Mkutano Mkuu
Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko

Tafuta pumziko kutokana na nguvu, kutokuwa na uhakika, na uchungu wa ulimwengu huu kwa kuushinda ulimwengu kupitia maagano yenu na Mungu.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, nashukuru kuwasabahi asubuhi hii tukufu ya Sabato. Daima mko katika mawazo yangu. Ninashamgazwa jinsi mnavyochipuka katika vitendo wakati wo wote mumwonapo mtu mwingine katika uhitaji. Ninashangazwa kwa imani na shuhuda zenu mnazoonyesha tena na tena. Ninalia juu ya maumivu yenu ya moyo, kukatishwa tamaa na wasiwasi unakuja juu yenu. Ninawapenda. Ninawahakikishieni kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, wanawapenda. Wanafahamu kwa ukaribu kabisa hali zenu, wema wenu, shida zenu, na sala zenu mwombapo msaada. Tena na tena, nina sali kwa ajili yenu muweze kuhisi upendo Wao.

Kutambua upendo Wao ni muhimu sana kama inavyoonekana kwamba kila siku tunashangazwa na habari za kutisha. Yawezekana umekuwa na siku ambapo ulitamani kuvaa pajama zako, ujikunje ndani ya mpira na umwombe mtu akuamshe wakati msukosuko huu wote umeisha.

Lakini, kaka zangu na dada zangu wapendwa, mambo mengi mazuri yako mbele yetu. Katika siku zijazo tutaona maonyesho makubwa zaidi ya nguvu za Mwokozi ambayo ulimwengu kamwe haujapata kuona. Kati ya sasa na wakati Yeye ajapo “kwa uweza na utukufu mkuu,”1 mapendeleo yasiyohesabika, baraka na miujiza kwa waaminifu.

Hata hivyo, kwa sasa sisi tunaishi katika wakati ambapo hakika ni mgumu zaidi katika historia ya ulimwengu. Ugumu na changamoto huwaacha watu wengi kujisikia kuzidiwa na kuchoka. Hata hivyo, zingatia tukio la hivi karibuni ambalo linaweza kutoa mwangaza juu ya jinsi wewe na mimi tunavyoweza kupata pumziko.

Wakati wa tukio la hivi karibuni la watu kuzuru Hekalu la Washington D.C , mjumbe mmoja wa kamati ya shughuli hiyo alishuhudia majibizano ya busara alipokuwa akiwasindikiza waandishi wa habari maarufu kadhaa kuzunguka hekalu hilo. Kwa namna fulani familia moja changa ikawa imejiunga katika ziara hii ya waandishi wa habari. Mtoa habari mmoja alikuwa akirudia rudia kuuliza kuhusu “safari” ya mhudumu wa hekalu anapokuwa anatembea tembea humu hekaluni. Yeye alitaka kujua kama safari za hekaluni humu ni ishara ya changamoto katika safari ya maisha.

Mvulana mdogo katika ile familia alidakia yale maongezi. Wakati kikundi kilipoingia katika chumba cha endaumenti, mvulana alionyesha kwa kunyoshea kidole madhabahu, mahali ambapo watu wanapiga magoti ili kufanya maagano na Mungu, na akasema, “ Oh, ile ni nzuri. Hapa ni mahali pa watu kupumzika kwa safari yao ya hekaluni.”

Nina shaka kama mvulana huyo alijua jinsi uchunguzi wake ilivyokuwa wa kina. Inawezekana hakuwa na wazo kuhusu uhusiano wa moja kwa moja kati ya kufanya maagano na Mungu hekaluni na ahadi ya ajabu ya Mwokozi:

“Njooni kwangu, ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, na mkajifunze kwangu; … nanyi mtapata pumziko nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”2

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, ninahuzunika kwa wale wanaoliacha Kanisa kwa sababu wanajisikia kuwa kuwa muumini kunahitaji mengi kupita kiasi kutoka kwao. Hawajagundua kwamba kufanya na kushika maagano kwa ukweli kunafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kila mtu anayefanya maagano katika visima vya ubatizo na hekaluni—na kuyashika—ameongeza upatikanaji wa uweza wa Yesu Kristo Tafadhali tafakari kuhusu ukweli huo wa ajabu!

Thawabu ya kushika maagano na Mungu ni uweza wa kimbingu- nguvu ambayo inatuimarisha sisi ili kuhimili majaribu, vishawishi, na maumivu yetu ya moyo vyema zaidi. Nguvu hii inarahisisha njia yetu. Wale wanao ishi sheria ya juu zaidi ya Yesu Kristo wanao uweza wa kufikia nguvu zake za hali ya juu zaidi. Hivyo, washika maagano wanayo haki ya aina maalumu ya pumziko ambalo huja kwao kupitia uhusiano wao wa kiagano na Mungu.

Kabla ya Mwokozi kujisalimisha mwenyewe kwenye mateso ya Getsemane na Kalvari, Alitamka kwa Mitume Wake, “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini furahini; Mimi nimeushinda ulimwengu.”3 Kisha, Yesu alimsihi kila mmoja wetu kufanya vivyo hivyo pale aliposema, “Mimi nataka kwamba na ninyi muushinde ulimwengu.”4

Wapendwa kaka na dada zangu, ujumbe wangu kwenu leo ni kwamba kwa sababu Yesu Kristo aliushinda huu ulimwengu ulioanguka na kwa sababu Yeye aliteseka kwa ajili ya kila mmoja wetu, wewe pia unaweza kuushinda huu ulimwengu uliojaa dhambi, wenye ubinafsi na mara nyingi wenye kuchosha.

Kwa sababu Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, alitukomboa sisi sote kutokana na udhaifu, makosa, na dhambi, na kwa sababu Yeye alipitia kila maumivu, wasiwasi na mzigo ambao utaupitia,5 basi unapotubu kwa dhati na kutafuta msaada Wake, unaweza kuinuka juu ya ulimwengu huu hatarishi wa sasa.

Unaweza kushinda mapigo ya kuchosha kiroho na kihisia ya ulimwengu huu, ikijumuisha majivuno, kiburi, hasira, uasherati, chuki, uchoyo, wivu na hofu. Licha ya usumbufu na upotoshaji ambao umetuzunguka, unaweza kupata pumziko la kweli—ilimaanisha utulivu na amani—hata katikati ya matatizo mengi ya kusumbua.

Ukweli huu muhimu unauliza maswali ya msingi matatu:

La kwanza, Inamaanisha nini kuushinda ulimwengu?

La pili, tunalifanyaje hilo?

Na la tatu, Je, ni kwa namna gani kuushinda ulimwengu kunabariki maisha yetu?

Inamaanisha nini kuushinda ulimwengu? Inamaanisha kushinda vishawishi vya kujali zaidi kuhusu mambo ya ulimwengu kuliko mambo ya Mungu. Inamaanisha kutumaini mafundisho ya Kristo zaidi kuliko falsafa za wanadamu. Inamaanisha kufurahia katika ukweli, kuukata udanganyifu, na kuwa “mfuasi mnyenyekevu wa Kristo.”6 Inamaanisha kuchagua kujiepusha na kitu cho chote kinachomfukuzia mbali Roho. Inamaaniisha kuwa tayari “kuachana” hata na dhambi tuipendeleayo.7

Sasa, kuushinda ulimwengu hakika hakumaanisha kuwa wakamilifu katika maisha haya, wala haimaanishi kwamba matatizo yako kichawi yatayeyuka—kwa sababu hayatayeyuka. Na haimaanishi kwamba wewe hautafanya makosa. Lakini kuushinda ulimwengu kunamaanisha kwamba uwezo wako wa kupinga dhambi utaongezeka Moyo wako utalainika imani yako katika Yesu Kristo inapoongezeka.8 Kuushinda ulimwengu inamaanisha kukua zaidi katika kumpenda Mungu na Mwanae Mpendwa kuliko kumpenda mtu mwingine ye yote au kitu cho chote.

Je, ni kwa jinsi gani tunaushinda ulimwengu? Mfalme Benyamini alitufundisha jinsi ya kufanya. Alifundisha kwamba “mwanadamu wa asili ni adui kwa Mungu” na atabaki hivyo milele “isipokuwa amekubali ushawishi wa Roho Mtakatifu, na kumvua mtu wa kawaida na kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana.”9 Kila wakati unapotafuta na kufuata ushawishi wa Roho, kila wakati unapofanya kitu chochote kizuri —mambo ambayo “yule mtu wa kawaida” asingefanya—wewe unaushinda ulimwengu.

Kuushinda ulimwengu siyo tukio ambalo hutokea katika siku moja au mbili. Inatokea maisha yote tunaporudia rudia kuyakumbatia mafundisho ya Kristo. Tunapanda imani katika Yesu Kristo kwa kutubu kila siku na kushika maagano ambayo hutuvisha nguvu. Tunabaki kwenye njia ya agano na tunabarikiwa kwa kuwa na nguvu kiroho, ufunuo binafsi, kuongeza imani, na kutumikiwa na malaika. Kuishi mafundisho ya Kristo kunaweza kuzalisha mzunguko imara zaidi, wenye kujenga kasi ya kiroho katika maisha yetu.10

Tunapojitahidi kuishi sheria ya juu zaidi ya Yesu Kristo mioyo yetu na asli yetu halisi inaanza kubadilika. Mwokozi anatuinua juu ya mvuto wa ulimwengu huu ulio anguka kwa kutubarika na hisani zaidi, unyenyekevu zaidi, ukarimu zaidi, wema zaidi, nidhamu binafsi, amani, na pumziko.

Sasa, yawezekana ukaanza kufikiria kama hii inaonekana kama kazi ngumu ya kiroho zaidi kuliko pumziko. Lakini hapa kuna ukweli mkuu: wakati ulimwengu unasisitiza kwamba nguvu, mali, umaarufu na starehe za kimwili ndizo ziletazo furaha, hivyo sivyo! Haviwezi! Havizalishi chochote bali ni mbadala mtupu wa zile “hali za baraka na furaha za wale [ambao] wanashika amri za Mungu.”11

Ukweli ni kwamba ni ya kuchosha zaidi kutafuta furaha mahali ambapo huwezi kamwe kuipata! Hata hivyo, unapojifunga mwenyewe nira kwa Yesu Kristo na kufanya kazi ya kiroho inayohitajika kuushinda ulimwengu, Yeye na ni Yeye pekee, aliye na uweza wa kukuinua juu ya mvuto wa ulimwengu huu.

Je, ni kwa namna gani kuushinda ulimwengu kunabariki maisha yetu? Jibu liko wazi: Kuingia katika uhusiano wa agano na Mungu kunatufunga sisi Kwake katika njia ambayo inafanya kila kitu kuhusu maisha kiwe rahisi zaidi. Tafadhali msinielewe vibaya:: Mimi sijasema kwamba kufanya maagano kunafanya maisha kuwa rahisi. Ukweli ni kwamba, tegemea upinzani, kwa sababu adui anataka wewe usigundue uweza wa Yesu Kristo. Kwa kujifunga mwenyewe nira na Mwokozi unapata kuzifikia nguvu Zake na uweza wa kukomboa.

Picha
Rais Ezra Taft Benson

Nathibitisha tena mafundisho ya kina ya Rais Ezra Taft Benson: “Wanaume na wanawake wanaompa Mungu maisha yao watagundua kwamba Yeye anaweza kufanya mengi zaidi kutoka katika maisha yao kuliko wao wanavyoweza. Yeye atawapa furaha ya kina, atapanua maono yao, atahuisha akili zao, … atainua roho zao, atazidisha baraka zao, kuongeza fursa zao, atafariji nafsi zao, atawainulia marafiki, na kuwamiminia amani.”12

Mapendeleo haya yasiyofananishwa yanawafuata wale wanaotafuta msaada wa mbinguni ili kuwasaidia kuushinda ulimwengu huu. Kwa mwisho huu, ninatoa mwaliko kwa waumini wa Kanisa lote wito wa aina hiyo hiyo niliotoa jukumu kwa vijana wetu wakubwa mwezi Mei iliyopita. Niliwahimiza wakati huo—na ninawasihi ninyi sasa—kusimamia ushuhuda wenu wenyewe wa Yesu Kristo na injili Yake. Ufanyie Kazi. Ulee ili ukue. Ulishe ukweli. Msizichafue kwa falsafa za uongo za wanaume na wanawake wasioamini. Unapofanya ushuhuda wako kuwa kipaumbele chako cha juu zaidi, tazamia miujiza kutokea katika maisha yako.13

Ombi langu kwenu asubuhi hii ni kutafuta pumziko kutokana na nguvu,kutokuwa na uhakika, na uchungu wa ulimwengu huu kwa kuushinda ulimwengu kupitia maagano yenu na Mungu. Acha Yeye na ajue kupitia sala na matendo yako kwamba kwa kweli wewe unataka kuushinda ulimwengu. Mwombe aiangaze akili yako na kukutumia msaada unaohitaji. Kila siku, andika chini mawazo yako ambayo yanakujia unapokuwa unasali, kisha yafuatilie kwa bidii. Tumia muda zaidi hekaluni na tafuta kuelewa jinsi hekalu linavyokufundisha kuinuka juu ya ulimwengu ulioangulika.14

Nimeeleza kabla, kazi ya kukusanya Israeli ni kazi muhimu zaidi inayofanyika duniani leo. Kipengele kimoja muhimu katika ukusanyaji huu ni kuwaandaa watu ambao wanaweza, wako tayari, na wanastahili kumpokea Bwana wakati anapokuja tena, watu ambao tayari wamemchagua Yesu Kristo dhidi ya ulimwengu ilioanguka; watu ambao wanashangilia haki yao ya kujiamulia ili kuishi sheria za juu zaidi na takatifu zaidi za Yesu Kristo.

Natoa wito kwenu, wapendwa kaka zangu na dada zangu, kuwa watu hawa wenye haki. Thamini na kuheshimu maagano yenu zaidi ya ahadi zingine zote mlizofanya. Mnapoacha Mungu ashinde katika maisha yenu, ninawaahidi amani kuu, kujiamini, shangwe na ndiyo, pumziko.

Kwa nguvu za utume mtakatifu zilizo ndani yangu, ninakubariki katika jitihada zako za kuushinda ulimwengu huu. Ninakubariki uweze kuongeza imani yako katika Yesu Kristo na kujifunza vyema jinsi ya kuchota nguvu Zake. Ninakubariki uweze kutambua kati ya ukweli ya uongo. Ninakubariki uweze kujali zaidi kuhusu mambo ya Mungu kuliko mambo ya ulimwengu. Ninakubariki uweze kuona shida za wale wanaokuzunguka na kuwaimarisha wale uwapendao. Kwa sababu Yesu Kristo aliushinda ulimwengu huu, nawe pia unaweza. Ninashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Mihtasari

  1. Joseph Smith—Mathayo 1:36: “Kisha itajitokeza ishara ya Mwana wa Mtu mbinguni, na kisha makabila yote duniani yataomboleza; na ndipo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu ya mbinguni, akiwa na nguvu na utukufu mkuu.”

  2. Mathayo 11:28–30; msisitizo umeongezwa.

  3. Yohana 16:33; Msisitizo umeongezwa.

  4. Mafundisho na Maagano 64:2; mkazo umeongezewa.

  5. Ona Alma 7:11–13.

  6. 2 Nefi 28:14.

  7. Ona hadithi ya baba wa Mfalme Lamoni katika Alma 22, hususani Alma 22:18.

  8. Ona Mosia 5:7.

  9. Mosia 3:19; msisitizo umeongezwa.

  10. Ona 2 Nefi 31; 3 Nefi 27:16–20.

  11. Mosia 2:41.

  12. Teachings of Presidents of the Church: Ezra Taft Benson (2014), 42–43.

  13. Ona Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.

  14. Rais David O. McKay said that in the temple we take a “step-by-step ascent into the Eternal Presence” (in Truman G. Madsen, The Temple: Where Heaven Meets Earth [2008], 11).