2023
Kwa nini Sikuweza Kusamehe?
Januari 2023


“Kwa nini Sikuweza Kusamehe?,” Liahona, Jan. 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Kwa nini Sikuweza Kusamehe?

Nilisali kwamba Baba wa Mbinguni anisaidie kushinda hisia zangu mbaya na nisamehe.

Picha
mtu akifanya kazi kwenye bustani ya viwanja vya hekalu

Kielelezo na Allen Garns

Nilijiunga na akina kaka wengine wachache wa kata yangu kumsaidia dada mmoja kuhama. Lakini tulipofika kwenye nyumba yake, gari la mizigo ambalo halikuegeshwa vizuri lilituzuia kuingia na gari letu.

Nilipiga nambari ya simu iliyoandikwa ubavuni mwa ile gari nyingine ya mizigo kuomba kwamba mtu aje na kulihamisha lile gari. Mtu alijibu na kuahidi kwamba angekuja mara moja.

Baada ya dakika 15, nilipiga tena simu, lakini hakujibu. Hatimaye, baada ya kupiga mara moja zaidi, alitokea pamoja na watoto wawili. Alikuwa amekasirika na alisema kitu fulani ambacho kiliniudhi. Nilijaribu kusahau kuhusu hilo tulipokuwa tukiendelea na mambo ya kuhama.

Jioni ile niliwaza kuhusu tukio lile. Niliomba kwamba Baba wa Mbinguni anisaidie nisahau hisia zangu na nimsamehe mtu yule. Alijibu maombi yangu.

Muda mfupi baadaye, hata hivyo, nilikuwa nikisoma gazeti la sehemu ile na nikaona makala kuhusu mtu huyu. Ilijumuisha picha yake. Hisia zangu hasi juu yake zilirudi. Kwa hiyo, nilipitia tena mchakato ule ule. Nilimuomba Bwana kwamba jambo hili dogo lisinisumbue tena na kwamba Anisaidie nimsamehe mtu yule. Hisia nzuri zilinijia.

Haikuwa muda mrefu kabla ya kutokea kukutana na mtu yuleyule dukani. Hisia zangu mbaya bado zilinirudia tena. Nilishangazwa. Nilimwuliza Bwana kwa nini sikuweza kusahau tukio hili. Siku chache baadaye, Bwana alinifundisha somo.

Nilikuwa naondoka kutoka viwanja vya Hekalu la Helsinki Finland wakati nilipomwona mtu huyu huyu akifanya kazi katika bustani za hekalu. Sikuweza kuyaamini macho yangu. Akili yangu ilifunguka na nilielewa kwamba yeye, kama mimi, alikuwa akimtumikia Bwana na yeye, kama mimi, alikuwa na siku za kukatisha tamaa wakati vitu vinapokuwa haviendi sawa. Niliweza kumwona mtu huyu kama ndugu yangu. Kwa macho mapya, nilihisi heshima na upendo kwake. Baada ya hapo, hisia zote za mwanzo zilinitoka, kamwe hazitarudi.

Wakati tunapowaona wengine kama Bwana anavyotuona sisi, tunaweza kufuata amri yake ya kusamehe kabisa (ona Mathayo 6:14–15; Mafundisho na Maagano 64:9–10). Tukio hili lilikuwa huruma nyororo za Bwana za kukumbukwa, ambazo bado ninazitafakari ndani ya moyo wangu.