2022
Ibada na Baraka za Ukuhani
Machi 2022


Mambo muhimu ya Kitabu cha Maelekezo

Ibada na Baraka za Ukuhani

Bwana amesema, “tayarisheni kila kitu kinachohitajika” (M&M 88:119). Je, tumejiuliza hivi karibuni, “kila kitu kinachohitajika Ni NINI?” Kwa hakika kuna vitu vingi vya kimwili tunavyotayarisha na kuweka kwenye mpangilio kila siku, kila wiki, kila mwezi au kila mwaka. Lakini ni vitu gani vya kiroho ambavyo kwavyo tunahitaji kujitayarisha?

Mwaka huu, hebu tutenge muda wa kurejelea nyuma na kutafakari: tuko wapi kwenye njia ya agano kuelekea wokovu na kuinuliwa? Je, tumepokea ibada zote okozi? Kama bado, ni nini kingine tunahitaji kufanya?

Kitabu cha Maelekezo ya Jumla kuhusu ibada za ukuhani na baraka, kinafundisha kwamba ukuhani unajumuisha mamlaka ya kufanya ibada za injili zilizo muhimu kwa ajili ya wokovu na kuinuliwa.1 Wakati wenye ukuhani wanapotekeleza ibada na baraka hizi, wanafuata mfano wa Mwokozi wa kuwabariki wengine. Ibada na baraka za ukuhani huruhusu nguvu ya Mungu kujidhihirisha (ona M&M 84:20). Ibada na baraka lazima zifanywe kwa imani katika Mungu Baba na Yesu Kristo na kulingana na mwongozo wa Roho Mtakatifu.

Tunafanya maagano matakatifu na Mungu pale tunapopokea ibada hizi okozi. Kila moja ni muhimu kwa ajili ya wokovu na kuinuliwa kwetu. Hizi ni ubatizo, uthibitisho na kipawa cha Roho Mtakatifu, kutunukiwa Ukuhani wa Melkizedeki na kutawazwa kwenye ofisi (kwa wanaume), endaumenti ya hekaluni na kuunganishwa hekaluni. Ibada hizi ni kipaumbele cha kwanza katika kuendelea kwetu. Katika kuheshimu maagano haya matakatifu, tunapiga hatua muhimu kwenye njia ya agano kuelekea uzima wa milele.

Baba yetu wa Mbinguni ametupatia ibada na baraka zingine ambazo hufanya iwezekane kwetu kupokea nguvu Yake, uponyaji, faraja na mwongozo. Hizi hujumuisha kutoa jina na kuwabariki watoto, sakramenti, kutunukiwa Ukuhani wa Haruni, baraka za patriaki, kuitwa kwa ajili ya kutumikia katika miito, kuweka wakfu mafuta, kubariki wagonjwa, baraka ya faraja na ushauri (ikijumuisha baraka ya baba), kuweka wakfu makazi na kuweka wakfu makaburi.

Tunaweza kuwa tunapitia wakati mgumu ulimwenguni leo, lakini kama tukifokasi kwenye vitu vya umuhimu wa milele na kuhakikisha kwamba vitu vyote kiroho vimetayarishwa na kwa utaratibu, tunaweza kuwa na amani kadiri tunavyosonga mbele kila siku. Tunaweza kuwasaidia wengine njiani. Tunaweza kutazama mbele tukiwa na “mng’aro mkamilifu wa tumaini” (ona 2 Nefi 31:20).

Muhtasari

  1. Ona Kutabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.0–3.4.