Mkutano Mkuu
Taji la Maua Badala ya Majivu: Njia ya Uponyaji ya Msamaha
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Taji la Maua Badala ya Majivu: Njia ya Uponyaji ya Msamaha

Kuishi kwa njia ambayo unatoa taji la maua badala ya majivu ya maisha yako ni kitendo cha imani cha kumfuata Mwokozi.

Kitabu cha Samweli kinajumuisha hadithi isiyo maarufu ya Daudi, mfalme wa baadae wa Israeli, na mwanamke aliyeitwa Abigaili.

Baada ya kifo cha Samweli, Daudi na watu wake walienda mbali na Mfalme Sauli aliyekuwa akitafuta uhai wa Daudi. Walikuwa wakilinda kundi la mifugo na watumishi wa mtu tajiri aliyeitwa Nabali, aliyekuwa mwenye roho ya choyo. Daudi aliwatuma watu 10 kati ya watu wake ili wapeleke salamu kwa Nabali na waombe chakula na mahitaji mengine yaliyokuwa yanahitajika sana.

Nabali alijibu ombi la Daudi kwa matusi na kuwarudisha watu wake mikono mitupu.

Akiwa amekwazwa, Daudi aliwaandaa watu wake ili wapande dhidi ya Nabali na nyumba yake akisema, “amenilipa mabaya badala ya mema.”1 Mtumishi alimwambia Abigaili, mkewe Nabali, kuhusu mumewe alivyowatendea mabaya watu wa Daudi. Abigaili haraka alikusanya chakula na vifaa vilivyohitajika na kwenda kuingilia kati.

Abigaili alipokutana na Daudi, “alianguka kifulifuli mbele yake, na akainama hadi nchi.

“Na yeye akaanguka miguuni na kusema, Juu yangu mimi, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu huu. …

“Basi sasa, … Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe. …

“… Na sasa zawadi hii mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. …

“Nakuomba, ulisamehe kosa la mjakazi wako. …

“Naye Daudi akamwambia Abigaili, na ahimidiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki:

“Na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. …

“Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea, na akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; … nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.”2

Wote wawili wakaachana kwa amani.

Katika hadithi hii, Abigaili anaweza kuonekana kama mtu mwenye nguvu au mfano wa Yesu Kristo.3 Kupitia dhabihu Yake ya upatanisho, Yeye anaweza kutukomboa kutoka dhambini na kwenye hasira na chuki na kutupatia riziki tunazohitaji.4

Kama vile tu Abigaili alivyokuwa tayari kujichukulia juu yake dhambi ya Nabali, ndivyo Mwokozi alivyofanya—kwa njia isiyoelezeka—alijichukulia juu Yake dhambi zetu na dhambi za wale ambao wametuumiza au wametukwaza.5 Gethsemane na pale msalabani, Yeye alilipia dhambi hizi. Alitutengenezea njia ya sisi kuachana na moyo wa kulipiza kisasi. “Njia” hiyo ni njia ya kusamehe—ambayo inaweza kuwa moja ya mambo magumu sana tuliyowahi kufanya na moja ya mambo ya kiungu zaidi kuwahi kuyapitia. Juu ya njia ya msamaha, nguvu ya Yesu Kristo ya upatanisho inaweza kutiririka katika maisha yetu na kuanza kuponya nyufa za kina za moyo na roho.

Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba Mwokozi hutupatia sisi uwezo wa kusamehe:

“Kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, unaweza kuwasamehe wale waliokuudhi na ambao kamwe hawawezi kukubali kuwajibika kwa ajili ya ukatili wao kwako.

“Daima ni rahisi kumsamehe mtu ambaye kwa dhati na kwa unyenyekevu anatafuta msamaha wako. Lakini Mwokozi atakupa uwezo wa kumsamehe yeyote ambaye amekutendea vibaya katika njia yoyote. Kisha matendo yao ya kuumiza hayawezi tena kuumiza nafsi yako.”6

Abigaili kuleta wingi wa vyakula na vifaa kunaweza kutufundisha kwamba Mwokozi anatoa kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa, riziki na msaada tunaohitaji ili kuponywa na kuwa wazima.7 Hatuachiwi kushughulika na matokeo ya matendo ya watu wengine peke yetu, sisi pia tunaweza kufanywa wazima na kupewa nafasi ya kuokolewa kutokana na hasira na chuki na matendo yoyote ambayo yanafuata.

Bwana amesema: “Mimi, Bwana, nitamsamehe yule nitakaye kumsamehe, lakini ninyi mnatakiwa kuwasamehe watu wote.” Bwana anatutaka sisi kusamehe kwa faida yetu wenyewe.9 Lakini Yeye hatuombi sisi tufanye hivyo pasipo msaada Wake, upendo Wake na uelewa Wake. Kupitia maagano yetu na Bwana, tunaweza kila mmoja kupokea nguvu ya kuimarisha, mwongozo na msaada tunaohitaji ili kusamehe na kusamehewa.

Tafadhali jua kwamba kumsamehe mtu haimaanishi kwamba unajiweka kwenye nafasi ambapo utaendelea kuumia. “Tunaweza kufanyia kazi kumsamehe mtu na bado tukahisi kushawishiwa na Roho kukaa mbali nao.”10

Kama vile Abigaili alivyomsaidia Daudi asiwe na “hatia moyoni”11 na kupokea msaada aliohitaji, ndivyo Mwokozi atakavyo kusaidia wewe. Yeye anakupenda, na anakulaki kwenye njia yako akiwa “na uponyaji katika mabawa Yake.”12 Anatamani amani yako.

Mimi mwenyewe nimeshuhudia muujiza wa Yesu Kristo akiuponya moyo wangu wenye hasira na chuki. Kwa ruhusa ya baba yangu, ninashiriki kwamba nimekulia katika nyumba ambamo sikuwa siku zote nikihisi salama kwa sababu ya unyanyasaji wa kihisia na maneno. Katika miaka yangu ya ujana na kuelekea utu uzima, nilimchukia baba yangu na nilikuwa na hasira moyoni mwangu kutokana na maumivu hayo.

Baada ya miaka mingi, na katika jitihada zangu za kutafuta amani na uponyaji kwenye njia hiyo ya msamaha, nilikuja kutambua katika njia ya kina sana kwamba Mwana wa Mungu yuleyule aliyelipia dhambi zangu, ndiye Mkombozi yuleyule atakaye waokoa wale ambao wameniumiza mimi kwa kina sana. Sikuweza hakika kuamini ukweli wa kwanza pasipo kuamini ule wa pili.

Jinsi upendo wangu kwa Mwokozi ulivyokua, ndivyo na hamu yangu ya kubadilisha maumivu na hasira kwa mafuta Yake ya uponyaji ilivyokua. Umekuwa mchakato wa miaka mingi, ukihitaji ujasiri, mazingira magumu, ustahimilivu na kujifunza kutumaini katika nguvu ya kiungu ya Mwokozi ya kuokoa na kuponya. Bado nina kazi ya kufanya, lakini moyo wangu hauko tena kwenye njia ya vita. Nimepewa “moyo mpya”13—moyo ambao umehisi upendo wa kina wa Mwokozi mwenyewe, ambaye alikaa pembeni yangu, ambaye kwa upole na kwa uvumilivu aliniongoza mahali pazuri zaidi, ambaye alilia pamoja nami, ambaye aliijua huzuni yangu.

Mwokozi amenitumia baraka za fidia kama vile Abigaili alivyoleta vile ambavyo Daudi alivihitaji. Amenitumia washauri katika maisha yangu. Na mzuri zaidi na wa kubadilisha zaidi ya yote umekuwa uhusiano wangu na Baba yangu wa Mbinguni. Kupitia Yeye, kwa shukrani nimeujua upendo mkarimu, wenye ulinzi, na mwongozo wa Baba.

Mzee Richard G. Scott alisema: “Huwezi kufuta kile ambacho kimefanyika, lakini unaweza kusamehe.14 Msamaha unaponya majeraha ya kutisha, na ya kuhuzunisha, kwani unaruhusu upendo wa Mungu usafishe moyo na akili yako kutokana na sumu ya chuki. Unasafisha ufahamu wako wa hamu ya kulipiza kisasi. Hutengeneza nafasi kwa ajili ya utakaso, uponyaji, urejeshaji wa upendo wa Bwana.”15

Baba yangu wa duniani naye pia amepata badiliko la moyo la kimuujiza katika miaka ya hivi karibuni na amemgeukia Bwana—kitu ambacho sikukitarajia katika maisha haya. Ushuhuda mwingine kwangu wa nguvu kamili na yenye kubadilisha ya Yesu Kristo.

Ninajua kwamba anaweza kumponya mdhambi na wale waliotendewa dhambi. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu, ambaye aliyatoa maisha yake ili sisi tupate kuishi tena. Yeye alisema “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria masikini habari njema, amenituma kuponya waliovunjika moyo, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa.”16

Kwa wote walivunjika moyo, wafungwa, waliosetwa na pengine waliopofushwa na maumivu au dhambi, Yeye anatoa uponyaji, ahueni na ukombozi. Ninashuhudia kwamba uponyaji na ahueni atoayo ni halisi. Ratiba ya uponyaji huo ni binafsi na hatuwezi kuhukumu ratiba ya mtu mwingine. Ni muhimu kujipa sisi wenyewe muda muhimu wa kupona na tujitendee kwa ukarimu sisi wenyewe katika mchakato huo. Mwokozi daima ni mwenye rehema na msikivu na amesimama tayari kutoa msaada tunaohitaji.17

Kwenye njia ya msamaha na uponyaji kuna chaguo la kutoendeleza mifumo au uhusiano mbaya katika familia zetu au pengine popote. Kwa wote walio ndani ya ushawishi wetu, tunaweza kutoa ukarimu kwenye ukatili, upendo kwenye chuki, upole kwenye mikwaruzo, usalama kwenye wasiwasi na amani kwenye ugomvi.

Kutoa kile ulichonyimwa ni sehemu yenye nguvu ya uponyaji wa kiungu inayowezekana kupitia imani katika Yesu Kristo. Kuishi kwa njia ambayo unatoa, kama Isaya alivyosema, taji la maua badala ya majivu ya maisha yako18 ni kitendo cha imani ambacho kinafuata mfano mkuu wa Mwokozi ambaye aliteseka vyote ili Yeye apate kuwasaidia wote.

Yusufu wa Misri aliishi maisha ya majivu. Alichukiwa na kaka zake, alisalitiwa, aliuzwa utumwani, alitiwa gerezani kimakosa na kusahauliwa na mtu aliyemwahidi kumsaidia. Bado yeye alimtumaini Bwana. “Bwana alikuwa na Yusufu”19 na aliweka wakfu majaribu yake kwa baraka na ukuaji wake mwenyewe—na kwa wokovu wa familia yake na Misri yote.

Yusufu alipokutana na kaka zake akiwa kiongozi mkubwa huko Misri, msamaha wake na mtazamo uliotakaswa vilijidhihirisha katika maneno ya shukrani aliyoyazungumza:

“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku: maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. …

“Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu.”20

Kupitia Mwokozi, maisha ya Yusufu yakawa “taji la maua badala ya majivu”21

Kevin J. Worthen, rais wa BYU, amesema kwamba Mungu “anaweza kufanya mema yakaja … siyo tu kutokana na mafanikio yetu bali pia kutokana na kushindwa kwetu na kushindwa kwa wengine ambako hutusababishia maumivu. Mungu ni mwema na mwenye nguvu.”22

Ninashuhudia kwamba mfano mkuu zaidi wa upendo na msamaha ni ule wa Mwokozi, Yesu Kristo, ambaye katika uchungu mkali alisema, “Baba, wasamehe; kwani hawajui watendalo.”23

Ninajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni anataka wema na tumaini kwa kila mmoja wa watoto Wake. Katika Yeremia tunasoma, “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, mawazo ya amani.”24

Yesu Kristo ni Masiya wako binafsi, Mkombozi na Mwokozi wako mwenye upendo, anayejua kusihi kwa moyo wako. Anatamani uponyaji na furaha yako. Yeye anakupenda. Analia pamoja na wewe katika huzuni zako na anafurahia kukufanya wewe uwe mzima. Na tujipe moyo na kuushika mkono Wake wenye upendo ambao umenyoshwa25 wakati tunapotembea njia ya uponyaji ya msamaha ni sala yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.