2023
Ulikuwa wapi?
Januari 2023


“Ulikuwa Wapi?,” Liahona, Jan. 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Ulikuwa wapi?

Nilipaswa kukubali ratiba na makusudi ya Mungu pale nilipojifunza kumpenda bibi yangu kama vile Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanavyompenda.

Picha
bibi na mjukuu wa kiume wakicheka pamoja

Licha ya ugonjwa wa bibi, kila kitu anachofanya kwa ajili yangu ni kwa sababu ananipenda.

Picha kwa hisani ya mwandishi

“Ulikuwa wapi, mtoto wangu?” bibi yangu aliuliza alipokuwa akijibu hodi yangu kwenye mlango wake. Ndio kwanza nimerudi kutoka misheni yangu huko El Salvador. Macho ya bibi yalikuwa yamejaa kwa furaha kwa kuniona tena. Mikono yake ilisikika kuwa laini na yenye joto la uvuguvugu pale alipoizungusha shingoni mwangu.

Tulikuwa na burudani ya mazungumzo nilipokuwa nikijibu maswali yake kuhusu misheni yangu. Nilipatwa na hisia nilipokuwa namwelezea kuhusu watu, chakula, ugumu wa kazi na miujiza ya misheni yangu. Baada ya kumaliza, ghafla akawa kimya. Kisha aliuliza, “Ulikuwa wapi mwanangu?”

Ni wazi, hakuwa akisikiliza. Kwa hivyo, tulianza mazungumzo yetu tena. Sio zaidi ya dakika 20 baadaye, aliuliza kwa mara ya tatu, “ulikuwa wapi, mwanangu?”

Kitu fulani hakikuwa sawa. Baadaye niligundua kwamba takriban mwaka mmoja baada ya kuondoka kwenda misheni yangu, bibi yangu aligundulika ana ugonjwa wa kufa kwa seli za ubongo.

Nilihisi hamu kubwa ya kumsaidia Bibi. Kwa miaka miwili, nimekuwa nikihubiri upendo Mungu alionao kwa watoto Wake. Sasa nilikuwa na fursa ya kuishi mafundisho hayo. Ingawa nilijua ingekuwa vigumu, niliamua kwenda kuishi naye ili niweze kumsaidia.

Miezi michache ya mwanzo ilikuwa migumu zaidi. Kama vile kwenye uwanja wa misheni, kuwa na subira na kudhibiti kuvunjika moyo ikawa kazi ya muda wote. Na kama vile wakati nilipokuwa misheni, nilipaswa kukubali ratiba na makusudi ya Mungu wakati nilipokuwa nikijifunza kumpenda bibi yangu kama vile Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanavyompenda.

Kuishi na Bibi wakati mwingine ni kama kuishi na watu watatu tofauti. Wakati mwingine hawezi kuvumilia kuwa na mtu mwingine ndani ya nyumba. Wakati mwingine anataka kujali kwangu na umakini wangu, akifurahia kwamba hayuko peke yake. Wakati mwingine vyote anavyofikiria ni juu ya nini cha kumlisha mjukuu wake ambaye ndio kwanza amerudi kutoka misheni yake. “Usifanye hivyo!” haraka inaweza kuwa “Kwa nini hufanyi hivyo?”

Bibi yangu, hata hivyo, amekuwa baraka kubwa kwangu. Ninajua kwamba licha ya ugonjwa wake, kila kitu anachofanya kwa ajili yangu ni kwa sababu ananipenda.

Maneno matamu mno ya bibi yangu na ya dhati kabisa huja kila wakati nirudipo nyumbani kutoka shuleni au kazini. Kwa macho ya huruma, ananikumbatia, anabusu mashavu yangu na kwa upendo anauliza, “Ulikuwa wapi, mtoto wangu?”