2018
Tumaini huko Uholanzi
Oktoba 2018


Imani, Tumaini, na Neema—sehemu ya 3

Tumaini huko Uholanzi

Mwandishi anaishi New Jersey, Marekani

Grace ni msichana wa miaka 15 akiishi Uholanzi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Vita imeendelea kwa muda mrefu sana. Watu huko Uholanzi hawana chakula, na wanatumaini kwamba vita itaisha hivi karibuni.

Picha
Hope in Holland

Mwaka wa mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia ulikuwa ni mbaya zaidi kwa Uholanzi. Wanazi walichukua karibu kila kitu. Grace hakuweza kwenda shule. Hakukuwa na makaa kutia joto nyumba yao. Grace na familia yake walilazimika kula vitunguu vya mimea ya tulip ili kujikinga na njaa. Vilikuwa na ladha mbaya! Kibaya zaidi, Baba bado alikuwa ni mfungwa wa kivita.

Lakini tumaini lilikuwa angani. Watu walikuwa wakisema Wanazi walikuwa wakishindwa vita. Na mnamo Mei ya 1945, Wanazi walijisalimisha. Uholanzi hatimaye ilikuwa huru tena! Watu walisherehekea mitaani. Sasa Grace angeweza kwenda shuleni tena. Hakukuwa na wanajeshi wa kuwaogopa.

Jambo zuri zaidi, siku moja wakati Grace na kaka zake wakitembea kutoka shuleni, waliona bendera ya Uholanzi ikipepea mbele ya nyumba yao. Walijua kwamba hiyo ingemaanisha jambo moja tu.

“Baba yu nyumbani” Heber alisema kwa sauti.

Grace na kaka yake wakakimbilia ndani. Grace akaweka mikono yake kumzunguka baba yake na kumpa kumbatio kubwa. Baba yake naye akamkumbatia. Ilikuwa ya kupendeza sana kuwa na Baba nyumbani.

Punde baada ya hapo, vifurushi vya vyakula, nguo, na madawa vilianza kufika Uholanzi. Viongozi wa Kanisa huko Jiji la Salt Lake walituma misaada mingi kuwasaidia watu baada ya vita. Hata Grace alipata gauni jipya! Alikuwa amevaa gauni moja kwa miaka mitano, kwa hivyo alikuwa na furaha sana kupata linginge jipya.

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, Grace alikuwa na chakula cha kutosha. Urais wa misheni pamoja na serikali ya Uholanzi waliamua kuanzisha mradi wa kukuza viazi ili kupata chakula zaidi. Waumini wa kanisa walipanda viazi kwa wingi katika mashamba yaliyokuwa karibu yao. Majira ya kupukutika majani, wangekuwa na maelfu ya viazi kwa ajili ya kula.

“Tazama!” Grace alimwambia Baba, akionyesha mmea wa kiazi uliokuwa ukichipua. “Hatutakuwa na njaa tena!”

Baba aliitikia kwa kutikisa kichwa lakini hakutabasamu. Alisema, “Nilikuwa naongea na Rais Zappey. Aliniambia kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Ujerumani bado hawana chakula, kama vile ilivyokuwa kwetu. Hawapati msaada kutoka serikalini kama sisi.” Baba aliweka mikono yake kuzunguka mabega ya Grace. Rais Zappey ameniuliza kama tungeweza kutoa viazi vyetu kwa Watakatifu wa Ujerumani.”

“Tuwape viazi vyetu!” Grace alilia. Lakini Wanazi walitokea Ujerumani! Wanaweza kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, Baba, lakini bado ni Wajerumani.”

“Najua si rahisi,” Baba alisema. “Lakini wao pia ni watoto wa Mungu. Yeye anawapenda pia. Niliwasamehe kwa kunifanya mfungwa. Bwana anaweza kutusaidia sote kusamehe.”

Grace alimwangalia Baba yake. Alikuwa ni mtu jasiri aliyemjua, lakini hakujua kama alikuwa na ujasiri wa kuweza kusamehe kama yeye. Kisha akamkumbuka mmoja wa walimu wake shuleni wakati wa vita. Mwalimu wake alisema kwamba si kwamba Wajerumani wote walikuwa Wanazi, na si wanajeshi wote wa Nnazi walikuwa wabaya. Na sasa wavulana na wasichana huko Ujerumani walikuwa hawana chakula kama vile Grace alivyokuwa.

Grace akavuta pumzi ndefu. “Naelewa,” akasema. “Acha tuwapatie viazi vyetu.”

Baba alimkumbatia na kutabasamu. “Wewe ni msichana jasiri. Hiki si kitu rahisi kufanya. Lakini sisi ni wafuasi wa Yesu Kristo, vivyo hivyo kaka zetu na dada zetu wa Kijerumani.”

Grace alitabasamu. Hisia za hasira moyoni mwake zikayeyuka, na alihisi amani na utulivu. Angeweza kuwasamehe Wajerumani. Na Yesu angeweza kumsaidia kuwapenda pia.