2023
Miujiza ya Mungu Inaendelea
Julai 2023


“Miujiza ya Mungu Inaendelea,” Liahona, Julai 2023.

Taswira za Imani

Miujiza ya Mungu Inaendelea

Nilitambua kwamba imani ya Watakatifu wa Siku za Mwisho ilikuwa thabiti zaidi kwenye Biblia kuliko madai ya kwamba Biblia imechukua nafasi ya manabii na ufunuo. Nilihisi shangwe halisi nilipotambua ya kwamba ningekuwa naishi kwenye “nyakati za biblia” za sasa.

Picha
familia imesimama pamoja nje

Picha kwa hisani ya mwandishi

Mnamo Novemba 9, 1989, serikali ya Ujerumani ya Mashariki ilitangaza rasmi kimakosa kwamba kuanzia siku hiyo wananchi wa mji mkuu waliruhusiwa kuvuka Ukuta wa Berlin. Dakika chache baadaye walinzi waliokuwa wamechoka siku zote hawakuwa na chaguo lolote ila kuruhusu umati mkubwa na ulioongezeka kuondoka eneo hilo kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani.

Mimi pamoja na rafiki yangu kipenzi Jakub Górowski—wakati huo tukiwa bado wavulana—tulitazama muujiza usiotarajiwa ukifunuliwa kwenye televisheni kutokea nyumbani kwetu huko Poland. Ulimwengu ulikuwa unateketea lakini sio kwa moto haribifu. Roho ya uhuru na tumaini ilijaza mioyo ya mamilioni ya watu.

Kwangu mimi na Jakub, ndoto yetu ilikuwa ni kwamba siku moja tuondoke Poland kwenda Magharibi—Denmaki, Sweden, Ujerumani Magharibi. Tulishawishiwa na filamu za Kiamerika na maonesho ya TV. Filamu yangu pendwa ilikuwa The Wonder Years. Nilipenda hali ya maisha ya kitongojini ya Amerika.

Sidhani mtu yeyote kwenye pande zote za Pazia la Chuma alitegemea Vita Baridi kuisha. Lakini Baba wa Mbinguni alikuwa na mpango wa tofauti. Mnamo 1975, pasipo sisi kujua, Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) aliwaalika Watakatifu wa Siku za Mwisho “kuungana katika maombi endelevu ya dhati kwa Bwana ili afungue milango ya nchi na kulainisha mioyo ya wafalme na watawala kwa lengo kwamba wamisionari waweze kuingia ardhi zote na kufundisha injili.”1

Miaka miwili baadaye, Rais Kimball alitembelea Warsaw, Poland. Asubuhi moja, akiwa ameambatana na kikundi kidogo cha washirika wake, ikijumuisha Mzee Russell M. Nelson, Rais Kimball aliondoka hotelini, na kutembea mpaka kwenye kaburi la mwanajeshi asiyejulikana, na kuingia Bustani la Saski. Sio mbali na chemchemi kubwa ambayo bado ipo mpaka leo, alipiga magoti na kuiwekea tena wakfu Poland kwa ajili ya kuhubiri injili.

Muongo wa machafuko na maandamano makubwa ya kupinga yalifuata. Wakati watu wazima hawakuwaamini na kuwapinga viongozi wa siasa, vijana wengi walihoji baadhi ya maadili, desturi na mitazamo ya wazazi wao. Mimi na rafiki yangu Jakub tulihisi kukata tamaa kuhusu Ukristo kwa kadiri tulivyouelewa. Kiujumla Jakub hakuvutiwa na dini, wakati mimi nikivutiwa na falsafa zenye chimbuko lake huko Asia.

Mnamo Aprili 1990, mimi na Jakub tulidandia gari kwenda Austria. Huko Vienna tulikutana na wanawake wawili wema wamesimama kwenye barabara ya watembea kwa miguu ya mtaa wenye shughuli nyingi. Mmoja kati yao alikuwa amebeba Kitabu cha Mormoni kwa lugha ya Kipolishi. Alituambia kuhusu matembezi ya Yesu kwa watu wa Amerika ya kale na kuahidi kukituma kitabu majumbani mwetu kama tungempatia anwani zetu. Pia tulifungua vitabu vyetu vya anwani na kunakili anwani za marafiki zetu wengi. Tulidhani ingekuwa ni zawadi nzuri kwa wao kuipokea.

Miezi michache baadaye Misheni ya Poland Warsaw iliundwa na wamisionari wanne waliwasili kwenye jiji. Baadaye, niligundua kwamba idadi kubwa ya “watu wa kufundisha”—anwani za rafiki zetu—zilichangia sana katika kuufungua mji wetu kwa ajili ya wamisionari. Kwa mshangao wangu miezi michache baadaye, Jakub aliniambia kwamba wamisionari wawili wa “Kimormoni” walimtembelea na kwamba ameamua kujiunga na kanisa lao.

Niliumizwa na taarifa yake. Nilijaribu kwa miaka kumvutia kwenye dini lakini bila mafanikio. Inawezekanaje wageni kutoka nchi nyingine kumuongoa ghafla? Nilikuwa nimedhamiria kukutana nao na kumuonesha Jakub kwamba hawana lolote kwenye mazungumzo yao pamoja nami.

Nilijihisi mtu maalumu sana.

Nilipowaona wamisionari wawili vijana, wenye kutabasamu wakiwa wamesimama kwenye njia ya lango la makazi ya wazazi wangu, nilisahau lengo langu la kuwakosoa. Walikuwa wenye furaha. Waliniuliza maswali mengi kuhusu mimi mwenyewe na imani zangu. Waliheshimu imani zangu. Baadaye waliniambia kwamba wakati wa mkutano huo wa kwanza na mtu mwenye kiburi mwenye nywele ndefu na suruali iliyotatuka na aliyekuwa akivuta sigara, walikuwa na wakati mgumu kutafakari kama ningevutiwa kuwa mfuasi wa Yesu Kristo. Lakini mimi nilihisi kitu maalumu kwa uwepo wao, na nilivutiwa kwamba Kanisa lao ndio lilikuwa dhehebu pekee la Kikristo nililolijua ambalo liliamini juu ya maisha kabla ya haya ya duniani.

Pia nilivutiwa na shuhuda zao na imani thabiti ya Jakub na Robert Żelewski, rafiki yake mpya kutoka Kanisani. Robert alikuwa mwanasaikolojia, mtu mwenye akili lakini anayejishusha ambaye umaizi na uzoefu wake viliimarisha hamu yangu katika dini ya Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kila kitu ambacho wazee, Jakub na Robert walichoniambia kilikuwa kinavutia, hasa fundisho la mpango wa wokovu, kuanzia maisha kabla ya hapa duniani na kuishia na daraja tatu za utukufu. Lakini sikuona lolote la kujiunga na Kanisa mpaka nilipoweza kuelewa vyema imani zao za kipekee. Uelewa wangu wa Ukristo ulikuwa kwamba hapo kale, Mungu alitenda miujiza, alituma malaika, na kuita manabii, lakini vitu hivyo vyote ni vya enzi za biblia. Mara baada ya Biblia kukamilika, utu haukuhitaji miujiza na ufunuo kwa sababu maandiko yamejaa kila kitu tunachohitaji kujua.

Mwanga ulikuja wakati wa mjadala wetu kuhusu Ukengeufu Mkuu na Urejesho wa utimilifu wa injili kupitia Nabii Joseph Smith. Niligundua kwamba imani zao ziliendana zaidi na Biblia kuliko madai kwamba Biblia imechukua nafasi ya manabii na ufunuo. Nilihisi shangwe halisi nilipotambua ya kwamba ningekuwa naishi kwenye “nyakati za biblia” za sasa.

Nilikuwa tayari kumuuliza Mungu kwa dhati kwa ajili ya ufunuo binafsi, lakini jibu halikuja. Hatimaye nilisema, “Baba wa Mbinguni, kama ulimwita Joseph Smith kama nabii wako, nitatii kila amri uliyoifunua kupitia kwake.” Kisha kwa uhakika jibu lilikuja moyoni mwangu na akilini, na nilijua kwamba Mungu amerejesha utimilifu wa injili na kwamba unapatikana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Picha
wazee wamisionari gari moshi kwenye usuli.

Jakub alibatizwa Novemba 3, 1990, na kubakia mwaminifu mpaka kifo katika ajali mbaya ya kupanda mlima miongo miwili baadaye. Nilijiunga na Kanisa Januari 11, 1991, nikinuia kutumikia misheni. Robert aliitwa kama rais wa tawi letu na kunibeba kwa gari mpaka Freiburg, Ujerumani, ili nipokee endaumenti yangu ya hekaluni. Wakati wa usaili wangu wa mwisho pamoja naye, niliahidi kurejea Poland baada ya huduma yangu huko Misheni ya Illinois Chicago ili nitumie uzoefu wangu wa umisionari kuliimarisha Kanisa katika nchi yetu.

Miaka miwili baadaye, rais wangu wa misheni alinishawishi kwamba nipate elimu yangu huko Amerika kwenye Chuo Kikuu cha Brigham Young. Lakini sikusahau ahadi yangu kwa Robert.

Picha
mzee mmisionari kijana amesimama katikati ya wanandoa wazee

Baada ya kuoa mwaka 2000, nilihamia Poland pamoja na mke wangu, ambaye, mwaka 1988, alikuwa kama wa ziada katika sehemu ya sita ya filamu ya The Wonder Years. Tulihudhuria mikutano ya Kanisa huko Krakow, tukiwalea wavulana wawili na tukiwa na mawasiliano ya karibu na watoto wetu wawili wakubwa. Kijana wetu mkubwa hivi karibuni alisema ameamua kutumikia misheni.

Katika majira ya joto ya 2021, niliipeleka familia yangu Berlin, ambapo niliwaonyesha sehemu ambapo ukuta ulikuwepo. Ukuta huo hauwazuii tena watumishi wa Mungu kushiriki ujumbe wa Urejesho na watu wa Ulaya ya Mashariki. Miujiza ya Mungu inaendelea katika siku yetu.

Muhtasari

  1. Spencer W. Kimball, katika “Insights from June Conference,” Ensign, Okt. 1975, 70.