2023
Wito Wetu wa Kushiriki Injili ya Mwokozi
Julai 2023


“Wito Wetu wa Kushiriki Injili ya Mwokozi,” Liahona, Julai 2023.

Wito Wetu wa Kushiriki Injili ya Mwokozi

Kama watumishi wa Mungu, tumeitwa kushiriki tumaini ambalo Mwokozi hutoa kupitia maisha Yake, mafundisho, Upatanisho na injili ya urejesho.

Picha
wamisionari wawili wa kiume wakiangalia tableti

Kama wamisionari vijana huko Uingereza, mimi na mwenzangu tulimfundisha mwanaume ambaye alikuwa amepitia matukio mabaya ya kuhatarisha maisha yake wakati wa Vita ya Pili ya Dunia. Alikuwa kwenye mapambano ya vita vya nchi kavu na kisha kunusurika kutoka kwenye shambulio baya la meli aliyokuwemo kabla ya kurejea Uingereza. Hatimaye alipofika Uingereza, alijawa na hisia nyingi na shukrani kwa kurejea nyumbani salama kwamba alipiga magoti, akabusu ardhi na kutoa shukrani.

Tulipomfundisha kuhusu Urejesho na kuelezea Ono la Kwanza la Joseph Smith, alilia. Akiwa na machozi katika macho yake, alielezea ushuhuda mkubwa aliopokea. Alielezea kwamba ujumbe wa Urejesho ulimpa hisia sawa na alizozipata aliporejea salama kwenye ardhi ya Uingereza. Alihisi kwamba alikuwa na hatma ya milele.

Picha
kundi la wamisionari huko Uingereza

“Injili ya urejesho hutoa nuru ile ambayo watoto wa Mungu huihitaji wakati wa misukosuko,” anasema Mzee Quentin L. Cook (safu ya juu, wa tano kutoka kulia), aliyetumikia katika misheni ya Uingereza pamoja na Mzee Jeffrey R. Holland (safu ya juu, wa saba kutoa kushoto).

Kulia: picha kwa hisani ya mwandishi

Wito wetu kama Watumishi wa Mungu

Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tu watumishi wa Mungu. Kama watumishi Wake, misheni yetu ni kushiriki pamoja na wengine—kama wale niliowafundisha huko Uingereza—tumaini litokalo kwa Mwokozi kupitia maisha Yake, Upatanisho na injili ya urejesho (ona 3 Nefi 27:13–14). Hiyo siyo kazi rahisi katika ulimwengu uliojaa wasiwasi, kukata tamaa na giza, lakini injili ya urejesho hutoa nuru ile ambayo watoto wa Mungu huihitaji wakati wa misukosuko.

Rais Russell M. Nelson ametangaza kwamba ulimwengu unahitaji injili ya Yesu Kristo sasa kuliko hapo awali: “Injili Yake ni jibu pekee wakati wengi katika ulimwengu wanashtushwa kwa woga. Hili inasisitiza hitaji la haraka kwetu la kufuata maelekezo ya Bwana kwa wanafunzi wake la ‘enendeni … kote ulimwenguni, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe’ [Marko 16:15, msisitizo umeongezwa; ona pia Mathayo 28:19]. Tuna jukumu takatifu la kushiriki nguvu na amani ya Yesu Kristo na wale wote watakaosikiliza na wale wataomruhusu Mungu ashinde katika maisha yao.” Rais Nelson aliongezea, “Kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya katika kuikusanya Israeli.”1

Picha
wamisionari wa kike na wanandoa wakiangalia simu

Njia moja tunayotimiza jukumu hilo ni kwa kukubali wito wa kutumikia kama wamisionari. Tunajua, vile Rais Nelson alivyosisitiza karibuni, kwamba jukumu la kazi ya umisionari kimsingi huwaangukia wavulana ambao wamehifadhiwa kwa ajili ya kusanyiko la siku za mwisho. Kwao hawa, kazi ya umisionari ni “jukumu la kikuhani.” Ingawa kazi ya umisionari si lazima kwa wasichana, Rais Nelson amewaomba wamwulize Bwana kama Yeye angependa vilevile wao watumikie. “Kile mnachochangia katika kazi hii ni kikubwa sana!” aliwaambia. Na ndio, Bwana anahitaji wanandoa wazee kutumikia pale hali zao zinaporuhusu. “Juhudi zao,” kwa maneno ya Rais Nelson, “hazina mbadala.”2

Njia nyingine tunayotimiza jukumu letu katika kuikusanya Israel ni kukumbuka maagano yetu ya “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote” (Mosia 18:9). Hatuhitaji wito wa kuwa mmisionari ili kusimama kama shahidi. Tunapoishi injili, kuwapenda na kuwatumikia wengine, tukisimama imara dhidi ya majaribu na mateso, na kutoa ushuhuda kwa maneno na matendo, tutawaleta wengine kwa Yesu Kristo.

Kushiriki injili inaweza isiwe rahisi hata kwa wale ambao tayari wametumikia misheni. Lakini tunapokuwa na ushuhuda imara wa Mwokozi na Urejesho, tunapaswa kutoa ushuhuda wa kile tunachokijua.

Picha
mwanamke akitabasamu

Umuhimu wa Ushuhuda

Ni kwa jinsi gani tunaimarisha ushuhuda wetu ili tuwe wamisionari wenye ufanisi? Tunahitaji tu kufuata ushauri wa nabii wetu anayeishi. Shuhuda zetu hukua pale tunapo:

  • Kuza hali yetu ya kiroho.3

  • Tenga muda kwa ajili ya Bwana.4

  • Imarisha msingi wetu wa kiroho.5

  • Mruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu.6

  • Msikiliza Yeye.7

Tunapojifunza maneno ya Rais Nelson na kufuata ushauri wake, tutaimarisha ushuhuda wetu wa Mwokozi na injili Yake, jukumu ambalo Nabii Joseph Smith alikuwa nalo wakati wa Urejesho, ukweli wa Kitabu cha Mormoni na wito wa manabii na mitume wa sasa. Ushuhuda imara utatuandaa sisi—na kukuza hamu yetu—ya kusikiliza wito wa kinabii wa Rais Nelson wa kukusanya Israeli katika pande zote za pazia.

Ili kushiriki injili ipasavyo, hatupaswi kuwa wazungumzaji wenye vipawa. Hatuhitaji kujua kila kipengele na kichwa cha habari cha fundisho la injili. Hatuhitaji kukariri dazeni ya maandiko. Hatuhitaji hata kuwa tumeelimika sana. Vitu hivyo hutusaidia kushiriki ujumbe wetu, lakini nguvu halisi ya uongofu hutokana na moyo mnyenyekevu, ushuhuda imara na ushahidi wa dhati kutoka kwa Roho Mtakatifu.

“Hakuna mtu,” alisema Nabii Joseph Smith, “anaweza kufundisha injili pasipo Roho Mtakatifu.”8

“Moto katika Mifupa Yangu”

Mnamo 1830, baada ya kusikia wamisionari wakifundisha ujumbe wa urejesho wa injili, Brigham Young alitaka kujua mwenyewe ukweli wa kile walichokuwa wakifundisha. Kiuhalisia, alisoma Kitabu cha Mormoni na pia tabia za wale waliokishuhudia na ya Nabii Joseph Smith.

Kitu fulani kuhusu wamisionari hao wa mwanzo kiligusa moyo na nafsi ya Brigham. “Ushuhuda wao ulikuwa kama moto katika mifupa yangu,” alisema.9

Mmoja wa wamisionari hao, Eleazer Miller, alikuwa muumini wa Kanisa kwa miezi minne tu.10 Alikuwa, katika lahaja ya sasa ya kimisionari, ni “mchanga,” na hakuwa mzungumzaji mzuri kwa watu. Lakini vitu hivyo havikuwa kikwazo.

Picha
Eleazer Miller

Eleazer Miller

Miaka kadhaa baadaye, Rais Brigham Young alitangaza: “nilipomwona mtu asiye na lugha ya ushawishi, au talanta ya uzungumzaji kwa umma, ambaye angeweza tu kusema, ‘Najua, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli [na] kwamba Joseph Smith ni nabii wa Bwana[,]’ Roho Mtakatifu kutoka kwa mtu huyo aliangazia uelewa wangu, na nuru, utukufu na kutokufa [vilikuwa] mbele yangu.”

Rais Young alisema alikuwa amezungukwa na kujazwa na nuru hiyo na utukufu na kwamba alijua yeye mwenyewe kwamba ushuhuda wa Eleazer ulikuwa wa kweli.

“Ulimwengu pamoja na hekima yote na nguvu, na utukufu wote, pamoja na wafalme na watawala waliovikwa kwa dhahabu,” Rais Young anasema, “huishia kutokuwa wa muhimu ukilinganisha na ushuhuda rahisi, usiovikwa wa mtumishi wa Mungu.”11

Shangwe Yetu ni Kubwa Kiasi Gani

Nabii Joseph Smith alitangaza, “Baada ya yote yale ambayo yamesemwa, kazi kuu sana na muhimu sana ni kuhubiri injili.”12

Kuheshimu maagano yetu kama washiriki wa ufalme wa Mungu hujumuisha kushiriki injili ya Yesu Kristo. Kushiriki injili ni mojawapo ya maonesho makubwa sana ya kumpenda jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe (ona Mathayo 22:37–39). Kushiriki injili ni wito mkuu wa Mwokozi.

Wale miongoni mwetu waliosaidia kuleta nafsi kwa Kristo wameonja furaha ya milele iliyoahidiwa kwa wale watakaofanya kazi ya kuwaokoa watoto wa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 18:15–16). Bado ninafikiria huduma yangu ya misheni kama mmisionari kijana huko Uingereza—wenza niliotumikia nao, watu tuliokutana nao, wana na mabinti wazuri wa Mungu tuliosaidia kuwaleta kwenye zizi Lake. Maisha yangu kamwe hayakuwa hivyo hivyo badaaye.

Kutoka kwenye uzoefu binafsi, ninarejelea ahadi ya Urais wa Kwanza kwa wale “wanaouleta ukweli ulimwenguni,”13 iwe nyumbani au ugenini: “Bwana atakuzawadi na kukubariki kwa wingi unapomtumikia Yeye kwa unyenyekevu na kwa maombi. Furaha zaidi inakungojea kuliko ile uliyowahi kuipata unapofanya kazi miongoni mwa watoto Wake.”14

Mihutasari

  1. Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6.

  2. Russell M. Nelson, “Hubiri Injili ya Amani” 6, 7.

  3. Russell M. Nelson, “Nguvu ya Kasi ya Kiroho,” Liahona, Mei 2022, 97–100.

  4. Russell M. Nelson, “Tenga Muda kwa ajili ya Bwana,” Liahona, Nov. 2021, 120–21.

  5. Ona Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021, 93–96.

  6. Ona Russell M. Nelson, “Acha Mungu Ashinde,” Liahona, Nov. 2020, 92–95.

  7. Ona Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Liahona, Mei 2020, 88–92.

  8. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 332.

  9. Ona Leonard J. Arrington, Brigham Young: American Moses (1985), 20, 29.

  10. Ona Arrington, Brigham Young, 30.

  11. Ona Brigham Young, “A Discourse,” Deseret News, Feb. 9, 1854, 4.

  12. Teachings: Joseph Smith, 330.

  13. We’ll Bring the World His Truth,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 173.

  14. Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Huduma ya Umisionari (2019), v.