2022
Baraka za Ibada za Hekaluni katika Maisha yetu—Sasa na Milele
Januari/Februari 2022


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Baraka za Ibada za Hekaluni katika Maisha yetu—Sasa na Milele

“Uzoefu wa kutukuka uliowekwa kumbukumbu na babu yangu mkuu unatusaidia sisi kutambua kwamba wakati tunapowasaidia mababu zetu kwenye ibada zao za hekaluni, shangwe yao huwa kuu.”

Kwa zaidi ya miaka 40, babu yangu mkuu, J. Hatten Carpenter, alihudumu kama mtunza kumbukumbu kwenye Hekalu la Manti. Kila siku angetembea kutoka nyumbani kwake huko Manti, Utah, kwenda Hekalu la Manti ili kutimiza majukumu na wajibu wake huko. Kama mtunza kumbukumbu wa hekaluni, alifahamu uzoefu mtakatifu wa kiroho ambao ulitokea ndani ya hekalu.

Uzoefu mmoja sawa na huo alioshiriki ulimhusisha patriaki akiangalia ubatizo kwa niaba ya wafu ukifanyika ndani ya hekalu katika mojawapo ya siku.

Anaeleza kwamba Patriaki aliona “roho za wale ambao walikuwa wakiwahudumia ndani ya kisima cha ubatizo. Pale, roho zilisimama kusubiri zamu zao, na, mtunza kumbukumbu alipoita jina la mtu ili kubatizwa kwa niaba, patriaki aligundua tabasamu la furaha likitoka kwa roho ambayo jina lake limeitwa, na ingeondoka kutoka kwenye kundi la roho wenzake na kwenda upande wa mtunza kumbukumbu. Hapo ingeshuhudia ubatizo wake mwenyewe ukifanywa kwa niaba yake, na kisha kwa uso wenye furaha ingeondoka ili kumpisha kiumbe mwingine mwenye bahati ambaye alipaswa kufurahia fursa sawa na hiyo”1.

Kadiri muda ulivyosonga, patriaki aligundua kwamba baadhi ya roho zilionekana zenye huzuni sana. Alitambua kwamba watu ndani ya hekalu walikuwa wamemaliza ubatizo kwa siku hiyo. Roho zenye huzuni zilikuwa zile ambazo ubatizo wao haungefanywa siku hiyo.

Babu yangu mkuu alisema, “‘mara kwa mara ninafikiria kuhusu tukio hili, kwani mara kwa mara mimi huketi mbele, na kuita majina kwa ajili ya ibada kufanyika ambayo humaanisha jambo kubwa sana kwa wafu’”2

Babu yangu mkuu alikuwa na ushuhuda uliotukuka wa umuhimu wa kila nafsi kupokea ibada takatifu. Ibada hizi ni muhimu kwa ajili ya wale wanaowajibika mbele za Mungu katika upande huu wa pazia na kwa ajili ya wale walio kwenye upande mwingine wa pazia. Ibada zinawasaidia wao kuendelea katika njia yao kuelekea kuishi na Mungu milele yote.

Maandiko yanathibitisha, “Kwa hiyo, katika ibada hizo, nguvu za uchamungu hujidhihirisha.

Na pasipo ibada hizo, na mamlaka ya ukuhani, nguvu za uchamungu haziwezi kujidhihirisha kwa mwanadamu katika mwili;

Kwani pasipo hizi hakuna mwanadamu anayeweza kuuona uso wa Mungu, hata Baba, na kuishi.”3

Kupokea ibada hizi si kigezo cha mwanadamu—ni kigezo cha Mungu. Si tu ni muhimu kupokea ibada, bali pia ni muhimu kwamba pale tunapokuwa tumezipokea, tunabaki wakweli na waaminifu kwenye maagano tunayofanya wakati tunaposhiriki katika ibada hizi takatifu.

Mzee Ronald A. Rasband wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitoa wito huu: “Anza sasa mchakato wa ‘kujikabidhi kwa Bwana’ kwamba Roho Wake awe nawe kwa wingi na viwango Vyake vitakuletea ‘amani ya nafsi.’ Acha nisisitize, iwe unaweza kufikia hekalu au la, unahitaji kibali cha hekaluni kilicho hai ili kuendelea kuwa imara kwenye njia ya agano.”4

Kuwa na kibali hai cha hekaluni humaanisha ushuhuda wako wa Mungu Baba na Mwana Wake Yesu Kristo uko imara. Unao leo ushuhuda wa Urejesho wa Kanisa Lake, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Unawaunga mkono na kuwaidhinisha manabii na mitume walio hai na viongozi wako wa Kanisa. Na unatii amri takatifu na ni mkweli kwenye maagano uliyoyafanya. Haimaanishi kwamba wewe ni mkamilifu, bali inamaanisha unabaki kwenye njia ya agano na kujaribu kutumia mafundisho ya Yesu Kristo katika maisha yako.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, Mungu amelipa Kanisa Lake mamlaka ya ukuhani Wake ili kutusaidia kufanya na kutunza maagano matakatifu ambayo yataturejesha kwenye uwepo Wake. Mahekalu matakatifu hutoa nafasi kwetu ya kupokea ibada za kuinua ambazo zitatuongoza kwenye uzima wa milele ikiwa tu wakweli na waaminifu. Mahekalu haya matakatifu pia hutoa njia kwa ajili ya mababu zetu waliofariki kunufaika kutokana na ibada sawa na hizo za kuinua. Tunapaswa kuwasaidia. Wokovu wao ni muhimu na wa msingi kwenye wokovu wetu. Kama vile Paulo anavyosema kuhusiana na mababu—“kwamba wao pasipo sisi hawakamiliki—wala sisi hatuwezi kuwa wakamilifu pasipo wafu wetu.”5

Kama vile babu yangu mkuu alivyoshuhudia, tunapowasaidia mababu zetu kwa ibada hizi, shangwe yao inakuwa kuu. Tunapowasaidia, sisi pia tunasaidiwa katika safari yetu wenyewe kuelekea ukamilifu.

Rais Nelson, katika Mkutano Mkuu wa Aprili 2021, aliongeza onyo hili:

“Mahekalu ni sehemu muhimu ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake. Ibada za hekaluni hujaza maisha yetu kwa nguvu na uwezo usiopatikana kwa njia nyingine yoyote. Tunamshukuru Mungu kwa baraka hizo.”6

Kila mmoja wetu na aishi kwa kustahili kuwa na kibali hai cha hekaluni. Na tutafute daima kuwa na kibali hai cha hekaluni. Na tuhudhurie hekaluni mara nyingi kadiri hali zetu zinavyoruhusu. Tunapofanya hivyo, ninaongeza ushuhuda wangu kwenye ule wa Rais Nelson kwamba maisha yetu yatajazwa kwa nguvu na uwezo usiopatikana kwa njia nyingine yoyote. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Matthew L. Carpenter aliitwa kama Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Machi 2018. Amemuoa Michelle (Shelly) Kay Brown; wao ni wazazi wa watoto watano.

Muhtasari

  1. Imenukuliwa kutoka Joseph Heinerman, Temple Manifestations [Manti, Utah: Mountain Valley Publishers, 1974], uk. 101–2; ona pia The Utah Genealogical and Historical Magazine 11 [July 1920]:119.

  2. Joseph Heinerman, Temple Manifestations, 102.

  3. Mafundisho na Maagano 84:20–22.

  4. Ronald A. Rasband, “Kujikabidhi kwa Bwana”, Liahona, Nov. 2020, 24–25.

  5. Ona Mafundisho na Maagano 128:15.

  6. Russell M. Nelson, “COVID-19 na Mahekalu”, Liahona, Mei 2021, 127.