Liahona
Hazina Zangu Kuu
Januari 2024


“Hazina Zangu Kuu,” Liahona, Jan. 2024.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Hazina Zangu Kuu

Kujifanya kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho kuliniongoza kwenye ubatizo na maisha mapya katika injili ya Yesu Kristo.

Picha
mikono inaandaa chakula, na kitabu cha Mormoni kimelala pembeni

Kielelezo na Ben Simonsen

Kazi yangu kama mpishi ilikuwa ndio maisha yangu. Nilisafiri ulimwenguni nikipika katika mahoteli ya kifahari na meli za fahari. Nilijiunga na timu ya wapishi wakubwa ambao walikuwa wameshinda mashindano ya kimataifa ya mapishi.

Mara moja, nilikuwa mbali na nyumbani kwa miaka mitatu. Mama yangu angenipigia mara kwa mara akiwa katika kulia na kuniambia nirudi.

Siku moja nikiwa Milan, Italia, mahali nilipoweka mkataba wa kupika katika hoteli nilikutana na wamisionari kwenye kituo cha treni ya chini ya ardhi chenye watu wengi. Waliniambia kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na wakashiriki na mimi baadhi ya kanuni za injili. Hususani nilifurahia kile walichonifundisha kuhusu familia.

Wamisionari walinipa nakala ya Kitabu cha Mormoni na wakaniomba nisali juu ya kitabu hicho. Pia walinipa kipeperushi chenye maelekezo ya jinsi ya kusali.

Nilirudi hotelini kwangu kwa furaha, nikaingia chumbani mwangu, nikasali na kuanza kusoma. Kadiri nilivyosoma zaidi kitabu cha Mormoni, ndivyo nilivyotamani kusoma zaidi. Bahati mbaya, kazi ilinizuia kuwaona wale wamisionari tena. Mkataba wangu na hoteli yangu ulipomalizika nilirejea nyumbani Bari, nilianza kupika kwa ajili ya hoteli nyingine.

Siku moja kwenye mgahawa wa hoteli yangu, mpishi mwingine, kwa sababu isiyo sahihi alijaribu kupanga miadi na baadhi ya wahudumu wa kike wa hapo. Alikasirika kwa sababu wahudumu wale, ambao walikuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, walikataa kwenda kwenye miadi na yeye.

Nikiwakumbuka wamisionari wale niliokutana nao huko Milan, nilimwambia yule mpishi kwamba wale wahudumu walikuwa na haki ya kumkatalia.

“Kwa hiyo, na wewe ni Mmormoni pia?“ aliuliza.

Kwa sababu nilipenda kanuni walizonifundisha na kwa sababu nilihisi nilikuwa na haki katika kuwatetea wale wahudumu, nilijibu, “Ndiyo.”

Wakati mwingine yule mpishi alipowaona wale wahudumu, aliwaambia kwamba mimi nilikuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho. Walifurahia. Tulipokusanyika kwa ajili ya chakula cha mchana, walianza kuniuliza maswali kuhusu Kanisa huko Milan. Niliwaambia kuhusu jiji na kwamba nilikutana na wamisionari huko. Chakula chetu kilipofika, nilikamata glasi ya mvinyo mezani.

“Unafanya nini hapa unakunywa mvinyo?” mmoja wa wale wahudumu aliuliza.

“Kuna kitu chochote kibaya katika hilo?” Nilisema.

“Je, wewe kweli unahudhuria kikamilifu?” mwingine aliuliza.

“Kwa namna gani?” Nilisema.

“Ulivaaje siku ulipobatiwa?” waliniuliza.

“Sikumbuki,” niliwaambia. “Nilikuwa na mwezi mmoja tu.”

Walikasirika sana kwa sababu walifikiri nilikuwa nawatania. Niliwahakikishia kwamba sikuwa nawatania. Nilikubali kwamba sikuwa muumini wa Kanisa, lakini niliwaambia kwamba nilikipenda Kitabu cha Mormoni na kanuni za injili nilizojifunza. Kisha nikawauliza jinsi gani ningeweza kujifunza zaidi kuhusu kanisa lao.

Wale wahudumu punde wakanitambulisha kwa wamisionari. Hawakuamini wakati nilipomaliza majadiliano na wale wamisionari na kubatizwa.

Picha
mama na baba na wavulana wawili

Picha za familia kwa hisani ya mwandishi

Kwa ubatizo wangu, maisha yangu yalibadilika. Nilijifunza kwamba huwezi kuwa na mguu mmoja ulimwenguni na mwingine katika injili. Nilijifunza kwamba kazi siyo kitu muhimu zaidi katika maisha. Nilijifunza kwamba Bwana na familia yangu vinakuja kwanza. Mwishowe, nilielewa ile huzuni mama yangu aliyoihisi katika kutokuwepo kwangu, na nikamwomba anisamehe.

Nikaacha kusafiri ulimwenguni, nikaoa katika Hekalu la Bern Uswisi, nikaanzisha familia, nikapata kazi ya kupika kwenye hospitali ya mjini hapo, mahali ambapo nilitumia vipaji vyangu kuwasaidia watu walio wagonjwa wapone. Sasa mimi ni kiongozi katika idara ya rasilimali watu katika hospitali hiyo. Kufanya kazi sehemu moja kunanipa mimi muda wa kujitolea kwa familia yangu na miito yangu Kanisani.

Kuanzia siku niliyoenda hekaluni na kupokea endaumenti yangu miaka miwili baada ya ubatizo wangu, nimependa utakatifu wa hekalu na kazi za hapo. Baba yangu alipofariki miaka minne baadaye, nilivunjika moyo. Alikuwa shujaa wangu. Asante kwa injili ya Yesu Kristo, ninajua kwamba bado anaishi.

Nilipoingia chumba cha selestia baada ya kufanya kazi kwa niaba yake, nilihisi kumbatio lake. Wakati ule, nilijua kwamba baba yangu ameipokea injili na upendo wa Bwana alionao kwa watoto Wake.

Sisi Watakatifu wa siku za Mwisho tunayo baraka ya kujua injili ya kweli. Nashukuru kwa jinsi gani imebadilisha maisha yangu. Injili ndipo mahali ninapopata furaha ya kweli. Injili na familia yangu ndizo hazina zangu kuu.