2021
Mteja Wangu au Wito Wangu?
Septemba/ Oktoba 2021


Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Mteja Wangu au Wito Wangu?

Kadiri nilivyojitahidi kutekeleza wajibu wangu wa kikuhani, Bwana alinionyesha kuwa Alikuwa anafahamu hali yangu ya kiuchumi.

Picha
briefcase

Picha kutoka Getty Images

Wakati nilipoitwa kama rais wa akidi ya wazee wa ukuhani mnamo 2000, wazee saba tu ndio walikuwa wanahudhuria mkutano wa ukuhani. Pia, tulikuwa hatufanyi kazi nzuri ya kufundisha nyumbani—kwa sasa kuhudumia—kutembelea.

Nilijua tulikabiliana na changamoto kubwa kuwahamasisha wazee kusonga mbele. Kwa hiyo, kwa kuanzia, tuliamua kutambua majukumu na kuongeza usimamizi.

Kwa sababu ni wakili niliyejiajiri, nasafiri sana. Nina kazi nyingi, lakini nilitaka kutimiza majukumu yangu ya ukuhani.

Siku moja, nilisafiri kwa basi hadi mji mwingine kufuatilia mteja. Kwa sababu hali yangu ya kiuchumi ilikuwa ngumu, nilitumaini kwamba mteja wangu angekubali kunilipa kabla ya kazi.

Njiani kuelekea kupanda basi, niliamua kwenda kuwaona baadhi ya washiriki wa akidi na kuwahamasisha kutembelea familia zao. Wengine walikuwa wamesahau lakini walijitolea kufanya hivyo. Wengine walijitolea kutimiza matembezi yao wiki hiyo.

Nilishangazwa na kujitoa kwao kiasi kwamba niliamua kuwatembelea na kuwatia moyo washiriki wengine wa akidi. Kabla sijafahamu, ilikuwa mchana adhuhuri. Kwa hiyo, badala ya kuondoka mjini, niliamua kwenda ofisini kwangu kuipitia kesi ya mteja.

Kwa mshangao wangu, nilipofika ofisini kwangu, mteja wangu alikuwa amesimama nje na mtu mwingine. Nilimweleza mteja wangu kwamba nilikuwa karibu kuanza kuipitia kesi yake na ningekuwa na ripoti yake siku inayofuata. Alisema alikuwa amekuja kunitambulisha kwa mteja mpya. Baada ya rafiki yake na mimi kuongea, tulikubaliana kiasi cha malipo yangu kumsaidia kutatua tatizo lake la kisheria. Mara, ghafla, mteja wangu alijitolea kunilipa malipo ya awali.

Kwangu, huo ulikuwa muujiza. Baba wa Mbinguni alijua nilikuwa najitahidi kuwa mwaminifu Kwake. Alijua pia mahitaji yangu. Amenibariki katika njia nyingi kwa miaka mingi, ila kwa wakati huu baraka zake zilikuja kwa njia ya kifedha. Alitimiza maneno Yake katika maandiko kwa wale wanaomtumikia Yeye: “Tafuteni kwanza ninyi ufalme wa Mungu, na utakatifu wake; na vitu vyote mtaongezewa” (Mathayo 6:33).

Na akidi yetu ya wazee? Bwana alitubariki kadiri tulivyosonga mbele na moyo wetu wa umoja. Mafundisho yetu ya nyumbani yalipanda hadi asilimia 100, na mahudhurio ya ukuhani yaliongezeka hadi wazee 35 waaminifu.

Nashuhudia kwamba sote tunaweza kuwa vyombo katika kazi ya Bwana na kupata furaha na baraka katika kumtumikia Yeye kwa kuwatumikia wengine.