2023
Mabadiliko Tunayotaka—na Tusiyotaka—Kukabiliana Nayo
Julai 2023


“Mabadiliko Tunayotaka—na Tusiyotaka—Kukabiliana Nayo,” Liahona, Julai 2023.

Vijana Wakubwa

Mabadiliko Tunayotaka—na Tusiyotaka—Kukabiliana Nayo

Lengo lako la muda mrefu ni lipi? Kama unajua unachokitafuta, utajiandaa, na hata kuwa na furaha, kufanya mabadiliko katika maisha yako.

Picha
mwanaume akichagua uelekeo kutembea katika upande mmoja wa barabara

Je, umewahi kufanya badiliko ambalo kwa dhati hukuwa na hamu ya kulifanya? Au badiliko ambalo hukulitegemea kulifanya?

Takribani miaka 15 iliyopita daktari wangu aliniambia kwamba nilipaswa kubadili mtindo wa maisha: “Anza kujishughulisha zaidi, au hutaishi kwa muda mrefu,” aliniambia. Nilichukulia onyo lake kwa dhati. Niliamua kuanza zoezi la kukimbia.

Ili kufanya badiliko hili la maisha lifanikiwe, nilihitaji kuwa na mtazamo mkubwa akilini kwa sababu kama ningekuwa na mtazamo mdogo, nisingefika mbali.

Lengo langu kubwa ni la kujirudia la kukimbia mbio moja ya nyika kila mwaka. Lengo hili lilinisaidia kuamka na kukimbia kila siku kwa sababu najua kwamba katika siku fulani mwaka ujao, nitatakiwa kukimbia maili 26.2 (Kilometa 42.2). Nilikuwa mwenye nidhamu na kufanyia kazi malengo yangu madogo kila wiki kwa sababu najua yananiandaa kwa ajili ya siku ya mbio.

Wakati mwingine kuna mambo ambayo hunijaribu na kunizuia, kama hali ya hewa. Huenda nje kuna joto sana au baridi sana, au labda mvua inanyesha. Hivyo ninakimbia nikiwa ndani kwenye mashine ya kukimbilia, ingawa ninapendelea kukimbia mtaani. Majeraha pia hunijaribu na kunizuia. Labda sikujinyoosha vyema kabla ya kukimbia, hivyo natonesha mishipa yangu ya paja. Au labda sio kosa langu kwamba ninaumia. Lakini bila kujali linaokea vipi, siwezi kuacha kwa sababu najua nitakimbia mbio za nyika mwaka ujao. Hivyo ninafanya mabadiliko ya mazoezi yangu. Ninapona na kurejea kwenye kukimbia.

Kukimbia kumenifundisha mengi kuhusu injili. Sote tuna lengo la muda mrefu la kuvumilia mpaka mwisho na kupokea kuinuliwa. Lakini tunaweka malengo ya muda mfupi kama kupokea sakramenti kanisani kila wiki ambayo hutusaidia kufika pale. Tunapata jeraha kiroho tunapofanya makosa. Ila hatukati tamaa. Tunatubu, na kuendelea na safari. Njia pekee ya kufikia lengo letu la muda mrefu ni kwa kufanya mabadiliko madogo katika njia nzima ili kutusaidi kubakia katika njia.

Picha
mwanamke akichagua uelekeo wa kutembea upande mmoja wa barabara

Chagua Kubadilika

Kwa zaidi ya muongo, nimefanya kazi kama makamu wa rais mwandamizi wa Walmart huko Brazil. Familia yangu ilikuwa vyema kifedha, nilifurahia kazi yangu na maisha yalikuwa mazuri. Lakini kazi ilinihitaji kutumika sana. Ilinihitaji kusafiri sana, kitu ambacho kiliingiliana na familia yetu na huduma yangu Kanisani. Baada ya miaka 11 au 12, ilikuwa imezidi.

Mimi na mke wangu tulishauriana na kupendekeza kwamba niache kazi hii. Tulilizungumza hili na watoto wetu, na kwa pamoja tukasema, “Ni muda sasa wa sisi kufanya badiliko.”

Nilipoacha kazi nilidondoka kutoka makamu wa rais mpaka kutoajiriwa. Ilichukua takribani mwaka mmoja kupata na kukubali kazi nyingine. Niliposhika nafasi kwenye kampuni ya mali zisizohamishika huko Marekani, nilihisi vyema kuhusu jambo hili. Kazi hii ingeniruhusu kuweka wakfu muda wangu mwingi kwenye vitu vyenye thamani zaidi.

Lakini watu wengine waliniambia nilikuwa kichaa. Kwa nini kuacha kazi nzuri na kwenda kwenye kampuni ya mali zisizohamishika ambayo hakuna hata mtu aliwahi kuisikia? Na kuhama kutoka makazi yako kwenda Marekani?

Walikuwa sahihi kwamba hili ni badiliko kubwa tulilokuwa tunachagua. Lakini hawakuwa sahihi kwamba lilikuwa chaguo dhaifu.

Ilihitaji imani kubwa sana kwa sisi kubadili kazi zetu na kuhamia nchi mpya, lakini Bwana alitujali. Na nilikuwa na muda zaidi wa kutimiza majukumu yangu kama mume, baba na muumini wa kata.

Ninaamini badiliko ni la muhimu ili kufikia uwezekano wetu. Kamwe hatutakuwa kile Baba wa Mbinguni anatutaka tuwe kama hatupigi hatua kwenye maisha yetu. Na tunakuwa kama Yeye tunapofanya mabadiliko ya makusudi kwa imani.

Kulazimishwa Kubadilika

Badiliko jingine kubwa lililotokea katika familia yangu ni pale kaka yangu mdogo kabisa alipokufa katika ajali ya gari. Hatukuchagua au kutaka hilo kwetu wala kwake, na bado linaumiza, hata baada ya miaka 10. Badiliko la kulazimishwa si rahisi.

Lakini mabadiliko tusiyoyachagua yanaweza pia kuwa fursa ya kujenga imani yetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Ni rahisi kubaki waaminifu pale mambo yanapokuwa upande wetu. Lakini je, tunaweza kuitunza imani na kuendelea kusonga pale mabadiliko yasipokuwa upande wetu?

Talaka, ugumba, kukosa ajira, ugonjwa na uzoefu mwingine mchungu kama huu sio uzoefu tunaotumainia na kuupanga. Unaweza kutufanya tuhisi kama maisha yapo nje ya uwezo wetu. Lakini hilo sio kweli kabisa—katikati ya hali zako usizotegemea, kuna mambo ambayo bado unaweza kuyathibiti. Unaweza kuweka malengo madogo, hata lengo tu la kuivuka siku moja. Unaweza kutenda! Unaweza kuhimili vitu vyote kwa subira! (ona Alma 38:4).

Yusufu wa Misri ni mfano mkubwa wa hili. Maisha yake yalikuwa yamejaa mabadiliko ya kulazimishwa—alipoteza uhuru wake mara mbili! (Mara ya kwanza wakati kaka zake walipomuuza kwenye utumwa na tena wakati Potifa alipomtupa gerezani.) Lakini Yusufu hakuvunjika moyo kwa sababu hali zake hazikuwa nzuri au za kupangwa. Alijifunza kukua kupitia uzoefu wake. Na hatimaye, aliiokoa familia yake na nchi nzima. Bwana alikuwa anamfinyanga na kumwandalia njia nzima (ona Mwanzo 37–46).

Ni vigumu kuwa na subira wakati mabadiliko ya kulazimishwa yanaovuruga mpango wako, lakini kumbuka kwamba lengo la muda mrefu ni kufikia kuinuliwa. Baba wa Mbinguni anajua kile tunachohitaji kufika huko: “Ninyi hamwezi kustahimili uwepo wa Mungu sasa, wala kutumikiwa na malaika; kwa hiyo, endeleeni katika uvumilivu hadi mtakapokuwa mmekamilika” (Mafundisho na Maagano 67:13).

Picha
mwanaume akitembea njiani

Badiliko Hutusaidia Kuwa Kama Mwokozi

Baba wa Mbinguni anakupenda na anataka ufanikiwe. Anataka uwe na furaha. Kama alivyoweka mpango kwa ajili yako kupokea mambo hayo mawili.

Ninapoangalia maisha haya kwa kile ilichonuiwa kuwa—kujifunza—mabadiliko katika maisha yangu yanakuwa na lengo zaidi. Badiliko hunisaidia kufikia lengo langu la muda mrefu, ambalo ni kuwa kama Mwokozi wangu Yesu kristo. Ninajua Baba wa Mbinguni anashiriki lengo sawa la muda mrefu kwa ajili yangu na kwa ajili ya watoto Wake wote. Kama vile daktari wangu alijua nilihitaji kubadili kitu kwa ajili ya afya yangu, Mungu kwa dhahiri huona mabadiliko tunayohitajika kufanya ili kuwa kama Yeye. Anatujali na kutupatia nyenzo kama maandiko, mkusanyiko wa eneo husika na nabii anayeishi ili kutusaidia katika hamu yetu ya kubadilika kwa ajili ya wema.

Katika siku ngumu zaidi—siku hizo ambazo ni vigumu kutoka kitandani na kuvalia viatu vyako vya kukimbia, unapojua unahitaji kutubu, au unakabiliana na badiliko lingine lisilotarajiwa—tunajikumbusha kuhusu upendo usio na mwisho wa Mungu na hamu Yake ya sisi kuwa wenye furaha zaidi kuliko tulivyo sasa.

Ukumbusho huo hutupatia nguvu ya kufanya mabadiliko ambayo Roho hutuvuvia kuyafanya. Na hutusaidia kuamini kwamba mabadiliko tusiyotarajia tunayolazimishwa kufanya ni sehemu ya mpango Wake kwa ajili ya furaha yetu kuu.