2023
Hatimaye Kuelewa Kile Inachomaanisha Kupendwa na Mungu
Septemba 2023


“Hatimaye Kuelewa Kile Inachomaanisha Kupendwa na Mungu,” Liahona, 2023.

Vijana Wakubwa

Hatimaye Kuelewa Kile Inachomaanisha Kupendwa na Mungu

Nilikuwa nimesahau juu ya nguvu za kujua utambulisho wa kiungu.

Picha
nyuso za wasichana zikiwa na machozi

Kielelezo na Alecia Schubert

Nilipokuwa kijana, familia yangu ilihama katoka Hangari hadi Ujerumani. Nilikuwa na msisimko kuhamia huko, lakini iligeuka kuwa miaka tisa migumu ya maisha yangu.

Nilitaabika kujifunza Kijerumani, na daima nilikuwa mwepesi kukasirika, vitu ambavyo vilifanya iwe rahisi mimi kuonewa. Thamani yangu binafsi ilishuka. Baada ya muda nilihisi kama nilikuwa sipendwi na nikawa na matumaini kidogo kwa ajili ya siku za usoni. Nilijiuliza ikiwa ulimwengu ungekuwa bora bila mimi na wakati mwingine hata nilikuwa na mawazo ya kujiua.

Lakini kwa namna fulani, kupitia mateso yote, nilijua nilipatiwa uhai kwa sababu fulani, hata kama sikuelewa kikamilifu kwa nini. Nilijua ningeweza kupata nuru ya Mwokozi hata katika nyakati za kiza (ona Etheri 12:4). Wakati ulimwengu ulioneka kugeuka dhidi yangu, nilijua mahali pa kumpata Yeye na kile ambacho Yeye angenifanyia kama ningemtafuta katika maandiko, sala, na kufanya vyema niwezavyo kuwa mfuasi Wake. Ilikuwa hasa kuishi injili Yake ambako kulinipatia kiasi fulani cha amani na kunisaidia nisonge mbele katika kipindi hiki kigumu.

Ukweli Niliokuwa Nimeusahau

Hatimaye, mimi na familia yangu tulirejea tena Hangari. Nilikuwa nimehitimu shule ya upili, na ingawa siku zangu za uonevu zilikuwa zimeisha, bado nilikuwa ninakosa kujiamini. Matokeo ya kutendewa vibaya kwa kweli yaliniathiri, na wakati mwingine nilitilia shaka thamani yangu.

Na kama kijana mkubwa, nilitaka sana kujiamini katika kufanya maamuzi makubwa ya maisha na kuamua kile nilichotaka kutimiza katika maisha.

Wakati nikitaabika na haya, nilihisi kusukumwa kuhudhuria mkutano mkuu kwa ajili ya vijana wakubwa katika Ulaya mashariki. Nilihitaji mwongozo fulani wa kiroho katika maisha yangu ili unisaidie kuongeza thamani yangu na nilisali ili nipate majibu huko.

Usiku mmoja katika mkutano mkuu, chunusi zilisisimka kwenye mikono yangu wakati mnenaji kwenye mkutano alipoanza kuzungumza kuhusu jinsi alivyoonewa alipokuwa mtoto. Alizungumza kuhusu jinsi wakati mmoja alivyohisi kutokuwa na thamani na kutotambulika. Mara moja nilianza kulia.

Alieleza kile hasa nilichokuwa nimekipitia.

Mnenaji aliendelea na kushiriki ukweli aliokuwa ameushikilia wakati wa changamoto zake—ukweli niliokuwa nimeusahau:

“Mimi ni mwana wa Mungu.”

Kukumbatia Utambulisho Wangu wa Kiungu

Wakati mkutano ulipokwisha, bado nilikuwa na machozi yakitiririka usoni mwangu. Mnenaji aligundua na akaja na kuweka mikono yake kunizunguka. Aliniambia kwamba yeye kwa kawaida haji kuzungumza kwenye mikutano lakini alihisi msukumo kwamba kulikuwa na mtu mmoja aliyehitaji kusikia ujumbe wake moja kwa moja.

Mimi nilikuwa mtu huyo.

Uzoefu huu ulinionesha jinsi Baba wa Mbinguni anavyojua kikamilifu kuhusu watoto Wake na kwamba Yeye anajua hasa jinsi ya kutufikia ili tuweze hata kuhisi mng’aro wa upendo Wake wa mzazi. Alijua mimi nilihitaji kusikia ujumbe wa mnenaji huyu na alikuwa amenielekeza kuwa mahali sahihi kwa wakati sahihi.

Nimejua kirai hiki, “Mimi ni Mwana wa Mungu” maisha yangu yote, lakini ukweli wake ulivuma zaidi nafsini mwangu wakati huo. Hakika nilitambua kile inachomaanisha kuwa mwana wa Mungu mkamilifu ambaye anatupenda sisi kiasi kwamba Yeye alikuwa tayari kumtoa dhabihu Mwana Wake ili sisi tuweze kuishi tena na kukombolewa kutoka dhambi zetu. Ambaye ananipenda sana kiasi kwamba wakati Yeye daima hawezi kunilinda kutokana na uchungu, Yeye yu pamoja nami wakati huo na anaweza kunisaidia niinuke juu ya uchungu, nikue kutokana na uchungu na nirudi Kwake.

Yeye ananipenda sasa, na Yeye alinipenda bila kukoma wakati wa maisha yangu ya uonevu wakati nilipohisi hakuna yeyote aliyenipenda. Ninajua sasa kwamba ilikuwa hivyo kwa sababu nilijua ukweli huu kiasi kwamba nilichagua kusonga mbele.

Rais Russell M. Nelson hivi karibuni alifundisha juu ya nguvu za kujua utambulisho wetu wa kiungu. Alisema: “Marafiki zangu wapendwa, nyinyi kiuhalisia ni watoto wa kiroho wa Mungu. … Lakini je, huo ndiyo ukweli wa milele uliochapwa juu ya moyo wako? …

“Usifanye makosa kwenye hili: Uwezekano wako ni wa kiungu. Kwa utafutaji wako kwa bidii, Mungu atakupatia taswira ndogo ya kile unachoweza kuwa.”1

Sasa ninapojikuta nikitilia shaka thamani yangu, daima najikumbusha ukweli kwamba mimi ni mwana wa Mungu na kwamba maisha yangu ni zawadi kutoka Kwake.

Kumbuka kwamba wewe ni mtoto wa Mungu. Na kamwe usisahau nguvu za kiroho zinazohimili, zinazobadilisha maisha, na za kipekee ambazo hutokana na kukumbatia ukweli.

Mwandishi anaishi Szeged, Hungary.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.