2010–2019
Baki katika Mashua na Ujishikilie!
Oktoba 2014


Baki katika Mashua na Ujishikilie!

Tukiweka lengo letu kwa Bwana, tunaahidiwa baraka zisizo na kifani:

Hivi majuzi, rafiki yangu alimpeleka mwanawe kwenye safari katika Mto wa Colorado kupitia Cataract Canyon, iliyo kaskazini mashariki mwa Utah. Hili korongo kuu ni maarufu kwa ajili ya maili 14 (kilomita 23) ya mikondo mikali ambayo inaweza kuwa hatari sana.

Katika maandalizi ya safari yao isiyo ya kawaida, walikuwa wamerejelea kwa makini tovuti ya National Park Service, ambayo ina habari muhimu kuhusu uandalizi wa kibinafsi na hatari za kawaida zilizofichika.

Mwanzoni mwa safari, kiongozi mmoja wa mto aliye na uzoefu alirejelea maelezo muhimu ya usalama, akitilia mkazo sheria tatu muhimu ambazo zingehakikisha usafiri salama wa kikundi kupitia maji ya mikondo mikali. “Sheria nambari moja: baki katika mashua! Sheria nambari mbili: vaa koti la kuokoa kila wakati! Sheria nambari tatu: jishikilie kwa mikono yote kila wakati!” Kisha akasema tena, na himizo zaidi, “Juu ya yote, kumbuka sheria nambari moja: baki katika mashua!!”

Safari hii isiyokuwa ya kawaida inanikumbusha safari yetu duniani. Wengi wetu hupitia wakati katika maisha yetu ambapo utulivu maishani hufurahiwa. Wakati mwingine, sisi hupitia nyakati za shida ambayo kwa njia ya mfano inalinganishana na maji ya mikondo mikali yanayopatikana katika sehemu ya maili 14 kwenye Cataract Canyon---changamoto ambazo zinaweza kujumuisha maswala ya kimwili na kiakili, kifo cha mpendwa, ndoto na tumaini lililovunjwa, na---kwa wengine---hata mgogoro wa imani wanapokabiliwa na shida za maisha, maswali na shaka.

Bwana katika wema Wake ametoa usaidizi, ikiwa ni pamoja na mashua, vifaa muhimu kama vile makoti ya kuokoa, na viongozi wa mto walio na uzoefu amabo wanatoa mwongozo na maelekezo ya usalama kwetu ili kutusaidia kusafiri kwenye mto wa maisha hadi katika hitima yetu ya mwisho.

Tufikirieni kuhusu sheria ya nambari moja: “Baki katika mashua!”

Raid Brigham Young kwa kawaida alitumia “Old Ship Zion” kama mfano wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Alisema wakati moja: “Tuko katikati ya bahari. Dhoruba inakuja, na kama vile mabaharia husema, meli inang’ang’ana. ‘Sitabaki hapa,’asema mmoja; ‘Siamini hii ni “Ship Zion.”’ ‘Lakini tuko katikati ya bahari.’ ‘Sijali, sitabaki hapa’ Anavua koti lake, na kuruka kutoka kwenye mashua. Je, hatazama? Ndio. Hivyo pia, na wale wanaoondoka katika Kanisa hili. Ni ‘Ship Zion Nzee,’ tubakini ndani yake.”1

Wakati mwingine, Rais Young alisema kwamba alikuwa na wasiwasi juu ya watu kupoteza njia yao wakati wao walikuwa wanabarikiwa---wakati maisha yalikuwa mazuri: “Ni katika hali ya hewa shwari, wakati meli ya zamani ya Sayuni inasafiri na upepo mpole, na wakati mambo yote ni tulivu juu ya staha, ndipo baadhi ya ndugu wanataka kwenda nje katika mashua ndogo ili … kuogelea; na baadhi yao wamezama, wengine walipotelea mbali, na wengine tena wanarudi kwenye meli. Tubakini katika meli nzee, na itatubeba salama hata kwenye bandari. Hauhitaji kuwa na hofu.”2

Na mwisho, Rais Young aliwakumbusha Watakatifu: “Tuko ndani ya meli nzee ya Sayuni. ... [Mungu] yu katika usukani, na atabaki pale. … Yote yako sawa. Imba haleluya; kwa ajili Bwana yu hapa. Anaonyesha, anaongoza, na anaelekeza. Kama watu wana imani thabiti katika Mungu wao, wasiwahi kuacha maagano yao wala Mungu wao, atatuongoza vyema.”3

Na changamoto zote tunazokabiliana nazo leo, tutabakiaje kwenye Old Ship Zion?

Hivi ndivyo jinsi! Tunafaa kuwa na uongofu wa kuendelea kwa kuongeza imani yetu katika Yesu Kristo na uaminifu wetu kwa injili Yake maishani mwetu wote---siyo tu mara moja, lakini kila mara. Alma aliuliza, “Na sasa, tazama, ninawaambia, ndugu zangu [na dada], ikiwa mmepata mabadiliko ya moyo, na ikiwa mmesikia kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi, ningeuliza, mnaweza kuhisi hivyo sasa?”4

Viongozi wa mto walio na uzoefu leo wanaweza kufananishwa na mitume wa Kanisa na manabii, na viongozi wa ukuhani wenye maongozi wa maeneo yetu na wa vikundi saidizi. Wanatusaidia kufika salama kwa hitima yetu ya mwisho.

Hivi majuzi, nilizungumza katika semina ya marais wapya wa misheni na nikawashauri viongozi hawa:

“Wasaidieni wote walio katika misheni yenu kuwalenga viongozi wa Kanisa. … Hatutawapoteza … hatuwezi kuwapoteza.

“Mnapowafundisha wamisionari wenu kutulenga sisi, wafundisheni wasiwahi kuwafuata wale wanaofikiria wanajua zaidi kuhusu jinsi ya kusimamia mambo ya Kanisa kuliko Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo wanavyofanya kupitia viongozi wa ukuhani ambao wana funguo kuongoza.

“Nimegundua katika huduma yangu kwamba wale ambao wamepotea na kuchanganyikiwa kwa kawaida ni wale ambao mara nyingi zaidi … wamesahau kwamba wakati Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili wanapozungumza kwa sauti ya umoja, ni sauti ya Bwana kwa wakati huo. Bwana anatukumbusha, ‘Iwe kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa.’[M&M 1:38].”5

Kwa maneno mengine, wao huicha Old Ship Zion---wanaanguka mbali; wanaasi. Kwa bahati mbaya, mara nyingi wao hupitia matokeo yasiyotarajiwa ya muda mfupi na hatimaye muda mrefu, si tu kwao wenyewe lakini kwa familia zao pia.

Viongozi wetu wa Kanisa wa maeneo yetu, kama viongozi wa mto walio na uzoefu, wamefunzwa na uzoefu wa maisha; wamepata mafunzo na kushauriwa na mitume na manabii na maafisa wengine wa Kanisa; na muhimu zaidi, wamefunzwa na Bwana Mwenyewe.

Wakati mwingine mwaka huu, niliwazungumzia vijama wazima wa Kanisa katika tangazo la mkutano wa Ibada wa MEK wa mei. Nilisema:

“Nimesikia kwamba baadhi ya watu wanadhani viongozi wa Kanisa huishi katika ‘dunia yao ya kipekee.’ Wanachosahau ni kwamba sisi ni wanaume na wanawake wenye uzoefu, na tumeishi maisha yetu katika maeneo mengi na kufanya kazi na watu wengi kutoka asili mbalimbali. Kazi yetu ya sasa ya Kanisa inatupeleka duniani kote, ambapo tunakutana na viongozi wa kisiasa, kidini, biashara, na viongozi wa masuala ya kibinadamu ya dunia. Ingawa tumetembelea White House kule Washington, DC na viongozi wa mataifa duniani kote, tumetembelea pia nyumba zisizo za kifahari duniani, ambapo tumekutana na kuwahudumia [familia na watu] maskini. …

“Unapozingatia kwa kutafakari maisha yetu na huduma, huenda ukakubaliana kwamba sisi huona na kuishi duniani katika njia ambao wachache wengine huishi. Utafahamu kwamba sisi huishi katika “maisha yetu ya kipee” vichache kuliko watu wengi. …

“… Kuna kitu kuhusu hekima ya kibinafsi na ya jumla ya [viongozi wa Kanisa] ambacho kinapaswa kitoe kiwango cha faraja. Tumeyapitia yote, ikiwa ni pamoja na matokeo ya sheria mbalimbali ya umma na sera, kukatishwa tamaa, majanga, na vifo katika familia zetu wenyewe. Tunafahamu yale mnayopitia maishani mwenu.”6

Pamoja na sheria nambari moja kama nilivyoitumia, kukumbuka sheria nambari mbili na tatu: vaa koti ya kuokoa kila mara, na jishikilie kwa mikono yote miwili. Maneno ya Bwana, yanapatikana katika maandiko na mafundisho ya mitume na manabii. Yanatupatia ushauri na mwelekeo ambao, unapofuatwa, utakuwa kama koti la kuokoa la kiroho na utatusaidia kujua jinsi ya kushikilia kwa mikono yote miwili.

Tunahitaji kuwa kama wana wa Mosia ambao “waliongezwa nguvu kwa ufahamu wa ukweli.” Tunaweza kuwa wanaume na wanawake “wa ufahamu mwema.” Hii inaweza kutimizwa tu kwa “kuyapekua maandiko kwa bidii, ili [sisi] tujue neno la Mungu.”7

Katika kusoma maandiko na maneno ya manabii na mitume wa kale na wa sasa, tunapaswa tuzingatie kusoma, kuishi, na kupenda mafundisho ya Kristo.

Pamoja na kukuza desturi ya kusoma maandiko kibinafsi, tunafaa kuwa kama wana wa Mosia na tujitolee “kwa sala, na kufunga.”8

Inaonekana kwamba vitu hivi ambavyo haviwezi kupimwa kwa urahisi ni vya umuhimu mkuu. Baki ukizingatia vitu hivi rahisi na kuepuka kupotoshwa.

Nilivyowajua watu ambao hawajabaki katika mashua na hawajajishikilia kwa mikono yote miwili wakati wa nyakati za majaribio na matatizo au ambao hawajabaki katika mashua wakati wa utulivu kiasi fulani, Nimegundua kwamba wengi wao wamepoteza lengo lao kwenye kweli za msingi za injili---sababu kwa nini walijiunga na Kanisa mwanzoni, sababu walibaki kujitolea kikamilifu na kushughulika katika kuishi viwango vya injili na kuwabariki wengine kupitia huduma ya dhati, ya kujitolea, na jinsi Kanisa limekuwa katika maisha yao “mahali pa lishe ya kiroho na ukuaji.”9

Joseph Smith alifundisha ukweli huu wa msingi: “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa manabii na mitume kuhusu Yesu Kristo, … “kwamba alikufa, alizikwa, na alifufuka tena siku ya tatu, na kupaa mbinguni;’ na mambo mengine yote ni viambatisho kwa haya, ambayo yanahusiana na dini yetu.”10

Tukiweka lengo letu kwa Bwana, tunaahidiwa baraka zisizo na kifani: “Kwa hivyo, lazima msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, mkiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote. Kwa hivyo, kama mtasonga mbele mkila na kusheherekea neno la Kristo, na mvumilie hadi mwisho, tazama, hivyo ndivyo asema Baba: Mtapokea uzima wa milele.”11

Wakati mwingine Watakatifu wa Siku za Mwisho na wachunguzi waaminifu wanaojifunza kuhusu Kanisa huanza kuzingatia “viambatanisho” badala ya kanuni za msingi. Yaani, Shetani hutujaribu kupotoka kutoka kwa ujumbe rahisi na wazi wa injili rejesho. Wale ambao wanapotoshwa hivi mara nyingi huacha kupokea sakramenti kwa sababu wamelenga, hata kuhimiza kabisa, vitendo na mafunzo yasiyo ya muhimu.

Wengine wanaweza kuzingatia maswali na mashaka wanayopitia. Bila shaka, kuwa na maswali na kupitia mashaka si kuwa haiendani na uanafunzi wa kujitolea. Hivi majuzi, Baraza la Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili lilisema: “Tunaelewa kwamba mara kwa mara washiriki wa Kanisa watakuwa na maswali juu ya mafundisho, historia, au desturi za Kanisa. Washiriki daima wako huru kuuliza maswali kama hayo na kwa bidii kutafuta uelewa mkubwa.”12

Kumbuka, Joseph Smith mwenyewe alikuwa na maswali yaliyoanzisha Urejesho. Alikuwa mtafutaji wa ukweli na, kama Ibrahimu, alipata majibu ya maswali muhimu ya maisha.

Maswali muhimu huzingatia kile ambacho kina umuhimu zaidi---Mpango wa Baba yetu na Upatanisho wa Mwokozi. Kutafuta kwetu kunafaa kutuelekeze kuwa wafuasi wakarimu, wapole, wenye upendo, wenye subira, na wa kujitolea. Lazima tuwe tayari, kama Paulo alivyofundisha, “Mchukuliane mizigo na kuitimiza sheria ya Kristo.”13

Kuchukuliana mizigo kunajumuisha kusaidia, kuhimili, na kuelewa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wagonjwa, wanaoteseka, maskini kimwili na kiroho, mtafutaji na anayetaabika, na pia wafuasi wenginie washiriki---ikiwa ni pamoja na viongozi wa Kanisa ambao wameitwa na Bwana kuhudumu kwa muda.

Ndugu na dada, bakini katika mashua, tumieni makoti yenu ya kuokoa, shikilieni kwa mikono yenu yote miwili. Epukeni kupotoshwa! Na ikiwa yeyote mwongoni mwenu ameanguka nje ya mashua, tutawatafuta, tutawapata, na kuwatumikia na kuwavuta salama kurudi kwenye Old Ship Zion, ambapo Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo wako kwenye usukani na watatuongoza vyema, kwa hayo ninashuhudia kwa unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Teachings of Presidents of the Church: Brigham Young (1997), 82–83.

  2. Brigham Young, “Discourse,” Deseret News, Jan. 27, 1858, 373.

  3. Brigham Young, “Remarks,” Deseret News, Nov. 18, 1857, 291.

  4. Alma 5:26.

  5. M. Russell Ballard, “Mission Leadership” (hotuba iliyotolewa katika seminari kwa marais wapya wa musheni, June 25, 2014), 8.

  6. M. Russell Ballard, “Be Still, and Know That I Am God” (ibada ya Mpango wa Elimu wa Kanisa, May 4, 2014); lds.org/broadcasts.

  7. Alma 17:2.

  8. Alma 17:3.

  9. Barua ya Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili ya, Juni  28, 2014.

  10. Joseph Smith,Elders’ Journal,July 1838, 44.

  11. 2 Nefi 31:20.

  12. Barua ya Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili ya, Juni 28, 2014.

  13. Wagalatia 6:2.