Liahona
Mwokozi wa Wote, Injili kwa ajili ya Wote
Machi 2024


“Mwokozi wa Wote, Injili kwa ajili ya Wote,” Liahona, Machi 2024.

Mwokozi wa Wote, Injili kwa ajili ya Wote

Injili, Upatanisho, na Ufufuko wa Yesu Kristo vinabariki watoto wote wa Mungu.

Picha
Kristo na mtu mwenye kupooza

Kristo na Mtu mwenye Kupooza, na J. Kirk Richards, isinakiliwe

Injili ya urejesho ya Yesu Kristo, ni, chanzo cha kwanza, cha juu zaidi na cha milele cha shangwe ya kudumu, amani ya kweli, na furaha kwa ajili ya kila mtu katika siku hizi za mwisho. Baraka ambazo zinamiminika kutoka kwenye injili na kutoka ukarimu usio na mwisho wa Kristo kamwe hazikusudiwi kwa ajili tu ya wachache waliochaguliwa, hapo kale au nyakati hizi za sasa.

Bila kujali jinsi gani tunavyohisi upungufu, na licha ya dhambi ambazo zinaweza kutuweka mbali kutoka Kwake kwa muda, Mwokozi wetu anatuhakikishia kwamba “ananyoosha mikono yake [kwetu] siku nzima” (Yakobo 6:4), kutualika sisi sote tuje Kwake na tuhisi upendo Wake.

Baraka za Injili kwa ajili ya Ulimwengu Wote

Injili ya Yesu Kristo “imerejeshwa katika siku hizi za mwisho ili kukidhi … mahitaji ya kila taifa, ukoo, ndimi, na watu duniani.”1 Injili inavuka mipaka ya utaifa wote na rangi wakati ikivuka mistari yote ya kitamaduni kufundisha kwamba “wote ni sawa kwa Mungu” (2 Nefi 26:33).2 Kitabu cha Mormoni kinasimama kama shahidi wa kustaajabisha wa ukweli huu.

Kumbukumbu hii kuu inashuhudia kwamba Kristo anayakumbuka mataifa yote (ona 2 Nefi 29:7) na atajionesha “mwenyewe kwa wale wote wanaomwamini, … [na kufanya] miujiza yenye nguvu, ishara na maajabu, miongoni mwa watoto wa watu”.(2 Nefi 26:13). Miongoni mwa miujiza hii yenye nguvu, ishara, na maajabu ni kuenea kwa injili. Kwa hiyo, tunawatuma wamisionari ulimwenguni kote kushuhudia juu ya habari zake njema. Sisi pia tunashiriki injili na wale wanaotuzunguka. Matumizi ya funguo za ukuhani zilizorejeshwa kwa ajili ya walio hai na wafu yanahakikisha kwamba utimilifu wa injili hatimaye utakuwa unapatikana kwa kila mwana na binti wa wazazi wetu wa mbinguni—zamani, sasa, au baadaye.

Moyo wa injili hii—kiini cha ujumbe wa kila nabii na mtume aliyeitwa wakati wowote kwenye kazi hii—ni kwamba Yesu ndiye Kristo na kwamba alikuja kumbariki kila mtu. Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunatangaza kwamba dhabihu Yake ya kulipia dhambi ni kwa ajili ya ulimwengu wote.

Hitaji kwa ajili ya Upatanisho Usio na Kikomo na wa Milele.

Ninapokwenda kuzunguka ulimwengu, ninafanya mahojiano na waumini tofauti tofauti wa Kanisa. Ninavutiwa kusikia jinsi wanavyohisi baraka za Upatanisho wa Yesu Kristo katika maisha yao, hata wakati wanapoungama baadhi ya dhambi zao za zamani. Jinsi gani ilivyo ya kupendeza kwamba faraja ya kusafisha ya Upatanisho Wake siku zote inapatikana kwetu sisi sote!

“Lazima upatanisho ufanywe,“ Amuleki alitamka, “ama sivyo wanadamu wote ni lazima bila kuepuka waangamie.” Tungekuwa milele “tulioanguka na … kuopotea, … isipokuwa kupitia upatanisho,” ambao ulihitaji “dhabihu isiyo na kikomo na ya milele.” Kwani “hakuwezi kuwa na chochote ambacho kimepungua kuliko upatanisho usio na kikomo ambao utatosheleza dhambi za ulimwengu” (Alma 34:9, 10,12)

Nabii mkuu Yakobo pia alifundisha kwamba kwa sababu “kifo kimewapata wanadamu wote, … inahitajika lazima pawe na nguvu ya ufufuo” kutuleta katika uwepo wa Mungu. (2 Nefi 9:6)

Vyote dhambi na mauti zilihitajika kushindwa. Hii ilikuwa ni kazi maalumu ya Mwokozi, ambayo Yeye kwa ujasiri aliikamilisha kwa ajili ya watoto wote wa Mungu.

Picha
Kristo katika Gethsemane

Gethsemane, na J. Kirk Richards, isinakiliwe

Dhabihu ya Mwokozi wetu

Katika usiku Wake wa mwisho katika maisha yake ya duniani,Yesu Kristo aliingia Bustani ya Gethsemane. Pale, Yeye alipiga magoti katikati ya miti ya mizeituni na kuanza kuteremka kwenye kilindi cha mateso ambayo wewe na mimi kamwe hatuwezi kuyajua.

Pale alianza kujichukulia juu yake Mwenyewe dhambi za ulimwengu. Alihisi kila maumivu, maumivu ya moyo, na huzuni, na Yeye alivumilia machungu makali yote na mateso unayopitia wewe na mimi, na kila nafsi iliyowahi kuishi au itakayoishi. Maumivu haya makubwa yasiyo na mwisho yalimsababisha [Yeye],… “ mkuu wa vyote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo” (Mafundisho na Maagano 19:18). Ni Yeye pekee angeweza kufanya hivi.

Hakukuwa na mwingine mzuri wa kutosha

Kulipa gharama ya dhambi.

Ni Yeye tu angeweza kufungua lango

La mbinguni na kuturuhusu tuingine.3

Yesu kisha alichukuliwa kwenda Kalvari, na katika mateso makali katika historia ya ulimwengu huu, Yeye alisulubiwa. Hakuna mtu ambaye angeweza kuuchukua uhai Wake kutoka Kwake. Kama Mwana Pekee wa Mungu, Yeye alikuwa na uwezo juu ya kifo cha kimwili. Angeweza kuomba kwa Baba Yake, na vikosi vya malaika vingeweza kuja kuwashinda watesi Wake na kuonesha utawala Wake juu ya vitu vyote. “Yatatimizwaje basi maandiko,” Yesu aliwauliza wasaliti wake, kwamba “hivyo ndivyo ilivyopaswa kujiri? (Mathayo 26:54).

Kutokana na utii mkamilifu kwa Baba Yake—na upendo mkamilifu kwa ajili yetu—Yesu kwa hiari yake alitoa uhai Wake na kuikamilisha dhabihu Yake isiyo na mwisho na dhabihu ya milele ya kulipia dhambi, ambayo inarudi nyuma zamani na inaenda mbele kote kwenye milele yote.

Ushindi wa Mwokozi Wetu

Yesu aliwaagiza Mitume Wake kuiendeleza kazi Yake baada ya kifo Chake. Ni kwa jinsi gani wangefanya hivyo? Baadhi yao walikuwa wavuvi tu wa kawaida, na hawakufunzwa katika sinagogi kwa ajili ya kazi hiyo. Wakati ule, Kanisa la Kristo lilionekana kuelekea kufa. Bali Mitume walipata nguvu kubeba wito wao na kutengeneza historia ya ulimwengu.

Nini kilisababisha nguvu kuja kutoka kwenye unyonge wa wazi kama ule? Kiongozi wa kanisa la Angalikana msomi Frederic Farrar alisema “Kuna jibu moja, moja tu linalowezekana nalo ni—ufufuko kutoka kwa wafu. Mageuzi haya yote makubwa mno yalisababishwa na nguvu za ufufuko wa Kristo.”4 Kama mashahidi wa Bwana aliyefufuka, Mitume walijua kwamba hakuna kitu chochote ambacho kingeweza kusimamisha kazi hii kuendelea. Ushahidi wao ulikuwa chanzo cha nguvu ya kukubalika kadiri Kanisa la mwanzo lilivyoshinda mambo yote.

Majira haya ya Pasaka kama mmoja wa mashahidi Wake aliyetawazwa, ninatangaza kwamba mapema asubuhi moja nzuri ya Jumapili, Bwana Yesu Kristo alifufuka kutoka kifo ili kutuimarisha sisi na kukata kamba za mauti kwa ajili ya kila mtu. Yesu Kristo yu hai! Kwa sababu Yake, kifo siyo mwisho wetu. Ufufuko ni zawadi ya Kristo ya bure na kwa watu wote

Picha
Kristo na Mariamu Magdalena Kaburini,

Kristo na Mariamu Kaburini, na Joseph Brickey

Njooni kwa Kristo

Injili na Upatanisho wa Yesu Kristo ni kwa ajili ya kila mmoja—hiyo ni, kila mtu. Njia pekee tunayopata uzoefu wa baraka kamilifu za dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi ni kwa mtu binafsi kukubali mwaliko Wake: “Njoo Kwangu” (Mathayo 11:28),

Tunakuja kwa Kristo wakati tunapoonesha imani katika Yeye na kutubu. Tunakuja Kwake wakati tunapobatizwa katika jina Lake na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Tunakuja Kwake wakati tunaposhika amri, kupokea ibada, kuheshimu maagano, kukumbatia uzoefu wa hekaluni, na kuishi aina ya maisha ambayo wafuasi wa Kristo wanayaishi.

Kuna nyakati, utakatishwa tamaa na kuvunjika moyo. Moyo wako unaweza kuvunjika kwa ajili yako wewe mwenyewe au mtu unayempenda. Unaweza kulemewa na mzigo wa dhambi za wengine. Makosa uliyoyafanya—yanaweza kuwa makubwa—yanaweza kukusababishia uwe na woga kwamba amani na furaha vimekuacha milele. Kwa nyakati kama hizo, kumbuka kwamba Mwokozi siyo tu anainua mzigo wa dhambi bali pia “[aliteseka] maumivu na mateso na majaribu ya kila aina”(Alma 7:11), ikiwa ni pamoja na ya kwako! Kwa sababu ya kile alichokipitia kwa ajili yako, Yeye binafsi anajua jinsi ya kukusaidia pale unapokubali mwaliko Wake wenye kubadilisha maisha: “Njooni Kwangu.”

Wote Wanakaribishwa

Yesu Kristo amefanya iwe wazi kwamba watoto wote wa Baba wa Mbinguni wawe na madai yaliyo sawa juu ya baraka za injili Yake na Upatanisho Wake. Anatukumbusha kwamba “wote wana haki sawa,na hakuna anayekatazwa” (2 Nefi 26:28).

“Anawaalika wote kuja kwake na kushiriki wema wake, na hamkatazi yoyote ambaye anakuja kwake, mweusi na mweupe, mtumwa na huru, mwanamume na mwanamke” (2 Nefi 26:33)

“Anawaalika wote”—hiyo inamaanisha sisi sote! Hatupaswi kuweka vitambulisho vya ovyo na utofautishaji wa bandia juu yetu wenyewe au wengine. “Kamwe hatupaswi kuweka mipaka yoyote kwenye upendo wa Mwokozi au kukaribisha mawazo kwamba sisi au wengine wapo mbali na hawawezi kufikiwa. Kama nilivyosema mapema, “Haiwezekani kwa [yeyote] kujishusha chini kuliko zaidi ya mwanga usio na mwisho wa Upatanisho wa Kristo unavyong’ara.”5

Badala yake, kama Dada Holland, na Mimi tulivyofundisha miezi michache tu kabla ya kufariki kwake, tunaamriwa “kuwa na hisani, hisani ambayo ni upendo” (2 Nefi 26:30).6 Huu ni upendo Mwokozi anaotuonesha sisi, kwani “Hafanyi chochote ila tu kwa manufaa ya ulimwengu, kwani “anaupenda ulimwengu hata kwamba anautoa uhai wake ili awavute wanadamu wote kwake” (2 Nefi 26:24).

Ninashuhudia kwamba injili na Upatanisho wa Yesu Kristo ni kwa ajili ya watu wote. Ninaomba kwamba kwa shangwe tukumbatie kwa furaha baraka ambazo Yeye anazileta.

Muhtasari

  1. Howard W. Hunter, “The Gospel—A Global Faith,” Ensign, Nov. 1991, 18.

  2. Ona Howard W. Hunter, “All Are Alike unto God” (Brigham Young University fireside, Feb. 4, 1979), 1–5, speeches.byu.edu.

  3. Nje ya YerusalemuNyimbo za Dini, na. 107.

  4. Frederic W. Farrar, The Life of Christ (1994), 656.

  5. Jeffrey R. Holland, “Wafanyakazi katika Shamba la Mizabibu, Liahona, Mei 2012

  6. Ona Jeffrey R. Holland, na Patricia T. Holland, “Wakati Ujao Uliojawa na Tumaini” (worldwide devotional for young adults, Jan. 8, 2023), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.