2021
Kuwahudumia Wale wenye Changamoto za Afya ya Kimwili
Julai 2021


Kanuni za Kuhudumu

Kuwahudumia Wale wenye Changamoto za Afya ya Kimwili

Tunaweza kuwa mikono ya Mwokozi ya kufariji na kusaidia.

Picha
man delivering groceries

Ugonjwa, mzio, ulemavu, au umri vinaweza kuathiri uwezo wa muumini wa kuabudu au kuhudumu. Kama akina kaka na dada wahudumiaji ni wepesi kutambua mahitaji haya, kuna njia nyingi za kuwasaidia waumini walio na changamoto za kimwili kufurahia vizuri baraka za injili.

Baada ya mama kijana kugunduliwa ana saratani, alijihisi mpweke na alijawa na hofu. Lakini hata wakati habari za ugonjwa wake zilipoenea katika kata yake yote, alizungukwa mara moja na upendo na kujali kutoka kwa dada wenzake. Wakati matibabu yake magumu yalipoanza, akina dada walimsafirisha kwenda kwenye miadi yake na kukaa pamoja naye wakati wa vipindi vyake virefu vya tibakemikali. Walisali pamoja naye, walimtia moyo, walimletea vyakula vichache ambavyo angeweza kula na walileta milo kwa familia yake wiki baada ya wiki. Akina dada wengine walitenga muda kutoka shughuli zao nyingi ili kusafisha nyumba yake. Dada mmoja alijua matibabu fulani yatafanya iwe vigumu kwake kulala, kwa hiyo alipanga mara nyingi kumtembelea usiku kuangalia naye filamu za vichekesho. Badala ya kugaagaa kitandani, mama huyo kijana aliweza kuachana na hofu kwa muda na kuhisi nguvu ya uponyaji ya kicheko na urafiki. Kupitia huduma hizi, baraka za ukuhani, na mifungo ya kata, aliweza kuuvuka muda mgumu kwelikweli, na muunganiko imara wa upendo uliongezeka kati ya wote waliohusika.

Kuhudumu kwa wale wenye changamoto za kiafya sio siku zote rahisi. Bali tunaweza kufuata mfano wa Mwokozi wa kunyosha mkono kwa akina kaka na dada katika upendo wakati changamoto za kiafya zinapotokea. Tunaweza kuwa mikono Yake ili kufariji na kuwasaidia wale wanaotuzunguka, ikiwa ni pamoja na hao ambao changamoto zao bado hazionekana kwa dhahiri kwa macho yetu ya kimwili.

Mawazo ya Kuzingatia

1.Heshimu faragha zao. Baadhi ya watu wanakwazwa na maswala ya afya ambayo yanaweza yasikukwazwe wewe kabisa. Siku zote uliza kama ni SAWA kushiriki hali zao kwa wengine kabla ya wewe kufanya hivyo.

2. Himiza matibabu yenye kustahili. Epuka kushauri bidhaa za afya au huduma ambazo hazijathibitishwa au zilizo nje ya kiwango cha matibabu. Shiriki mawazo na uzoefu kulingana na msukumo utakaoupokea, bali himiza wengine kufanya utafiti wao wenyewe na kushauriana na wataalamu wa matibabu waliobobea.

Picha
adult woman helps her mother put on clothing

Vielelezo vya Picha kutoka Getty Images

3. Wahudumie na sali kwa ajili yao. Wakati watu wanapokabiliana na matatizo ya kiafya ya muda mfupi au hali za kutabirika kama kujifungua, au upasuaji, huduma yako, milo, wema, na sala huonesha unajali. Katika dharura, utayari wako wa kusaidia unaweza kuwa si wa thamani.

4. Saidia kuwapa nguvu. Hususani wakati watu wanapokabiliana na matatizo hatari ya kiafya au ya muda mrefu, wanahitaji zaidi ya msaada wako au huduma, kulingana na umuhimu wake. Wanaweza pia kuhitaji msaada kujifunza kufanya yafuatayo kwa ajili yao wenyewe:

  1. Kutambua mahitaji yao. Ni nini wanajua mpaka sasa kuhusu hali zao? Wanajihisi vipi kuhusu hali hiyo? Ni upi wasiwasi wao kwa sasa na baadaye na mahitaji yao? Sikiliza kwa huruma na bila kuhukumu ili kuwasaidia kwa uaminifu kukabiliana na uhalisia.

  2. Kumbuka uimara wao. Uliza kuhusu aina zingine za shida walizowahi kukabiliana nazo na ni kipi walijifunza kutokana na uzoefu huo. Toa sifa, thamani, na ujuzi chanya uliouona kwao. Uliza ni mambo gani ya kibinafsi ambayo ni ya muhimu sana wawapo kwenye hali hii mpya. Ni jinsi gani wanaweza kuyaishi mambo hayo?

  3. Tengeneza mpango. Ni maamuzi gani yanahitajika kufanywa mapema, na ni ipi taarifa ya ziada wanayohitaji ili kufanya maamuzi hayo? Ni msaada gani wa haraka au nyenzo wanazohitaji, na watahitaji nini kwa muda mrefu? Ni machaguo gani wanayoyaona? Ni yapi mazuri na mabaya ya kila uchaguzi?

  4. Panga timu yao. Nani anaweza kusaidia? Familia ya karibu ina wajibu wa kusaidia, bali familia ya jamaa, marafiki, waumini wengine wa kata, wataalamu wa afya, huduma zinazopatikana za umma, wewe na mwenza wako, na Roho Mtakatifu wote wanaweza kuwa sehemu ya timu yao. Kama inafaa na kwa ruhusa yao, muhusishe rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama na rais wa akidi ya wazee katika kujua jinsi wewe, waumini wengine, na nyenzo za Kanisa zinaweza kusaidia.

  5. Mwalike Roho. Sali pamoja nao na kwa ajili yao, ukimwalika Bwana kuthibitisha na kuongoza maamuzi yao na kuwasaidia kuhisi upendo Wake.