Mkutano Mkuu
Kwamba Wakujue Wewe
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Kwamba Wakujue Wewe

(Yohana 17:3)

Tamanio langu la dhati ni kwamba utakuja kumjua Yesu kwa majina Yake mengi na kwamba utakuwa kama Yeye.

Miaka michache iliyopita, nilipata uzoefu wenye kubadili maisha wakati wa mkutano wa sakramenti huko nyumbani kwetu Arizona. Wakati sala ya sakramenti ilipobainisha utayari wetu wa “kujichukulia [juu yetu] jina la [Yesu Kristo],”1 Roho Mtakatifu alinikumbusha kwamba Yesu anayo majina mengi. Swali hili kisha lilikuja moyoni mwangu: “Ni jina lipi kati ya majina ya Yesu ninapaswa kujichukulia wiki hii?”

Majina matatu yalikuja mawazoni mwangu na niliyaandika. Kila moja ya majina hayo matatu lilikuwa na sifa kama za Kristo ambazo nilitaka kuzikuza zaidi. Katika wiki iliyofuatia, nilifokasi kwenye majina hayo matatu na kujaribu kukumbatia sifa na tabia za majina husika. Tangu wakati huo, nimeendelea kujiuliza swali hilo kama sehemu ya kuabudu kwangu binafsi: “Ni jina lipi kati ya majina ya Yesu ninapaswa kujichukulia wiki hii?” Kujibu swali hilo na kujitahidi kukuza sifa kama za Kristo zinazohusika kumebariki maisha yangu.

Katika sala yake kuu ya Maombezi, Yesu alielezea ukweli huu muhimu: “Na uzima wa milele ndio huu, kwamba wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.”2 Leo ningependa kushiriki nanyi baraka na nguvu zinazokuja kutokana na kumjua Yesu Kristo kwa majina Yake mengi.

Njia moja rahisi tunayoweza kumjua mtu ni kwa kujua majina yao. Imekuwa ikisemwa kwamba “jina la mtu ni sauti tamu sana na muhimu sana kwa mtu yule katika lugha yoyote.”3 Je, umewahi kupata uzoefu wa kumwita mtu kwa jina lisilo sahihi au kusahau majina yao? Mimi na mke wangu, Alexis, mara kadhaa tumemwita mmoja wa watoto wetu “Lola.” Kwa bahati mbaya, kama ambavyo ungeweza kukisia, Lola ni mbwa wetu! Kwa raha au shida, kusahau jina la mtu kunatoa taswira kwa mtu yule kwamba pengine huwafahamu vyema.

Yesu aliwajua na kuwaita watu kwa majina. Kwa Israeli ya kale, Bwana alisema, “Usiogope: maana nimekukomboa, nimekuita kwa jina lako; wewe u wangu”.4 Asubuhi ya Pasaka, ushahidi wa Mariamu wa Kristo aliyefufuka uliimarishwa wakati Yesu alipomwita kwa jina.5 Vivyo hivyo, Mungu alimwita Joseph Smith kwa jina katika kujibu sala yake ya imani.6

Katika baadhi ya matukio, Yesu aliwapa wanafunzi wake majina mapya ambayo yalikuwa kiashiria cha asili yao, uwezo wao na uwezekano wao. Yehova alimpa Yakobo jina jipya la Israeli, ambalo lina maana “Mtu anayeshinda pamoja na Mungu” au “Acha Mungu ashinde.”7 Yesu alimpa Yakobo na Yohana jina la Boanerge, ambalo lilimaanisha “wana wa ngurumo.”8 Akiona uongozi wake wa siku zijazo, Yesu alimpa Simoni jina la Kefa au Petro, ambalo humaanisha mwamba.9

Kama vile Yesu anavyotujua kila mmoja wetu kwa jina, njia moja tunayoweza kumjua vyema Yesu ni kwa kujifunza majina Yake mengi. Kama vile majina ya Israeli na Petro, majina mengi ya Yesu ni vyeo vinavyotusaidia kuelewa misheni Yake, lengo, tabia na sifa Zake. Tunapopata kujua majina mengi ya Yesu, tutafikia uelewa mzuri wa misheni Yake ya kiungu na tabia Yake isio ya ubinafsi. Kujua majina Yake mengi pia kunatupatia msukumo wa kuwa zaidi kama Yeye—kukuza sifa kama za Kristo ambazo huleta shangwe na lengo kwenye maisha yetu.

Miaka michache iliyopita, Rais Russell M. Nelson alijifunza maandiko yote kuhusu Yesu Kristo kwenye Mwongozo wa Mada.10 Kisha aliwaalika vijana kujifunza maandiko sawa na aliyojifunza. Kuhusu majina mengi ya Yesu, Rais Nelson alisema, “Jifunze kila kitu kuhusu Yesu ni nani kwa sala na kwa bidii ukitafuta kuelewa kile ambacho kila moja ya vyeo na majina yake humaanisha kwako binafsi.11

Kufuatia mwaliko wa Rais Nelson, nilianza kutengeneza orodha yangu mwenyewe ya majina mengi ya Yesu. Orodha yangu binafsi sasa ina zaidi ya majina 300 na nina hakika yapo mengi zaidi ambayo bado sijayagundua.

Wakati kukiwa na majina ya Yesu ambayo yametunzwa kwa ajili Yake pekee,12 Ningependa kushiriki majina na vyeo vitano ambavyo vina matumizi kwa kila mmoja wetu. Ninawaalika mtengeneze orodha yenu pale mnapokuja kumjua Yesu kwa majina Yake mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata kwamba yapo majina mengine—sambamba na sifa husika kama za Kristo—ambazo utataka kujichukulia kama mfuasi wa agano wa Yesu.13

Kwanza, Yesu Kristo ni Mchungaji Mwema.14 Kama ndivyo, Yesu anawajua kondoo Wake,15 “huwaita kondoo wake kwa majina yao,”16 na, kama Mwana-kondoo wa Mungu, aliutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.17 Vivyo hivyo, Yesu anataka tuwe wachungaji wema, hususan kwenye familia zetu na kama akina kaka na akina dada wahudumiaji. Njia moja tunayoonesha upendo wetu kwa Yesu ni kwa kuwalisha kondoo Wake.18 Kwa kondoo wale wanaoweza kuwa wanatanga tanga, mchungaji mwema huenda nyikani kuwatafuta kondoo waliopotea, kisha hubaki nao mpaka wanaporejea kwenye usalama.19 Kama wachungaji wema na pale hali za eneo zinaporuhusu, tunapaswa kutafuta kutumia muda mwingi kuwahudumia watu katika nyumba zao. Katika huduma yetu, ujumbe mfupi na teknolojia vinapaswa kutumika kuimarisha, si kuzuia kukutana.20

Pili, Yesu ni Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yatakayokuwapo.21 Akijua kwamba kusulubiwa kwake kulikuwa karibu, Yesu alisema: “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani. Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”22 Leo, wakati ulimwengu wetu mara nyingi unafuata upepo na umegawanyika, kuna hitaji kubwa kwetu kuhubiri na kufanyia kazi uchanya, ujasiri na tumaini. Licha ya changamoto zozote za nyuma, imani daima huelekeza kwenye wakati ujao,23 uliojaa tumaini, ikituruhusu kutimiza mwaliko wa Yesu wa kujipa moyo.24 Kuishi injili kwa shangwe hutusaidia kuwa wafuasi wa mambo mema yatakayokuwapo.

Kingine kati ya vyeo vya Yesu ni kwamba Yeye ni yule yule, jana, leo na milele.25 Uthabiti ni sifa kama ya Kristo. Yesu daima alifanya mapenzi ya Baba Yake,26 na mkono wake kwa uthabiti umenyooshwa ili kutuokoa, kutusaidia na kutuponya.27 Tunapokuwa thabiti zaidi katika kuishi injili, tutakuwa zaidi kama Yesu.28 Japokuwa ulimwengu utapitia misukosuko mikubwa katika fasheni zake maarufu wakati watu wakitupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu,29 kuishi injili kwa uthabiti hutusaidia kuwa imara na wasioondoshwa wakati wa dhoruba za maisha.30 Tunaweza pia kuonesha uthabiti kwa kukubali mwaliko wa Rais Nelson wa “kutenga muda kwa ajili ya Bwana.”31 Nguvu kubwa ya kiroho huja kutokana na vitu vidogo na rahisi32 kama vile kukuza “tabia takatifu na ratiba inayotekelezeka”33 ya sala, toba, kujifunza maandiko na huduma kwa wengine kila siku.

Nne, Yesu ni Mtakatifu wa Israeli.34 Maisha ya Yesu yalikuwa mpangilio wa utakatifu. Tunapomfuata Yesu, tunaweza kuwa watakatifu katika Israeli.35 Tunaongezeka katika utakatifu pale tunapotembelea hekaluni mara kwa mara, ambapo “Utakatifu kwa Bwana” umechorwa juu ya kila mlango. Kila mara tunapoabudu hekaluni, tunaondoka tukiwa tumevikwa nguvu kuu ya kuzifanya nyumba zetu mahali patakatifu.36 Kwa yeyote ambaye kwa sasa hana kibali cha kuingia ndani ya hekalu takatifu, ninakualika ukutane na askofu wako na ujitayarishe kuingia au kurejea mahala pale patakatifu. Muda hekaluni utaongeza utakatifu kwenye maisha yetu.

Jina moja la mwisho la Yesu ni kwamba Yeye ni Mwaminifu na Mkweli.37 Kama vile ambavyo Yesu amekuwa mwaminifu na mkweli daima, tamanio lake la dhati ni kwamba tuoneshe sifa hizi kwenye maisha yetu. Imani yetu inapoyumba, tunaweza kumlilia Yesu, “Bwana, niokoe” kama vile Petro wakati alipoanza kuzama kwenye bahari yenye dhoruba ya Galilaya.38 Siku hiyo, Yesu alienda kumwokoa mwanafunzi aliyekuwa akizama. Amefanya vivyo hivyo kwangu, na atafanya vivyo hivyo kwako. Kamwe usimkatie tamaa Yesu—Yeye kamwe hatakukatia tamaa!

Tunapokuwa waaminifu na wakweli, tunafuata wito wa Mwokozi wa “Kaeni ndani yangu,” ambao pia huweza kumaanisha “bakini pamoja nami.”39 Tunapokabiliwa na maswali, tunapodhihakiwa kwa sababu ya imani yetu, wakati vidole vya dharau vikituelekea vya wale walio katika jengo kuu na pana la ulimwengu, tunabakia waaminifu na tunaendelea kuwa wakweli. Katika nyakati hizi, tunakumbuka ombi la Yesu, “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.”40 Tunapofanya hivyo, Yeye hutupatia imani inayohitajika, tumaini na nguvu ya kubaki Naye milele.41

Wapendwa akina kaka na akina dada, Yesu anataka tumjue Yeye kwa sababu Lake ndilo jina pekee chini ya mbingu ambalo kwalo tunaokolewa.42 Yesu ni njia, kweli na uzima—mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya Yeye.43 Yesu ndiye njia pekee! Kwa sababu hiyo, Yesu anaita, “Njoni kwangu,”44 “Nifuate,”45 “Nenda pamoja nami,”46 na “Jifunze kwangu.”47

Kwa moyo wangu wote, ninatoa ushahidi wa Yesu Kristo—kwamba yu hai, kwamba anakupenda na kwamba anakujua kwa jina. Yeye ni Mwana wa Mungu,48 Mwana Pekee wa Baba.49 Yeye ni Mwamba wetu, Ngome yetu, Ngao yetu, Kimbilio letu na Mkombozi wetu.50 Yeye ni nuru ing’aayo gizani.51 Yeye ni Mwokozi52 na Mkombozi wetu.53 Yeye ni Ufufuo na Uzima.54 Tamanio langu la dhati ni kwamba utakuja kumjua Yesu kwa majina Yake mengi na kwamba utakuwa kama Yeye pale unapoonesha sifa Zake za kiungu kwenye maisha yako. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.