Mkutano Mkuu
Kanuni ya Milele ya Upendo
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Kanuni ya Milele ya Upendo

Upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wa watoto Wake ni halisi. Yeye yuko kwa ajili ya kila mmoja.

Kanuni ya milele ya upendo inajidhihirisha kwa kuishi amri mbili kuu: Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.1

Nakumbuka majira yangu ya kwanza ya baridi nikiishi hapa Utah—theluji kila mahali. Nikitokea Jangwa la Sonoran, siku za kwanza nilifurahia, lakini baada ya siku chache, niligundua kwamba nilitakiwa kuamka mapema ili kuondoa theluji kwenye njia ya uani.

Siku moja, katikati ya dhoruba ya theluji, nikiwa natokwa jasho, kuondoa theluji, nilimwona jirani yangu akifungua gereji yake upande mwingine wa mtaa. Ni mzee kuliko mimi, hivyo nilifikiri ningeweza kumaliza haraka, ningemsaidia. Nikapaza sauti yangu, nikamuuliza, “Kaka, unahitaji msaada?”

Akatabasamu na kusema, “Asante, Mzee Montoya.” Kisha akatoa mashine ya kuondoa theluji kutoka kwenye gereji yake, akaiwasha, na ndani ya dakika chache, akaondoa theluji yote mbele ya nyumba yake. Kisha akavuka mtaa na mashine yake na kuniuliza, Mzee, unahitaji msaada?”

Kwa tabasamu nikajibu, “Ndiyo, asante.”

Tu tayari kusaidiana kwa sababu tunapendana, na mahitaji ya kaka yangu yanakuwa yangu na yangu yanakuwa yake. Bila kujali ni lugha gani kaka yangu anaongea au ni nchi gani anatokea, tunapendana kwa sababu sisi ni ndugu, watoto wa Baba mmoja.

Wakati uhudumiaji ulipotangazwa, Rais Russell M. Nelson alisema, “Tutatekeleza mfumo mpya, mtakatifu wa kuwatunza na kuwahudumia wengine.”2 Kwangu mimi, mtakatifu humaanisha njia ya kibinafsi zaidi, ya kina zaidi, sawa na ile ya Mwokozi: “Mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,”3 mmoja mmoja.

Haitoshi kuepuka kuwa kikwazo kwa wengine; haitoshi kuona wenye uhitaji barabarani na kuwapita. Acha tuchukue kila fursa kumsaidia jirani yetu, hata kama ndiyo mara ya kwanza na wakati pekee kukutana naye katika maisha haya.

Kwa nini upendo kwa Mungu ndiyo amri kuu ya kwanza?

Nafikiria ni kwa sababu ya kile Yeye humaanisha kwetu. Sisi ni watoto Wake, Yeye husimamia ustawi wetu, tunamtegemea Yeye, na upendo Wake hutulinda. Mpango Wake hujumuisha haki ya kujiamulia, hivyo, kuna uwezekano tukafanya baadhi ya makosa.

Yeye pia huruhusu tujaribiwe. Lakini ijapokuwa tunafanya baadhi ya makosa au kuingia majaribuni, mpango huu hutupatia Mwokozi ili tuweze kukombolewa na kurudi kwenye uwepo wa Mungu.

Majaribu katika maisha yetu yanaweza kututia shaka kuhusu utimizwaji wa ahadi ambazo tayari zimekwishatolewa kwetu. Tafadhali mtumainie Baba yetu. Yeye daima hutimiza ahadi Zake, na tunaweza kujifunza kile Yeye anataka kutufundisha.

Hata tunapofanya kile kilicho chema, mazingira ya maisha yetu yanaweza kubadilika kutoka kuwa mazuri hadi mabaya, kutoka furaha kwenda huzuni. Mungu hujibu maombi yetu kulingana na rehema na upendo Wake usiyo na mwisho na katika wakati Wake Mwenyewe.

  • Kijito ambacho Eliya alikunywa maji kilikauka.4

  • Upinde wa chuma wa Nefi ulivunjika.5

  • Mvulana alibaguliwa na kufukuzwa shule.

  • Mtoto aliyesubiriwa sana alikufa katika siku chache baada ya kuzaliwa.

Mazingira hubadilika.

Wakati mazingira yanapobadilika kutoka mazuri na chanya hadi mabaya na hasi, bado tunaweza kuwa na furaha kwa sababu furaha haitegemei mazingira bali mtazamo wetu juu ya mazingira hayo. Rais Russell M. Nelson alisema: “Furaha tunayohisi haichangiwi kwa kiasi kikubwa na mazingira ya maisha yetu isipokuwa chochote kinachohusiana na fokasi ya maisha yetu.”6

Tunaweza kukaa na kungojea mazingira kubadilika yenyewe, au tunaweza kutafuta na kuleta mazingira mapya.

  • Eliya alitembea hadi Zarepati, ambapo mjane alimpa chakula na maji.7

  • Nefi alitengeneza upinde wa mbao na kuwinda wanyama kwa ajili ya chakula.8

  • Mvulana alisikiliza na kuandika karibu na dirisha, na leo ni mwalimu wa elimu ya msingi.

  • Wanandoa wamekuza imani kubwa katika Mwokozi Yesu Kristo na kutumainia mpango wa wokovu. Upendo wao kwa ajili ya mtoto aliyesubiriwa kwa muda mrefu ambaye kwa ghafla alifariki ulikuwa mkuu kuliko huzuni yao.

Ninaposikia maswali “Baba wa Mbinguni, je, kweli upo? Na je, unasikia na kujibu sala ya [kila] mtoto?,”9 ninapenda jibu, Yeye amekuwepo, Yeye yupo, na Yeye daima atakuwepo kwa ajili yako na mimi. Mimi ni mwana Wake, Yeye ni Baba yangu, na mimi ninajifunza kuwa baba mzuri kama vile Yeye alivyo.”

Mke wangu na mimi daima tunajaribu kuwepo kwa ajili ya watoto wetu wakati wowote, na katika hali yoyote, na kwa njia yoyote. Kila mtoto ni wa kipekee, thamani yao kwa Mungu ni kubwa, bila kujali ni changamoto gani, dhambi, na udhaifu walionao, Mungu anawapenda wao, nasi vivyo hivyo.

Nilipopokea wito huu kama Kiongozi Mkuu mwenye Mamlaka, siku ya mwisho kabla ya safari yetu kuja Salt Lake, watoto wetu wote na familia zao walikuwepo pamoja katika nyumba yetu kwa ajili ya jioni ya familia nyumbani, ambapo tulionyesha upendo wetu na shukrani zetu. Baada ya somo, nilitoa baraka za kikuhani kwa kila mmoja wa watoto wetu. Kila mmoja alitokwa machozi. Baada ya baraka, mwana wetu wa kwanza alisema maneno ya shukrani kwa niaba ya kila mmoja juu ya upendo mkubwa tuliowaonyesha toka siku walipozaliwa hadi wakati ule.

Wabariki watoto wako, hata kama wana umri wa miaka 5 au 50. Kuwa nao; na kwa ajili yao. Ingawaje kukidhi mahitaji ni jukumu lililowekwa kupitia mpango mtakatifu, hatupaswi kusahau kushiriki muda wa furaha pamoja na watoto wetu.

Upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wa watoto Wake ni halisi. Yeye yuko kwa ajili ya kila mmoja. Sijui ni kwa namna ipi Yeye hufanya hivyo, lakini Yeye hufanya hivyo. Yeye na Mzaliwa Wake wa Kwanza ni wamoja katika kufanya kazi na utukufu wa Baba, “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”10 Wamemtuma Roho Mtakatifu kwetu kutuongoza, kutuonya, kutufariji pale inapohitajika.

Yeye alimwelekeza Mwanawe Mpendwa kuumba ulimwengu huu mzuri. Yeye aliwafundisha Adamu na Hawa na Akawapa wao haki ya kujiamulia. Amekuwa akiwatuma wajumbe kwa miaka na miaka ili kwamba tuweze kupokea upendo Wake na amri Zake.

Yeye alikuwepo kenye Kijisitu Kitakatifu kujibu swali la uaminifu la kijana Joseph na kumwita kwa jina lake. Yeye alisema: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”11

Ninaamini onyesho kuu la upendo wa Mungu kwa ajili yetu lilikuwa pale Gethsemane, ambapo Mwana wa Mungu aliye hai aliomba, “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”12

Nimeona kwamba sehemu ndogo ambayo ninaweza kuielewa ya Upatanisho wa Yesu Kristo huongeza upendo wangu juu ya Baba na Mwana Wake, na hupunguza nia yangu ya kutenda dhambi na kutotii, na huongeza utayari wangu wa kuwa bora na kutenda vyema.

Yesu alitembea bila uoga na shaka hadi Gethsemane, akimtumainia Baba Yake, akijua kwamba angetakiwa kupitia mateso. Alivumilia uchungu na kudhalilishwa kote. Alituhumiwa, kuhukumiwa, na kusulubishwa. Wakati wa uchungu na mateso msalabani, Yesu alifokasi kwenye mahitaji ya mama Yake na mwanafunzi Wake mpendwa. Alijitolea uhai Wake.

Siku ya tatu Alifufuka. Kaburi li tupu, Yeye anasimama mkono wa kuume wa Baba Yake. Wao wanatumaini tutachagua kuyashika maagano yetu na kurudi katika uwepo Wao. Hii hali ya pili siyo hali yetu ya mwisho; sisi si wa hii nyumba ya ulimwenguni, bali sisi ni watu wa milele tukiishi uzoefu wa muda.

Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yeye yu hai, na kwa sababu Yeye yu hai, watoto wote wa Mungu wataishi milele. Asante kwa dhabihu Yake ya upatanisho, tunaweza kuishi pamoja na Wao. Katika jina la Yesu Kristo, amina.