2021
Yesu Kristo Anaujua Uchungu Tunaohisi kutokana na Chuki
Septemba/ Oktoba 2021


Yesu Kristo Anaujua Uchungu Tunaohisi kutokana na Chuki

Mwandishi anaishi Jimbo la Gauteng, Afrika Kusini.

Ombi langu ni kuwaona watu kama ambavyo Mwokozi angewaona.

Picha
people gathered on the Rome Italy Temple grounds

Wakati wa ufunguzi wa Hekalu la Rumi Italia, waumini na marafiki walizunguka sanamu ya Christus, kama inavyoonekana kupitia dirisha la kituo cha wageni.

Nimepitia chuki au unyanyapaa katika hali moja au nyingine kwa takribani miaka 20.

Baada ya kujiunga na Kanisa huko Msumbiji, nilihamia Afrika Kusini. Ni nchi nzuri, mojawapo ya nchi zilizofanikiwa Afrika. Uzuri wake unakuzwa na utofauti wa watu wake na utajiri wa tamaduni.

Afrika Kusini ni nchi ambayo bado inayojiponya kutokana na historia iliyogubikwa na ubaguzi wa rangi. Ingawa siasa ya ubaguzi wa rangi ilikoma rasmi mnamo 1994, makovu ya sera hii ya serikali ya ubaguzi wa rangi bado yapo.

Kama mwanamke mweusi wa Siku za Mwisho wa Msumbiji ninayeishi Afrika Kusini kwa miaka 18 iliyopita, nauona unyanyapaa na kutengwa, mara nyingi ukionyeshwa kama uchokozi mdogo. Ubaguzi wa rangi, matabaka, ukabila, jinsia na chuki dhidi ya wageni ni baadhi ya mifano michache ya machungu ya unyanyapaa ambao jamii bado inaupitia. Kuna kitu ndani ya mwanadamu wa tabia ya asili ambacho kinaonekana kutaka kuigawa jamii na kutuaminisha kwamba kuwa tofauti ni vibaya.

Tunachojaribu Kufanya

Je, waumini wa Kanisa wanaathiriwa na namna hii ya kufikiri? Bila shaka. Tunapaswa kumvua mwanadamu wa tabia ya asili katika juhudi zetu za maisha yote za kuwa watakatifu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo (ona Mosia 3:19).

Pale ambapo mimi pamoja na watoto wangu tunahisi kutengwa, kupuuzwa, kukandamizwa, au kutazamwa kwa wasiwasi, tunarejea nyumbani na kuzungumzia hilo. Tunajiuliza, “Nini kimetokea? Hebu tulisahau hili. Hebu tuzungumze kuhusu kwa nini watu wana tabia hii.” Kulizungumzia hutusaidia kupoza hisia zinazochemka ndani yetu

Ninajaribu kuwafundisha watoto wangu kwamba ubora wetu unapimwa kwa jinsi tunavyowatendea watu walionyanyapaliwa au kutengwa katika jamii (ona Mathayo 25:40). Hiyo inaweza kumaanisha kutafuta njia za kuwafikia wengine ili tusiwatenge.

Ninajaribu Kuwa Kama Yesu

Kadiri ambavyo uzoefu mwingine ulivyo na uchungu, mafunzo tunayojifunza yanawafanya watoto wangu kuwa watu bora. Na mimi pia. Kukata kwetu tamaa kumetusaidia kukuza huruma na faraja kwa ajili ya wengine.

Uzoefu wa chuki unanipa fursa ya kuchagua. Je, niwe mwenye chuki na kutojali, au nimpe mtu huyo sio tu fursa nyingine bali fursa ya pili, ya tatu, na ya nne? Je, niione jamii kama sehemu mbovu au niwe chachu ya mabadiliko chanya?

Mwokozi pia alipitia chuki kwa sababu ya vile Alivyokuwa, kile Alichoamini na kule Alikotoka (ona Yohana 1:46). Lakini bado hakujibu kwa fujo, hasira, uchungu au chuki. Alifundisha dhidi ya mambo haya yote na kutenda kwa upendo na ukweli. Alifundisha kwamba nguvu na ushawishi huja kupitia mazungumzo mazuri, uvumilivu, upole unyenyekevu, na upendo (ona Mafundisho na Maagano 121:41). Alifundisha kwamba tunapokosewa, tunapaswa kumwendea mkosaji na kulitatua kwa pamoja (ona Mathayo 18:15). Alitufundisha kuomba kwa ajili ya wale wanaotutesa (ona Mathayo 5:38–48). Na alipohukumiwa bila haki na kutundikwa msalabani ili afe, alitufundisha kusamehe (ona Luka 23:34).

Hatimaye, ni upendo Wake utakaotubadilisha sisi na ulimwengu (ona 2 Nefi 26:24)

Na Nitaendelea kujaribu

Mimi sio mkamilifu; sisamehi haraka kila mara baada ya mtu kunikwaza. Inahitaji muda, inahitaji uponyaji na inahitaji Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nami. Wakati mwingine ninachagua kukwazika, na inachukua muda kukumbatia msukumo Wake. Lakini kama mimi ni muwazi Kwake, Roho kwa subira hufanya kazi pamoja nami mpaka niweze kuelewa kile ambacho Baba wa Mbinguni angependa nifanye katika hali hiyo.

Ombi langu ni kuwaona watu kwa dhati kabisa kama ambavyo Mwokozi angewaona. Ili kufanya hivyo, ni lazima tuwe tayari kutambua kwamba hatuna majibu yote. Tunapokuwa radhi kusema, “mimi sio mkamilifu; nina mengi ya kujifunza. Ninaweza kujifunza nini kutoka kwenye mtazamo wa wengine?”—hapo ndipo tutaweza kwa dhati kusikiliza. Hapo ndipo kwa dhati tutaweza kuona.

Ninapopita katika safari hii, inanisaidia kukumbuka kwamba niko hapa kwa sababu maalum, kwamba magumu ya maisha ni ya muda tu—sehemu muhimu ya maisha—na kwamba siko peke yangu. Kupitia yote, mimi ninajaribu kuwa kama Yesu! Kujaribu ni tendo hai na pale tunaposhindwa, tunaweza kujaribu tena.