2023
Nina Shukrani “Kumsikiliza Yeye”
Septemba 2023


“Nina Shukrani “Kumsikiliza Yeye,’” Liahona, Sept. 2023.

Nina Shukrani “Kumsikiliza Yeye”

Nimekuwa na wakati mgumu kusikia kanisani, lakini hadithi kutoka katika Agano Jipya ilinisaidia nione hali yangu kwa njia tofauti.

Picha
mtu amesimama kwenye mimbari

Nimekuwa na matatizo makubwa sana ya kusikia maishani mwangu na ninaweza tu kuelewa karibu asilimia 20 ya kile kinachosemwa kwenye mimbari wakati wa mkutano wa Kanisa. Mara kwa mara, kutokusikia kwangu hunifanya nihisi mpweke na kutengwa, kama vile wakati mkusanyiko unapocheka maneno ya ucheshi ya mnenaji lakini mimi sicheki kwa sababu sikusikia. Na sikuwa peke yangu. Waumini wazee wa kata walinipa siri kwamba wao pia wana shida ya kusikia.

Wakati mwingine, baada ya kutaabika kumwelewa mnenaji mwenye sauti ya chini katika mkutano wa sakramenti au wakati mwalimu wa shule ya Jumapili anapotangaza hakuna haja ya kutumia kipaza sauti kwa sababu kila mtu anaweza kusikia, mimi hujiuliza kwa nini naenda kanisani hali ninasikia kidogo tu. Je, isingekuwa vyema kutumia muda wangu nikisoma masomo ya Njoo, Unifuate au kujifunza maandiko?

Bado, nilitaka kuwa mtiifu na kuendelea kuhudhuria pamoja na familia yangu kufanya upya maagano yangu ya ubatizo na kumkumbuka Mwokozi kwa kupokea sakramenti. Daima imekuwa baraka kumhisi Roho, na daima nilihisi kuinuliwa na mambo yale ambayo ningeweza kuyasikia.

Picha
Yesu na mwanamke mwenye kutokwa na damu

Jumapili moja mshauri mkuu ambaye alizungumza katika mkutano wa sakramenti alikuwa mmoja wa wale wenye sauti safi, ya kusikika ambayo ilifanya iwe rahisi kusikia. Alizungumzia hadithi ya mwanamke ambaye aliteseka kutokana na kutokwa na damu kwa miaka 12 na alikuwa na imani kwamba angeponywa ikiwa angenyosha mkono na kugusa joho la Yesu alipokuwa akitembea (ona Luka 8:43–48).

Mnenaji kisha alitoa umaizi wa kugusa moyo ambao ulinichoma ndani, alieleza kwamba kwa sababu ya hali yake, mwanamke huyu angechukuliwa kuwa mchafu na yawezekana sana asingeruhusiwa kuhudhuria kanisani. Kwa miaka 12!

Matokeo ya hilo yalinishusha pumzi. Ingawa ni mgonjwa, mwanamke huyu pengine hakuwa akijisikia vibaya kwamba hangeweza kuhudhuria kanisani, angalau mara kwa mara. Lakini kwa sababu ya desturi za kijamii za nyakati hizo, yeye hakuruhusiwa kuhudhuria. Ni jaribu baya kiasi gani kwa imani ya mtu!

Nilipokuwa nikitafakari maumivu ya moyo aliyopitia kwa kuzuiwa kumwabudu Mungu na waaminio wenzake kwa sababu ya hali yake ya kimwili—jambo ambalo yeye hakuwa na udhibiti nalo—Roho alinifungua macho yangu kwa jinsi hali yake ilivyolingana na yangu mwenyewe. Nilipata uelewa kwamba ingawa nisingeweza kuwa mshiriki kikamilifu, angalau nilikuwa na fursa ya kuhudhuria kanisani na kusikia kile ambacho ningesikia. Mwanamke huyu hakuwa na uchaguzi sawa na huo. Nilihisi kuaibika kwa nyakati nilizofikiria kubaki nyumbani.

Papo hapo, Mungu alizungumza na moyo wangu, akinijulisha kwamba Yeye hakutaka mimi nihisi hatia. Yeye alitaka mimi nihisi shukrani—shukrani kwa ajili ya fursa ya kuhudhuria kanisani na kuimarishwa na kujumuika na wafuasi waaminifu wa Kristo. Ingawa nisingeweza kusikia kila kitu, ningeweza kuelewa baadhi ya vitu—na kila kimoja kilibariki maisha yangu. Kulikuwa pia na nyakati maalumu wakati Roho aliponisaidia nielewe vile vitu ambavyo nisingeweza kuvisikia.

Nilihisi shukrani kwa ajili ya uhuru wa kumwabudu Mungu na kufurahia baraka za kwenda kwenye nyumba Yake. Roho alinishuhudia kwamba ilikuwa vyema, vyema sana kwangu kuwa katika mikutano ya Kanisa, kupokea sakramenti, na kujifunza kile ambacho ningeweza kujifunza kuliko kutohudhuria kabisa.

Siku hiyo mtazamo wangu ulibadilika. Badala ya kuhisi kukata tamaa kwa ajili ya upungufu wangu, amani ilijaza moyo wangu, na niliamua kufokasi kwenye baraka za kuhudhuria kanisani. Niliamua kufanya juhudi za dhati kuwa na shukrani kwa ajili ya kile ambacho ningeweza kusikia badala ya kuvunjwa moyo na kile ambacho nisingeweza kusikia.

Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema: “Kuwa na shukrani wakati wa nyakati za dhiki haina maana kwamba tunapendezwa na hali zetu. Ina maana kwamba kupitia macho ya imani tunatazama zaidi ya changamoto zetu za sasa.”1 Yule mwanamke aliyenyoosha mkono kugusa joho la Yesu alikuwa ukumbusho wa kupendeza kwangu kuwa na imani ya kutosha katika Bwana ili kuona zaidi ya upungufu wangu na tumaini la kutosha katika Mungu ili kujua Yeye atanibariki kuinuka juu ya upungufu wangu wa kimwili.

Maisha huja na aina zote za changamoto ambazo zitatushinikiza kiroho, kihisia, au kimwili, lakini hata nyakati za dhiki, tunahimizwa kuwa na shukrani kwa ajili ya baraka tunazopata. Bwana alisema:

“Ninawaambia marafiki zangu, msiogope, mioyo yenu na ifarijike; ndiyo, furahini siku zote, na toeni shukrani katika kila kitu. …

“… Na mambo yote ambayo kwayo mmeteswa yatafanya kazi kwa pamoja kwa faida yenu, na kwa utukufu wa jina langu” (Mafundisho na Maagano 98:1, 3).

Mwandishi anaishi Utah, Marekani.

Muhtasari

  1. Dieter F. Uchtdorf, “Shukrani katika Hali Zozote,” Liahona, Mei 2014, 76.