2010–2019
Sheria ya Mfungo: Jukumu la Kibinafsi Kuwajali Maskini na Walio na Mahitaji
Oktoba 2014


Sheria ya Mfungo: Jukumu la Kibinafsi Kuwajali Maskini na Walio na Mahitaji

Kama wanafunzi wa Mwokozi, tuna jukumu la kibinafsi kuwajali maskini na wenye mahitaji

Kina ndugu zangu wapendwa, ninaupenda ukuhani, na ninapenda kuwa nanyi. Ninashukuru sana kwamba tunaweza kuhudumu pamoja katika kazi hii kuu.

Tunaishi nyakati nzuri sana. Maendeleo ya kimiujiza katika maswala ya afya, sayansi, na teknologia yameboresha uzuri wa maisha kwa watu wengi. Bado kuna ushahidi wa mateso makuu na dhiki ya binadamu. Zaidi ya vita na matishio ya vita, ongezeko la majanga---ikiwa ni pamoja na mafuriko, moto, mitetemeko ya ardhi, na ugonjwa---vinaathiri maisha ya mamilioni duniani kote.

Uongozi wa Kanisa unafahamu na kutazamia hali njema ya maisha ya watoto wa Mungu kila mahali. Wakati wowote na popote pawezekanapo, raslimali ya Kanisa ya dharura hutolewa kupitia juhudi za kusaidia ili kutekeleza mahitaji hayo. Kwa mfano, Novemba uliyopita, Typhoon Haiyan iligonga kisiwa cha taifa la Philippines.

Kibunga kikali cha kategori ya 5, Haiyan kilisababisha madhara makuu na mateso. Miji mzima iliharibiwa; wengi walikufa, mamilioni ya nyumba ziliharibiwa vibaya na kuvunjwa; na huduma za msingi kama vile maji, mifereji ya maji machafu na stima hazikufanya kazi.

Raslimali za Kanisa zilitolewa punde tu kufuatia janga hili. Washiriki wa Kanisa wanaoishi Philippines walijitolea kwa pamoja kuwaokoa kina ndugu na dada zao kwa kuwapa chakula, maji, nguo, na vifaa vya usafi kwa washiriki wa Kanisa na wasio washiriki bila ubaguzi.

Nyumba za mikutano za Kanisa zikawa mahali pa faraja kwa maelfu ya watu ambao nyumba zao zilikuwa zimeharibiwa. Chini ya uongozi wa Urais wa Eneo na viongozi wa ukuhani wa eneo, wengi ambao walikuwa wamepoteza kila kitu walichokuwa nacho, makadirio yalitolewa ili kuangazia hali na usalama wa washiriki wote. Mipango iliyovutiwa ikaanza kutekelezwa ili kusaidia kurejesha washiriki katika hali sawa ya kuishi na kujitegemea.

Vifaa visivyokuwa vya kifahari vilitolewa ili kusaidia washiriki wa Kanisa kujenga upya makazi ya framu ya mbao na nyumba. Hii haikuwa tu toleo la bure. Washiriki walipata mafunzo na wakafanya kazi iliyohitajika kwao wenyewe na kisha kwa wengine.

Baraka moja iliyokuja na haya yote ilikuwa kwamba washiriki walikuza ujuzi wa useremala, ufundi wa mabomba, na wa ujenzi, waliweza kupata fursa za maana za kufanya kazi wakati miji na jamii jirani zilipoanza kujenga upya.

Kuwatunza maskini na wahitaji ni fundisho la kimsingi la injili na jambo muhimu katika mango wa milele wa wokovu.

Kabla ya utumishi Wake duniani, Yehova alitangaza kupitia kwa nabii Wake “Kwa maana masikini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, masikini wako, katika nchi yako” 1

Katika siku zetu, kuwajali maskini na wenye mahitaji ni mojawapo wa majukumu yaliyotolewa kiungu yanayosaidia watu binafsi na familia kustahili kuinuliwa. 2

Kuwajali maskini na wenye mahitaji kunazingatia uokovu wa kimwili na kiroho. Kunajumuisha huduma ya washiriki binafsi wa Kanisa wanapowatumikia kibinafsi masikini na walio na mahitaji, pamoja na usaidizi rasmi wa Kanisa, ambao hutolewa kupitia mamlaka ya ukuhani.

Kitovu cha mpango wa Bwana katika kuwatumikia maskini na walio na mahitaji ni sheria ya mfungo. “Bwana ametoa sheria ya kufunga na kutoa sadaka ili kubariki watu Wake na kutoa njia kwao kuhudumia wale walio na mahitaji”3

Kama wafuasi wa Mwokozi, tuna jukumu la kibinafsi kuwatumikia maskini na walio na mahitaji. Washiriki waaminifu wa Kanisa kila mahali husaidia katika kuwatumikia maskini na walio na mahitaji kwa kufunga kila mwezi---kutokula na kunywa maji kwa masaa 24--- na kisha kutoa kwa Kanisa toleo la pesa sawa na angalau bei ya chakula ambacho wangekula.

Maneno ya Isaya yanapaswa yazingatiwe kwa maombi na kufundishwa katika kila nyumba:

“Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

“Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaletea masikini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? 4

Isaya kisha aliendelea na kuorodhesha baraka za ajabu zilizoahidiwa na Bwana kwa wale ambao wanatii sheria ya mfungo. Yeye Alisema:

“Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

“Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa...

“Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako; na kuisababisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri:

“Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji.” 5

Kuhusu andiko hili, Rais Harold  B. Lee alikuwa na haya ya kusema: “Baraka kuu zinazokuja [kutokana na kufunga] zimewekwa wazi katika kila nyakati, na hapa katika maandiko Bwana anatuambia kupitia nabii huyu mkuu kwa nini kuna kufunga, na baraka zinazokuja kutoka kwa kufunga. … Ukichanganua … mlango wa 58 wa kitabu cha Isaya utapata sababu ya kwa nini Bwana anataka tulipe toleo la mfungo, kwa nini anataka tufunge. Ni kwa sababu ya kustahili hivi tunaweza kumwita na Bwana anaweza kuitika. Tunaweza kulia na Bwana atasema, ‘Mimi hapa.’”

Rais Lee anaongeza: “Je, tunataka kuwa katika hali ambapo tunaweza kumwita na hasijibu? Tutalia katika shida yetu na hatakuwa nasi? Nafikiria ni wakati tufikirie kuhusu kanuni hizi za msingi kwa sababu hizi ndizo siku zijazo, ambapo tutahitaji zaidi na zaidi baraka za Bwana, wakati hukumu inatolewa pasipo kuchanganywa juu ya duniani yote.” 6

Nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, ameshiriki ushuhuda wake wa kanuni hizi---ushuhuda uliokuja kupitia uzoefu wa kibinafsi. Alisema: “Hakuna mshiriki wa Kanisa ambaye amesaidia kutolea wale walio katika mahitaji atawahi kusahau ama kujuta tukio hilo. Bidii, uwekevu, kujitegemea, na kushiriki na wengine si mambo mapya kwetu.” 7

Ndugu, washiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni watu wa kufanya maagano na kutii amri. Siwezi kufikiria juu ya sheria yoyote, amri yoyote, ambayo, ikitiiwa kwa uaminifu, ni rahisi zaidi kutii na ambayo inatoa baraka zaidi kuliko sheria ya mfungo. Tunapofunga na kutoa toleo aminifu la mfungo, tunachangia kwa gala ya Bwana kile ambacho kingetumika kwa bei ya chakula. Haihitaji kujitolea zaidi kifedha kuliko kile kingetumika kwa kawaida. Wakati huo huo, tunaahidiwa baraka zisizo za kawaida, kama ilivyosemwa hapo mapema

Sheria ya kufunga inahusu kila mshiriki wa Kanisa. Hata watoto wadogo wanaweza kufundishwa kufunga, wakianza na mlo moja kisha miwili, wanapoweza kuelewa na kimwili kutii sheria ya mfungo. Mabwana na wake, washiriki waseja, vijana, na watoto wanapaswa waanze kufunga kwa maombi, wakitoa shukrani kwa baraka katika maisha yao wakiwa wanatafuta baraka za Bwana na nguvu wakati wa kufunga. Timizo la kikamilifu la sheria ya mfungo hufanyika wakati toleo la mfungo linapolipwa kwa wakala wa Bwana, askofu.

Maaskofu, mnaongoza usaidizi katika kata. Mnalo jukumu tukufu kuwatafuta na kuwatumikia maskini. Na usaidizi kutoka kwa viongozi wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama na jamii ya Ukuhani wa Melkizedeki, lengo lenu ni kuwasaidia washiriki waweze kujisaidia wenyewe na kujitengemea. Mnahudumia mahitaji ya kimwili na kiroho ya washiriki kwa kutumia matoleo ya mfungo kwa uangalifu kama usaidizi wa muda na kama ongezeko kwa rasilimali kutoka kwa familia na jamii. Unapotumia funguo za ukuhani na uwezo wa kubaini kwa maombi katika kuwasidia maskini na walio na mahitaji, utakuja kufahamu kwamba matumizi mema ya matoleo ya mfungo yamekusudiwa kuhimili maisha, na si maisha ya kifahari.

Marais wa jamii ya Ukuhani wa Haruni, mna funguo na mna nguvu za kuhudumu katika maagizo ya nje. Mnafanya kazi na askofu na kuwaelekeza washiriki wa jamii kuhusu wajibu wao katika ukuhani na kuwatafuta washiriki wa Kanisa ili kuwapa fursa ya kuchangia mfungo. Ninyi wenye Ukuhani wa Haruni mnapopanua majukumu yenu ya ukuhani na kutoa fursa hii kwa washiriki wa Kanisa, mara nyingi ninyi husaidia kutekeleza baraka zilizoahidiwa za kufunga kwa wale ambao huenda wakazihitaji zaidi. Mtashuhudia kwamba roho ya kuwajali maskini na walio na mahitaji ina nguvu ya kulainisha mioyo ambayo kawaida ni migumu na hubariki maisha ya wale ambao huenda hawahudhurii Kanisa kila mara.

Rais Monson alisema, “Wale maaskofu ambao hupanga jamii zao za Ukuhani wa Haruni kushiriki katika kuokota matoleo ya mfungo watapata mafanikio zaidi katika jukumu hili tukufu.”8

Maaskofu, kumbukeni kwamba hali zinatofautiana sana eneo moja hadi lingine na kutoka nchi moja hadi nyingine. Kwenda kwa washiriki wa jamii ya Ukuhani wa Haruni mlango moja hadi mlango huenda isiwezekane katika maeneo ambapo mnaishi. Hata hivyo, tunawaalika kwa maombi mzingatie ushauri wa nabii na mtafute kupata uvutio juu ya njia zinazofaa ambazo wenye Ukuhani wa Haruni katika kata yenu wanaweza kushiriki katika kuokota matoleo ya mfungo.

Katika mlango wa 27 wa 3 Nefi, Bwana aliyefufuka aliuliza, “Mnapaswa kuwa watu wa aina gani?” Alijibu, “Hata vile nilivyo.”9 Tunapochukua juu yetu wenyewe jina la Kristo na kutia bidii kumfuata Yeye, tutapokea mfano Wake katika nyuso zetu na kuwa zaidi kama Yeye. Kuwajali maskini na walio na mahitaji ni sehemu isiyoweza kutolewa katika utumishi wa Mwokozi. Iko katika kila kitu Yeye anachofanya. Anafikia kila mtu na kutuinua. Nira yake ni laini, na mzigo wake ni mwepesi. Ninaalika kila mmoja wetu kuwa zaidi kama Mwokozi kwa kuwatumikia maskini na walio na mahitaji, kwa kutii sheria ya mfungo, na kwa kuchanga toleo la ukarimu la mfungo. Ninashuhudia kwa unyenyekevu kwamba kuwatumikia kwa uaminifu maskini na walio na mahitaji ni onyesho la kukua kiroho na kutawabariki mtoaji na mpokeaji. Katika jina tukufu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Kumbukumbu la Torati 15:11.

  2. Ona Handbook 2: Administering the Church (2010), 2.2.

  3. Handbook 2, 6.1.2.

  4. Isaya 58:6–7.

  5. Isaya 58:8–11.

  6. Harold B. Lee, “Listen, and Obey” (Welfare Agricultural Meeting, Apr. 3, 1971), nakala ya kazi iliyopigwa chapa, 14, Church History Library, Salt Lake City.

  7. Thomas S. Monson, “Are We Prepared?” Ensign auLiahona, Sept. 2014, 4.

  8. Thomas S. Monson, katika mkutano na Uaskofu Simamizi, Feb. 28, 2014.

  9. 3 Nefi 27:27.