Mkutano Mkuu
Kweli ni Nini?
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Kweli ni Nini?

Mungu ni chanzo cha ukweli wote. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linakumbatia ukweli wote ambao Mungu anaufikisha kwa watoto Wake.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, asanteni kwenu nyote kwa kikao hiki cha kuvutia! Tokea mkutano wetu wa mwisho wa Aprili, tumeshuhudia matukio mengi ya ulimwengu, kuanzia ya kuhuzunisha hadi ya kustaajabisha.

Tunafurahishwa na ripoti ya mikutano mikubwa ya vijana inayofanyika kote ulimwenguni.1 Kwenye mikutano hii, vijana wetu wazuri wanajifunza kwambabila kujali kile kinachotokea katika maisha yao, nguvu yao kubwa inatoka kwa Bwana.2

Tunashangilia kwamba mahekalu zaidi yanajengwa kote ulimwenguni. Kwenye uwekaji wakfu wa kila hekalu, nyongeza ya nguvu za Mungu inakuja ulimwenguni ili kutuimarisha sisi na kupinga jitihada inayoongezeka ya yule adui.

Unyanyasaji unajumuisha ushawishi wa yule adui. Ni dhambi kubwa.3 Kama Rais wa Kanisa, nathibitisha mafundisho ya Bwana Yesu Kristo katika jambo hili. Hebu niwe wazi kabisa: aina yo yote ya unyanyasaji kwa wanawake, watoto, au mtu ye yote ni chukizo kwa Bwana. Yeye anahuzunika na mimi nahuzunika mtu ye yote anapoumizwa. Anaomboleza na sisi sote tunaomboleza kwa kila mtu anayekuwa mwathirika kwa unyanyasaji wa aina yo yote. Wale wnaoendeleza vitendo hivi vya kutisha sio tu wanawajibika kwenye sheria za mwanadamu bali pia watakabiliana na hasira ya Mwenyezi Mungu.

Kwa miongo kadhaa sasa, Kanisa limechukua hatua za kina kuwalinda- hasa -watoto dhidi ya unyanyasaji. Kuna misaada mingi kwenye tovuti ya Kanisa. Nawaalika kujifunza.4 Misaada hii imewekwa ili kuwalinda wasio na hatia. Ninawasihi kila mmoja wetu kuwa macho kwa ye yote ambaye anaweza kuwa katika hatari ya kunyanyaswa na kuchukua hatua ya haraka ya kumlinda. Mwokozi hawezi kuvumilia unyanyasaji, na kama wafuasi Wake, sisi pia hatuwezi kuvumilia.

Yule adui anazo mbinu nyingine za kusumbua. Miongoni mwa hizo ni jitihada zake za kuweka ukungu kati ya ukweli na kile kisicho kweli. Mafuriko ya taarifa yanayopatikana kwenye nje ya vidole vyetu, cha kushangaza, inafanya kuwa vigumu zaidi kuamua kile kilicho kweli.

Changamoto hii inanikumbusha juu ya tukio ambalo Dada Nelson na mimi tulilipata wakati tulipomtembelea mtu maarufu katika nchi ambayo kiasi kidogo tu cha watu walikuwa wamewahi kusikia juu ya Yesu Kristo. Huyu rafiki mpendwa mzee amekuwa mgonjwa sana. Yeye alituambia kwamba wakati wa siku zake nyingi akiwa kitandani, mara nyingi aliangalia darini na akijiuliza, “Kweli ni nini?”

Watu wengi duniani,”wamezuiliwa mbali na ukweli kwa sababu hawajui pa kupata ukweli huo.5 Watu wangetaka tuamini kwamba ukweli ni kadiri—ambavyo kila mtu anapaswa kujiamulia mwenyewe kile kilicho kweli. Imani kama hiyo ni matamanio tu kwa wale wanaodhani kimakosa kuwa hawatakuwa na uhusiano na Mungu.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, Mungu ni chanzo cha ukweli wote. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linakumbatia ukweli wote ambao Mungu anaufikisha kwa watoto Wake, iwe wamejifunza kutoka katika maabara za kisayansi au umepokelewa moja moja kwa ufunuo kutoka Kwake.

Kutoka kwenye mimbari hii leo na kesho, mtaendelea kuusikia ukweli. Tafadhali andikeni mihtasari ya mawazo yanayokuvutieni na yale yanayokuja akilini mwenu na kukaa moyoni mwako. Kwa sala mwombeni Bwana athibitishe kwamba kile ulichokisikia ni kweli.

Ninawapenda, kaka zangu na dada zangu wapendwa. Ninaomba kwamba mkutano huu utoe karamu ya kiroho mnayoitafuta. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.