa umeshawishika, pengine, sanaa ni kwa watu waliosoma sana, na sio kwa kila mtu.

Kutazama Polepole

Ili kuelezea tatizo hili, majumba ya makumbusho ya sanaa ulimwenguni kote yanawahimiza wageni kufanyia kazi kitu wanachokiita “kutazama polepole.”2 Wanawaalika watu kuchagua kazi moja ya sanaa katika jumba la makumbusho ya sanaa, waridhike nayo, na kuichunguza kwa uangalifu kwa muda kidogo—dakika 5 hadi 10. Kuitazama kutoka pembe tofauti tofauti. Isogelee karibu ili kugundua umahiri wake. Rudi nyuma kidogo na uitazame yote kama ilivyo. Wakati mwingine, wageni hata wameambiwa wasisome alama za maelezo ya ufafanuzi ya jumba la makumbusho ambayo yanaiainisha kazi hiyo ya sanaa—angalau, siyo hadi wamekuwa na nafasi ya kuunda maoni yao binafsi na kufanya ugunduzi wao wenyewe.

Kutazama polepole kumebadilisha uzoefu wa majumba ya makumbusho ya sanaa kwa watu wengi. Baadhi ya watu ambao katu hawakujifikiria wenyewe kuwa ni wapenzi wa sanaa wamekuwa wapenzi kuhusu sanaa. Wanapata kujiamini kwamba wanaweza kugundua maana katika kazi yoyote ya sanaa, na wanapata shangwe katika kile wanachokigundua. Wanajifunza kwamba hawahitaji shahada ya chuo kikuu katika historia ya sanaa ili kuvutiwa na sanaa, wanahitaji tu kupunguza mwendo na kuipa sanaa nafasi ili ifanye kile ilichoumbwa kukifanya.

Je, ingewezekana kanuni hiyo hiyo ikatumika katika kusoma maandiko—kwa mfano kujifunza kwetu Njoo, Unifuate ya Kitabu cha Mormoni mwaka huu?

Tunajua kwamba Kitabu cha Mormoni, kama ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo, kiliandikwa kwa madhumuni ya kuimarisha imani yetu katika Mwokozi (ona 1 Nefi 6:4). Tunajua kwamba kiliandikwa na manabii waliokuwa na maongozi ya Mungu, mahususi kwa ajili ya siku yetu (ona, kwa mfano, Mormoni 8:35). Tunajua kwamba manabii wa kale ambao waliandika Kitabu cha Mormoni walifanya hivyo kwa dhabihu kubwa kwao binafsi. Hata tu mchakato wa kuchonga maneno kwenye mabamba ya mabati ilikuwa ya maumivu na jasho jingi (ona Yakobo 4:1). Na baadhi yao walihatarisha maisha yao ili kuhifadhi kumbukumbu hiyo ili itufikie sisi leo (ona Mormoni 6:6; Moroni 1).

Bado nyakati zingine, katika kuwa kwetu na shughuli nyingi, tunaharakisha katika kusoma kwetu Kitabu cha Mormoni. Pengine tunapitia kwa haraka mistari michache kwenye kifungua kinywa chetu au tukiwa njiani kwenda kazini. Yawezekana tukapitisha macho yetu juu ya kila neno katika sura, lakini siyo mengi ya hayo maneno yamezama ndani. Siyo kila wakati, lakini nyakati zingine, tunakifunga kitabu ua aplikesheni tukihisi hakuna tofauti ya hisia na wakati tulipoanza.

Kusoma Polepole

Kama kazi ya sanaa inastahili kusifiwa kupitia kutazama polepole, yawezekana Kitabu cha Mormoni kinastahili “kusoma kwetu polepole” Hilo si lazima limaanishe kusoma kwetu maandiko kuchukuwe muda mrefu zaidi, ni kwamba tu tunaweza kufaidika kwa kubadili muda tunaotumia. Badala ya kuharakisha kumaliza sura nzima, pengine kujifunza kwetu leo kunaweza kufokasi kwenye mistari mitatu au minne tu Lakini hakika tunajizamisha wenyewe kwenye mistari hiyo. Tunagundua maelezo ya kina, maneno na vifungu vya maneno. Tunatafakari kwa nini kila kimoja kinaweza kuwa muhimu—je, kinanifundisha kitu chochote kuhusu Mwokozi? Je, kinaongeza upendo wangu Kwake na imani yangu katika Yeye? Je, kuna kitu chochote anachotaka mimi nijue?

Kusoma polepole kunaniruhusu mimi kujua vitu katika Kitabu cha Mormoni ambavyo vinginevyo tusingeviijua. La muhimu zaidi, inaweza kutusaidia sisi kumwona Mwokozi mara kwa mara katika hiki kitabu ambacho kimeandikwa kushuhudia juu Yake. Kusoma polepole ni njia ya kufungua macho, akili na mioyo yetu kwa ushuhuda wenye nguvu wa Kitabu cha Mormoni juu ya Yesu Kristo. Kazi ya sanaa yenye maongozi ya kiungu, tunapotoa muda wetu ili kuiangalia, inaweza kuwa yenye kubadilisha maisha. Katika hata njia ya kina zaidi, kumwona Mwokozi katika maandiko kunaweza kwa kina kushawishi mawazo yetu na hisia—na, kama matokeo yake, maisha yetu.

Kwa mfano, kama unasoma 1 Nefi sura ya 1. Umakini wako unakamatwa na mstari wa 6, hivyo unapunguza mwendo na unabaki hapo kwa muda. Yawezekana ukavutiwa na “nguzo ya moto” Lehi aliyoiona ambayo “ilitua juu ya mwamba.” Hiyo ni tabia isiyo ya kawaida kwa moto. Hilo lingeweza kumaanisha nini? Mawazo yako yangeweza kwenda kwenye nguzo nyingine za moto zilizotajwa katika maandiko (tanbihi ingeweza kukusaidia hapo). Unaweza kutafakari ni kwa nini uwepo wa Bwana mara nyingi unalinganishwa na moto. Hilo linasema nini kuhusu Yeye? Je, Yeye amewahi kuwa kama nguzo ya moto katika maisha yako?

Ni mengi ya kufikiria kuhusu hilo. Na hata hujamaliza mstari huo bado.

Ipo, ndiyo, thamani ya kusoma Kitabu cha Mormoni chote kwa haraka. Inaweza kutusaidia kujifunza hadithi yote na kuchagua dhima zinazojirudia. Lakini kuna mengi ya kujifunza kuhusu Yesu Kristo katika maelezo ya kina ya Kitabu cha Mormoni na nyakati zingine njia bora zaidi ni kupunguza mwendo na kutazama kwa makini.

Nefi alisema juu ya maneno aliyoandika katika Kitabu cha Mormoni, “Maneno haya … ni maneno ya Kristo, na amenipa mimi; na … Kristo atayaonyesha kwenu, kwa nguvu na utukufu mkuu, kwamba ni maneno Yake” (2 Nefi 33:10–11). Hupaswi kuwa msomaji mzoefu kuyapata maneno ya Mwokozi katika Kitabu cha Mormoni. Unapaswa tu kupunguza mwendo na kukipa Kitabu cha Mormoni nafasi ya kufanya kile kilichoumbwa ili kukifanya kuijenga imani yako katika Yesu Kristo.

Muhtasari

  1. Ona Trent Morse, “Slow Down, You Look Too Fast,” ARTnews, Apr. 1, 2011, artnews.com.

  2. Ona “Slow Art Day,” slowartday.com/about.