2010–2019
Wazazi: Ni Walimu wa Kimsingi wa Watoto Wao
Oktoba 2014


Wazazi: Ni Walimu wa Kimsingi wa Watoto Wao

Baada ya kila kitu, nyumbani ndilo baraza linalofaa kwa kufunza injili ya Yesu Kristo.

Ben Carson alisema kujihusu yeye mwenyewe. “Mimi nilikuwa mwanafunzi mdhaifu sana katika darasa langu lote la 5.” Siku moja Ben alifanya mtihani wa hesabu ukiwa na maswali 30. Mwanafunzi aliyekaa nyuma yake alisahihisha na kumrudishia. Mwalimu, Bi Williamson, alianza kumwita kila mwanafunzi ataje alama alizopata. Mwishowe, akafikia kwa Ben. Kwa aibu, alitaja alama yake kwa sauti ya chini. Bi Williamson, akifikiri alisema “9” akirejea alichosema Ben alama 9 kati ya 30 alikuwa ameonyesha bidii. Mwanafunzi nyuma ya Ben kisha akapaza sauti, “Siyo tisa! … Hakupata chochote … sahihi.” Ben alisema alitamani kuingia ardhini.

Wakati huo huo mama yake Ben, Sonya, naye alikumbana na pingamizi zake mwenyewe. Alikuwa mmoja wa watoto 24, alikuwa na elimu ya darasa la tatu, na hakuweza kusoma. Aliolewa akiwa na umri wa miaka 13, alitalikiwa, alikuwa na wana wawili, na alikuwa akiwalea katika mitaa ya Detroit. Hata hivyo, alikuwa anajitegemea sana na alikuwa anaamini kwamba Mungu angemsaidia yeye na mwanawe kama wangefanya wawezavyo.

Siku moja mambo yakabadilika katika maisha yake na yale ya wanawe. Aligundua kwamba watu waliofanikiwa ambao alikuwa akiwasafishia nyumba walikuwa na maktaba--walisoma. Baada ya kazi alirudi nyumbani na kuzima televisheni ambayo Ben na kaka yake walikuwa wakiangalia. Alisema: Ninyi vijana mnaangalia sana televisheni. Kuanzia sasa mtaangalia vipindi vitatu kwa wiki. Katika muda wenu wa ziada mtakwenda kwenye maktaba – someni vitabu viwili kwa wiki na mnipe taarifa.

Wale wavulana walishtuka. Ben alisema hajawahi kusoma kitabu katika maisha yake yote isipokuwa pale inapohitajika kufanya hivyo shuleni. Walipinga, walilalamika, walibishana, lakini aliweka wazi alichotaka kifanyike. “Aliweka sheria. Sikupenda sheria, lakini juhudi zake za kutaka sisi tufanikiwe zilibadilisha mwelekeo wa maisha yangu.”

Na je, ni mabadiliko makubwa jinsi gani ilileta. Akiwa katika darasa la saba alikuwa namba moja darasani. Aliendelea na kujiunga na Chuo Kikuu cha Yale kwa udhamini, kisha Chuo cha Udaktari cha Johns Hopkins, ambako akiwa na miaka 33 akawa Daktari Mkuu wa Upasuaji wa nurolojia wa watoto na akajulikana ulimwenguni kote. Je, iliwezekana vipi? Ni kwa sababu ya mama ambaye bila ya msaada wa maisha alitumikia wito wake kama mzazi.1

Maandiko yanazungumzia juu ya majukumu ya wazazi---hayo ni wajibu wao wa kuwafundisha watoto wao “mafundisho ya toba, imani katika Yesu Mwana wa Mungu aliyehai, na ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu” (M&M 68:25).

Kama wazazi tunatakiwa kuwa walimu wakuu wa injili na mfano kwa watoto wetu---siyo askofu, Shule ya Jumapili, Wasichana au Wavulana, bali wazazi. Kama walimu wao wa kimsingi wa injili, tunaweza kuwafundisha uwezo na uhalisia wa Upatanisho---kujitambua kwao na kudura takatifu---na kwa kufanya hivyo tunatoa msingi imara ambao juu yake hujengwa. Hatimaye, nyumbani ndiyo sehemu muhimu kwa mafundisho ya injili ya Yesu Kristo.

Karibu mwaka mmoja uliopita nilikuwa katika jukumu huko Beirut, Lebanon. Nikiwa huko nilijifunza juu ya msichana wa miaka 12, Sarah. Wazazi wake na ndugu zake wawili walijiunga na Kanisa huko Romania lakini walitakiwa kurudi nchini kwao wakati Sarah akiwa na miaka saba. Wakiwa nchini kwao hapakuwa na Kanisa, hakuna kikundi kilichoanzishwa, hapakuwa na Shule ya Jumapili, au mipango ya wasichana. Baada ya miaka mitano familia hii iligundua tawi huko Beirut na kabla sijafika huko walimpeleka binti yao wa miaka 12 Sarah, akisindikizwa na ndugu zake wakubwa, ili kuja kubatizwa. Wakiwa huko nilifundisha juu ya mpango wa wokovu. Sarah mara nyingi alinyoosha mkono na kujibu maswali.

Baada ya mkutano, na kufahamu kuwa alikuwa hajui chochote kuhusu Kanisa, nilimwendea na kumwuliza, “Sarah, ulijuaje majibu ya maswali yale?” Kwa haraka akajibu, “Mama yangu alinifundisha.” Hawakuwa na Kanisa katika jamii yao, lakini walikuwa na injili katika nyumba yao. Mama yake alikuwa mwalimu wa kimsingi wa injili wake.

Alikuwa ni Enoshi aliyesema, “Maneno ambayo nimeyasikia mara nyingi baba yangu akiongea juu ya uzima wa milele, na furaha ya watakatifu, yalizama ndani ya moyo wangu” (Enoshi 1:3). Hakuna swali la kujiuliza ni nani alikuwa mwalimu wa injili wa Enoshi.

Ninakumbuka baba yangu akijinyosha kando ya moto akisoma maandiko na vitabu vingine vizuri, nami nilimkaribia kando yake. Ninakumbuka kadi yake aliyoitunza katika mfuko wake wa shati ikiwa na nukuu za maandiko na Shakespeare na maneno mapya ambayo angeyakariri na kujifunza. Ninakumbuka swali la injili na mahojiano wakati wa chakula cha jioni. Ninakumbuka mara nyingi baba yangu alinichukua ili kwenda kuwatembelea wazee---jinsi tulivyosimama na kununua barafu kwa ajili ya mtu mmoja au kuku kwa mtu mwingine au kusalamiana kwa mkono ukiwa na pesa. Ninakumbuka hisia nzuri na kutamani kuwa kama yeye.

Ninakumbuka mama yangu akiwa na miaka 90 au zaidi, akipika jikoni na kisha akitoka jikoni na sinia la chakula. Nilimwuliza alikuwa akienda wapi. Alijibu, “Oo, napeleka chakula kwa wazee.” Nikajiuliza mwenyewe, “Mama, wewe mwenyewe ni mzee.” Ninashindwa kutoa shukrani za kutosha kwa wazazi wangu ambao walikuwa walimu wangu wa kimsingi wa injili.

Mojawapo ya vitu vya maana sana tunavyoweza kufanya kama wazazi ni kuwafundisha watoto wetu juu ya nguvu za maombi, siyo tu maombi ya kila siku. Nilipokuwa na miaka 17, nilipiga magoti karibu na kitanda changu nikiomba. Bila ya kujua, mama yangu alikuwa amesimama mlangoni. Nilipomaliza, alisema, “Tad, unamwomba Bwana akusaidie kupata mke mwema?”

Swali lake hakika lilinishangaza sana. Hayo yalikuwa mawazo tofauti na yangu. Mimi nilikuwa nafikiria kuhusu mpira na shule. Na hivyo, nikamjibu, “Hapana,” ambapo yeye alijibu, “Sawa, unatakiwa kufikiria hayo, kijana, utakuwa ni uamuzi muhimu ambao unaweza kuufanya katika.” Maneno hayo yaliingia moyoni mwangu kwa kina, na hivyo, kwa miaka sita iliyofuata niliomba Mungu ili anisaidie kupata mkwe mwema. Na, Oo, amejibu maombi yangu.

Kama wazazi, tunaweza kuwafundisha watoto wetu kuomba kwaajili ya mambo ya milele---kuomba ili kuwa wasafi kimwili katika dunia hii yenye changamoto, kuwa watiifu, na kuwa na msukumo wa kusimama katika haki.

Bila shaka vijana wetu wengi wanakuwa na sala za jioni, lakini inawezekana wengi wao wanapata shida katika sala ya asubuhi. Kama wazazi, kama walimu wao wakuu wa injili, tunaweza kulirekebisha hili. Ni mzazi gani katika nyakati za Kitabu cha Mormoni angeweza kuwaacha vijana wake waende vitani wakiwa mstari wa mbele bila ngao na kinga na jambia ili kujikinga na maadui? Lakini ni wangapi kati yetu tunawaacha watoto wetu wakitoka nje ya mlango kila asubuhi kwenda sehemu za hatari za vita, kukutana na Shetani, na majaribu yake mengi, bila ya kinga yao ya kiroho na ngao na jambia litokanalo na nguvu za uwezo wa maombi? Bwana alisema, “Ombeni daima .…ili muweze kumshinda Shetani” (M&M 10:5). Kama wazazi tunaweza kuanzisha kwa watoto wetu tabia na uwezo wa sala za asubuhi.

Pia tunaweza kuwafundisha watoto wetu kutumia muda wao vizuri. Wakati mwingine, kama vile Sonya Carson, tutahitaji kulazimisha kwa upendo ili kupunguza muda wa televisheni kwa watoto wetu na vifaa vingine vya michezo, ambavyo mara nyingi huchukua muda mwingi wa maisha yao. Badala yake tutahitajika kuuongoza muda wao katika mambo mazuri zaidi ambayo yanahusiana na juhudi za injili. Panaweza pakatokea na ukaidi, kulalamika, lakini kama Sonya Carson, tunahitaji kuwa na mtazamo mzuri na nia ya kuuendeleza. Siku moja watoto wetu wataelewa na kushukuru kwa kile tulichokifanya. Tusipofanya hivyo, ni nani atafanya?

Wote tunaweza kujiuliza: je, watoto wetu wanapata msaada wa kiroho, kiakili, na ufumbuzi, au wanapata mabaki ya muda wetu na talanta zetu baada ya kujitolea katika miito yetu ya Kanisa au kazi zetu? Katika maisha yajayo, sijui kama cheo cha uaskofu au Rais wa Muungano wa Kina Mama vitanusurika, lakini ninajua kwamba vyeo vya mume na mke, baba na mama, vitaendelea bila ya kikomo. Hiyo ndiyo sababu moja ni muhimu kuheshimu majukumu yetu kama wazazi hapa duniani ili tuweze kujiandaa kwa yale yaliyo makubwa, lakini yanayofanana, majukumu ya maisha yajayo.

Kama wazazi, tunaweza kuendelea tukiwa na uhakika kuwa Mungu hatatuacha pekee yetu. Mungu hatupi majukumu bila ya kuandaa msaada wake wa kiungu---kwa hayo ninashuhudia. Ninaomba katika majukumu yetu matakatifu kama wazazi, tukishirikiana na Mungu, tuwe walimu wa kimsingi wa injili na mfano kwa watoto wetu, ninaomba katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Ben Carson, Gifted Hands: The Ben Carson Story (1990).