2021
Maharagwe Yaliyookwa na Maboksi: Funzo langu la imani kutoka mwaka 2020
Machi 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Maharagwe Yaliyookwa na Maboksi: Funzo langu la imani kutoka mwaka 2020

“Kuchukua hatua ile ya kwanza ya imani ilikuwa kitu kigumu na cha kuogopesha kwangu. Lakini matokeo?”

Bado nakumbuka wakati nilipofurahia kujitenga kijamii.

Nilikuwa nimepewa taarifa kwamba, wakati Afrika Kusini ilipoingia kwenye zuio la kubaki nyumbani katika juhudi za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya COVID-19, watoto wa shule wapatao milioni 9.6 wa Afrika Kusini wangekuwa bila chakula.

Mpango wa chakula shuleni katika Afrika Kusini unaunda utaratibu muhimu wa msaada wa kijamii. Kwa watoto wengi nchini, ni mlo pekee wanaoweza kutazamia kupata kila siku.

Kama mwandishi wa habari, nilikuwa nimekamilisha mahojiano ya aina tano yanayofuatana na viongozi mbalimbali kutoka asasi za kiraia. Walikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi watoto watakavyostahimili miezi kadhaa ijayo.

“Nina hofu nyingi na wasiwasi mkubwa kuhusu kile watoto wanachokula,” dada mmoja ambaye mara kwa mara huendesha mpango wa chakula kwa watoto 150 katika moja ya miji ya Johannesburg alikuwa ameniambia. “Na hakuna chochote, chochote kabisa ninachoweza kufanya kuhusu hilo.”

Baada ya masaa mengi ya mazungumzo kama hayo, ningeweza kusikia sauti yangu ikianza kukwama kutokana na hisia. Mwishoni mwa mahojiano ya kuhitimisha, nilikata simu, nikaweka mikono yangu kichwani na kulia.

Ilikuwa ni hapo kwamba nilifurahia kujitenga kijamii. Katika nyakati za kawaida, pengine ningekuwa na mazungumzo hayo uso kwa uso. Kulia ingekuwa ni jambo la aibu, nikisema kwa uchache.

Angalau kwa njia hii ningeweza kulia kwa sauti bila kuonekana.

Nilipata hisia nyingi za uzito na kukata tamaa. Ninawezaje kukaa nyumbani kwangu bila kufanya chochote wakati mamilioni wanaonizunguka walikuwa wakilala njaa? Nilihisi nilihitajika kufanya kitu, na bado, kutokana na hali, sikujua nini cha kufanya.

Na kisha ujumbe wa pili ulikuja.

Ulikuwa kutoka kwa dada katika kata yangu, mtenda mema wa kudumu. Aliniambia kuhusu nyumba ya wazee ambayo alikuwa akiisaidia. Nyumba iliruhusiwa kuendelea kufanya kazi kipindi cha zuio la kubaki nyumbani na sasa ilikuwa ikisaidia kulisha watu wa ziada ambao kwa kawaida walitegemea mpango wa chakula ambao ulikuwa umelazimika kufungwa. Walihitaji chakula, na kilihitajika kingi.

Mwanzoni, nilipanga kwenda tu nyumbani kwa rafiki yangu na kupeleka misaada ya chakula. Lakini kadiri muda ulivyoenda, wazo lilinijia. Vipi ikiwa nitafungua nyumba yangu iwe kama kituo cha makusanyo? Vipi ikiwa, badala tu ya kutoa msaada kwenye tatizo, nitengeneze “uwanja wa nguvu” ya ushawishi wangu mwenyewe?

Nilitengeneza bango la kidijitali kwa ajili ya kusambaza. Nilihakikisha uhalali wa kile nilichokuwa nakifanya. Nilikusanya makontena ya plastiki na kuyapanga nje ya geti langu. Kisha ilikuja sehemu ngumu: kutuma bango, sambamba na wito wa kusaidia, kwenye kundi langu la ujirani la WhatsApp (mtandao wa kijamii).

Kulikuwa na takriban washiriki 250 kwenye kundi, na nilijua baadhi wangekuwa wakosoaji makatili. Vipi ikiwa watanishambulia kwa kupendekeza kwamba watu watoke majumbani ili kuleta chakula? Vipi ikiwa nilikuwa nashutumiwa kimakosa kusambaza virusi? Vipi ikiwa nilimuweka mmoja wa watoto wangu wadogo watatu kwenye maambukizi ya COVID-19? Niseme tu ukweli mkamilifu, niliogopa.

Baada ya kurudia kuandika ujumbe takriban mara 20, moyo wangu ukiwa kwenye koo langu, hatimaye nilibofya tuma. Dakika chache baadaye nilipokea ujumbe kutoka kwa mtu nisiyemfahamu.

“Tutafurahia kupanga vyakula ndani ya boksi kwa ajili yako,” alisema. “Asante kwa hili.”

Kwa mara ya pili ndani ya siku chache, nilihisi macho yangu yakijawa na machozi.

Simu zilianza kupigwa muda mfupi baada ya hapo. Kulikuwa na watu ambao sikuwahi kukutana nao ambao walisikia kuhusu mradi kutoka kwa rafiki na walitaka kusaidia. Marafiki—wa ndani na nje ya nchi—wakitaka kutuma pesa taslimu kutoka mbali. Dada kutoka kwenye kata yangu akituma gari lenye mzigo kutoka kwenye bidhaa zake za jumla. Na mtiririko ulioonekana kutokoma wa watu nisiowafahamu kwa siri wakiweka unga wa mahindi, mchele na vyakula vya kwenye makopo nje ya geti langu.

Hatimaye, nilipata R100 000 pesa taslimu na misaada ya chakula. Baadhi ya akina dada kutoka kwenye kata yangu walishona barakoa 150 za vitambaa. Badala ya kusaidia nyumba moja, tuliweza kusaidia tatu. Mamia ya familia zilisaidiwa katika kipindi cha hitaji kubwa shukrani kwa muunganiko wa juhudi ndogo ndogo nyingi. Akisukumwa na uzoefu huu, rafiki yangu alianzisha shirika lisilo la kupata faida liitwalo Bubele (likimaanisha wema na ukarimu kwa lugha ya isiXhosa), kuwasaidia watu wasio na ajira kusafisha jiji na kupokea vifurushi vya chakula kama malipo.

Je, uzoefu huu ulinifunza nini? Ulinifunza muunganiko mtakatifu kati ya imani, tumaini na hisani.

Kuchukua hatua ile ya kwanza ya imani ilikuwa kitu kigumu na cha kuogopesha kwangu. Lakini matokeo?

Hisia kwamba Baba yetu wa Mbinguni anamjua na anamkumbuka kila mmoja wa watoto wake. Hisia kubwa ya upendo kwa binadamu wenzangu. Uwezo wa kuona vyema uwezo kwa kila mtu anayenizunguka. Ufahamu wa hisani, katika maana ya kweli ya neno hilo.

Sehemu ya kupendeza kuhusu hilo, hata hivyo, ilikuwa tumaini. Nilihisi kwamba hisia ya kukata tamaa inaanza kupotea. Nilihisi, kama Mzee Jeffrey R. Holland anavyoiweka, kwamba wakati ninapoonyesha imani na msimamo, ninaweza “kuendelea kusonga, kuendelea kuishi,” na muhimu zaidi, ninaweza “kuendelea kuwa na shangwe”.1

MUHTASARI

  1. Ona Jeffrey R. Holland, “This, the Greatest of All Dispensations“, Liahona, July 2007, 20.