Mkutano Mkuu
Jivike Nguvu Zako, Ee Sayuni
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Jivike Nguvu Zako, Ee Sayuni

Kila mmoja wetu anapaswa kutathimini vipaumbele vyetu vya kimwili na kiroho kwa uaminifu na maombi.

Mafumbo ni sifa kuu ya njia ya ufundishaji mahiri wa Bwana Yesu Kristo. Kwa urahisi, mafumbo ya Mwokozi ni hadithi zilizotumiwa kulinganisha kweli za kiroho na vitu vya ulimwengu na uzoefu wa kidunia. Kwa mfano, Injili za Agano Jipya zimejaa mafundisho yanayofananisha ufalme wa Mbinguni na punje ya haradali,1 hata lulu ya thamani kuu,2 na mwenye nyumba na watenda kazi katika shamba lake la mzeituni,3 hadi wanawali kumi,4 na vitu vingine vingi. Wakati wa sehemu ya huduma ya Bwana ya Galilaya, maandiko yanaonyesha kwamba “wala pasipo mfano hakusema nao.”5

Maana au ujumbe uliodhamiriwa wa fumbo kwa kawaida hauelezwi waziwazi. Badala yake, hadithi hutoa kweli pekee kwa mpokeaji kulingana na imani yake katika Mungu, maandalizi binafsi ya kiroho, na utayari wa kujifunza. Hivyo basi, mtu binafsi sharti aamue mwenyewe na kwa bidii “kuomba, kutafuta, na kubisha”6 ili kugundua kweli zilizomo ndani ya fumbo.

Naomba kwa dhati kwamba Roho Mtakatifu atatufunulia kila mmoja wetu wakati tufukiriapo umuhimu wa fumbo la karamu ya harusi ya kifalme.

Karamu ya Harusi ya Kifalme

“Yesu … akawaambia tena kwa mithali, akisema,

“Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe harusi,

“Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja harusini; nao wakakataa kuja.

“Akawatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu: ng’ombe wangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari: njoni harusini.

“Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake.”7

Nyakati za kale, mojawapo ya wakati wa furaha sana katika maisha ya Wayaudi ulikuwa ni sherehe za harusi—tukio ambalo lilichukua wiki nzima au hata mbili. Tukio kama hilo lilihitaji mipango mingi, na wageni walitaarifiwa siku nyingi kabla, na kumbusho likitumwa siku ya kuanza kwa sherehe. Mwaliko kama huu wa harusi toka kwa mfalme kwenda kwa watawaliwa ulikuwa ukichukuliwa kama amri. Lakini bado, kwenye fumbo hili wengi wa wageni walioalikwa hawakuhudhuria.8

“Kukataa kuhudhuria karamu ya mfalme ilikuwa tendo la makusudi la uasi dhidi ya mamlaka ya kifalme na utovu binafsi wa nidhamu dhidi ya wote mfalme aliye kwenye enzi na mwanawe. Kwa mtu mmoja kwenda shambani kwake na mwingine kwenda kwenye [biashara yake]”9 huonyesha vipaumbele vyao potovu na upuuzwaji wa mapenzi ya mfalme.10

Fumbo linaendelea:

“Kisha akawaambia watumwa wake, Harusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.

“Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni harusini.

“Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; harusi ikajaa wageni.11

Desturi katika siku hizo katika fumbo hili ilikuwa kwa mwenyeji wa karamu ya harusi—mfalme—kupanga mavazi kwa ajili ya wageni. Mavazi hayo ya harusi yalikuwa ya kawaida, majoho ambayo wahudhuriaji wote walivaa. Kwa njia hii, vyeo na hadhi viliondolewa, na kila mmoja katika karamu angechangama kwa usawa.12

Watu walioalikwa kutoka barabarani kuhudhuria harusi hawangekuwa na muda au fedha za kununua vazi lifaalo kwa maandalizi ya tukio hili. Kwa hiyo, kuna uwezekano mfalme aliwapa wageni mavazi kutoka nguo zake mwenyewe. Kila mmoja alipatiwa nafasi ya kuvaa mavazi ya kifalme.13

Mfalme alipoingia katika ukumbi wa harusi, akautazama umati na mara moja akamwona mgeni mmoja aliyeonekana wazi kutokuwa kwenye vazi la harusi. Mtu yule akaletwa mbele, na mfalme akauliza, “Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la harusi? Naye hakuwa na jibu.”14 Kiuhalisia, mfalme aliuliza, “Kwa nini hauko kwenye vazi la harusi, japokuwa ulipewa?15

Mtu yule bila shaka hakuwa amevaa ipasavyo kwa ajili ya tukio hili maalum, na kirai “Naye hakuwa na jibu” kinaonyesha kwamba mtu yule hakuwa na sababu yoyote.16

Mzee James E. Talmage anatoa maoni ya mwongozo kuhusu umuhimu wa matendo ya mtu huyu: “Mgeni aliyekuwa hakuvaa joho alikuwa na hatia ya kupuuza, kukosa heshima makusudi, au kosa kubwa sana, ni wazi kutokana na muktadha. Mfalme mwanzo alikuwa na huruma na busara, akiuliza tu ni kwa jinsi gani mtu huyu alikuwa harusini bila vazi la harusi. Kama mgeni huyu angeweza kujieleza kuhusu mwonekano wake, au kama angekuwa na sababu ya kufaa, hakika angezungumza; lakini tunaambiwa kwamba hakuwa na jibu. Mwaliko wa mfalme ulikuwa umetolewa bila ubaguzi kwa wote ambao watumishi wake waliwapata, lakini kila mmoja wao alitakiwa kuingia kwenye kasri kupitia lango; na kuwa kwenye vazi la harusi kabla ya kufika kwenye chumba cha karamu, ambacho mfalme angekuja; lakini huyu mwasi, kwa njia fulani aliingia kupitia njia nyingine; na akiwa hajapita lango ambalo bawabu walikuwepo, alikuwa mvamizi.”17

Mwandishi wa Kikristo, John O. Reid, alisema kwamba kukataa kwa mtu yule kuvaa vazi la harusi kulionyesha “utovu wa nidhamu kwa wote mfalme na mwanawe.” Hakukosa vazi la harusi; bali, alichagua kutolivaa. Kwa uasi alikataa kuvaa ipasavyo kwa ajili wakati huo. Maamuzi ya mfalme yalikuwa ya upesi na wazi: “Mfungeni mikono na miguu, na mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”18

Uamuzi wa mfalme kwa mtu huyu haukutokana na mtu huyu kukosa vazi la harusi—lakini kwamba “yeye alikuwa amenuia, kutovaa. Mtu huyu … alitamani heshima ya kuhudhuria karamu ya harusi lakini … hakutaka kufuata desturi za mfalme. Alitaka kufanya mambo kwa njia yake mwenyewe. Kutokuwa na vazi linalofaa kulionyesha uasi wake wa ndani dhidi ya mfalme na maelekezo yake.19

Waitwao Ni Wengi, bali Wateule Ni Wachache

Fumbo kisha linahitimisha na andiko hili: “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.”20

Cha kupendeza, Joseph Smith alifanya marekebisho yafuatayo kwenye mstari huu kutoka Mathayo katika tafsiri ya Biblia: “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache kwa hivyo wote hawajavalia vazi la harusi.”21

Mwaliko kuhudhuria karamu ya harusi na uchaguzi wa kuhudhuria karamu vinahusiana lakini ni tofauti. Mwaliko ni kwa wote wanaume na wanawake. Mtu bado anaweza kuukubali mwaliko na kuketi karamuni—lakini asikubalike kushiriki kwa sababu yeye hana vazi lipasalo la imani ya kuongoa katika Bwana Yesu Kristo na rehema Yake takatifu. Hivyo basi, tuna vyote mwaliko toka kwa Mungu na uitikiaji wetu binafsi wa mwaliko huo, na wengi wanaweza kuitwa, bali wateule ni wachache.22

Kuteuliwa au kuwa mteule si hali ya lazima iwekwayo juu yetu. Badala yake, wewe na mimi tunaweza kuchagua kuwa wateule kupitia matumizi sahihi ya haki yetu ya kujiamulia kimaadili.

Tafadhali tazama matumizi ya neno wateule katika mistari inayofahamika ifuatayo kutoka kwenye Mafundisho na Maagano:

“Tazama, wengi huitwa, lakini wachache huteuliwa. Na ni kwa nini hawakuteuliwa?

“Kwa sababu mioyo yao imekuwa juu ya mambo ya ulimwengu huu, na kutafuta kupata heshima kutoka kwa wanadamu.”23

Ninaamini maana ya mistari hii ni wazi kabisa. Mungu hana orodha ya watu pendwa ambayo sharti tuitazamie kwamba majina yetu siku moja yatakuwepo. Hana idadi ya “wateule” kuwa wachache pekee. Badala yake, mioyo yetu, hamu zetu, kuheshimu kwetu maagano na ibada zetu takatifu za injili, utiifu wetu wa amri, na, muhimu sana, neema ya Mwokozi huamua kama tunahesabiwa kama mmoja wa wateule wa Mungu.24

“Kwani tunajitahidi kuandika, kuwashawishi watoto wetu, na pia ndugu zetu, kumwamini Kristo, na kupatanishwa na Mungu; kwani tunajua kwamba ni kwa neema kwamba tunaokolewa, baada ya kutenda yote tunayoweza.25

Katika wingi wa shughuli za maisha yetu ya kila siku na katika hekaheka za ulimwengu wa kisasa tunamoishi, tunaweza kutolewa kutoka mambo ya umilele yenye thamani sana kwa kuweka anasa, kulimbikiza mali, umaarufu na hadhi kuwa vipaumbele vyetu. Kushikilia sana kwetu kwa muda mfupi “mambo ya ulimwengu huu” na “sifa za wanadamu” kunaweza kupelekea kupoteza kwetu haki ya uzaliwa wa kiroho kwa ajili ya kitu duni kisicho na thamani.26

Ahadi na Ushuhuda

Ninarudia onyo la Bwana kwa watu Wake lililotolewa kupitia nabii Hagai wa Agano la Kale: “Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.”27

Kila mmoja wetu anapaswa kutathimini vipaumbele vyetu vya kimwili na kiroho kwa dhati na kupitia sala ili kutambua mambo katika maisha yetu ambayo yanazuia baraka nyingi ambazo Baba wa Mbinguni na Mwokozi wanatamani kututunukia. Na hakika Roho Mtakatifu atatusaidia kujiona tulivyo kiuhalisia.28

Tutafutapo ipasavyo kipawa cha kiroho cha macho ya kuona na masikio ya kusikia,29 ninaahidi kwamba tutabarikiwa na uwezo na uamuzi kuimarisha muunganiko wetu wa kimaagano na Bwana aliye hai. Pia tutapokea nguvu za uungu maishani mwetu30—na hatimaye tuitwe na kuteuliwa kwa ajili ya karamu ya Bwana.

“Inuka, inuka; jivike nguvu zako, Ee Sayuni.”31

“Kwani Sayuni lazima iongezeke katika uzuri, na katika utakatifu; mipaka yake lazima ipanuliwe; na vigingi vyake lazima viimarishwe; ndiyo, amini ninawaambia, Sayuni lazima ichomoze na kuvaa mavazi yake mazuri.”32

Kwa furaha ninatangaza ushuhuda wangu wa utakatifu na uhalisia wa Mungu, Baba yetu wa Milele, na Mwanawe mpendwa, Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu, na kwamba Yeye yu hai. Na pia ninashuhudia kwamba Baba na Mwana walimtokea mvulana Joseph Smith, kwa hiyo alianzisha Urejesho wa injili ya Mwokozi katika siku za mwisho. Na kila mmoja wetu atafute na abarikiwe na macho ya kuona na masikio ya kusikia, ninaomba katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.