2023
Ubatizo wa Usiku wa Ijumaa
Septemba 2023


“Ubatizo wa Usiku wa Ijumaa,” Liahona, Sept. 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Ubatizo wa Usiku wa Ijumaa

Tamanio langu la kutubu lilinisaidia kumpata Mwokozi na Kanisa Lake.

Picha
mwanamke akiwa amesimama mbele ya kanisa

Kielelezo na Katy Dockrill

Baada ya kupata uzoefu wa msisimko wa mwanzo wa kuja Marekani kutoka China ili kupata PhD yangu, nilizidiwa na utafiti wa mara kwa mara niliopaswa kuusoma na kuuandika. Pia sikuwa na uhakika kuhusu jinsi ya kuchangamana na mshauri wangu wa kitaaluma, ambayo iliniongezea shinikizo. Nilihisi kupotea na upweke, na sikujua cha kufanya.

Nilihitimisha kwamba makosa yangu ya awali yalisababisha mateso yangu na nilihitaji kutubu. Ilikuwa jioni, kwa hiyo nilitafuta “kanisa” mtandaoni. Nilipata kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lilikuwa ndilo kanisa pekee lililokuwa wazi hadi saa 3 usiku. Nikiazimia kutubu kanisani, nilianza kutembea kwa muda wa saa moja.

Nilipowasili kanisani saa 12 jioni, niliona taa na kusikia kicheko na muziki vikitokea ndani. Nilitafuta kwenye jengo hilo lakini sikuweza kupata mlango. Kupitia dirishani, nilimwona baba pamoja na mwanawe katika mojawapo ya vyumba. Niligonga dirisha ili apate kuniona. Akanielekeza mlangoni, akanikaribisha ndani, na akaniambia kwamba kulikuwa na mtu akibatizwa.

Nilifuata mwongozo wake na nikaingia chumba ambapo kulikuwa na mwanamume akitoa baraka kwa mvulana ambaye alikuwa amebatizwa punde. Nilisimama karibu na mlango, kusikiliza baraka zilizotolewa, nilihisi kwamba Mungu alikuwa pia ananong’oneza baraka kwangu. Moyo wangu ulichangamka, na nilihisi kile ambacho baadaye nilikuja kujua kilikuwa Roho Mtakatifu. Pia nilisikia sauti ikisema kwamba nilikuwa nimesamehewa.

Baada ya ubatizo, nilikusanyika na wengine na kukutana na watu wengi wakarimu. Sikuhisi mpweke tena. Mtu ambaye alijitambulisha kama “rais wa tawi” wa awali alijitolea kunirudisha nyumbani kwa gari. Miezi kadhaa baadaye, baada ya kupata masomo ya wamisionari, nilibatizwa.

Katika siku yangu ya ubatizo mnamo 2018 huko Cambridge, Massachusetts, kaka mmoja alizungumza kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni alivyokuwa amepanga huo ubatizo wa siku ya Ijumaa. Alieleza kwamba ubatizo ulikuwa ufanyike Jumapili iliyofuata, lakini kwa sababu ya mpishano wa muda, ilibidi upangwe usiku wa Ijumaa. Bila mabadiliko hayo, kamwe nisingeweza kulijua Kanisa, Mwokozi wetu, na Baba yetu wa Mbinguni, na akina kaka na akina dada katika injili.