2021
Kuwa Mwenye Kujitegemea ili Kumtumikia Bwana Vizuri
Machi 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO

Kuwa Mwenye Kujitegemea ili Kumtumikia Bwana Vizuri

“Tunapofanyia kazi kanuni za kujitegemea, tunaweza kupokea baraka muhimu za kiroho na kimwili kwa ajili yetu wenyewe pamoja na familia zetu.”

Maandiko na Kitabu cha Mwongozo cha Kanisa vilinisaidia kuelewa kwa nini, vipi na jinsi gani ningeweza kuwa mwenye kujitegemea katika maisha yangu tangu siku zangu za awali kama muumini wa Kanisa. Nilikuza hamu ya kujifunza na kutumia Maandiko na maneno ya manabii wa leo—na nimeweza kujua kwamba ni ya kweli.

Katika Kitabu cha Mwongozo cha Kanisa tunasoma: “Kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu mwenyewe na familia. Pale waumini wanapokuwa wenye kujitegemea, pia wanakuwa wenye kuwatumikia vyema na kuwajali wengine.

Waumini wa kanisa wanawajibika kwa ajili ya ustawi wao wa kiroho na kimwili. Wakiwa wamebarikiwa kwa zawadi ya haki ya kujiamulia, wana haki na wajibu wa kufanya walipendalo, kutatua matatizo yao wenyewe na kujitahidi kuwa wenye kujitegemea. Waumini hufanya hili chini ya ushawishi wa Bwana pamoja na kazi za mikono yao wenyewe”1.

Baada ya anguko, Adamu na Hawa, walifukuzwa kutoka bustani ya Edeni ili kuilima ardhi na kujikimu kwa mahitaji yao wenyewe na kuwa mtawala juu ya wanyama wote wa mwituni, na kula mkate kwa jasho la uso wake, kama vile Mimi Bwana nilivyomwamuru. Naye Hawa, pia, mke wake, alifanya kazi pamoja naye2.

Baba yetu wa Mbinguni aliamuru kwamba tufanye kazi ili kukimu mahitaji yetu na mahitaji ya familia zetu wenyewe. Tunapaswa kujitahidi kufanya hili pamoja na amri zote za Baba. Anatutaka sisi kuelewa vyema umuhimu wa kazi na kujifunza kanuni sahihi za kupangilia kipato chetu kwa ajili ya ustawi mzuri wa familia zetu na kutumikiana vyema.

Katika Kitabu cha Mormoni tunasoma kuhusu Wanefi na utamaduni wao wa kufanya kazi kwa bidii:

Watu wa Amoni “walikuwa wenye bidii, na walifanya kazi sana”3.

Wayaredi “walikuwa wenye bidii sana . . .

Na walifanya kazi katika kila aina ya madini . . . na kila aina ya chuma;

Na walishona aina yote ya nguo.

Na walitengeneza kila aina ya vyombo kulimia mashamba.

Na hakungekuwa na watu waliobarikiwa kuliko hao, na kufanikishwa zaidi kwa mkono wa Bwana”4.

“Kwa hivyo, Bwana Mungu amemruhusu mwanadamu kujitendea mwenyewe . . . [na wanaume na wanawake wako huru] kujitendea wenyewe na sio kutendewa”5.

Pia tunasoma katika Mafundisho na Maagano, ambapo Bwana anafunua:

“Usiwe mvivu; kwani yule aliye mvivu hatakula mkate wala kuvaa mavazi ya mfanya kazi”6.

Bila kujali kile ambacho wazazi wetu au mababu zetu wamefanya au hawajafanya kwenye kufanya kazi na kujikimu wenyewe, msimamo wa Bwana ni dhahiri: tuna jukumu la kufanya kazi ili kujikimu sisi na familia zetu, na kusimamia rasilimali katika njia itakayotunufaisha sisi na familia zetu kwa maisha yetu yote hapa duniani.

Manabii wawili wa siku za leo wametushauri katika kanuni hizi:

Rais Spencer W. Kimball (1895–1985), Rais wa Kanisa kuanzia 1973 mpaka 1985 alifundisha: “Hakuna Mtakatifu wa Siku za Mwisho wa Kweli, wakati akiwa anajiweza kimwili na kihisia, kwa makusudi atahamishia mzigo wa ustawi wake mwenyewe au wa familia yake kwa mwingine. Kadiri anavyoweza, chini ya ushawishi wa Bwana na kwa kazi zake mwenyewe, atakidhi kwa ajili yake mwenyewe na familia yake mahitaji muhimu ya maisha ya kiroho na kimwili”7.

Rais Thomas S. Monson (1927–2018), Rais wa Kanisa kuanzia 2008 mpaka 2018 alifundisha: “Kujitegemea . . . ni kigezo muhimu katika ustawi wetu wa kiroho pamoja na wa kimwili. . . . Acha tufanye kazi kwa ajili ya kile tunachohitaji. Acha tujitegemee na kuwa huru. Wokovu haupatikani kwa kanuni nyingine yoyote. Wokovu ni swala la mtu binafsi, na lazima tufanyie kazi wokovu wetu wenyewe katika mambo ya kimwili pamoja na ya kiroho”8.

Kujitegemea kimwili na kiroho haviwezi kutenganishwa. Tunapotumia kanuni za kujitegemea, tunaweza kupokea baraka muhimu za kiroho na kimwili kwa ajili yetu na familia zetu.

Mzee D. Todd Christofferson, wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alifundisha kuhusu uhusiano kati ya kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii: “Mungu amepangilia maisha haya ya duniani ili yahitaji juhudi endelevu. Nakumbuka kauli rahisi ya Nabii Joseph Smith: ‘kwa kuendelea kufanya kazi mara kwa mara [sisi] tuliwezeshwa kupata mahitaji ya kutosha’ (Joseph Smith—Historia ya 1:55). Kwa kufanya kazi tunakidhi na kubariki maisha. Kunatusaidia kuvuka vikwazo na majanga ya uzoefu wa maisha ya duniani. Mafanikio yapatikanayo kwa jitihada huleta hisia ya ustahiki binafsi. Kazi hujenga na kuboresha tabia, hutengeneza uzuri, na ni chombo cha huduma yetu kwa kila mmoja na kwa Mungu. Maisha yaliyowekwa wakfu yamejazwa kwa kazi, wakati mwingine ikijirudia, wakati mwingine utumishi wa nyumbani, wakati mwingine kazi isiyopongezwa lakini siku zote ni kazi inayojenga, inayoagiza, inayokidhi, inayoinua, inayohudumu, inayotamanisha”9.

Nimekuja kujua kwamba Yesu Kristo ni mwokozi wangu, kwamba Kanisa la Yesu Kristo ndilo kanisa la kweli pekee juu ya uso wa Ulimwengu kwamba tunao tena Manabii walio hai duniani leo.

Elie K. Monga alitajwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2017. Anaishi Kinshasa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Amemuoa Vianney Mwenze; ni wazazi wa watoto wanne.

MUHTASARI

  1. General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints [2020], 22.1.1.

  2. Ona Musa 5:1.

  3. Ona Mosia 23:5.

  4. Ona Etheri 10:22–25, 28.

  5. Ona 2 Nefi 2:16, 26.

  6. Mafundisho na Maagano 42:42.

  7. Teachings of Presidents of the Church: Spencer W. Kimball [2006], Sura ya 11.

  8. Thomas S. Monson, “Guiding Principles of Personal and Family Welfare”, Ensign, September 1986, 3.

  9. D. Todd Christofferson, “Reflections on a Consecrated Life”, Mkutano Mkuu wa Oktoba 2010.