2023
Kuwa Mwenye Kujitegemea
Desemba 2023


Ujumbe wa Kiongozi wa Eneo

Kuwa Mwenye Kujitegemea

Familia yangu ilikuwa ikipitia baadhi ya changamoto za matumizi yasiyo mazuri ya fedha na kukabiliana na gharama zisizotarajiwa, licha ya jitihada zetu zote.

Katika siku moja ya Sabato, dada mmoja alishiriki changamoto sawa na hiyo na kwa pamoja tulishauriana na mtaalamu wa maswala ya kujitegemea. Tulijisajili kwa ajili ya Programu ya Kujitegemea katika maswala ya Pesa Binafsi. Tulifuata wito wa Mzee David A. Bednar kwamba “kupiga hatua ni zoezi la imani”1 na kwamba hatua muhimu sana katika kujitegemea ni kuanza. Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba “Bwana hupenda jitihada’’2 na aliahidi kwamba “Bwana atakuza juhudi zetu ndogo lakini zilizo endelevu.”3

Safari yetu ndiyo ilikuwa imeanza; mume wangu, kijana wetu mkubwa pamoja na mimi tulijiunga katika programu hiyo pamoja na waumini wengine tisa. Ilikuwa ni dhabihu kweli. Tulikuwa na mikutano ya mtandaoni kila Jumamosi saa 12 asubuhi na kila muumini alihakikisha kwamba mwenza wake wa kumsaidia kutenda alihudhuria.

Washiriki wa kundi letu walikuwa maridadi kweli kwa majibu yao ya hatua walizochukua kwa kipindi cha wiki nzima. Mazoezi ya tathmini ya juhudi zetu na katika kutunza ahadi yalifanyika kwa dhati na kutolewa ripoti. Ramani ya usimamizi wa mafanikio wa fedha ni safari ya kiroho. Kupitia uaminifu na uwazi katika kushiriki uzoefu katika kundi, urafiki na uhusiano chanya ulijengeka. Kama wafuasi wa Yesu Kristo, kwa uaminifu tulihudumiana katika mahitaji ya kimwili na kiroho, tukiongozwa na upendo wa Mungu.

Kama familia, tulipokea miujiza kupitia programu hii, na imani yetu katika Mwokozi Yesu Kristo iliongezeka na pia tulifanya mabaraza ya familia kila mara.

Hapa tulishauriana juu ya mahitaji ya kiroho na kimwili na dhamira yetu ya kuwa wenye busara na watumishi waaminifu.

Kujitegemea ni kanuni ya wokovu na ya kuonesha imani kwa Yesu Kristo katika mapato yetu, familia au mtu binafsi. Programu hii ya kanisa ni kwa waumini wote, kama Bwana alivyotangaza (M&M 104:15–17) “Ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu … kwani dunia imejaa, na viko vya kutosha na kubaki.”

Urais wa Kwanza ulitangaza, “Ufunuo huu ni ahadi kutoka kwa Bwana kwamba atatujalia baraka za kimwili na kufungua milango ya kujitegemea ambao ni uwezo wa sisi kujikimu kwa vitu vya msingi vya maisha kwa ajili yetu na wanafamilia.”4

Kujitegemea ni amri, na baraka za kimwili na kiroho ni sawa kwa Mungu: “Kwa hiyo, amini ninawaambia kwamba mambo haya yote kwangu mimi ni ya kiroho” (M&M 29:34).

Baba wa Mbinguni anatutegemea sisi tutii amri Zake: “Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru” (Ibrahimu 3:25).

Mzee Jeffrey R. Holland alifundisha, “Bwana huwabariki wale wanaotaka kuwa bora, ambao hukubali amri na kujaribu kuzitii….Atakusaidia utubu, ufanye marekebisho, utengeneze chochote unachotaka kutengeneza na usonge mbele. Punde utafikia mafanikio unayoyatafuta.”5

Mchoro unaoonesha ramani ya usimamizi wenye mafanikio wa fedha--nyumba--inayochochea sana safari yetu ya kiroho. Msingi wa nyumba ni imani katika Yesu Kristo, umoja na mwenza na dhamira ya kujitegemea, wakati kuta zinazoshikilia ni kazi na bajeti.

Hatua ya kwanza ni kulipa zaka na matoleo, pili ni kulinda familia yako dhidi ya magumu, tatu ni kufutilia mbali madeni, nne ni kutunza na kuwekeza kwa ajili ya baadaye na bati ambalo ni hatua ya tano, ni kuendelea kutoa na kubariki wengine. “Mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu” (Mosia 2:17). Tunapaswa kuwafundisha watoto wetu kanuni hiyo hiyo ikijumuisha kuwasaidia masikini (Mosiah 4:26) na kusonga mbele katika Kristo (2Nefi 31:20).

Tunapofanya kazi, tunaondoa utegemezi wetu wa kimwili kwa wengine kwani “chochote kinachotusababisha tuwe tegemezi kwa mwingine kwa ajili ya maamuzi au rasilimali ambazo tunaweza kujitafutia wenyewe hutudhoofisha kiroho na huzuia ukuaji wetu kufikia kile ambacho mpango wa injili umenuia sisi tuwe.”6

Kutoa zaka na dhabihu ni kanuni ya imani katika Mwokozi na huambatana na baraka zilizoahidiwa pale tunapotii kwani “hufungua madirisha ya mbinguni hata isiwepo nafasi ya kutosha” (Malaki 3:10).

Matoleo ya mfungo hutumika kuwasaidia masikini na wenye mahitaji. Tunapotoa matoleo ya mfungo kwa uaminifu, uwezo wetu wa kujitegemea huongezeka. Lengo la kujitegemea kimwili na kiroho ni kujiinua sisi wenyewe juu ili tuweze kuwainua wengine wenye mahitaji.”7

Kuwa mwenye kujitegmea huhitaji mtu kufanya mabadiliko kwenye mazoea na tabia, na kuvaa jukumu binafsi. Ingawa hili linaweza kuwa changamoto mwanzoni, imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake utamsaidia mtu huyo kupitia mabadiliko haya kwa amani. Kadiri mtu anavyozidi kujaribu, kufanya mabaraza ya familia, kushauriana na Bwana na kutafuta msaada Wake, atapata uwezo wa kuhimili.

Katika Mosia 3:9, Mfalme Benjamini anafundisha kuhusu kumshinda “mwanadamu wa asili,” ambaye anaweza kutupeleka kwenye madeni na msongo wa kifedha. Manabii wametushauri tuepuke madeni na tuishi ndani ya uwezo wetu. Tunaposoma Kitabu cha Mormoni na kutumia kanuni zake, tutatafuta kufuata “ushawishi wa Roho Mtakatifu” tutawezeshwa kwa nguvu ya Upatanisho kuwa imara wakati wa dhiki. “Na tena, amini ninawaambia, juu ya madeni yenu—tazama, ni mapenzi yangu kuwa mlipe madeni yenu yote” (M&M 104:78).

Tuapowasiliana na Baba yetu wa Mbinguni kupitia sala, tuzungumze Naye kuhusu majaribu yetu, uzoefu na baraka.

“Baba yetu wa Mbinguni husikiliza maombi ya watoto Wake duniani kote wakiomba chakula ili wale, nguo ili wafunike miili yao na heshima ambayo huja kutokana na uwezo wa kujikimu wenyewe.”8

Ninaomba Roho Mtakatifu atuongoze ili tutii amri ya Bwana ya kuwa wenye kujitegemea.

Tanbihi

  1. My Foundation for Self-Reliance [2016], 7.

  2. Russell M. Nelson, in Joy D. Jones, “Wito Uliotukuka Zaidi,” Liahona, Mei 2020, 16.

  3. Christopher W. Waddell “Palikuwa na Chakula”, Liahona, Novemba 2020.

  4. My Foundation for Self-Reliance, 3.

  5. Jeffrey R. Holland “Kesho Bwana Atafanya Miujiza miongoni Mwenu”, Liahona, Mei 2016.

  6. Dallin H. Oaks, “Repentance and Change”, Liahona, Novemba 2003.

  7. Robert D. Hales, “Kuzingatia moyoni mwetu na Kuweza kujitegemea Kiroho: Sakramenti, Hekalu, na Kujitolea katika Huduma,” Liahona, Mei 2012, 36.

  8. Henry B. Eyring, “Opportunities to Do Good”, Liahona, Mei 2011.