2010–2019
Sakramenti---Kufanywa Upya kwa Nafsi
Oktoba 2014


Sakramenti---Kufanywa Upya kwa Nafsi

Roho huponya na hufanya upya nafsi zetu. Ahadi iliyoahidiwa juu ya sakramenti ni kwamba “daima Roho Wake atakuwa pamoja [nasi].”

Wakati mmoja, kundi la wasichana liliniuliza, “Unatamani ungelijua nini ulipokuwa na umri wetu?” Kama ningejibu swali hili sasa, ningejumuisha wazo hili: “Ningependa wakati nilipokuwa umri wenu nielewe umuhimu wa sakramenti vyema kuliko nilivyokuwa nikielewa. Ningependa nielewe sakramenti katika njia ambayo Mzee Jeffrey  R. Holland alielezea. Alisema, ‘Mojawapo ya mialiko katika ibada ya sakramenti ni kwamba iwe kweli tukio la kiroho, Ekaristi Takatifu, kufanywa upya kwa nafsi.’1

Je! Sakramenti inawezaje “kuwa tukio la kweli la kiroho, ekaristi takatifu, kufanywa upya kwa nafsi” kila wiki?

Sakramenti huja kuwa tukio la kuimarisha roho tunaposikiliza sala yake na kuahidi kushika upya maagano yetu. Ili kufanya hivyo, ni lazima tuwe tayari kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo.2 Akiongea kuhusu ahadi hii, Rais Henry  B. Eyring alifundisha: “Hii inamaanisha kuwa sisi lazima tujione wenyewe kuwa ni mali Yake. Tutamweka mbele katika maisha yetu. Tutataka kile anachotaka wala si kile sisi tunachotaka au kile ulimwengu unafundisha tutake.”3

Tunapopokea sakramenti, sisi pia hufanya agano la “daima kumkumbuka”4 Yesu Kristo. Katika usiku ule kabla ya kusulubiwa kwake, Kristo aliwakusanya Mitume Wake karibu Naye na akaanzisha sakramenti. Aliumega mkate, akaubariki, na kusema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu ambao nimeutoa kama ukombozi kwa ajili yenu”5 Kisha akatwaa kikombe cha mvinyo, akatoa shukrani, akawapa mitume Wake wanywe, na kusema, “Hii ni ukumbusho wa damu yangu … , imwagikayo kwa ajili ya wengi watakaoamini katika jina langu.”6

Miongoni mwa Wanefi, na tena katika Urejesho huu wa Kanisa Lake katika siku za mwisho, Yeye alirudia kwamba tunapaswa kupokea sakramenti kwa ajili ya ukumbusho Wake.7

Tunapopokea sakramenti, tunashuhudia kwa Mungu kwamba tutamkumbuka Mwanawe daima, siyo tu wakati wa ibada fupi ya sakramenti. Hii inamaanisha kwamba sisi kila mara tutatazama mifano na mafundisho ya Mwokozi ili yaongoze mawazo yetu, chaguo zetu, na matendo yetu.8

Sala ya sakramenti pia hutukumbusha kwamba sisi lazima “tushike amri zake.”9

“Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”10 Sakramenti hutupatia nafasi ya kujitathmini na nafasi ya kugeuza mioyo yetu na matakwa yetu kwa Mungu. Utiifu kwa amri huleta nguvu za injili katika maisha yetu, amani kuu na kuimarisha roho.

Sakramenti hutoa muda wa tukio la kweli na la kiroho pale tunapotafakari juu ya nguvu za Mwokozi za ukombozi na uwezeshaji kupitia Upatanisho Wake. Kiongozi wa Wasichana majuzi alijifunza kuhusu nguvu tunazopokea tunapojitahidi kupokea sakramenti kwa umakini. Akishughulikia kukamilisha moja ya mazoezi yaliyoko katika Kijitabu cha Maendeleo Binafsi kwa Wasichana, alijiwekea lengo la kuzingatia maneno yaliyomo katika nyimbo na sala za sakramenti.

Kila wiki, alijifanyia tathmini ya kibinafsi wakati wa sakramenti. Alikumbuka makosa aliyokuwa amefanya, na akajiwekea ahadi ya kufanya vyema wiki ifuatayo. Alishukuru kuwa aliweza kurekebisha mambo na kuwa msafi. Akitazama nyuma, kuhusu jambo hilo alisema, “Nimekuwa nikiitendea kazi toba ambayo ni sehemu ya Upatanisho.”

Jumapili moja baada ya kujitathmini mwenyewe, alianza kujiona mnyonge na mwenye kukosa raha. Aliweza kuona kwamba alikuwa anafanya makosa yale yale tena na tena, wiki hadi wiki. Lakini kisha akaona taswira ya kipekee kwamba alikuwa anaipuuza sehemu kubwa ya Upatanisho---nguvu za Kristo za uwezeshaji. Alikuwa anasahau wakati wote kwamba Mwokozi alikuwa akimsaidia kuwa kile alichohitaji kuwa na kutoa huduma zaidi ya uwezo wake.

Akiwa na jambo hilo akilini, alitafakari tena juu ya wiki iliyopita. Alisema: Hisia za furaha zilipenya katika huzuni wangu nilipotambua kwamba Yeye alikuwa amenipa nafasi kubwa na uwezo mwingi. Nilitambua kwa shukrani uwezo niliokuwa nao wa kuelewa mahitaji ya mtoto wangu wakati haikuwa wazi. Nilitambua kwamba katika siku ambayo nilihisi singeweza kutimiza kitu, niliweza kutoa maneno ya kumuimarisha rafiki. Nilionyesha subira katika hali ambayo kwa kawaida ni kinyume changu.”

Alihitimisha, “Nilipomshukuru Mungu kwa uwezo wa uwezeshaji wa Mwokozi katika maisha yangu, nilijiona mwenye matarajio makubwa juu ya mchakato wa toba niliokuwa ninaushughulikia na nilitazamia wiki inaokuja kwa tumaini mpya.”

Mzee Melvin  J. Ballard alifundisha jinsi sakramenti inavyoweza kuwa tukio la uponyaji na utakasaji. Alisema:

“Ni nani kati yetu ambaye hajaumiza roho yake kwa neno, wazo, au tendo, kutoka Sabato hadi Sabato? Tunafanya vitu ambavyo tunavijutia na tunapenda kusamehewa. … Mbinu ya kupokea msamaha ni … kutubu dhambi zetu, kuwaendea wale ambao tumewatendea mabaya au kuwakosea na kupata msamaha wao na kisha kurekebishwa hadi kwenye meza ya sakramenti ambapo, kama tumetubu kwa uaminifu na kujiweka kwenye hali nzuri, tutasamehewa, na uponyaji wa kiroho utakuja kwenye nafsi zetu.  …

“Mimi ni shahidi,” Mzee Ballard alisema, “kwamba kuna roho anayeshughulikia usimamizi wa sakramenti ambaye huchangamsha nafsi kutoka kichwani hadi miguuni; unaweza kusikia vidonda vya roho vikiponywa, na mzigo ukiinuliwa. Faraja na furaha huja kwenye nafsi ambayo ni stahiki na kwa kweli inatamani kupokea hiki chakula cha kiroho.”11

Nafsi zetu ambazo zilijeruhiwa zinaweza kuponywa na kufanywa upya siyo tu kwa sababu mkate na maji yanatukumbusha dhabihu ya Mwokozi ya mwili na damu Yake bali ni kwa sababu nembo hizi zinatukumbusha kwamba Yeye daima atakuwa “mkate wa uzima” wetu 12 “maji ya uzima.”13

Baada ya kutoa sakramenti kwa Wanefi, Yesu alisema:

“Yule ambaye anaula huu mkate anakula mwili wangu kwa nafsi yake; na yule ainywaye hii divai, anakunywa damu yangu kwa nafsi yake; na nafsi yake haitaona njaa wala kiu, lakini itajazwa.

“Sasa baada ya umati kunywa na kula, tazama, walijazwa na Roho.”14

Kwa maneno haya, Kristo anatufundisha kwamba Roho huponya na hufanya upya nafsi zetu. Baraka iliyoahidiwa ya sakramenti ni kwamba sisi “daima Roho wake atakuwa pamoja [nasi].”15 Kwa maneno haya, Kristo anatufundisha sisi kwamba Roho huponya na hufanya upya nafsi zetu

Ninapopokea sakramenti, wakati mwingine ninachora mchoro akilini mwangu ambao unamwonyesha Mwokozi Mfufuka akiwa na mikono Yake imenyoshwa, kana kwamba Yeye yu tayari kutupokea katika kumbatio Lake la upendo. Naupenda mchoro huu. Ninapoufikiria wakati sakramenti inapoandaliwa, nafsi yangu huinuliwa kabisa kana kwamba ninaweza kusikia maneno ya Mwokozi: “Tazama, mkono wangu wa rehema umenyoshwa kwenu, na yeyote atakayekuja, nitampokea; na heri wao ambao huja kwangu.”16

Wenye Ukuhani wa Haruni humwakilisha Mwokozi wanapotayarisha, kubariki, na kupitisha sakramenti. Mwenye ukuhani anyooshapo mkono wake kutupa nembo hizo takatifu, ni kama vile Mwokozi Mwenyewe anavyonyoosha mkono Wake wa rehema, akimwalika kila mmoja wetu kupokea vipawa vya thamani vya upendo vinavyopatikana kupitia dhabihu Yake ya upatanisho---vipawa vya toba, msamaha, faraja, na tumaini.17

Kadiri tunavyozidi kutafakari umuhimu wa sakramneti, ndivyo inavyozidi kuwa takatifu na yenye maana kwetu. Hivi ndivyo Baba mkongwe wa miaka 96 alivyosema wakati mwanawe alipomwuliza, “Baba, kwa nini wewe huenda kanisani? Wewe huwezi kuona, huwezi kusikia, ni vigumu kwako kutembea. Kwa nini wewe huenda kanisani?” Baba yule alijibu, “Ni sakramenti. Mimi huenda kupokea sakramenti.”

Acha kila mmoja wetu aje kwenye mkutano wa sakramenti akiwa tayari kuona “tukio kweli la kiroho, ekaristi takatifu, kufanywa upya kwa nafsi.”18

Najua kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu wanaishi. Ninashukuru kwa ajili ya fursa ambayo sakramenti hutoa ili tuuone upendo Wao na kumpokea Roho Mtakatifu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.