2023
Kuhudumu kwa Tumaini na Imani
Machi 2023


“Kuhudumu kwa Tumaini na Imani,” Liahona, Machi 2023.

Kanuni za Kuhudumu

Kuhudumu kwa Tumaini na Imani

Tunapotunza maagano yetu kwa imani, tunaweza kusaidia kuwaongoza wengine kwenye chanzo cha tumaini.

Picha
mwanamke akigusa pindo la vazi la Yesu

Mfano wa Tumaini na Imani

Katika Injili ya Marko, tunasoma maelezo ya kusisimua kuhusu “mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili.” Tunajifunza kwamba alikuwa “ameteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyonavyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya” (Marko 5:25–26).

Miaka kumi na miwili ni muda mrefu sana kuteseka. Vitu vyote ni kiasi kikubwa sana kugharamia. Na hali ilizidi kuwa mbaya. Ikiwa kuna mtu alikuwa na haki ya kuhisi kukosa tumaini, alikuwa ni mwanamke huyu.

Na bado, “aliposikia habari za Yesu, [mwanamke] alipita katika mkutano nyuma ya [Yesu], akaligusa vazi lake,” kwa sababu aliamini, “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.”

Marko anaeleza kwamba kwa sababu ya imani yake, “mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule” (Marko 5:27–29).

Tumaini na imani katika Yesu vilijibiwa kwa baraka. “Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena” (Marko 5:34).

Katika changamoto yoyote, licha ya ukubwa au urefu wa muda, tumaini linahitajika sana. Hofu na kukata tamaa vinaweza kutufadhaisha. Lakini tumaini na imani katika Yesu Kristo hualika nguvu na baraka Zake kwenye maisha yetu.

Kufanyia kazi Tumaini na Imani katika Kuhudumu

Kama akina kaka na akina dada wahudumiaji, tutahitajika kuomba tumaini na imani sawa na hiyo. Kuhudumu kunaweza kuwa vyote tuzo na changamoto. Wakati mtu tunayetaka kumsaidia haonekani kuhitaji msaada, inaweza kuwa rahisi kupoteza tumaini. Pengine unakabiliana na hali hii sasa kwa mwanafamilia, rafiki au mtu ambaye kwa sasa umepangiwa kumsaidia. Pengine, kama vile mwanamke mwenye tatizo la damu, ni Bwana pekee ajuaye ni muda na juhudi kiasi gani umetumia kujaribu kutafuta jambo linaloweza kusaidia. Lakini kama vile yule mwanamke, ikiwa tutatafuta tumaini la kuendelea kufikia kwa imani, nguvu ya Mwokozi inaweza kuleta tofauti.

Wakati mwingine changamoto ni kuwahudumia wale ambao wanapambana wenyewe kuhisi tumaini la kutosha kufanyia kazi imani. Kuna baadhi ambao, kama vile mwanamke katika Marko, wanaweza kukabiliwa na ugonjwa sugu, vikwazo vya kifedha au majaribu yoyote yanayoonekana kutokuwa na idadi. Kujua kwamba hawako peke yao katika mapambano yao kunaweza kuwa chanzo chenye nguvu cha tumaini. Tunaweza kuwasaidia wapate tumaini hili wakati tunapoonesha utayari wetu wa kubeba mizigo yao, kuomboleza pamoja nao, kuwafariji na kusimama kama mashahidi wa Mungu (ona Mosia 18:9–10).1

Picha
wanaume wawili wakisoma gazeti pamoja na msichana

Kukuza Tumaini na Imani

Tunawezaje kukuza sifa kama za Kristo za tumaini na imani? Hapa kuna baadhi ya mawazo:

  1. Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha kwamba tumaini ni kuamini kwamba Yesu Kristo atatimiza ahadi Zake kwako.2 Kwa sababu “tumaini ni kipawa cha Roho [ona Moroni 8:26],”3 ni jambo ambalo tunaweza kuliomba (ona Mafundisho na Maagano 46:7–9).

  2. Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba kukuza imani huitaji kazi. Alishiriki jinsi tunavyoweza kukuza imani yetu kupitia kujifunza, kuchagua kuamini, kutenda kwa imani, kupokea ibada takatifu kwa kustahili na kumwomba Baba wa Mbinguni usaidizi.4

Muhtasari

  1. Jeffrey R. Holland, “Kuchukuliana Mizigo,” Liahona, Juni 2018, 26–28.

  2. Ona Dieter F. Uchtdorf, “The Infinite Power of Hope,” Liahona, Nov. 2008, 22.

  3. Dieter F. Uchtdorf, “The Infinite Power of Hope,” 21.

  4. Ona Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima,” Liahona, Mei 2021, 103.