2023
Andaa Udongo Wako wa Kiroho
Januari 2023


“Andaa Udongo Wako wa Kiroho,” Liahona, Jan. 2023.

Njoo, Unifuate

Andaa Udongo Wako wa kiroho

Fumbo la mpanzi linaweza kutusaidia kuwa tayari kwa ajili ya kujifunza kwetu Njoo, Unifuate ya Agano Jipya mwaka huu.

Moja ya mafumbo niyapendayo katika Agano Jipya ni fumbo la mpanzi, kama linavyopatikana katika Mathayo 13:3–23 (Ona pia Marko 4:3–20; Luka 8:5–15). Katika fumbo hili, njia ambazo watu wanapokea neno (mbegu) zinafananishwa na aina mbalimbali za udongo. Tunajifunza kuwa kila udongo una sifa muhimu, ama mzuri au mbaya.

Mara kwa mara tunasoma fumbo hili na kudhani kwamba linaelezea utayari wa watu kukubali na kuishi injili. Wakati huu ukiwa ni ukweli, nafikiri fumbo linaweza pia kuelezea maendeleo yetu binafsi tunapokua katika imani na uelewa wa injili. Kwa maneno mengine, hatukufungwa milele katika aina fulani au kiwango fulani cha kuamini. Tunaweza, kwa imani na juhudi, kuboresha udongo wetu wa kiroho ili kwamba uweze kuzaa matunda mazuri zaidi.

Ningependa kuchunguza fikira hii pamoja na wewe kwa sababu imenisaidia mimi kuelewa fumbo hili kwa kina zaidi. Ninaamini kwamba tunapokuwa tunajiandaa kwa ajili ya kujifunza kwetu Njoo, Unifuate ya Agano Jipya kwa ajili ya mwaka ujao, kupitia upya fumbo la mpanzi kunaweza kutusaidia kuandaa mioyo yetu ili kupokea ukweli wa injili.

Kupokea Mbegu za Injili

Katika fumbo, tunajifunza kwamba mpanzi alipopanda:

  • Baadhi ya mbegu zilianguka kando ya njia, na ndege wakazila.

  • Baadhi zilianguka juu ya sehemu zenye mawe. Ziliota lakini zilipigwa na jua zikanyauka.

  • Baadhi zilianguka penye miiba, na ile miiba ikazisonga.

  • Baadhi zilianguka kwenye udongo mzuri na zikazaa matunda.

Bwana anafafanua:

“Wakati mtu yoyote anapolisikia neno la ufalme, na halielewi, ndipo anapokuja mwovu na kuondoa, kile ambacho kilipandwa ndani ya moyo wake. Huyu ni yeye ambaye alipokea mbegu kando ya njia.

“Lakini yeye ambaye alipokea ile mbegu kwenye sehemu zenye mawe, huyu ni yule ambaye analisikia neno, na punde kwa furaha analipokea;

“Lakini kwa kuwa hana mizizi ndani yake, linadumu kwa muda: kwani taabu au mateso yanapotokea kwa sababu ya neno, kidogo kidogo huanza kuchukizwa.

“Yeye pia ambaye alipokea mbegu penye miiba ni yeye ambaye analisikia neno na shughuli za dunia hii na udanganyifu wa mali, hulisonga lile neno na likawa halizai.

“Bali yule ambaye anapokea mbegu kwenye udongo mzuri ni yeye ambaye analisikia neno na analielewa; ambaye pia huzaa matunda, baadhi mia, baadhi sitini baadhi thelathini”(Mathayo 13:19–23; msisitizo umeongezwa).

Acha tuangalie kila aina ya udongo na tuone nini kinachoweza kufanywa ili kuuboresha.

Picha
mbegu na ndege

Vielelezo na David Green

Udongo wa Kando kando ya Njia

Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alisema: Mbegu ambazo ‘zilianguka kando ya njia’ (Marko 4:4) hazikuufikia udongo mzuri ambapo pengine zingeweza kukua. Zinakuwa kama mafundisho ambayo yanaanguka kwenye moyo mgumu au ambao haujatayarishwa.”1

Kwa nyongeza, wakati mwingine hatuelewi nini tunachosikia au kusoma katika maandiko kwa sababu mioyo yetu haikutayarishwa. Wakati hivyo ndivyo, tunapaswa kufanya nini?

Tunaweza kutafuta ufafanuzi kutoka kwa wale wanaoelewa. Tunaweza kuwauliza wamisionari, mwalimu wetu wa Shule ya Jumapili, kiongozi wetu wa ukuhani au kikundi, mwalimu wetu wa seminari au chuo, wale wanaotuhudumia au wazazi wetu na wanafamilia walio waaminifu. Tunaweza kujifunza hotuba za mkutano mkuu. App ya Maktaba ya Injili inatoa nyenzo nyingi ambazo zinaweza kutusaidia kutafuta uelewa zaidi.

Tunapaswa pia kuomba kwa Mungu na kumwuliza kwa ajili ya kupata nuru zaidi. Kama nia yetu ni ya dhati, dhamira yetu ni halisi na tunayo imani katika Kristo, tutapokea maarifa juu ya kweli za injili (ona Moroni 10:4–5). Bwana alisema:

“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata, bisheni, nanyi mtafunguliwa.

“Kwani kila mmoja ambaye huuliza hupata; na yule anayetafuta, huvumbua; na yule ambaye hubisha, hufunguliwa.” (3 Nefi 14:7–8).

Picha
mbegu na mawe

Udongo katika Sehemu zenye Mawe

Baadhi ya watu huisikia injili ya urejesho kupitia wamisionari, wanahisi upendo wa Kristo na kuhudhuria na kufurahia mikutano ya Kanisa. Hata hivyo, baada ya muda, magumu ya maisha yanaendelea. Wanaona kwamba maisha hayajabadilishwa kuwa kijito cha baraka zisizoisha kamwe. Imani yao inapungua na wanajitenga mbali.

Baadhi pia wanaona “sehemu zenye mawe” wanapohudhuria ibada au mkutano mkuu na kuhisi kutiwa moyo kufanya kila kitu kwa usahihi kutokea wakati huo na kuendelea. Lakini kisha siku ya Jumatatu wanarudi kwenye majukumu yao ya siku zote. Changamoto kazini zinabaki kuwa ngumu. Majaribu yanaonekana ya kuvutia na yasiyovumilika kabisa. Na hivyo hamu yao ya kuwa bora kiroho inapungua au inapotea.

Wanajifunza kwa namna ngumu kwamba bila kina kirefu cha mizizi ya kiroho ili kutushikilia wakati wa upepo, kutulisha wakati tunapokuwa na njaa au kutuburudisha wakati joto la jua liwapo kali, tunaweza kuangamia kiroho.

Je, tunawezaje kuboresha udongo wenye mawe? Ondoa mawe na zamisha kwa kina mizizi yetu ya kiroho.

Kuondoa mawe kunaweza kuwa changamoto. Inaweza kuhitaji kujenga mazingira ambapo imani inasisitizwa. Inaweza kuhitaji kuanzisha urafiki mpya na kujitenga mbali na ubaya (ona 1 Wathesalonike 5:22).

Picha
mikono imeshikilia mawe

Kuwa na nguvu za kuondoa mawe, tunahitaji msaada wa Mwokozi. Msaada huo huja wakati tunapokubali maagano ambayo Yeye anatoa. Hii inaanza kwa kukubali mwaliko wa kubatizwa. Inamaanisha kuthibitishwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Inamaanisha kukubali maaagano yoyote ambayo bado hatunayo, kama vile kupokea ukuhani au kwenda hekaluni. Inamaanisha kuhudhuria kanisani na kufanya upya maagano kwa kushiriki sakrament kila wiki.

Wakati majaribu na vishawishi vinapokuja, tunaweza kushikilia kwa nguvu kwenye maagano tuliyoyafanya na Bwana. “Tunafungamana kwa uthabiti pamoja na Mwokozi wakati tunapokumbuka kwa uaminifu na kufanya kadiri ya uwezo wetu kuishi kulingana na masharti tuliyokubali,” alisema Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Na muunganiko huo pamoja na Yeye ni chanzo cha nguvu za kiroho katika majira yote ya maisha yetu.”2

Picha
mbegu na miba

Udongo kati ya Miiba

Udongo huu unaruhusu mimea kukua, ikiwa ni pamoja na miiba. Miiba ni “shughuli na mali na anasa za maisha haya” ambavyo vinaweza kusababisha sisi “tusiivishe lolote” (Luka 8:14).

Nini hutokea wakati tunapokubali maagano lakini hatutembei tena kwenye njia ya agano? Au tunashiriki sakramenti lakini hatuombi msamaha, kwa sababu hatufikirii hata kuhusu makosa yetu tena. Au tunaweza kuomba msamaha lakini tunakataa kuwasamehe wengine. Tunayakubali maagano ya hekaluni lakini tunashindwa kuwahudumia wale wenye shida. Tunaweka pembeni fursa za kushiriki injili kwa sababu tunaogopa inaweza kuonekana isiyofaa au inatia aibu au kwa sababu hatujui tena nini cha kusema.

Suluhisho ni kuishi maagano tuliyoyafanya tulipobatizwa, “kuomboleza na wale ambao wanaomboleza; … [kuwafariji] wale ambao wanahitaji kufarijiwa na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote na katika mahali popote ambapo [sisi] tunaweza kuwapo, hata hadi kifo” (Mosia 18:9).

Tunatoa magugu wakati tunapotubu kila siku, tukifanya urekebishaji mdogo au mkubwa na kurejea kwenye njia nyembamba na iliyosonga ya agano.

Tunakataa kuacha magugu ya maisha yatukabe. Tunafanya hivi kwa kubadilisha nyumba zetu kuwa mahali patakatifu pa imani. Tunatafuta kitu chochote kinachoalika ushawishi wa Roho. Tunakataa kitu chochote kile kinachoondoa ushawishi huo wa Roho. Na tunahudumu katika ufalme wa Mungu—katika miito yetu, hekaluni, katika kazi ya umisionari, katika familia zetu.

Udongo Mzuri

Kuna wengi wanaosikia neno, wanalielewa na wanaruhusu likue katika mioyo yao. Kwa hao Bwana anasema, “Mimi nimewachagua ninyi, nami nikawaweka, mwende mkazae matunda na matunda yenu yapate kukaa” (Yohana 15:16). Kwa watu kama hao, jibu ni kusonga mbele kwa imani na kuvumilia katika kazi nzuri.

Rais Oaks aliuliza, “Tunafanya nini kwa mafundisho ya Mwokozi pale tunapoishi maisha yetu?”3 Mwaka huu, tunapojiandaa kujifunza Agano Jipya, na tusogee karibu na Mwokozi na tuboreshe udongo wetu wa kiroho ili kwamba tuweze kulipokea neno. Kisha tunaweza kuzaa matunda anayotuomba tuyalete kwa kukubali na kufanya upya maagano ambayo yanatufunga sisi kwake, kwa kumtumikia Mungu na kuwapenda jirani zetu na kwa kuendelea kwenye njia ya agano ambayo siku moja itaturudisha nyumbani kwetu mbinguni.