2023
Wakati wa Kihistoria pale Viongozi wa Imani mbalimbali nchini Kenya Wanapolikaribisha Kanisa
Desemba 2023


Kihistoria

Wakati wa Kihistoria pale Viongozi wa Imani mbalimbali nchini Kenya Wanapolikaribisha Kanisa

Viongozi kutoka jumuia ya kidini nchini Kenya walikaribishwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Nairobi mnamo Jumanne Mei 9, 2023. Mzee Thierry K. Mutombo na Mzee Ian S. Ardern, washiriki wa Urais wa Eneo, waliwakaribisha viongozi wa dini kutoka Uislamu, Hindu na imani za kikristo kwenye chakula rasmi cha mchana na matembezi ya wazi Kanisani.

Tukio lilifanywa kwa ushirirkiano na baraza la dini mbalimbali la Kenya (IRCK) na lilifanyika Kituo cha Kigingi cha Nairobi, mji mkuu wa taifa. IRCK inafikiria ushirikiano wa muda mrefu na Kanisa na wawakilishi walitaka kujionea wenyewe na kukutana na viongozi wa Kanisa na waumini.

Mzee Ian S. Ardern, mshauri wa pili katika urais wa Eneo la Kati, akizungumza kwa niaba ya Kanisa alisema, “ninafahamu kwamba kufurahia chakula pamoja ni njia nzuri ya kushinda vikwazo na kujenga madaraja, jambo ambalo sote tunataka tulifanye.” Aliendelea, “tunatumaini kupata kuwajua na hilo kamwe haliwezi kutokea kutokana na kusoma kuhusu ninyi. Kanisa lolote linatambulishwa vyema na waumini wake na hivyo ilikuwa muhimu kwetu kukusanyika na kujifunza juu ya kila mmoja na kumhusu kila mmoja. Kinachotuunganisha ni kikubwa zaidi ya tofauti zetu za kithiolojia zilivyo.”

Akizungumza kwa niaba ya baraza la dini mbalimbali la Kenya, Mchungaji Baba Joseph Mutie, Mwenyekiti wa IRCK alisema, “tunaye rafiki mpya, karibu kwenye familia ya IRCK, asante kwa dhihirisho lako la ukarimu na upendo katika kutukaribisha hapa leo.” Aliendelea, “sala yangu ni kwamba tutafanya kazi pamoja kama familia na tuone kile ambacho Mungu ametuita tukifanye pamoja.”

Mwenyekiti aliwauliza washiriki wengine wa IRCK mtazamo wao juu ya kuunga mkono ushirikiano na muunganiko wa karibu kwa Kanisa. Ilikubalika wazi kulijumuisha Kanisa katika njia yoyote iliyowezekana ya kusonga mbele.

“Hili ni jambo la kustaajabisha,” alisema Askofu John Warari wa Evangelical Alliance of Kenya. “Huu ni wakati ulioacha alama katika historia ya dini mbalimbali nchini Kenya,” alisema.

Kufuatia wasilisho la Mzee Ardern lililoonesha ushirikiano madhubuti wa Kanisa na dini zingine, kazi ya kibinadamu na kazi katika uhuru wa dini, Sheikh Abdullahi Abdi, Mwenyekiti wa jumuia ya Viongozi wa Kiislamu Kitaifa wa Kenya, NAMLEF, alisema, “Mzee Ardern alizungumza kutoka moyoni mwake kwa mapenzi, yeye ni Mkristo, Mimi ni Muislamu, angeweza kuwa anazungumza ndani ya msikiti, ni kwamba tu hakunukuu Quran. Tunakubaliana kikamilifu. Sisi sote kama watu wa Mungu lazima tufanye kazi pamoja kuokoa utu na kumtumikia Mungu, kama NAMLEF sisi tuko tayari kushirikiana nanyi, nitakuwa wa kwanza kuwaunga mkono’, alisema kwa shauku.

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linafikia kote nchini kushirikiana na makundi ya dini mbalimbali kwenye vipaumbele na changamoto zinazofanana. Kanisa linatafuta kuimarisha ushirikiano wake na IRCK nchini Kenya. Katika sherehe za mwaka za hivi karibuni za Pasaka na Eid al-Fitr ulikuwa ni wakati mzuri kukusanyika, kusherehekea, kukutana na kusambaza maelewano ya imani mbalimbali na kutazama uwezekano wa siku za baadaye.