2022
Kujifunza zaidi kuhusu Ukuhani wa Haruni
Januari/Februari 2022


NJIA YANGU YA AGANO

Kujifunza zaidi kuhusu Ukuhani wa Haruni

Gundua jinsi wanaume wa miaka 11 na zaidi wanavyoweza kubariki maisha ya wengine kupitia kutumia kwa haki mamlaka ya Mungu hapa duniani.

Ni siku ya furaha iliyoje kwa familia ya Mqadi. Baada ya milango ya hekalu kufungwa kwa miezi 14 kutokana na janga la ulimwengu la Uviko 19, hatimaye Nala Mqadi (msichana wa miaka 11) alipata fursa ya kutembelea hekalu kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2021.

Akikumbuka uzoefu huo baadaye, Nala anatoa baadhi ya mambo muhimu ya uzoefu huo. Alipenda amani na usafi wa jengo. Na alipenda kwamba angeweza kubatizwa na kaka yake mkubwa, Ntando.

Ntando (miaka 15) aliweza kufanya ibada hii takatifu kwa sababu anashikilia ukuhani wa Haruni. Ametawazwa hivi karibuni kwenye ofisi ya kuhani.

Ukuhani ni nguvu na mamlaka ya Mungu yanayotolewa kwa wanaume wenye kustahili wenye miaka 11 na zaidi. Ukuhani wa Haruni ni ukuhani wa utangulizi au wa maandalizi. Wanaume na wavulana wanaotawazwa kwenye Ukuhani wa Haruni wanayo mamlaka ya kupitisha, kuandaa na kubariki sakramenti na kuwabatiza wengine.

Ukuhani wa Haruni ulitolewa kwa Joseph Smith mnamo 1829 na Yohana Mbatizaji—Yohana Mbatizaji yule yule aliyembatiza Yesu. Kushikilia na kutumia Ukuhani wa Haruni huwaandaa wanaume kupokea ukuhani wa juu au Ukuhani wa Melkizedeki.

“Ilikuwa ya kupendeza kupata fursa ya kumbatiza dada yangu kwa mara yake ya kwanza,” Ntando anasema. “Pia nilimbatiza mama yangu kwa mara yangu ya kwanza kuweza kubatiza hekaluni. Ninayo fursa ya kuingia hekaluni na ninao uwezo wa kufanya ibada takatifu. Nimebarikiwa sana na uwezo huo na nimepokea baraka ya kumtumikia Bwana katika hekalu Lake.”

Kama ilivyo dhahiri kupitia uzoefu wa familia ya Mqadi, ingawa ukuhani hushikiliwa na wanaume, hutumika kubariki watoto wote wa Mungu.

Rais Dallin H. Oaks amesema, “Nguvu ya ukuhani hutubariki sisi sote. Funguo za ukuhani huongoza wanawake pamoja na wanaume, na ibada za ukuhani na mamlaka ya ukuhani huusika kwa wanawake pamoja na wanaume.”1

“Nilihisi kubarikiwa nilipokwenda hekaluni,” Nala aliongeza baadaye. “Ilikuwa ya kupendeza kubatizwa na kaka yangu.”

Kwa kaka mkubwa wa Nala, Ntando, ilikuwa pia ni siku ya kufanya mambo kwa mara ya kwanza. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya ubatizo wa wafu ndani ya hekalu. Kuweza kufanya hili kwa ajili ya wanafamilia yake ilikuwa ya muhimu kwake.

Mama wa ndugu hawa, Tshepiso, alisema, “Kuwa hekaluni kwa mara ya kwanza pamoja na Nala, na kumtazama Ntando akitumia ukuhani wa Haruni pia kwa mara ya kwanza kwenye kisima cha ubatizo ilikuwa maalum kwangu.

“Nashukuru kwa Roho aliyeshuhudia kwao juu ya utakatifu wa hekalu na huduma zinazofanywa ndani yake. Iligusa moyo wangu pale ambapo wote wawili kwa furaha waliomba kuhudhuria tena ubatizo wa hekaluni. Ni sala yangu kwamba uzoefu huu umeamsha hamu ndani yao ya kufanya zaidi ili kushiriki na kuwa sehemu ya kazi ya Bwana kadiri wanavyokuwa wakubwa.”

Muhtsari

  1. Dallin H. Oaks, “Funguo na Mamlaka ya Ukuhani,” Mkutano Mkuu Aprili 2014.