Liahona
Huruma Nyororo Miaka 25 Baadaye
Machi 2024


“Huruma Nyororo Miaka 25 Baadaye,” Liahona, Machi 2024.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Huruma Nyororo Miaka 25 Baadaye

Ninamshukuru Mungu kwa kutumia barua iliyosahauliwa kuonesha moja ya huruma Zake nyororo.

Picha
baba na binti kwenye Maporomoko ya Maji ya Niagara

Picha kwa hisani ya mtunzi

Nilipokuwa nafundisha seminari ya mapema asubuhi huko Eureka, Carlifornia, Marekani, niliwaomba wanafunzi wangu wajifikirie wenyewe miaka 10 ijayo. Kisha niliwaomba wajiandikie barua yenye ushuhuda wao juu ya injili na lolote lingine ambalo wangependa kushiriki kwao wenyewe wakiwa wazee. Niliwaambia nitawatumia barua baada ya miaka 10.

Muda ulipita na kamwe sikuweza kuzituma barua hizi. Siku moja miaka 25 baadaye, binti yangu Heidi aliziona barua na akauliza kuhusu barua hizo. Baada ya kueleza kile nilichokuwa nimekipanga, alitafuta anwani za wanafunzi wangu wa zamani kwa kutumia nyenzo za vyombo vya habari.

Picha
mkono mmoja ukipitisha baadhi ya bahasha kwa mkono mwingine.

Kielelezo na Alex Nabaum

Baada ya kuzituma barua, tulipokea baadhi ya majibu adhimu. Mmoja wa wanafunzi wangu wa zamani wa seminari aliandika.

“Ninahitaji baba yako ajue kwamba ameziona barua hizo sasa kwa sababu fulani. Binti yangu wa miaka 18 amekuwa akihangaika na ushuhuda wake na kuhisi kwamba kuwa ‘msichana mkamilifu Mtakatifu wa Siku za Mwisho siyo kwa ajili yake. Hashiriki hisia zake pamoja na sisi Imekuwa vigumu.”

Mwanafunzi wangu wa zamani, akiwa amefadhaishwa na baadhi ya vitu ambavyo binti yake alikuwa ameviandika karibuni katika blog, aliongeza:

“Nilijua nilitakiwa kuzungumza naye kuhusu hilo. Kama kawaida, tunapokuwa na mazungumzo haya, uso wake ulikuwa mkali na usiojali, na hakusema lolote. Nilimpa barua yangu na nilimwambia nilimtaka aisome.

“Nilimwona akirudia kusoma aya ya kwanza mara kadhaa. Nilikuwa nimeandika kwamba sikujua kama nilikuwa na ushuhuda, kwamba kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho mkamilifu ilikuwa kitu kikubwa na pengine siyo kwa ajili yangu.

“Binti yangu alianza kulia. Nilimtaka ajue kwamba kwa kweli ninaelewa mahangaiko yake. Kamwe asingeweza kuamini bila barua hiyo! Sehemu ya ukuta wake umebomoka, na hakika ninahisi kama mpangilio wa muda wa barua hii ulikuwa huruma nyororo. Kama ningekuwa nimeipokea miaka 10 iliyopita, yawezekana ningekuwa nimeitupilia mbali au kuipoteza! Tafadhali mshukuru baba yako kwa kutufanya tuandike barua na kwa kuziweka mahali paliposahaulika kwa miaka yote hii! Hakuna kilicho bahati nasibu.”

Baba yetu wa Mbinguni anawalinda kondoo Wake wote, na katika mpangilio Wake wa ajabu wa muda Wake, Yeye anaweza kuonesha huruma nyororo na miujiza kupitia kila mmoja wetu ili kuwaleta wale ambao wanapotea warudi kundini.