2022
Kupokea Endaumenti Yako
Septemba 2022


Njia Yangu ya Agano

Kupokea Endaumenti Yako

Endaumenti ni fursa takatifu inayotolewa kwa waumini wote wa kanisa wanaostahili na waliojitayarisha wenye miaka angalau 18 na walio tayari kuipokea.

Kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni baraka maalum. Kupitia injili ya urejesho ya Yesu Kristo, tunao utimilifu wa injili ya milele. Tunaweza kujifunza “kweli zilizo wazi na za thamani”1 ambazo zinahitajika kwa ajili ya wokovu wetu. Katika maandiko, tunajifunza kwamba “haiwezekani kwa mwanadamu kuokolewa katika ujinga” (M&M 131:6). Mkombozi wetu alisisitiza kwamba uzima wa milele ni kumjua Mungu wa kweli pekee—Baba Yetu wa Mbinguni na Yeye—Yesu Kristo. Moja ya njia za uhakika za kumjua Mwokozi wetu na Baba yetu wa Mbinguni ni kupitia kupokea endaumenti katika mahekalu matakatifu.

Katika programu ya Njia Yangu ya Agano, tunasoma: “Endaumenti ya hekaluni ni zawadi ya baraka takatifu kutoka kwa Mungu kwa kila mmoja wetu. Endaumenti inaweza kupokelewa katika njia Yake pekee na ndani ya hekalu Lake takatifu. Baadhi ya vipawa unavyovipokea kupitia endaumenti ya hekaluni ni pamoja na:

  • “Ufahamu mkubwa wa malengo na mafundisho ya Bwana.

  • “Nguvu ya kutenda yote ambayo Mungu hututaka tufanye.

  • “Mwongozo wa kiungu na ulinzi wakati tunapoomtumikia Bwana, familia zetu na wengine.

  • “Ongezeko la tumaini, faraja na amani

  • “Baraka zilizoahidiwa sasa na milele.”

Endaumenti ni fursa takatifu inayotolewa kwa waumini wote wa kanisa wanaostahili na waliojitayarisha wenye miaka angalau 18 na walio tayari kuipokea. Ni muhimu kuwa mwenye kustahili, ni muhimu kuwa tayari, ni muhimu kujiandaa. Ninakumbuka kile nilichokifanya ili kuwa mwenye kustahili, tayari na niliyejiandaa kwa ibada hii takatifu: kujitahidi kutii amri, kutubu kila siku, maombi ya kila siku, kujifunza maandiko kila siku, kutegemea kikamilifu kwenye upatanisho, kuhudhuria darasa la maandalizi ya hekaluni na kusoma mahubiri kuhusu hekalu.

Miezi michache kabla ya kwenda kutumikia misheni yangu, mimi pamoja na familia yangu tulikuwa na baraka mbili za kuunganishwa hekaluni na kupokea endaumenti zetu katika siku hiyo hiyo. Kumbukumbu hiyo daima itabakia ya thamani moyoni mwangu. Hatimaye nilipoingia hekaluni, kwa shangwe nikishikilia kibali changu cha hekaluni, nikijua nilikuwa nimekubaliwa kwa Bwana, kulikuwa na nuru ndani mwa nafsi yangu!

Rais Russell M. Nelson ametukumbusha kwamba “Kila shughuli, kila somo, yote tufanyayo Kanisani, huelekeza kwa Bwana na nyumba Yake takatifu. Juhudi zetu za kutangaza injili, kuwakamilisha watakatifu na kuwakomboa wafu yote huongoza hekaluni. Kila hekalu takatifu husimama kama ishara ya uumini wetu ndani ya Kanisa, kama ishara ya imani yetu katika maisha baada ya kifo na kama hatua takatifu kuelekea utukufu wa milele kwa ajili yetu na familia zetu”.2

Unapojiandaa kupokea endaumenti yako, utapata shangwe.

Muhtasari

  1. “Je, ni Kweli Zipi za Wazi na za Thamani Zilizorejeshwa na Kitabu cha Mormoni?”, Ensign, Januari 2020.

  2. Russell M. Nelson, “Personal Preparation for Temple Blessings”, Ensign, May 2001, 32.