2021
Kulindwa kwa madhumuni: vita, uingiliaji mtakatifu na kuwa chombo katika mikono ya Bwana
Septemba/ Oktoba 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Kulindwa kwa madhumuni: vita, uingiliaji mtakatifu na kuwa chombo katika mikono ya Bwana

Jinsi Bwana alivyotuma miujiza ili kuilinda familia ya Turay wakati wa kipindi cha machafuko huko Liberia na Sierra Leone.

Mwaka mmoja baada ya Mohamed Turay kujiunga na Kanisa huko Caldwell, Liberia, vita ya mwaka 1989 ililipuka. Waasi walipokuwa wanakaribia Caldwell, aliwaona watu kwenye jumuiya yake wakiondoka. Alikuwa amepata ndoto ambapo bomu lilianguka karibu na nyumbani kwake. Hatimaye, baada ya kuona makala kwenye gazeti ikielezea jinsi watu walivyokuwa wakikatwa vichwa, Mohamed alijua kwamba yeye na familia yake walikuwa hatarini na alipanga kuikimbia Caldwell. Mohamed aliamini kwamba ndoto ile ilikuwa ni onyo kutoka kwa Mungu. “Ilikuwa ni baraka kwa familia yangu,” Mohamed alisema. “Baraka ya muhimu.”

“Njoo,” alimwambia Abie, mkewe. “Leo, hatutalala hapa.” Mohamed alimchukua Abie na watoto wao hadi mpakani ambapo wangekuwa salama. Lakini alihitaji kurudi Caldwell ili kufanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuondoka kwao. Masaa kadhaa tu kabla waasi hawajauteka mji, Mohamed alifanikiwa kutoroka na kujiunga na familia yake.

Familia ya Turay ilianzisha makazi mapya huko Bo, Sierra Leone. Ingawa hapakuwa na uwepo wa Kanisa huko, walihimizwa kubaki na kusaidia kuanzisha tawi. Walianzisha kikundi cha nyumbani chenye washiriki watano tu wa familia ya Turay. Haikuchukua muda baada ya wao kuanza kuzungumza na watu kuhusu Kanisa, wamisionari waliwasili na huduma ya kwanza ya ubatizo ikafanyika huko Bo. Katika siku hiyo maalum, watu 31 walibatizwa katika Mto Sewa. Mohamed punde aliitwa kusimamia Wilaya mpya ya Bo Sierra Leone. Chini ya uongozi wa Mohamed, tawi moja dogo hatimaye lilikua kuwa matawi manne.

Mnamo 1991 vita ililipuka tena—wakati huu ikiwa ni Sierra Leone—iliyopelekea miaka kumi ya njaa na vurugu. “Waasi walikuwa wakiwaua wananchi na barabara ya kwenda Freetown ilifungwa,” alisema Mohamed. Hakukuwa na chakula cha kutosha kuwalisha watoto wao na Mohamed pamoja na Abie walijua kuwa walihitaji msaada wa Bwana, hivyo walipiga magoti pamoja katika sala. Punde tu walipomaliza sala yao, kiongozi wa Kanisa alifika kwenye mlango wao akiwa na kifurushi kilichokuwa na pesa ya kutosha kununulia mfuko wa mchele kwa kila familia kwenye wilaya. Sala yao ilikuwa imejibiwa.

Mapigano yalipofika Bo, Mohamed aliwindwa kama kiongozi wa dini katika jumuiya hiyo. Alilazimika kutengana na familia yake na kujificha dhidi ya waasi mpaka ilipowezekana kuungana tena na familia yake. Wakati familia ilipoungana tena, walijua walipaswa kuondoka. Lakini kwenda wapi? Na kwa jinsi gani? Walipokuwa wakiandaa mpango wao, mvulana mmoja aliwajia na kuwauliza walipokuwa wakienda. “Tunataka kutoroka kutoka hapa,” Mohamed alisema. “Nifuateni,” mvulana yule aliwaambia. Baada ya kumfuata mvulana yule porini kwa masaa kadhaa, ghafla alitoweka. “Tulipopepesa macho yetu, hatukumuona,” alisema Mohamed. “Huo ulikuwa ni muujiza mkubwa sana ambao kamwe hatutausahau.”

Waliendelea na safari yao lakini walijua usalama wao ulitegemea wao kusafiri katika ardhi yenye hatari bila kufanya kelele. Walihofia kwamba kilio cha mtoto wao mdogo kingewaweka kwenye hatari, lakini, kama Mohamed alivyokumbuka baadaye, “malaika walifumba kinywa chake; hakulia kabisa.” Waliendelea kusafiri kupita vijiji vingine vitatu—safari ngumu sana katika eneo lenye hatari—mpaka walipofika kwenye usalama.

Baada ya kuondokana na hatari iliyokuwa mbele yao, Mohamed na Abie walirudi Bo na kujiunga na Watakatifu wengine katika kutafuta kila mmoja yuko wapi. “Karibu kila siku, tulitoka kwenda kuzunguka kuwaangalia waumini wetu,” alisema. “umoja ulikuwa umejengwa miongoni mwa waumini wa Kanisa.” Kwa kuongezea, chakula, blanketi, mavazi na vifaa vya usafi vilitolewa kupitia matoleo ya mfungo ya Watakatifu ulimwenguni kote—zawadi iliyowasaidia familia ya Turay kutambua thamani ya zaka zao wenyewe pamoja na matoleo ya mfungo.

Baada ya vita, Watakatifu huko Bo walisaidia kujenga upya jumuiya yao. Abie alifanya kazi katika vituo vya afya na kushiriki mafunzo yake pamoja na wataalamu wengine katika kuwasaidia watoto wanaozaliwa kupumua. Mnamo 2004 viongozi wa serikali na kabila wa eneo walihudhuria sherehe ya uchimbaji ardhi kwa ajili ya jengo la kwanza la Kanisa huko Sierra Leone. Miaka miwili baadaye, Mohamed alipumzishwa baada ya kuhudumu kwa miaka 14 kama Rais wa Wilaya. Katika kurejelea huduma hii, alisema “ninajua kwamba Bwana alihitaji kunitumia kama chombo katika mikono Yake ili kuifanya kazi Yake.”