2021
Tunawezaje Kushughulikia Unyanyasaji
Julai 2021


Tunawezaje Kushughulikia Unyanyasaji

Haya ni baadhi ya mapendekezo kwa ajili ya wahanga wa unyanyasaji, viongozi wao wa Kanisa, na familia zao.

Picha
sad boy looking out window

Picha kutoka Getty Images

Mwokozi alizungumza kwa uzito kabisa juu ya unyanyasaji: “Bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa katika kilindi cha bahari” (Mathayo 18:6; ona pia Marko 9:42; Luka 17:2).

Unyanyasaji ni kutendewa vibaya au kutelekeza wengine (kama vile mtoto au mwanandoa mwenza, wazee, au walemavu) katika njia inayosababisha madhara kimwili, kihisia, au kijinsia. Msimamo wa Kanisa ni kwamba unyanyasaji wa aina yoyote hauwezi kuvumiliwa.

Mawazo yafuatayo yanaweza kusaidia, kama wewe ni mhanga wa unyanyasaji au mhanga wa kiongozi wa Kanisa au mzazi.

Kwa Mhanga

Kama mhanga1 wa unyanyasaji, hulaumiwi kwa ajili ya unyanyasaji uliokutokea, wala huhitaji kusamehewa kwa vitendo ambavyo mtu fulani alivyochukuwa dhidi yako. Unaweza kustaajabu jinsi Mwokozi anavyoweza kukuponya. Unaweza kufikiri kwamba dhabihu ya Upatanisho ya Mwokozi ilikuwa tu kwa ajili ya wale wanaotenda dhambi na kuhitaji kutubu.

Kwa hiyo ni kwa jinsi gani Mwokozi anakusaidia? Kwa sababu ya dhabihu Yake, Yeye Anaelewa. Mwokozi anayo huruma ya kiungu. Ingawa hatuwezi kujua kwa ukamilifu jinsi Mwokozi alivyoweza kuhisi maumivu yetu yote, tunaweza kuwa na imani kwamba anaelewa, katika njia kamilifu, kila mwanaume, mwanamke, na mtoto (ona 2 Nefi 9:21). Anaweza kutoa amani na nguvu ya kusonga mbele.2

Kupitia Upatanisho Wake, Mwokozi anawasaidia wale walioumia. Anaweza kusaidia “kwa kutuponya na kutufidia kwa mateso yoyote tunayopitia bila kosa.”3

Bila kujali lini au jinsi gani mkosaji atawajibishwa, unaweza “kuwa na hakika kwamba Hakimu Mkamilifu, Yesu Kristo, mwenye uelewa kamili wa kila kitu, atawawajibisha wanyanyasaji wote kwa kila tendo lisilo la haki.”4 Jua pia kwamba wale “wanao wanyanyasa wenza au watoto … siku moja watawajibika mbele za Mungu.”5

Kwa Viongozi wa Kanisa

Picha
priesthood leader talking to a young man

Viongozi wote na waalimu wanaowahudumia vijana na watoto wanahitajika kupata mafunzo ya mtandaoni “Kuwalinda Watoto na Vijana.”6

Hakuna kiongozi wa Kanisa anapaswa kamwe kutupilia mbali ripoti ya unyanyasaji au kumshauri muumini kutotoa taarifa ya shughuli za kihalifu.7 Viongozi wa Kanisa na waumini wanapaswa kutimiza wajibu wote wa kisheria wa kutoa taarifa za unyanyasaji kwa mamlaka za umma. Hata hivyo, maeneo yana sheria tofauti za kutoa taarifa. Baadhi ya maeneo yanahitaji wachungaji kufahamisha watekelezaji wa sheria, bali maeneo mengine yanakataza.

Ni muhimu kwa viongozi kuelewa kwamba waathiriwa wa unyanyasaji wanaweza kuwa na muda mgumu kuwaamini watu wengine—hususani wale walio katika nafasi za mamlaka. Hali inaweza kuwa yenye changamoto za kihisia; ugumu wa mwathiriwa kuzumgumzia kuhusu jambo hilo hauwezi kuhusishwa kibinafsi na wewe katika njia yoyote ile. Kukutana na viongozi peke yako kunaweza kuwa kwa kuogopesha kwa waathiriwa wa unyanyasaji. Waathiriwa wanaweza kumwalika mtu mzima anayeaminika kuwa pamoja nao wanapokutana na viongozi wa ukuhani.8

Haijalishi lini mtu fulani alinyanyaswa, yeye anaweza kunufaika kutokana na kuungwa mkono na msaada wa kitaalamu. Waathiriwa wengi wanapona vizuri sana wakati hisia zao zinapokuwa zimetambulika, wanajihisi salama na wenye ulinzi, wanaamini kwamba mtu fulani anawaamini, na wanaelewa jinsi unyanyasaji ulivyowaathiri. Uungwaji mkono unaweza kuwasaidia kupata amani na kutojihisi wapweke wanapotafuta kupata uponyaji.9

Kusimama dhidi ya unyanyasaji bila kujali nani anahusika yapaswa kuwa kiwango chetu. Wakati wakosaji wanapokuwa katika nafasi za mamlaka na sehemu za kuaminika, hata hivyo, unyanyasaji ni mkubwa zaidi na unaweza kuwa wenye madhara zaidi kwa mwathiriwa. Wale kwenye nafasi za kuaminiwa wanaowanyanyasa wengine wanatakiwa kuwajibishwa kwa kiwango cha juu zaidi kwa sababu wamekiuka imani ya mwathiriwa. Kanisa lina sera ya kutovumilia kabisa unyanyasaji, na kwamba hiyo ni kweli zaidi kwa wale walio katika nafasi za kuaminiwa na mamlaka.

Kwa Wazazi

Ingawa hadithi za unyanyasaji na mtu fulani mwenye mamlaka zinapokea usikivu zaidi katika habari, waathiriwa wananyanyaswa mara nyingi na mtu fulani wanayemjua. Mkosaji anaweza kuwa mwanafamilia, jamaa, au jirani. Mkosaji anaweza kuwa mwenye umri wowote. Mkosaji mara chache ni mgeni kabisa.10

Bali kuna ishara kadhaa za unyanyasaji ambazo tunaweza kuwafundisha watoto wetu ili kuwasaidia kutambua na kuepuka unyanyasaji. Wafundishe watoto wako kwamba kama mtu anawataka kufanya kitu fulani wanachokijua kuwa ni kibaya, wanaweza kusema hapana. Hapa ni baadhi ya mifano ya jinsi wakosaji wanaweza kulazimisha, kutishia, au kulaghai waathiriwa:

  • Wakosaji wanatumia nafasi zao, mamlaka, umri, ukubwa, au elimu kuwalazimisha waathiriwa kufanya kile wanachotaka.

  • Wanasena kwamba hawataki kuwa rafiki wa mwathiriwa isipokuwa mwathiriwa anafanya kile wanachosema.

  • Wanachukuwa kitu fulani na hawakirudishi isipokuwa mwathiriwa afanya kile wanachosema.

  • Wanatishia kusambaza uongo kuhusu mwathiriwa isipokuwa mwathiriwa akubali.

  • Watoa zawadi, upendeleo, au tuzo zingine ili kupata kile wanachokitaka.

  • Wanawaambia waathiriwa kwamba hakuna atakaye waamini na wataingia matatani kama watamwambia mtu kuhusu unyanyasaji huo.

  • Wanatishia kumuumiza mwathiriwa au mpendwa wake kama mwathiriwa hatafanya kile wanachokisema.11

Kushughulikia unyanyasaji ni jambo gumu sana. Hakuna majibu rahisi, bali tunaweza kupata faraja kuu katika maneno ya Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Hakuna maumivu ya kimwili, wala kidonda cha kiroho, wala uchungu wa nafsi au maumivu ya moyo, wala magonjwa au unyonge ambavyo wewe au mimi wakati wowote tunakabiliana navyo katika maisha haya ambavyo Mwokozi hakuvipitia. Katika wakati wa unyonge tunaweza kupiga kelele, ‘Hakuna anyeelewa ni nini. Hakuna anayeelewa.’ Bali Mwana wa Mungu anajua kikamilifu na anaelewa, kwa kuwa Yeye amehisi na kubeba mizigo yetu binafsi. Na kwa sababu ya dhabihu Yake ya milele na isiyo na mwisho (ona Alma 34:14), Yeye ana uwezo mkamilifu wa kuhisi hisia zetu na anaweza kutunyooshea mkono Wake wa rehema. Anaweza kutufikia, kutugusa, kutusaidia, kutuponya, na kutuimarisha tuwe zaidi kuliko tunavyoweza kuwa na kutusaidia kufanya kile ambacho kamwe hatungeweza kufanya kama tukitegemea tu nguvu zetu wenyewe.”12

Picha
Savior in Gethsemane

Ee Baba Yangu, na Simon Dewey

Basi na tumgeukie Mwana mfalme wa Amani na kupitia Yeye tupate tumaini na uponyaji.

Muhtasari

  1. Baadhi ya watu hupendelea neno aliyesalimika badala ya mwathiriwa.

  2. Ona “Mwokozi Anawezaje Kunisaidia Mimi kama Mwathiriwa wa Unyanyasaji?” abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  3. D. Todd Christofferson, “Redemption,” Liahona, May 2013, 110.

  4. Richard G. Scott, “To Heal the Shattering Consequences of Abuse,” Liahona, May 2008, 42–43.

  5. “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ChurchofJesusChrist.org.

  6. Ona “Protecting Children and Youth,” ChurchofJesusChrist.org/callings/church-safety-and-health/training-and-video-resources/youth-protection.

  7. Ona “Protecting Members and Reporting Abuse,” abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  8. Ona Kitabu cha Miongozo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 31.1.1, ChurchofJesusChrist.org.

  9. Ona “Should I Get Professional Help?” abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  10. Ona “Recognizing Patterns of Abuse,” abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  11. Ona “Talking to Children about Abuse,” abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  12. David A. Bednar, “Bear Up Their Burdens with Ease,” Liahona, May 2014, 90.

  13. Ona “Talking to Children about Abuse,” abuse.ChurchofJesusChrist.org.