2023
Umuhimu wa Hekalu la Mungu katika Maisha Yako
Septemba 2023


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Umuhimu wa Hekalu la Mungu katika Maisha Yako

Mnamo Jumapili, Aprili 3, 1836—miaka chini ya 200 iliyopita—kufuatia uwekaji wakfu wa Hekalu la Kirtland, Nabii Joseph Smith na Oliver Cowdery walikuwa katika Hekalu la Kirtland ambalo lilikuwa limewekwa wakfu wiki moja iliyopita.

Joseph na Oliver walikuwa wakisali, mfuatano wa wajumbe wa mbinguni walikuja na kutunuku ushauri na mamlaka ili kukamilisha kazi kuu ya Mungu katika kipindi hiki cha mwisho ili kusaidia kuandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo wa kuongoza na kutawala Ulimwenguni.

Mjumbe wa kwanza alikuwa Yesu Kristo mwenyewe. Baada ya kuthibitisha Yeye ni nani na misheni Yake, aliwatangazia Joseph na Oliver kwamba dhambi zao zimesamehewa, na kwamba alilikubali hekalu la Kirtland ambalo lilikuwa ndio limejengwa na kuwekwa wakfu. Alitangaza kwamba “jina langu litakuwa humu; nami nitajionyesha kwa watu wangu kwa rehema katika nyumba hii” (M&M 110:7). Akaelezea zaidi kwamba angetokea (katika hekalu) kwa watumishi Wake na kuongea nao, na makumi elfu watashangilia kwa sababu ya baraka za hekaluni. Mwishowe, aliahidi kwamba umaarufu wa hekalu utasambaa ulimwenguni kote na baraka zingeanza kumiminwa juu ya vichwa vya watu Wake.

Kufuatia ziara ya Yesu Kristo, Musa alitokea na kutunuku mamlaka na funguo za ukuhani kwa ajili ya Kusanyiko la Israel. Kisha Elia alitokea na kukabidhi kipindi cha injili ya Ibrahimu, akiahidi kwamba kupitia sisi (waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho), uzao wetu na vizazi vyote baada yetu vitabarikiwa. Hatimaye, nabii Eliya alitokea na kutunuku funguo za kugeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto, na ya watoto kuwaelekea baba.

Wajumbe hawa wa mbinguni walikuja na kutoa mamlaka sahihi ili kwamba watoto wa Mungu wangepokea mwongozo endelevu kutoka kwa Yesu Kristo, na kazi kuu ya kukusanya pamoja watoto wa Mungu katika pande zote za pazia ingesonga mbele. Mamlaka yaliyotolewa kwa Joseph Smith ya kukamilisha kazi hii huendelea leo na yamewekwa kwa Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Rais Russell M. Nelson kwa sasa anashikilia na ameruhusiwa kutumia funguo zote za ukuhani ambazo huturuhusu sisi kupokea ibada ambazo huunganisha Duniani na Mbinguni.

Tunaposhiriki katika ibada za hekaluni sisi wenyewe, au kuwasaidia mababu zetu waliokufa kupokea ibada za hekaluni kwa niaba yao, tunafungua mbingu ili kwamba baraka ziweze kumiminwa kwa wingi juu yetu. Leo, mahekalu zaidi na zaidi yanaijaza Dunia.

Rais Russell M. Nelson alituhimiza kwa kusema: “Ni muhimu kwamba Mwokozi alichagua kutokea kwa watu hekaluni. Ni nyumba Yake. Imejazwa na nguvu Zake. Kamwe tusipoteze uoni wa kile Bwana anachotutendea sasa. Anafanya mahekalu Yake kufikika zaidi. Anaongeza kasi ya sisi kujenga mahekalu. Anaongeza uwezo wetu ili kusaidia kukusanya Israeli. Pia anafanya iwe rahisi zaidi kwa kila mmoja wetu kutakaswa kiroho. Ninaahidi kwamba muda wa ziada katika hekalu utayabariki maisha yako katika njia ambazo hakuna kingine kiwezacho. Wapendwa kaka na dada zangu, na mfokasi kwenye hekalu katika njia ambazo hamjawahi hapo kabla.” (Russell M. Nelson, Fokasi kwenye Hekalu, Oktoba 2022).

Unafanya nini ili kufokasi kwenye hekalu kuliko hapo awali katika maisha yako mwenyewe?

Kila muumini mwenye miaka 12 na zaidi anaweza kuwa na kibali cha hekaluni. Kama kwa sasa hustahili kuwa na kibali cha hekaluni, tafadhali kutana na askofu wako/rais wako wa tawi ili kujua unachohitaji kufanya ili upate kibali kwa kustahili.

Kama hujawahi kuwa hekaluni, na una kibali hai cha hekaluni, kutana na askofu wako/rais wa tawi ili ujiandae kuhudhuria hekaluni. Kama kwa sasa unaishi mbali na hekalu na unahitaji msaada wa gharama za usafiri kwenda hekaluni, kutana na askofu wako/rais wa tawi ili kupanga jinsi unavyoweza kunufaika kutoka kwenye Mfuko wa Msaada wa Hekalu. Gharama za usafiri zisikuzuie kuhudhuria hekaluni kwa ajili ya ibada zako binafsi za hekaluni.

Unapokwenda hekaluni kwa ajili ya ibada zako binafsi za hekaluni, zingatia pia kufanya historia ya familia na kukaa muda mrefu ili kufanya ibada kwa niaba ya mababu zako waliokufa ili na wao waweze kupokea ibada za hekaluni.

Mnamo Aprili 3, 1836, Yesu Kristo alianza kumimina baraka juu ya watu Wake wanaohudhuria hekaluni. Je, uko tayari kumruhusu Yeye kumimina baraka zaidi juu yako? Kama uko tayari, chukua hatua kuhudhuria hekaluni haraka iwezekanavyo.

Ninashuhudia kwamba unapojiandaa kuhudhuria hekaluni kwa kustahili na kufanya maagano matakatifu huko, na kuyatunza maagano hayo, utakuwa na amani kubwa katika maisha yako, nguvu kubwa ya kiroho na baraka zaidi kutoka mbinguni katika maisha yako. Katika jina la Yesu Kristo. Amina.